BandariBandari ya Dar es Salaam inapoteza wastani wa Sh bilioni 200 kwa mwaka kutokana na mtandao wa wizi ‘unaouza kazi’ na vyanzo vya mapato kwa wafanyabiashara binafsi.

Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI unaonyesha nyaraka mbalimbali zilizopelekwa kwa wakubwa zimeorodhesha majina, mtandao wa wizi unavyofanyika na hasara inayopatikana ambapo kwa mwaka 2015 pekee Bandari ilipoteza wastani wa dola milioni 90, zinazokisiwa kuwa Sh bilioni 200.

Kilichobainika ni kuwa tangu mwaka 2008 Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) walianza kuhudumia makontena kwa ushindani na kampuni ya Tanzania International Container Terminal Services (TICTS). Baada ya mwaka huo ndipo mambo yalipoanza kwenda kombo kwa Bandari.

Ukiacha ukweli kwamba TICTS iliyobinafishishiwa gati Na 8, 9, 10 na 11, ambazo zimejengwa mahususi kwa ajili ya makontena na zina vifaa vya kushusha na kupakia makontena, hata mzigo kidogo uliostahili kuja Bandari ulianza kupata shida.

Ushindani huo uliifanya Bandari ya Dar es Salaam kubaki na gati Na. 7 tu lenye uwezo wa kuhudumia meli kubwa za mizigo, hali iliyoipunguzia uwezo wa Bandari. TICTS wenye mkataba wa miaka 25 kuanzia mwaka 2000, ikiwa sasa mkataba wao bado una uhai wa miaka 9, sasa wanafanya kazi za Bandari kwa asilimia 75.

Ukiacha ushindani kutoka TICTS kutokana na msongamamo, mwaka 2008 TPA iliruhusu utaratibu wa Bandari Kavu (ICDs) ambao nao sasa umegeuka mrija wa kunyonya mapato ya Bandari.

“TPA na baadhi ya wamiliki wa Bandari Kavu waliingia mikataba. Kati ya makubaliano waliyokubaliana kwenye mikataba hiyo, ni pamoja na kwamba TPA watapeleka kontena/magari kwenye ICD endapo Bandari itakuwa imejaa mizigo.

“Mfano, TPA ikiwa ina shehena ya kontena 8,500 (import) kwa wakati mmoja, basi ziada ya hizo kontena 8,500 zihamishiwe kwenye Bandari Kavu, lakini kinyume na mikataba waliyoingia wanapeleka kontena kwenye ICD wakati Bandari ina nafasi ya kutosha kuhifadhi kontena/magari husika,” inasema sehemu ya waraka mzito uliokabidhiwa serikalini.

Waraka huo unaonyesha kuwa viongozi wa Bandari wanachofanya wanaelewana na wamiliki wa ICD, kisha mizigo yote inatolewa bandarini na kupelekwa kwenye ICD moja kwa moja, kisha wanalipwa kamisheni, huku Bandari ikipoteza mapato kwa kukosa tozo mbalimbali.

Takwimu zinatisha. Mfano kwa mwaka 2011, takwimu zinaonyesha kuwa Bandari ya Dar es Salaam ilihudumia kontena 468,939,000, ila kati ya hizo TICTS walihudumia kotena 346,884 (sawa na asilimia 74), huku TPA ikihudumia kontena 122,055 (sawa na asilimia 26).

Kipindi cha Juni 2015 hadi Mei 2016, Bandari ya Dar es Salaam ilihudumia jumla ya konteana (import) 187,815. Kati ya kontena hizo, TICTS ilihudumia kotena 148,227 na TPA ikahudumia kontena 39,588. Ripoti hiyo inahoji kwa nini kontena za TPA ndizo zinashuka kwa kasi, hata kama kuna tatizo la mzigo kupungua bandarini.

Ingawa maafisa wa Bandari wanajenga hoja kuwa gati wanazomiliki wao hazina kina kirefu na nyingine zinahitaji kuondolewa tope kwa nia ya kuruhusu meli kubwa kutia nanga, ripoti hiyo inahoji inakuwaje TICTS yenye mashine (crane) 4 na eneo dogo inaweza kuhudumia kontena nyingi ikilinganishwa na TPA yenye crane 8 (Gattward) na eneo kubwa la kuhifadhia makontena?

