*Hoja ya Mnyika yawekwa kapuni

Utangulizi

Kituo Kikuu cha Mabasi Ubungo (UBT) kilifunguliwa rasmi Desemba 6, 1999 pamoja na mambo mengine, uanzishwaji wa kituo hiki ulikuwa na madhumuni ya kutoa huduma kwa wasafiri pamoja na watumiaji wengine na pia kuongeza mapato ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.

Katika kipindi cha kati ya mwaka 2004 mpaka 2008 tumeibua tuhuma mbalimbali za ufisadi na upotevu wa mapato katika Kituo hicho zikiwemo zinazohusu Kampuni ya Smart Holdings ya Familia ya Kingunge Ngombare-Mwiru; hata hivyo katika kipindi chote zimekuwa zikikanushwa na Serikali na chama kinachotawala.

Hatimaye Machi 15, 2009 Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliagiza ufanywe uchunguzi maalumu (Special Audit) na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhusu makusanyo ya Kituo Kikuu cha Mabasi cha Ubungo (UBT) ili kuboresha mapato ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.

 

Julai 28, 2009 Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Ludovick Utoh, alikabidhi ripoti hiyo kwa Waziri Mkuu ambayo pamoja na mambo mengine, ilieleza kasoro za ukusanyaji wa ovyo na tuhuma za ubadhirifu wa mapato ya Kituo Kikuu cha Mabasi cha Ubungo.

 

Kutokana na matatizo ya kiuendeshaji na kiutawala yaliyoripotiwa katika taarifa za Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali pamoja na taarifa zingine kuhusu kituo kutofanyiwa kazi kwa ukamilifu, nawasilisha hoja binafsi kwa mujibu wa Kanuni ya 19 (1) na (5) ya Kanuni za kudumu za Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam (ambayo katika hoja hii itajulikana kwa upande mwingine kama Halmashauri) ambayo mimi ni mjumbe ili hatua stahili ziweze kuchukuliwa.

 

Maelezo ya Hoja

Kutokana na ukaguzi maalumu uliofanywa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali, mambo yafuatayo yalibainika:

 

• Kuwa Halmashauri iliingia mkataba na kampuni ya M/s Smart Holding kama wakala wa kukusanya mapato katika kituo cha mabasi Ubungo. Kutokana na mkataba huo kampuni tajwa ilitakiwa kuilipa Halmashauri kiasi cha shilingi 1,500,000 kwa siku kwa mapato ya magari yanayoingia kwenye kituo pamoja na tozo ya ulinzi wa magari yaliyokuwa yakiegeshwa na ada ya kuingia. Hata hivyo, baada ya ukaguzi uliofanywa uligundua kuwa kiasi cha Sh 4,618,629 ilikuwa ni mapato ya kila siku ukilinganisha na kiasi kilichopo kwenye mkataba huo ambacho Halmashauri ilikuwa ikipokea.

 

• Kuwa ilibainika kuna upangishaji holela wa majengo ya biashara bila idhini ya mmiliki. Kwa mfano mpangaji alilipa kiasi cha Sh 130,000 kwa mwezi kama kodi kwa mmiliki wakati mpangaji alikuwa anapata mapato ya kiasi cha Sh 600,000 kwa kupangisha watu wengine (subletting).

 

• Kuwa kiasi cha Sh 146,692,226 zilikusanywa na wakusanyaji wa mapato, lakini mapato hayo hayakupelekwa benki.

 

• Kuwa Halmashauri iliingia mkataba na wafanyabiashara ndogondogo 100 kuendesha shughuli za biashara ndani ya kituo bila kuainisha maeneo au majengo ambayo watayatumia kwa shughuli zao.

 

• Kuwa Halmashauri iliingia mkataba wa miaka 14 na M/s Riki Hill Hotel na mkataba utaisha Julai 20, 2023; hata hivyo mapitio ya makubaliano hayo yanaonyesha upungufu ufuatayo:

 

i. Mkataba ulisainiwa miaka miwili baada ya shughuli kuanza.

 

ii. Mkataba ulisainiwa na Mkurugenzi wa Halmashauri na siyo Mstahiki Meya kama ambavyo taratibu zinataka.

 

iii. Uongozi wa Halmashauri ulishindwa kutoa nyaraka za kwa namna gani mkodishwaji huyo alivyopatikana na pia mkodishwaji alikuwa anatumia eneo kubwa kuliko ilivyokuwa ikionekana katika mkataba.

