*Uongozi wa Bunge wahofia Pinda atajiuzulu

*Wakubwa wavuta milioni 100 hadi bilioni 8

*Jaji Werema, Tibaijuka wapumulia mashine

*Wafadhili wasitisha tirioni 1 hadi kieleweke

 

Serikali ya Awamu ya Nne chini ya uongozi wa Rais Jakaya Kikwete, kwa mara nyingine imekutana na mtihani mgumu ambako Waziri Mkuu wake, Mizengo Pinda yupo chini ya shinikizo la kujiuzulu kutokana na malipo ya karibu Sh bilioni 400 kwa Kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL).

Shinikizo la Pinda kujiuzulu limetokana na msukumo mkubwa wa wafadhili kutoka nchi zilizoendelea ambao wamesitisha msaada  wa Sh trilioni 1; hali iliyoifanya miradi ya maendeleo kukosa fedha na kuifanya Serikali iwe katika wakati ngumu.

Wachambuzi wa mambo, wameitafsiri safari ya Rais Kikwete kwenda Marekani kufanyiwa uchunguzi wa afya yake ni zaidi ya kufanya hivyo kwani shinikizo la kutikiswa Serikali yake huenda ikawa ni sababu ya ziada.

Taarifa ya Ikulu kwa vyombo vya habari iliyotolewa Ijumaa iliyopita, inasema kuwa Rais Kikwete aliondoka Jumatano ya wiki jana na kwamba kulingana na ratiba ya uchunguzi wa afya yake anatarajiwa kurejea nchini Alhamisi ya wiki hii.

Katika hali ya ‘zima moto’, baada ya nchi wafadhili kusitisha misaada karibu miezi miwili iliyopita, Serikali imelazimika kubadili matumzi yake na kuchukua fedha za matumizi ya kawaida ikaziingiza katika matumizi ya maendeleo kwa nia ya kutuliza hasira kwa makandarasi hasa wanaojenga barabara.

Uchunguzi unaonesha kuwa hatua ya kuhamisha fedha za matumizi ya kawaida kwenda kwenye matumizi ya maendeleo kumeikosesha Serikali uwezo wa kulipa mishahara kwa wabunge na watendaji wengine wa Serikali, hivyo kuilazimu Serikali kutembeza bakuli na kuomba mikopo ya kibiashara benki kwa ajili ya kulipa mishahara.

Benki ya Makabwela (NMB) ndio imenusuru hali, kwa kutoa mishahara na posho za wabunge mwezi uliopita, lakini kuna kila dalili kuwa ingawa Serikali imebana; wakati umefika ambapo lazima itaachia. Wafadhili wanasema hawataachia fedha hadi matokeo ya uchunguzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) itakapotoka.

Wakati hayo yakitokea, taarifa za uhakika zinaonesha bayana kuwa Waziri Mkuu Pinda analo chaguo la, ama kuwatosa watendaji na mawaziri wenzake ili Serikali inusurike kuvunjika; au kufanya uamuzi mgumu kama alivyofanya Edward Lowassa mwaka 2008 kwa kujiuzulu, Baraza la Mawaziri livunjike siku ya Novemba 28, mwaka huu wakati hoja hii itakapojadiliwa bungeni.

 

Mgao wa fedha

Baada ya fedha kutolewa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwenye akaunti ya Tegeta Escrow, inaelezwa kuwa watendaji na watumishi mbalimbali wamemegewa donge nono linaloanzia dola 40,000 (Sh milioni 100) hadi dola milioni 5 (Sh bilioni 8). Wengi wa waliopokea fedha hizi wanatajwa kuwa walisaidia mchakato wa upatikanaji wake.

JAMHURI limeiona orodha ya watuhumiwa waliopewa mgao, ambako viongozi wengi wameingiziwa fedha kutoka benki. Fedha alizoingiziwa kwenye kaunti yake, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka kiasi cha dola milioni 1.4 karibu Sh bilioni 2.38 kutoka kampuni ya VIP huenda zikagharimu uwaziri wake.

Ingawa Tibaijuka mwenyewe amekanusha mara kadhaa akisema kuwa fedha hizo alipewa na ‘kaka yake’ James Rugemalira, ambaye ni Mkurugenzi wa VIP Engineering- kampuni iliyokuwa na ubia na IPTL, akisema amempatia kama ndugu yake wa damu kwa nia ya kuendeleza shule yake, sasa zimetafsiriwa kama rushwa.

