Mwaka 2008 nilibahatika kuwa mmoja wa watu waliopata fursa ya kusafiri na Rais Jakaya Kikwete kwenda jijini Washington, Marekani. Safari hii ilikuwa ikihusiana na mambo mbalimbali lakini kubwa ni kushawishi Serikali ya Marekani kuridhia Mpango wa Millennia Challenge Cooperation (Account) – MCC.

Tukiwa jijini Washington nilipata fursa ya kuzungumza na maafisa kadhaa wa Serikali ya Marekani. Kwa bahati nzuri ukiwa nchini mwao huwa Wamarekani wanasema ukweli wote. Wamelelewa katika mazingira ya kusema ukweli na wanafuatilia ukweli. Mmoja wa maafisa hao aliniambia hivi. “You are lucky to have such a serious President [Kikwete], who not only fair well at the international level, but also at home has managed to combat bank crimes.”

‘Kikurya’ hicho nilichoambiwa nikikitafsiri katika Kiswahili afisa huyu alimaamisha hivi: “Mna bahati kuwa na Rais makini  [Kikwete], ambaye si tu anatenda vyema katika ngazi ya kimataifa, bali hata nyumbani ameweza kudhibiti uhalifu wa kibenki.” Mmarekani huyu alinishangaza kuona anafuatilia hadi masuala ya hapa nyumbani na kufahamu kuwa tulikuwa na tatizo sugu la wizi katika benki zetu.

Sitanii, baniani mbaya lakini kiatu chake dawa. Yapo mambo ananikera Kikwete, na naamini hata yeye na familia yake wanafahamu hivyo kuwa ananikera katika hayo. Na mambo haya si mengine, bali ni tabia yake ya kutofanya uamuzi katika masuala ya msingi. Kila linapotokea jambo anakimbilia kuunda Tume, wakati alistahili kutumia kitu tunachoita executive powers (nguvu za kidola) kuweka mambo sawa.

Lakini ndugu yangu huyu Mkwele yeye anataka kila jambo aendelee kuonekana ni mwema bali wanaomwangusha ni wasaidizi wake. Ndiyo maana unakuta anasaini miswada ya sheria yenye makosa inafumuliwa hata kabla ya kutumika, anakabidhi hundi yenye maneno na tarakimu zinazotofautiana viwango, anakabidhi magari ya wagonjwa kwa watendaji wa halmashauri za wilaya wasio wenyewe, na mengine mengi lakini hachukui uamuzi wa kumfukuza kazi mtu aliyemwaibisha kwa kutenda hayo.

Ukiacha hayo, ipo sura nzuri ya Kikwete. Hii si nyingine ni ile aliyoieleza Mmarekani niliyezungumza naye mwaka 2008. Wakati Kikwete anaingia madarakani mwaka 2005 ilikuwa kila mtu anatumia kila senti aliyonayo kuweka mlango wa chuma wenyewe wanaita geti. Ilikuwa ukienda baa majambazi wanakulaza chini na kuchukua hata ada ya watoto uliyokuwa umeihifadhi usiinywee pombe.

Benki na kwenye maduka ya kubadilisha fedha majambazi ndiko walikuwa wakifanyia mazoezi. Nilisafiri kwenda Lubumbashi katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, ambako nilikuta watu wanauza fedha (bureau de change) kwenye stuli katika viambaza vya maduka na barabara. Unakuta kijana mchuuzi wa fedha ameshikilia hadi dola milioni tano na madafu ya faranga, lakini hakuna anayethubutu kumwibia.

Nilijaribu kuwauliza wenyeji wa Lubumbashi na hata Kinshasa, kuwa inakuwaje fedha zinaanikwa nje na kukandamizwa kwa jiwe zisipeperushwe na upepo lakini majambazi hawazigusi? Jibu nililopewa lilinifariji. “Mwizi ni adui wa maendeleo. Tukimuona hatusubiri kumufikisha polisi. Tunamumaliza papo hapo na wengine wanajifunza somo hawaibi tena,” alisema kijana wa Kicongo.