Kati ya mwaka 2011/2012 Bandari ya Dar es Salaam ilikuwa na uwezo wa kuhudumia kontena (import) 6,248 kwa wakati mmoja na baadaye mwaka 2004 wakavunja Shed Na. 2, 3 na 4 hali iliyoongeza uwezo wa kuhifadhi kontena na kufikia 8,500 ingawa wanadai kuwa eneo lililoongezeka bado halijarekebishwa kujengwa kwa ajili ya kuhimili uzito wa kuhifadhi kontena tano kwenda juu.

“Inashangaza kuona TPA inapokea wastani wa meli moja kwa wiki yenye wastani wa kontena 600 (import) lakini zaidi ya nusu ya idadi ya kontena au wakati mwingine kuontena zote zinazosushwa kutoka melini kwa wiki nzima zinapelekwa kwenye Bandari Kavu (ICDs) za watu binafsi, huku Bandari ikiwa na nafasi ya kutosha kuhudumia zaidi ya kontena 8,500,” inasema sehemu ya waraka huo nyeti.

Ingawa sera ya kupeleka kontena za mizigo ya ndani kwenye ICDs ilipitishwa kwa nia ya kupunguza msongamano bandarini, kwa nia ya kuhakikisha Bandari haikosi mapato yatokanayo na tozo mbalimbali, kanuni inataka mizigo ya kupelekwa kwenye ICD ipelekwe baada ya nafasi kujaa bandarini, ila sasa inafanyika kinyume na inalalamikiwa na wateja kuwa inaongeza gharama.

“Mizigo yote ya local inapelekwa kwenye ICD kama sera inavyotaka, na mizigo ya transit kwa maana ya kimataifa inabakizwa bandarini, hivyo si kweli kwamba tunahamishia mizigo kwenye ICDs kuwaongezea gharama wenye mizigo,” anasema mmoja wa maafisa.

Taarifa za uhakika zinaonyesha kuwa akiwa Waziri wa Uchukuzi, Mzee Samuel Sitta alipiga marufuku magari na kontena kupelekwa kwenye ICD kabla eneo la Bandari halijajaa, lakini alipoondoka tu wizarani utaratibu ukarejea kama kawaida.

“TPA ilikuwa inahudumia shipping line zaidi ya saba. Leo tunavyozungumza imebaki na shipping line moja ya PIL. Hii inatokana na njama za viongozi kulihujumu shirika kwa kuelewana na watu wa ICDs na wafanyabiashara binafsi mzigo wote unasukumiwa huko, na meli zenye mzigo ‘zinauzwa’ kwa washindani, hivyo Bandari inakosa mapato kabisa,” anasema mtoa habari wetu.

 Hata hivyo, maisha ya kuponda mali na kuinyofoa Bandari ya Dar es Salaam nchini yanaelekea ukingoni baada ya kuteuliwa Mkurugenzi Mkuu wa Bandari mpya, Injinia Deusdedit Kakoko.

“Wiki hii [wiki iliyopita] mzigo wote ulioshushwa na meli umebaki hapa hapa Bandari. Kama tutaendelea hivi, ICDs nyingi zitafungwa. Nenda Bandari ulione leo, magari yamepangwa hadi kwenye kingo za bahari. Wateja wanapunguziwa gharama na Bandari inapata fedha halali. Kiasi kinachozidi, ndicho kiende ICD kwa mujibu wa sheria lakini si uhuni uliokuwa unafanyika,” anasema.

 

Kakoko aanza kufyeka posho

Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI, umebainisha kuwa Injinia Kakoko ameanza kutumbua majipu moja kwa moja bila kusubiri baada ya kufika na kukuta mambo yanaenda kwa kudra za mwenyezi Mungu katika Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA).

“Siku walipokuwa wanatambulisha Bodi ya Wakurugenzi, Injini Kakoko akapelekewa ombi la kuidhinisha Sh milioni 73 ikiwa ni posho ya kikao kwa wafanyakazi 3,700 walioshiriki hicho kikao. Kila mfanyakazi anapaswa kulipwa Sh 20,000 kwa kikao.

“Lakini wala hiyo isingekuwa shida kubwa. Wakati kikao kinaendelea, Injinia Kakoko akaambiwa hiki kikao kikipitiliza hata dakika moja baada ya saa 9:30, basi kitahesabiwa kama vikao viwili na itabidi wafanyakazi walipwe mara mbili… hii ilimshitua sana Injinia Kakoko.