 

• Kuwa Halmashauri iliingia mkataba na kampuni ya M/s Abood Bus Service kupanga katika eneo la 2070 sqm kujenga na kutumia na badae kulitoa jengo kwa mmiliki na kutakiwa kulipa 500,000 kwa mwezi; hata hivyo mapungufu yafuatayo yalionekana:

 

i. Hakuna ushahidi wa kimaandishi uliotolewa kwa wakaguzi kuthibitisha kiasi cha Sh 44,220,660 kama gharama za ujenzi.

 

ii. Hakuna nyaraka iliyoonyesha jinsi mkataba wa ukodishwaji ulivyopatikana.

 

iii. Mkataba haukuonesha eneo ambalo lilipaswa kuendelezwa.

 

iv. Hakuna vigezo vilivyotolewa kuhalalisha malipo ya Sh 500,000 kwa mwezi kwa eneo hilo .

• Kuwa uongozi wa Kituo cha Ubungo kwa makusudi kabisa ulibadilisha kiwango cha upangaji cha Sh 6,000 kwa futi za mraba 784.08 hadi Sh 5,000 ambazo zilitakiwa kulipwa na kampuni ya M/s Clear Channel, kiwango ambacho kilitakiwa kutozwa kwa kampuni ya Bill Board Advertisement kinyume cha kiwango kilichowekwa na Kanuni za Halmashauri ya Jiji ya 1997 na hivyo kusababisha hasara ya kiasi cha Sh 3,920,420 kwa Halmashauri kwa miaka mingi mfululizo.

 

• Uongozi wa Halmashauri kwa makosa yao wenyewe ya kivipimo ulisababisha kushuka kwa kiwango cha mapato kiasi cha Sh 74,529,840 kwa miaka miwili kuanzia Julai 2007 hadi Juni 2009.

 

• Kuwa katika mkataba kati ya Halmashauri na kampuni ya M/s Globe Accountancy Services (wakala) ili kukusanya mapato kwa niaba ya Halmashauri kwa miaka mitatu kutoka Oktoba 5, 2001 hadi Oktoba 4, 2004 bila ushahidi wowote wa kimaandishi kuonyesha kuwa taratibu zote za kitenda zilifuatwa na pia taratibu za manunuzi hazikufuatwa.

 

• Kuwa hakuna utaratibu uliozingatiwa katika kuwapa mikataba M/s Scandnavia Express Service Ltd, Riki Hill Hotel, Kiwembo Motors na Smart Holding kama wakala wa kukusanya mapato, na pia nyaraka kwa ajili ya ukaguzi hazikuweza kutolewa.

 

• Pamoja na mambo mengine, kampuni ya Smart Holding kama wakala wa kukusanya mapato ilitumia vitabu vya risiti ambavyo ni vigumu kwa Halmashauri kudhibiti na hivyo kuwa vigumu kugundua kiasi cha mapato walichokuwa wanakusanya.

 

• Kuwa kampuni ya Scandnavia ilikuwa haina mkataba rasmi na Halmashauri katika eneo walilokuwa wanalitumia na pia kampuni haikulipa kiasi cha Sh 236,486,400 kuanzia Septemba 2005 hadi Mei 2009 kama ilivyotakiwa.

 

Pamoja na upungufu huo ulioelezwa na taarifa ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali; yamejitokeza pia masuala mengine katika kipindi cha kati ya mwaka 2009 mpaka 2011 yanayohitaji kushughulikiwa:

 

• Hata hivyo, mnamo Oktoba 30, 2010 Halmashauri ilisaini mkataba na kampuni ya Konsad Investments Limited kwa ajili ya kukusanya mapato kwa niaba ya Halmashauri. Hata hivyo, kampuni hiyo imekuwa wakati mwingine haiwasilishi makusanyo ya Sh 5,650,000 kwa siku kwa Halmashauri kama ilivyokubaliwa.

 

• Kampuni ya Konsad imeanza kutekeleza Sheria Ndogo mpya (By Law) ya kupandisha viingilio vya kituoni bila ridhaa ya Jiji. Pamoja na Uongozi wa Kituo kukanusha wakati wa ziara ya Mstahiki Meya ya Februari 4, 2011 ushahidi wa risiti unaonyesha kwamba tayari walishaanza kutoza, hususani wananchi wanaoingia kwenye kituo. Suala la kupandisha viwango vya viingilio vinavyowagusa wananchi wengi wakati vyanzo vingine vyenye kuleta fedha nyingi zaidi vinaachwa huku huduma zikiwa hazijaboreshwa linahitaji kufanyiwa uamuzi mbadala na kutolewa tamko kwa umma.