Sitanii, sisemi twenda mkondo huo wa Wacongo, wenye kurasimisha sentensi ya “wananchi wenye hasira kali” lakini kama inasaidia kumaliza ujambazi, nadhani si wazo baya. Ni katika hatua hiyo namkumbuka Kikwete. Alituahidi kuwa tutakuwa tunalala milango wazi baada ya kudhibiti majambazi wote nchini.

Hakika hili kwa muda lilikuwa limetekelezeka. Desemba yote mwaka jana hakuna basi la abiria lililotekwa kanda ya Ziwa wakati wakubwa wakienda kula Krismasi. Matukio ya ujambazi, ukiacha Tabata Kisukuru na Tungi kwa akina Nyaronyo Kicheere, kwa kiasi kikubwa ulidhibitiwa. Katika hili nasema hongera Kikwete.

Kwa upande wa uhuru wa kujieleza, Tanzania imepiga hatua kubwa. Vyombo vya habari vimekuwa huru zaidi, wananchi wamepata uhuru wa kuandamana na kutoa mawazo yao tofauti na ilivyokuwa enzi za utawala wa mkono wa chuma, Benjamin William Mkapa. Wananchi sasa wameandamana mpaka wakaishiwa hamu ya maandamano ikafikia hatua baadhi ya vyama vya siasa vikakosa waandamanaji.

Hata hivyo, pamoja na haya yote kufanyika lipo jambo moja Kikwete hajalifanya. Tunasifiwa kimataifa kwa Kikwete kukuza uhuru wa vyombo vya habari, lakini Serikali yake nayo imetumbukia kwenye mtego ule ule sawa na watangulizi wake. Hadi leo Serikali yake imeigomea Sheria ya Haki ya Kupata Habari na Sheria ya Utumishi katika Vyombo vya Habari.

Sheria hizi mbili zingetungwa, Kikwete angehitimisha heshima yake na kuipeleka nchi hii mbele kimaendeleo kwa kasi kubwa. Ni kwa bahati mbaya ahadi za kutunga sheria hizi zimekuwa nyingi, na kila wakiguswa mawaziri wenye dhamana wanasema sheria hizi zimefikia hatua nzuri. Zamu hii wameahidi kikao cha mwezi Oktoba kuwa tutapata sheria hizi. Tunasubiri sasa kuona kama wataishi ahadi zao.

Hapa ndipo ubaya wa Kikwete ulipolala. Kwamba vyombo vya habari vinaendeshwa kwa huruma yake si kwa mujibu wa sheria. Atatusogeza hivyo, hadi anaondoka madarakani. Kikwete angejenga heshima ya pekee ikiwa tu angepata ujasiri wa kutunga sheria hizi, wananchi na waandishi wa habari wakafanya kazi zao kwa mujibu wa sheria bila hofu ya sheria hizi mbaya tulizonazo leo.

Sitanii, kichwa cha habari cha makala haya kinasema ‘Kikwete polisi wanaanza kuyeyusha heshima uliyojijengea’. Kwa kurejea niliyosema hapo juu kuwa tunafanya kazi kwa huruma ya Kikwete na si kwa mujibu wa sheria, polisi sasa wameanza kuzitumia sheria mbaya ambazo zipo tangu enzi kudhibiti vyombo vya habari.

Tumeshuhudia uvumilivu ukimwishia Kikwete na kutumia Sheria ya Magazeti ya Mwaka 1976 kufungia gazeti la Mwanahalisi. Nilipata kuandika na kwa kuwa naamini hili ni jambo jema naomba nilirudie. Serikali haiheshimu vyombo vya habari. Mbona Chama cha Walimu Tanzania (CWT) walipotangaza mgomo Serikali ilikimbilia mahakamani na kutumia hati ya dharura kusitisha mgomo huo? Kama inaheshimu vyombo vya habari na utawala wa sheria ilishindwa nini kulipeleka gazeti la Mwanahalisi Mahakamani?