“Alihoji kwa nini wafanyazi walipwe kufanya kikao na menejimenti, wakasema ndiyo utaratibu ulivyo. Akahoji utaratibu huo ulipitishwa kwa maandishi yapi, na hasa hili la kikao kimoja kulipwa mara mbili hakuna aliyejibu.

“Alichosema ni kwamba vikao ni sehemu ya kazi alizoajiriwa mfanyakazi kufanya. Amesema chini ya uongozi wake atafuta hizo posho. Ameongeza kuwa hata viongozi wa chama cha wafanyakazi kila wanapokutana wanalipana Sh 200,000 hivyo atafanya utaratibu kufuta malipo haya kwani vikao ni sehemu ya kazi,” anasema mtoa habari wetu.

JAMHURI lilipomtafuta Injinia Kakoko, amesema kwa ufupi tu; “Kuna mambo hatuwezi kuruhusu yaendelee. Nia yetu ni njema kuboresha utendaji bandarini.” Suala la nia ya kukata posho za vikao, nalo amesema; “aliyekwambia hakukudanganya.”

Watu walio karibu na Injinia Kakoko wamesema amezamilia kusafisha uozo katika Bandari zote nchini kwa kufuta ajira za upendeleo, kuwajibisha wafanyakazi wala rushwa, kuhamasisha kila mfanyakazi kuchapa kazi na kuiwezesha Bandari ya Dar es Salaam kuwa namba moja katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Jangwa la Sahara.

“Tangu ateuliwe anafanya kazi hadi Jumapili. Hana mapumziko. Nilimsikia anamwambia mtu mkubwa tu, kuwa kuanzia sasa chini ya uongozi wake kila kitu kitakwenda kwa mujibu wa sheria. Iwe ni ajira, malipo ya wafanyakazi, mizigo ya wateja, tozo mbalimbali kitakachotawala ni uwazi,” kinasema chanzo chetu.

Juni 25, 2016 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa alimteua Mhandisi Deusdedit Conatus Vitalis Kakoko kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania. Kabla ya uteuzi huo, Kakoko alikuwa Meneja Miradi wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS).

Kakoko alitajwa kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Ephraim Mgawe, ambaye kwa sasa yuko mahakamani Kisutu akishitakiwa kwa matumizi mabaya ya madaraka. Kabla ya Kakoko, Mhandisi Madeni Kipande anayetajwa kuwa naye huenda akafikishwa mahakamani wakati wowote kuanzia sasa, aliteuliwa na Dk. Harrison Mwakyembe kuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bandari, lakini kwa bahati mbaya alizalisha vurugu kubwa katika uongozi wake hadi Waziri Samuel Sitta akamuondoa baada ya kumuundia Kamati ya uchunguzi.

Baada ya Kipande kuondoka, Awadh Masawe aliteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Bandari, lakini naye hivi karibuni uteuzi wake umetenguliwa kutokana na kashfa ya upotevu wa makontena, ambayo wakati yanapotea Masawe alikuwa Meneja wa Bandari ya Dar es Salaam, ambayo ilinyang’anywa mamlaka yote na Kipande kazi zake zikahamishiwa Makao Makuu ya TPA, hadi makontena kupotea.

Masawe naye baada ya kuondolewa, aliteuliwa Injinia Aloyce Matei kukaimu nafasi hiyo ambaye sasa amekabidhi mikoba kwa Injinia Kakoko.

 

Vibarua hewa washuka hadi 28

Tangu Machi, mwaka huu Gazeti la JAMHURI limechapisha habari za kuwapo mchezo wa vibarua hewa katika Bandari ya Dar es salaam. Uchunguzi wa gazeti hili umeonyesha kuwa kwa mwezi wakubwa ndani ya Bandari ya Dar es Salaam kupitia kampuni waliyo na vinasaba nayo ya Hai Sub Supplier wamekuwa wakiingiza vibarua hewa hadi 2500 na hivyo kupokea malipo hayo.

Baada ya kuchapisha habari hizi, Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa aliamua kulifanyia uchunguzi suala hili. Mkurugenzi Mkuu Injini Kakoko naye alipoingia akaagiza vibarua waingie kazini kulingana na kazi zilizopo, ndipo ikatokea aibu ya mwaka.