Vyanzo vya habari vinaeleza kuwa Profesa Tibaijuka ana kibarua kigumu kufafanua mbele ya wabunge hata waweze kumwelewa imekuwaje anagawiwe wastani wa Sh bilioni 2.38 hivi hivi.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema, anayetajwa kuwa naye amemegewa pande kubwa la fedha hizi, ameliambia JAMHURI kuwa anasikitika kusikia habari hizo alizodai kwamba hazina chembe ya ukweli.

“Unayaamini haya kuwa yana ukweli wowote? Ikiwa unayaamini, niombee, ninayo safari ndefu kuondoka katika umaskini, kama huyaamini sikitika kama ninavyosikitika mimi,” ameliambia JAMHURI.

Ameongeza kuwa mara zote masuala ya kisheria anataka yapelekwe mahakamani kwa yeyote mwenye malalamiko, ila hafurahishwi na mwenendo wa watu kutumia Bunge kusambaza uongo.

Pamoja na kauli hii ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, inaelezwa kuwa yeye na Profesa Tibaijuka ‘wanapumulia mashine’ kutokana na ripoti ilivyoandikwa.

“Ripoti hii inaweza kuumiza hadi watendaji wakuu wa Serikali wasiopungua saba, ila hata ikiwa vipi, kuna wawili hawaponi,” kimesema chanzo chetu.

Inaelezwa kuwa wengi waliopokea mgao huu, ni vigogo wazito serikalini, hivyo uongozi wa Kamati ya Bunge umeona ni vyema uiweke ajenda hii mwisho wa Bunge la 16 na 17 kuepusha kiama iwapo Serikali italazimika kuvunjika.

Kutokana na wafadhili kusitisha misaada inaelezwa kuwa ndani ya siku 10 kuazia Jumatano ya wiki iliyopita, hospitali nyingi nchini zitakuwa hazina dawa na hivyo wagonjwa wengi wapo katika hatari ya kupoteza maisha.

Nchi wafadhili zimesitisha msaada wa kibajeti zikisubiri uchunguzi wa TAKUKURU na CAG. Hatua ya kusitisha misaada hii imeleta shida kubwa katika kipato cha Serikali.

Uchunguzi wa JAMHURI ingawa unaonesha hakuna popote ambako Waziri Mkuu Pinda amepokea fedha, ila kwa nyakati tofauti amepokea barua kutoka idara za Serikali, zikieleza mpango wa kulipa fedha hizo kwa kampuni ya PAP.

Nakala za barua hizi, ambazo JAMHURI imeziona zimesambazwa kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Nishati na Madini, Wizara ya Fedha, Benki Kuu na Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi.

 

Escrow akaunti ilivyofunguliwa

Akaunti ya Tegeta Escrow ilifunguliwa mwaka 2006 baada ya Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO) kudai kuwa IPTL inadai malipo makubwa kuliko uhalisia. Mgogoro huu ulipoanza TANESCO ilifungua kesi katika Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi kwa mujibu wa Mkataba wa IPTL na TANESCO.

Hata hivyo, wakati kesi hiyo inaendelea, mbia wa IPTL; Kampuni ya VIP Engineering alifungua kesi katika Mahakama Kuu ya Tanzania, kesi iliyotolewa hukumu Septemba 5, mwaka jana. Katika kesi hii, Jaji Utamwa aliamuru mali zote za IPTL zikabidhiwe kwa kampuni ya Mechmar iliyokuwa imenunua hisa asilimia 70 za IPTL.

Taarifa zilizopo kwenye ripoti hiyo na kwa mujibu wa Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila; Novemba 15, mwaka jana Kampuni ya Mechmar iliyokuwa inaimiliki IPTL kwa asilimia 70 iliuza hisa zake kwa Kampuni ya Pipelink kwa Sh milioni 6 na kulipa kodi ya Sh 490,000.