Hili tuliache. Katika historia ya nchi hii hatukuzoea kusikia watu wakiuawa na vyombo vya dola. Leo limegeuka jambo la kawaida. Inawezekana Kikwete ukasema hujawatuma polisi, lakini hapa ndipo nakwambia heshima uliyojijengea ndani na nje ya nchi inayeyuka kwa kasi kubwa kutokana na mauaji yanayoendelea.

Najua polisi wako ni wataalam wa kutunga. Watakuwa wanakupa taarifa kuwa watu wanaofariki katika maandamano wamebainika kurushiwa kitu kizito. Inawezekana waliokuzunguka wanakushawishi kuwa Rais umeachia mno. Wanakwambia tumia nguvu kidogo hata ikibiti watu kadhaa kufariki haina madhara. Najua wapo ulio karibu nao wanaoona uhuru ulioutoa unaelekea kuiondoa CCM madarakani na wenyewe hawapendi.

Kikwete usiyapuuze mauaji haya yanayotokea Arusha, Mwanza, Mbeya, Morogoro na sasa Iringa ambapo maisha ya mwanahabari mwenzetu, Daud Mwangosi ametumbuliwa tumbo kwa bomu la machozi. Binafsi sikubaliani na kauli inayopenyezwa kwenye masikio ya Watanzania kuwa damu inayomwagika ni mbegu itakayoota.

CCM msitumie risasi kubaki madarakani. Wapinzania pia msiwazoeshe Watanzania kuuana, kwa maelezo kuwa harakati za ukombozi lazima kumwaga damu. Mchezo huu tunaouanzisha ni mauti yetu. Rais wa Tunisia Ben Ali, aliondolewa madarakani kutokana na mauaji ya kijana mmoja. Wananchi waliingia mitaani, wakaandamana polisi wakaua hadi wakachoka na matokeo yake serikali yake ikaondoka kwa aibu.

Sitanii, wanasiasa wetu nawasihi mshindanishe sera si ubabe. Ndugu yangu Dk. Wilbrod Slaa ukishikilia sera yako ya kushusha bei ya mabati, saruji na kutoa elimu bure hii inatosha kushawishi wananchi. Epuka kauli zisizo za lazima za kuhamasisha watu kuwa tayari kufa. Tufanye siasa za kistaarabu. CCM nanyi mkiambiwa Sera ya Elimu ya Juu imewashinda, msiwe wababe.

Kubalini kuwa uwezo wenu wa kufikiri umefikia kikomo. Siasa zichukulieni kama mchezo wa mbio. Hivi ukiwa kwenye riadha ya kupokezana vijiti ukichoka si unamkabidhi mwenzio kijiti anaendeleza kasi na timu yenu inashinda? Kama ni mbio ndefu tumeshuhudia kwenye Olimpiki wengi wakiona maji yamezidi unga wanatembea na kuwaacha wenye nguvu wakimbie. Kwani ni lazima CCM?

Tunachotafuta ni maisha bora si visasi wala migogoro. Uongozi wa kujilinda na bunduki, kamwe hauwezi kuwa na mamlaka ya wananchi. Leo tunaua waandamanaji badala ya kuwalinda, kesho tutaua wasaidizi wetu kwa kuwatuhumu kuwa hawafanyi kazi ya kudhibiti wimbi la wapinzani wetu vizuri. Hii ni kanuni ya msingi tu.

Katika hili nasema Kikwete funga breki. Wambie polisi wako damu waliyomwaga inatosha. Rejea ulipokuwa wakati unachukua nchi hii. Polisi wako wamerudi ulikowatoa. Juzi tumewasikia majambazi wameiba benki ya CBA mambo tuliyoanza kuyasahau katika nchi yetu. Polisi wametuhumiwa kushirikiana na wezi bandarini kuiba shaba, mambo tuliyokwishayasahau yamerejea. Ebu waonye polisi wako. Nchi zote zilizopata matatizo duniani, mengi yalitokana na kuwachekea polisi. Chukua hatua.

 

1023 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!