“Wiki ya kwanza ya Julai, Bandari imeingiza vibarua 28 tu kila siku, wakati ilikuwa kila siku orodha inaonyesha wanaingia vibarua 200. Injinia Kakoko tumeanza kuona matunda yake na tunaunga mkono hili analolifanya. Ataiokoa Bandari ya Dar es Salaam ambayo ni moyo wa uchumi wa Mamlaka yote.

“Kampuni ya (jina linahifadhiwa) imelipwa zaidi ya Sh bilioni 9.6 kwa vibarua hewa kwa mwaka 2015/2016. Hili ndilo linawafanya viongozi wa Bandari kutumia fedha za umma kutetea kampuni binafsi mahakamani kuwa ipewe zabuni. Kampuni ya Hai Sub Suppliers inapewa kila kazi ndani ya Bandari pamoja na Mahakama kuikataa kuwa haina sifa,” kinasema chanzo chetu.

Mgogoro mkubwa unafukuta bandarini hapo, kutokana na zabuni AE/016/2012/DSM/NC/01B ya kutoa huduma za kupakua na kupakia mizigo bandarini, iliyotangazwa mwaka 2013 ikatolewa kwa mizengwe kwa kampuni ambayo viongozi wa Bandari wana vinasaba nayo.

Kibaya zaidi, tangu Machi 1, 2016 kampuni hiyo inayolalamikiwa, ya Hai Sub Suppliers na nyingine kama Portable Enterprises na Freight Meridian, zimeendelea kufanya kazi kwa mikatabaya miezi miwili miwili inayotolewa kwa njia ya nyongeza.

Zabuni inayosumbua vichwa ilitangazwa kwa nia ya kupata mrithi wa kampuni hizo ifikapo mwaka 2014, mwaka uliolengwa kuwa kampuni hizo zingekuwa zimemaliza mkataba kwa mujibu wa sheria.

Hata hivyo, kutokana na mvutano wa kisheria, hadi sasa zabuni hiyo haijatolewa kwa kampuni yoyote, baada ya nia ya kuipa Hai Sub Suppliers kuzimwa, hali iliyoulazimu uongozi wa Bandari ya Dar es Salaam kuziongezea muda wa kati ya mwezi mmoja na mitatu hadi atakapopatikana mzabuni mwingine.

Afisa Mwandamizi wa Bandari, ameiambia JAMHURI kuwa kitendo kinachofanywa na Bandari kutumia kampuni yao waliyotumia ujanja wa kumtanguliza mfanyakazi wa chini aonekane ndiye mwenye kampuni (bila kujali mgongano wa maslahi), ni cha hatari.

“Kaka nakwambia hii kitu ni hatari mno. Kampuni hii ya Hai Sub Suppliers imeendelea kupewa kila kazi ya Bandari ya Dar es Salaam, hali inayotishia hata usalama wa Bandari.

“Kampuni hii sasa imehodhi asimilia 90 ya kazi zote, na hofu yangu ni kuwa ikitokea siku kampuni hii ikaamua kugoma, Bandari ya Dar es Salaam itasimamisha shughuli zote.

“Kwa kiwango cha kazi ilizopata kampuni hii nisiyojua inapata wapi nguvu, inaweza kufika mahala ikahujumu Bandari au ikaigeuza Bandari kuwa mateka wake. Uamuzi huu wanaofanya mameneja wa Bandari ya Dar es Salaam ni wa hatari kweli, ni lazima Serikali iingilie kati na kuvunja mtandao huu, kazi zigawanywe kwa kampuni tatu hadi tano, kwa nia ya kuongeza ushindani na kulinda usalama wa Bandari,” amesema afisa huyo kwa uchungu.

Kampuni hii inayopokea kati ya Sh milioni 300 na 400 kwa mwezi kutoka Bandari, malipo yake yalianza kuongezeka baada ya Bandari kupata Kaimu Mkurugenzi, Hebel Mhanga. Mhanga alianza kukaimu kazi hiyo Desemba, 2013 na ilipofika Mei, 2015 inaelezwa alianza kuzinyang’anya kazi kampuni nyingine na kuzirundika kwa Kampuni ya Hai Sub Suppliers, iliyotajwa na Mahakama kuwa haina sifa ya kufanya kazi za Bandari.