 

• Katika ziara yangu ya Kituoni ya Januari 28, 2011 ya kusikiliza malalamiko ya mawakala nilibaini kuwapo kwa haki zao ambazo zinaminywa na mazingira magumu ya kufanyia kazi ikiwemo uchache wa ofisi za kukatia tiketi. Pia, kuna matitizo ya ulinzi kituoni, hususani nyakati za usiku kwa ajili ya abiria wanaoshuka usiku. Kadhalika, kumekuwa na matatizo ya umeme yanayohusisha ubovu wa baadhi ya taa, umeme kuwa mdogo ukilinganisha na mahitaji na pia jenereta la kituoni haiwashwi kwa wakati umeme unapokatika.

 

• Mpango wa Biashara (Business Plan) wa kuwezesha Jiji kukiendeleza kituo husika kuwa cha kisasa kwa lengo la kukuza biashara na kupanua huduma utakaohusisha ujenzi wa majengo ya kisasa yanayoendana na mahitaji ya kitaifa na kimataifa haujaanza kutekelezwa. Pamoja na changamoto za kiutendaji, sababu mojawapo inayoelezwa ni kusudio la ujenzi wa miundombinu (Depot and Transfer Station) unatarajiwa kufanywa na Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART).

 

HOJA:

Kutokana na maelezo hayo naomba kutoa hoja kwamba Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam lipitishe maazimio yafuatayo:

 

(1) Taarifa Kamili ya Ukaguzi Maalumu (Special Audit) uliofanywa na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhusu Kituo Kikuu cha Mabasi cha Ubungo (UBT) itolewe hadharani na ijadiliwe katika Baraza la Madiwani wa Jiji.

 

(2) Mikataba yote iliyoingiwa kinyume cha taratibu ivujwe au ipitiwe upya ili kuwa na mfumo ambao utawezesha Halmashauri kuweza kupata mapato ya kutosha kwa mujibu wa thamani ya mali na kanuni zinazohusika.

 

(3) Uchunguzi ufanyike wa tuhuma za mazingira ya ufisadi na ukiukwaji wa kanuni katika kuingiwa kwa mikataba tajwa ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa kwa wahusika.

 

(4) Malimbikizo yote ya madeni yafuatiliwe na kulipwa ili Halmashauri iweze kupata mapato kwa ajili ya kutoa huduma za msingi za wananchi.

 

(5) Kwa kuwa Kituo cha Mabasi Ubungo kinachangia takribani nusu (50%) ya mapato ya jiji, basi mkazo uwekwe katika kuboresha mazingira ya kituo kwa kufanya ukarabati na uendelezaji. Aidha, upungufu wa dharura ambao unaathiri zaidi watumiaji wa kituo ufanyiwe kazi katika mwaka wa fedha wa 2011/12.

 

(6) Kwa kuwa hakuna mgawo wowote ambao ngazi za Manispaa, Kata na Mtaa zinapata kutokana na mapato yanayotokana na Kituo cha Mabasi Ubungo; wakati majadiliano yakiendelea kuhusu suala hili, Jiji litenge bajeti ya Kituo Cha Mabasi Ubungo (UBT) kuchangia shughuli za kijamii (Corporate Social Responsibility) katika maeneo ya Jimbo la Ubungo.

 

(7) Taarifa ya Kina kuhusu Mradi wa Mabasi yaendayo kwa Haraka (DART) iweze kuwasilishwa eneo linalohusika na mradi huo liweze kufahamika ili Jiji lianze kutekeleza Mpango wa Biashara wa kuendeleza Kituo husika katika maeneo ambayo yataendelea kuwa kwenye usimamizi wa Jiji.

 

(8) Pendekezo lililotolewa katika kikao cha Kamati ya Fedha na Uongozi cha Mei 11, 2011 liidhinishwe na kutekelezwa ili kusitisha kutekeleza Sheria ndogo ya kuongeza kiwango cha kiingilio kwa wananchi toka Sh 200 hadi Sh 300 na kufanya mapitio ya sheria ndogo husika ili nguvu za ukusanyaji mapato zielekezwe katika vyanzo visivyoongeza mzigo kwa wananchi wa kawaida wanaotumia Kituo Kikuu Cha Mabasi cha Ubungo.

 

Naomba kuwasilisha,


John Mnyika(Mb)

Jimbo la Ubungo

Mjumbe wa Baraza la Madiwani Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam

 

 

 

 

 

By Jamhuri