*Ahakikisha wanne wa familia yake wanapita

*Naye akichaguliwa uenyekiti atakamilisha ‘The Kikwete 5’

*Mwanae mwingine ni Mjumbe Chipukizi Taifa

*NEC ijayo itakuwa ya Baba, Mama na Watoto (BMW)

 

Mjadala mkali umeibuliwa katika mitandao mbalimbali ya kijamii, ukihusisha familia ya Kikwete kuwa na wagombea watano wa nafasi tofauti ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Tayari majina manne yameshapitishwa, huku jina la Rais Jakaya Kikwete likisubiriwa kuwa la tano wakati atakapojitokeza kuwania nafasi ya Mwenyekiti wa CCM Taifa.

 

Wakati hali ikiwa hivyo kwenye uchaguzi huu unaoelekea ukingoni, mtoto mwingine wa Rais Kikwete, Khalfan Kikwete ni Mjumbe wa Baraza Kuu Idara ya Chipukizi ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM). Mwenyekiti wa Idara hiyo ni Gabriel Makalla, ambaye ni mtoto wa Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Amos Makalla.

 


Kwenye orodha ya sasa, mke wa Rais Kikwete, Mama Salma Rashidi, amepitishwa rasmi kuwania ujumbe wa NEC Wilaya ya Lindi akiwa hana mpinzani. Hii ni mara ya kwanza katika historia ya Tanzania kwa mke wa Rais aliye madarakani kuwania nafasi kubwa kama hiyo ndani ya chama.


Katika mjadala unaoendelea kwenye mitandao, baadhi ya wachangiaji wamelinganisha “undugu” huo ndani ya CCM kwa kuuita “The Kikwete 5”, wakiufananisha na kundi maarufu la wanamuziki la “The Jackson 5” lililoundwa na wanandugu.


Wanahoji mantiki ya Mama Salma kujitokeza kuwania nafasi ilhali, akiwa tayari na heshima kubwa ya ‘First Lady’ katika jamii.


Mchangiaji mwingine amerejea kwa familia za viongozi wakuu waliopita na kuhoji, “Lini tulimsikia Mama Siti Mwinyi akiwania ujumbe wa NEC? Wapi umepata kusikia Mama Maria Nyerere akihangaika kwenye siasa badala ya kufuga kuku wake na kumtunza mumewe…Mkapa pamoja na maovu yake ya kufanya biashara akiwa Ikulu, hukumsikia Mama Anna akitaka ujumbe hata wa mtaa!”


Mtoto wa Rais Kikwete, Ridhiwani Jakaya, kama ilivyo kwa Mama Salma, naye amepita bila kupingwa kuwania ujumbe wa NEC kupitia Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani.


Baadhi ya wana-CCM na wananchi wengine wa kawaida wanahoji siri ya mafanikio hayo ya kupita bila kupingwa, ilhali chama hicho kikiwa na idadi kubwa ya wanachama wenye sifa za kutoa ushindani.


Mmoja wa wachangiaji kwenye mtandao wa Jamiiforums amesema, “Hawa wamepita bila kupingwa si kwa sababu wana sifa tu, bali wana nguvu. Unajua ukionekana unapingana nao ni sawa na kupingana na mkubwa (Rais Kikwete).”


Ameongeza, “Iliyobaki sasa ni Katiba mpya ijayo itambue kuwapo kwa mke na watoto wa rais au mwenyekiti wa chama. Kokote watakakojitokeza kugombea wapite bila kupingwa.”


Mwingine amesema, “Mke wa rais (mwenyekiti wa chama) kuchaguliwa kwenye chama si tatizo, maana anaweza kuwa na sifa zinazotakiwa na huwezi kumnyima haki yake ya kugombea kwa sababu tu eti ni mke wa rais/mwenyekiti.


“Tatizo ni mfumo wa kuchaguana ndani ya chama. Je, mifumo iko tayari kuhakikisha kuwa huyu hachaguliwi kwa kuwa tu ni mke wa rais/mwenyekiti. Kwa sababu hazuiwi kugombea kwa sababu tu ni mke wa rais/mwenyekiti, lakini pia hachaguliwi kwa kuwa tu ni mke wa rais/mwenyekiti.


Undugunaizesheni unakuja pale tu ambapo kuwa na uhusiano na kiongozi fulani ni sifa pekee ya kuchaguliwa! Ndiyo falme zilivyo. Unazaliwa mtoto wa mfalme, basi hiyo ni sifa tosha kukufanya uwe mfalme – huhitaji kingine chochote.