“Serikali ikaingie kwa wahasibu ione invoice na kiasi kinacholipwa kwa Hai Sub Suppliers ione malipo yalivyoanza kuongezeka tangu Mei, 2015. Kampuni hii ina uhusiano wa moja kwa moja na baadhi ya mameneja wa Bandari wachunguzwe,” anasema mtoa habari wetu.

Uchunguzi wa JAMHURI, unaonesha kuwa Kampuni ya Hai Sub Suppliers kwa sasa imepewa kazi katika gati 7 kati ya 8, imepewa kazi za maghala 7 kati ya 8, imepewa kazi ya usafi wa ofisi, usafi wa jumla, kushusha na kupakia malori na mabehewa.

Kampuni ya Portable Enterprise Limited imepewa kazi moja kwenye gati Na 8 na Kampuni ya Freight Meridian imepewa kazi moja tu katika ghala Na 8. Mkataba wa awali wa Hai Sub Suppliers ulikuwa wa kupakua na kupakia meli za magari.

Katika hali isiyoelezeka, kampuni hii ilipata mkataba mnono wa kufanya kazi na taasisi kubwa kama Bandari bila kuwa na sifa stahiki. Tangu mwaka 2012 ilipopewa mkataba wa kwanza, Hai Sub Suppliers kumbukumbu zinaonesha haikuwa na Namba ya Mlipa Kodi (TIN) badala yake ilikuwa inatumia Na 102-303-229, ambayo ni namba ya mtu binafsi anayejulikana kwa jina la Hidaya Ibrahim Amri.

Hapana shaka kadri muda ulivyokwenda walipata ushauri wa kisheria na hasa masuala ya kodi yasiyoelezeka kama kampuni hii ilikuwa inalipa kodi kwa njia ipi, ilipofika Mei 22, 2015 ikiwa imekwishafanya kazi miaka zaidi ya mitano na Bandari, ndipo kampuni hii iliposajiliwa Brela na kisha Mei 25, 2015 ilipata TIN namba 127-110-069, kisha ikaomba ipewe zabuni kubwa zaidi na ikapigiwa chapuo na uongozi wa Bandari ya Dar es Salaam kuwa ndiye mshindi.

Januari 19, mwaka huu Mamlaka ya Rufaa ya Zabuni za Umma (PPAA), ilitoa hukumu juu ya kesi iliyofunguliwa na kampuni – Nagla General Services Limited, Portable Enterprises Limited na Carnival Investment Limited wakipinga upendeleo unaovunja sheria kwa kuipatia zabuni Hai Sub Suppliers bila kuwa na sifa.

Katika hukumu hiyo, iliieleza Bandari ya Dar es Salaam kusitisha utoaji wa zabuni kwa kampuni ya Hai Sub Suppliers Limited, kwani haikuwa na uzoefu wa miaka miwili unaotakiwa kisheria. Uongozi wa Bandari ya Dar es Salaam unajenga hoja kuwa Hai Sub Suppliers ni taasisi ile ile kwani ilichofanya ni kujiondoa katika kufanya biashara na Bandari kama mtu binafsi (sole proprietor) na kugeuka kampuni ilipofika mwaka 2015.

JAMHURI limezungumza na mfanyakazi wa Bandari, ambaye ni mmoja wa wamiliki wa kampuni ya Hai Sub Supplier, Yusufu Ibrahim, ambaye anamiliki asilimia 50 ya kampuni hiyo yenye zabuni ya kufanya kazi katika Bandari ya Dar es Salaam, aliyesema: “Ni kweli nilikuwa namiliki kampuni hii, lakini nimefilisika.”

Alipoulizwa ni lini amefilisika na ni lini ameacha kumiliki kampuni hii, akasema: “Sikusikii.” Akakata simu. JAMHURI lilimpigia simu mara mbili tena, akawa anapokea na kuiacha simu hewani bila kuzungumza.

JAMHURI limepata nakala za malalamiko ya wazabuni waliomwomba Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, na Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, kuingilia mgogoro huu unaotishia amani kwani vibarua kutoka kampuni nyingine wanajipanga kugoma kutokana na wale wa kampuni ya Hai Sub Suppliers kupata kazi kila siku, huku wengine wakipiga miayo.