“Siku hiyo hiyo ya Novemba 15, siku zilipouzwa hisa za Mechmar kwa Pipelink, Pipelink iliuza hisa hizo hizo kwa Kampuni ya PAP kwa gharama ya Sh milioni 480 na kulipa kodi Sh milioni 46,” anasema Kafulila na kuongeza:

“Chakushangaza na kusikitisha, kampuni hizi mbili ziliuza hisa kabla ya kulipa kodi ya ongezeko la mtaji (capital gains tax). Ilipofika Desemba 6, 2013 Kampuni ya Mechmar na Pipelink zote zililipa kodi ya ongezeko la mtaji katika Benki ya CRDB Tawi la Water Front Dar es Salaam katika kaunta Na. 4 na aliyelipa ni mtu mmoja,” anasema Kafulila.

Anasema hatua ya kodi hii kulipwa na mtu mmoja kwa ajili ya kampuni zote mbili inaashirika uhusiano wa aina yake kati ya kampuni hizi mbili. Anaongeza kuwa malipo haya yalifanyika baada ya TRA Ilala kuwezesha malipo hayo, bila nyaraka za msingi zinazohusiana na tathmini ya kampuni zinazouzwa.

Kafulila ameliambia JAMHURI kuwa malipo haya hata kama yalikuwa yanamilikiwa na IPTL, lakini kwa kuwa yanahusisha kulipa kodi ni wazi kuwa yalikuwa na maslahi kwa Taifa.

Mbunge huyo anasema wakati kampuni hizi zinauziana hisa, kwenye akaunti ya Escrow kulikuwamo Sh bilioni 250 na wameingia mkataba na Serikali kuwa kila mwezi watakuwa wanalipwa Sh bilioni 8 hadi deni hilo liishe.

Utata wa Hukumu ya Mahakama Kuu

Wakati Mahakama Kuu ya Tanzania imetoa hukumu Septemba 5, mwaka jana ikielekeza mali za IPTL zikabidhiwe kwa PAP, Kifungu cha 18 (3) cha Mkataba wa IPTL na TANESCO kinazuia Mahakama Kuu ya Tanzania kuendesha kesi inayohusiana na mkataba huo.

Kifungu hiki kinataka mgogoro wowote unaohusiana na mkataba huu usuluhishwe kwenye Kituo cha Kimataifa cha Kusuluhisha Migogoro nchini Uingereza au Marekani. Pia Hukumu ya Mahakama ya Rufaa chini ya Jaji Mkuu wa wakati huo, Barnabas Samatta mwaka 1999 ilisema bayana kuwa Mahakama ya Tanzania haina uwezo wa kuendesha kesi za IPTL.

Wakati IPTL ilipata hukumu ya kuruhusu mali zake kukabidhiwa kwa PAP, TANESCO iliyokuwa imefungua kesi kwenye Mahakama ya Kimataifa,Februari 12, 2014 ilishinda kesi na ikaamuriwa kuwa ndani ya siku 90 yafanyike marekebisho ya gharama ilizokuwa ikilipa TANESCO kwa IPTL.

Hata hivyo, hukumu hii haijatekelezeka kwa sababu fedha ilikuwa zimekwishachukuliwa kwenye akaunti ya Escrow na hivyo kupitia hesabu ingekuwa ni kupoteza muda.

Serikali kwa kujua kuwa haina pa kutokea, imetumia hoja kuwa haiwezi kufanya tathmini ya gharama halisi kwani ilikuwa imebadili wakili wake na hivyo mawakili wapya wanahitaji muda kusoma mwenendo wa kesi na kuuelewa.

 

Maswi alipinga malipo

Taarifa za uhakika zinaonesha kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi alikataa kuidhinisha malipo haya kwa maelezo kuwa hakuwa na uhakika wa nani mmiliki halisi wa kampuni ya PAP.

Hata hivyo, taarifa zinaeleza kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Werema alimwambia Maswi kuwa kukataa kulipa fedha hizo ambazo kuna amri ya Mahakama inayotaka zilipwe angekuwa anavunja amri ya Mahakama na hivyo angeweza kuadhibiwa.

“Ni kutokana na shinikizo hili, Maswi alilazimika kusaini fedha hizo zitoke BoT na kulipwa kwa PAP, sasa walioidhinisha wakiwamo watumishi waandamizi wa Hazina kuna kila dalili kuwa Bunge litawawajibisha mwezi huu,” kimesema chanzo chetu.

Kwa vyovyote iwavyo, mjadala wa fedha za IPTL utaliweka taifa njia panda mwezi huu na hasa ikitiliwa maanani kuwa wafadhili wamesitisha misaada hadi taarifa sahihi zipatikane.

1251 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!