“Sasa kwa Lindi Mjini na Bagamoyo, ndiyo sehemu pekee wagombea wanasimama bila kupingwa na wote wawili wana sifa moja inayofanana – wana uhusiano na rais/mwenyekiti. Hiyo peke yake haitoshi kuhalalisha undugunaizesheni. Swali je, mfumo wa uchaguzi ulikuwa tayari kuhakikisha kuwa hawapendelewi? Tufanye uchunguzi mdogo tu. Je, wapo wana-CCM waliojitokeza wakashinikizwa wasigombee?


“Katika uchaguzi wetu, inawezekana mtu akataka kugombea lakini akapigwa mkwara asithubutu? Na wangegombea wengine, katika mfumo huu, nafasi zao kushinda zingekuwaje? Maana wengine wanaweza kusema ‘aah unagombea na mke wa Mwenyekiti, utapata kweli?’”

 

Ikijulikana wazi kuwa vikao vyote vya uteuzi ndazi ya Taifa vipo chini ya Rais Kikwete, kwa mara nyingine tena jina la dadake limepita bila shaka yoyote kwenye mchujo wa Kamati ya Maadili, Kamati Kuu (CC) hadi NEC.


Dadake Rais Kikwete, Mwanaisha Halfani Kikwete, amepitishwa kugombea Ujumbe Baraza Kuu/Halmashauri Kuu ya Umoja wa Wanawake (UWT) Mkoa wa Pwani. Kwenye orodha hiyo, kakake Rais Kikwete, Mohamed Mrisho Kikwete, amepitishwa kuwania nafasi ya Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Bagamoyo.


Kinachojadiliwa zaidi kwenye mtandao ni kile kinachoonekana kuwa Mwenyekiti Rais Kikwete alipuuza kupunguza machungu kwa waliong’olewa, kwa kumtosa japo ndugu yake mmoja.


Mchangiaji mwingine amesema, “Kama angemtosa japo mmoja kati ya wanafamilia wake angekuwa ame-balance equation…”


Mwingine kasema, “Hatujifunzi lolote kutoka nchi za Kiarabu? Gaddafi alipindua ufalme. Akaishia kuwa mfalme. Wanawe wakawa na nguvu za ajabu. Yuko wapi sasa! Huyu Rais wa sasa wa Syria alimrithi baba yake. Subirini muone atakavyoondoka madarakani.

 

Hosni Mubarak wa Misri alikuwa na nguvu sana yeye na familia yake. Wako wapi sasa! CCM ya sasa inayafanya mambo haya waziwazi. Tulidhani ingekuwa chama cha mfano. Akina Chadema wangeacha hiki walichokianza kwenye ubunge wa viti maalumu.”


Mwingine ameongeza, “Sema tu kukaa sana Ikulu au kupitapita mle kunakufanya uwe mwanasiasa na kiongozi mzuri sana! Akili zinaongezeka, unapendwa na watu, unachagulika au unapita bila kupingwa, unakuwa na vipaji hata ambavyo haukuzaliwa navyo!”


Wakati Mwenyekiti Rais Kikwete akibariki familia yake kuwania madaraka mbalimbali ndani ya CCM, Julai 28 mwaka huu alikemea tabia ya wanandugu kujazana kwenye kampuni. Alikuwa akizindua Karakana ya Ndege ya Kampuni ya Precision Air, Dar es Salaam.


Alisema kampuni nyingi nchini zimeshindwa kuendelea kutokana na kuendeshwa kifamilia, badala ya kuuza hisa na kumilikiwa na umma. Akazitaka zibadili mfumo wa uendeshaji.

“Watanzania wanaimiliki Precision Air kwa asilimia 59, huu ni mfano wa kuigwa kwa sababu ziko kampuni nyingi zimebaki kuwa za familia tu,” alisema.


Hata hivyo, wakati akirejesha fomu za kuteuliwa na CCM kuwania urais kwa muhula wa pili mjini Dodoma mwaka 2010, alitetea suala la familia. Kauli yake ilikuja baada ya kuwapo minong’ono mingi kwamba alikiweka kando chama wakati wa kutafuta wadhamini, badala yake akamtumia mwanawe, Ridhiwani.