Kaimu Meneja wa Bandari, Mhanga, alipoulizwa juu ya tuhuma hizo kuwa yeye ni mmiliki wa kampuni ya Hai Sub Suppliers kwa mgongo wa mfanyakazi wa kada ya chini wa Bandari, alisema yeye hahusiki na kampuni hiyo anasingiziwa.

“Mimi napenda nikuhakikishie kwamba kwa kitu ambacho nimekifanya, kama nilikifanya juzi, kweli nitaendelea kukwambia kwamba ni kweli ni mimi niliyekifanya, kwa sababu naamini kwamba wakati nakifanya, nilikuwa na nia gani. Hata kama mazingira yamebadilika, lakini nitakwambia kwamba hiki wakati nakifanya, mazingira yalikuwa moja, mbili, tatu…

“Mimi si mtu wa kutafuta makampuni ya kufanya biashara bandarini. Mimi mtazamo wangu wa maisha siyo mtu wa kutafuta utajiri. Mimi ni mtu ambaye nafikiria kutumikia nchi, nimefanya kitu gani ambacho nitakapokuwa nimeondoka kitakuwa kinatazamwa kwamba kile pale kilisimamiwa na Mhanga.

“Lakini maisha yangu nataka kuishi maisha ya kawaida kabisa ya Mtanzania, maisha ya watoto wangu waende shule, waishi maisha mazuri, siyo niwe na mali ya kujilimbikizia. Mimi nitafika mahala nitakufa tu,” amesema Mhanga.

Suala la Hai Sub Suppliers kufanya shughuli karibu zote za Bandari, amesema hata yeye kwa ajili ya usalama wa Bandari linamtia hofu, na alipoulizwa wanazipataje, akasema: “Kwa mujibu wa sheria na taratibu za zabuni.”

Ameishutumu Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2011 inayowapa nafasi wazabuni wanaoshindwa kulalamika, akisema imezaa mvutano usio na ukomo kwa maana waliokosa zabuni hawakubali kushindwa.

Mhanga alipoulizwa kama Hai Sub Suppliers walishinda kihalali, kwa nini PPAA imeamuru wasipewe zabuni? Alisita kidogo kisha akasema, kinachopiganiwa ni maslahi binafsi ya hizo kampuni kwani Hai Sub Suppliers wamekuwa wakifanya nayo kazi tangu mwaka 2012, hivyo anashangaa kuona hawaitambui iliposajiliwa rasmi mwaka 2015.

“Kimsingi hata vibarua ni wale wale, hivyo iwe hiyo Hai Sub au nyingine, wanachopigania ni maslahi binafsi tu,” amesema.

Amezishutumu kampuni shindani katika zabuni hiyo kuwa mkurugenzi mmoja amekuwa anaingiza zaidi ya kampuni tatu kwenye zabuni moja, hivyo inaposhinda yoyote kati ya zinazoteuliwa, basi anabaki mtu yuleyule, lakini akasema yeye si msemaji wa Hai Sub Suppliers watafutwe wenyewe.

Kuhusu suala la hatima ya zabuni hiyo inayopigwa danadana tangu mwaka 2013, Mhanga amesema wao mara zote wanaomba ushauri wa PPRA na wamefanya hivyo katika hili, hivyo ikibidi kuitisha upya zabuni au kuwapa wazabuni waliokuwa na sifa wanaofuata baada ya Hai Sub Suppliers kutamkwa na Mahakama kuwa haina sifa, atafuata ushauri wa PPRA. Hata hivyo, Bandari imefungua kesi Mahakama Kuu kupinga hukumu ya PPAA wakitaka Hai Sub Suppliers ndiyo ipewe zabuni hiyo.

 

Wasafiri nje ya nchi bila kibali

 Katika hatua ya kushangaza, wafanyakazi wawili wa Mamlaka ya Bandari ambao ni Wajumbe wa Kamati Tendaji ya Chama cha Netiboli Tanzania (CHANETA), Hilder Mwakatobe na Judith Ilunda, wamesafiri nje ya nchi bila kibali cha Ikulu.

Awali, Baraza la Michezo la Taifa (BMT) liliandika barua TPA kuomba wajumbe hao wapewe ruhusa ya kushiriki mashindano ya Afrika Mashariki nchini Uganda kuanzia Aprili 2 – 9, 2016 na kwamba Bandari iwalipie gharama.