 

Baadhi ya wachunguzi wa mambo wanaamini kuwa hata ushindi mdogo alioupata mwaka huo ulitokana, pamoja na mambo mengine, na dosari ya wana-CCM kuona chama ni cha kifamilia zaidi.


Akimtetea Ridhiwani, alisema, “Wako waliouliza kwanini Ridhiwani, na mimi nikauliza kwa nini asiwe Ridhiwani? Nataka kusema kugombea urais ni jambo nililoamua mwenyewe, siyo chama, kwa hiyo lazima nifanye juhudi zangu binafsi kutafuta wadhamini kwa hiyo kumtumia mwanangu ambaye ni mtu wa karibu…halikuwa tatizo,” alifafanua Rais Kikwete akizungumzia timu hiyo ya vijana 32 iliyoongozwa na mwanawe.


Alisema wako watu waliodai amewadharau viongozi wa wilaya, kata na vijiji, hoja aliyoipinga na kueleza kuwa jukumu la viongozi hao ni kuandaa watu watakaomdhamini, lakini jukumu la kuzunguka kutembeza fomu kuomba udhamini ni la mgombea (la familia).

CCM waipa nafuu Chadema

Wachangiaji wengine wamesema uamuzi wa Mwenyekiti Kikwete kuibeba familia yake kumewasaidia mno Chadema ambao walionekana kujipa vyeo kwa misingi ya nasaba. Freeman Mbowe ambaye ni Mwenyekiti wa sasa wa Chadema, alishika nafasi hiyo kutoka kwa mkwewe, Edwin Mtei.


Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, ana dadake, Christina ambao wote ni wabunge. Mbunge wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo (Ndesa Pesa) ana binti yake Lucy Owenya na mkwe wake, Grace Kiwelu. Wote ni wabunge. Rose Kamili ambaye ni Mbunge wa Viti Maalumu, ni mzazi mwenziwe na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbroad Slaa.

Wazee

Wakati wa kikao cha NEC mjini Dodoma wiki iliyopita, Rais Kikwete alisema vijana wengi wamepewa nafasi ili kukiandaa chama. Hata hivyo, aliweza kusimamia upitishwaji majina ya baadhi ya wana-CCM ambao wameanza kuchoka kiumri.


Baadhi yao ni Balozi Patrick Chokala (64).  Huyu amekuwa Mwandishi wa Habari wa Rais (Awamu ya Pili) na Balozi wa Tanzania nchini Russia. Amewania ujumbe wa NEC kupitia Shinyanga Vijijini. Mwaka 2005 Chokala alijitokeza kuomba ridhaa ya kuiwakilisha CCM mwenye uchaguzi wa rais, lakini akashindwa.


Mwanasiasa mkongwe, Ali Mchumo (67 ). Amewania NEC kupitia Wilaya ya Kilwa. Ameshika nyadhifa mbalimbali za uwaziri na ubalozi.


Mwanasiasa wa siku nyingi, Kate Kamba (61). Huyu ameshika nyadhifa mbalimbali katika CCM na Serikali. Wadhifa wake wa mwisho alikuwa Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki. Amewania u-NEC kupitia Wilaya ya Masasi.


Mwingine ni Dk. Amani Kabourou (63) anayewania nafasi ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kigoma. Amewahi kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kabla ya kuhamia CCM.


Akiwa na wadhifa huo, aliwahi kuwa mbunge katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Aliporejea CCM alichaguliwa kuwa mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki.

 

Mzee mwingine aliyepitishwa ni Lumuli Kasyupa (73). Huyu amewania ujumbe wa NEC kupitia Wilaya ya Kyela. Amewahi kuwa Mbunge wa Kyela katika miaka ya 1970 na 1980.

 

Waziri wa zamani wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Gideon Cheyo (73), amepitishwa kuwania ujumbe wa NEC kupitia Wilaya ya Ileje, Mbeya.


Aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa, Meja Jenerali Makame Rashid (68), alipitishwa kuwania ujumbe wa NEC kupitia Wilaya ya Tandahimba, Mtwara. Baada ya kung’atuka ukuu wa JKT, aliteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchi Malawi.


Mkuu wa Wilaya mstaafu, Seif Mpembenwe (65), amepitishwa kuwania nafasi ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Pwani.


Mkongwe mwingine ambaye amekuwa mbunge kwa miaka kadhaa, Dk. Zainab Gama (63), amepitishwa kuwania nafasi ya Katibu Uenezi wa CCM Mkoa wa Pwani.

 

By Jamhuri