Barua ya kuwaombea ruhusa ya Machi 22, 2016 yenye Kumb. Na. BMT/C.4/32/Vol.2/11 ilisema BMT ingependa wajumbe hao washiriki. Mkurugenzi wa Rasilimali Watu wa Bandari, Erasmo Mbilinyi alijibu baraua hiyo kwa kuwakubalia kushiriki kwa barua yenye Kumb. Na. HR/5/13 ya Machi 30, 2016 akimwambia Katibu wa BMT kuwa Bandari ingewalipa fedha za kujikimu kwa siku 10.

Hata hivyo, baada ya dokezo sawili la aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu, Aloyce Matei katika barua yenye Kumb. Na. HA.29/373/05/B ya Aprili 1, 2016 alipohoji fomu za ruhusa ya kusafiri nje ya nchi ziko wapi, ndipo Mbilinyi mbiombio aliagiza Hilder na Judith wasipewe malipo hayo.

Katika kinachoonyesha mkanganyiko, Mbilinyi alimwandikia Kaimu Mkurugenzi wa Fedha, Machi 31, 2016 (siku moja kabla ya Matei kuhoji) baada ya kuona mambo yameharibika kupitia memo Na TPA 0555, iliyosema: “Safari ya Michezo ya Viongozi wa Chama cha Netiboli. Pamoja na idhini iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu na hatua ya malipo ilipofikia, na baada ya kufanya “consultations” nimejiridhisha kuwa ili safari iweze kufanyika ni lazima wafanyakazi hawa wapate kibali cha Ikulu. Hivyo, naomba usitole hundi ya malipo ya safari hadi hapo kibali kitakapopatikana.”

Hata hivyo, Mbilinyi alifunga zizi wakati ng’ombe wameishatoka. Hilder na Judith, kwa kuwa tayari walikuwa na tiketi mkononi, walisafiri kwenda Uganda bila kibali. Taarifa za ndani zinaonyesha kuwa malipo yao ya kujikimu yaliyokuwa yanakaribia Sh milioni 10 kila mmoja, yalisitishwa na hadi leo wanaendelea kuhojiwa kwa kusafiri nje ya nchi bila kibali.

 

 Viongozi wa wafanyakazi ‘wahongwa’

Katika hali isiyo ya kawaida, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu, Erasmo Mbilinyi ameanzisha utaratibu wa kuwapa ziara zinazotia shaka viongozi wa chama cha wafanyakazi DOWUTA.

Ziara hizo anazoziita za mafunzo kwa wafanyakazi hao, zinatajwa kuwa hazina tija ambapo wanapangiwa kusafiri kutembelea bandari zote nchini kwa siku kati ya 40 na 45.

Mei 19, 2016 alimpangia Mwajuma Issa siku 41 atembelee Bandari zote nchini. Mwajuma ni Afisa Mwandamizi Rasilimali Watu. Alipaswa kusafiri kwenda Mwanza, Kigoma, Dar es Salaam, Kyela, Bagamoyo, Tanga na Mtwara.

Maajambu makubwa ni aina ya usafiri waliotengewa. Hata Dar es Salaam – Bagamoyo, Mwajuma amepangiwa usafiri wa ndege. Mwajuma hakuwa peke yake katika safari hii, bali alikuwa na Mkutubi Mwanamizi, Adelaide Komba. Ziara ya wawili hao, I lianzia Mwanza Mei 22 na kuhitimishwa Mtwara – Dar es Salaam Julai, Mosi, 2016.

Viongozi wengine wa DOWUTA walioonja ‘ukarimu’ wa Mbilinyi ni pamoja na Katibu wa DOWUTA, Abrahm Lukumai na Mwenyekiti wake, Ovacatus Komba, ambao nao wamepewa siku 40 za ‘kutembelea’ Bandari wakalipwa posho nono.

Hatua hii imelalamikiwa na wafanyakazi ndani ya Bandari wakisema wenzao wanaopewa ziara hizi ni wazi wataacha kutetea masilahi yao na kuanza kushirikiana na uongozi wa juu kuwakandamizi kama ilivyofanyika kwa Edmund Njowoka, aliyeteuliwa kwenye Bodi ya Wakurugenzi na Madeni Kipande akaanza kuzungumza lugha ya menejimenti badala ya kutetea haki za wafanyakazi. Juhudi za kumpata Mbilinyi na wanufaika wa safari hizo hazikuzaa matunda.

2124 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!