Katika kipindi hiki cha mageuzi ya kijamii, kumekuwa na mashirika mbalimbali yaliyoanzishwa nchini yakijitanabaisha kuwa yanalea watoto yatima na wanaoishi katika mazingira hatarishi, kwa mashirika hayo kuwapatia watoto hao mahitaji muhimu kama vile chakula, malazi, mavazi, matibabu na elimu.

Hata hivyo, baadhi ya mashirika hayo yamekuwa yakilalamikiwa na wananchi kwamba yapo kibiashara zaidi, na viongozi wake wamekuwa wakitumia kivuli cha watoto wa aina hiyo kujipatia manufaa binafsi.


Hivi karibuni, Mkuu wa Mkoa wa Mara, John Tuppa, alizuru kituo cha watoto yatima na wa mazingira hatarishi kilichoanzishwa na Dk. John Chacha (anayeishi Marekani), kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wilayani Tarime.


Kituo hicho kinachojulikana kama City of Hope (Jiji la Matumaini), kilifunguliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete, mwaka 2009, katika Kijiji cha Ntagacha.


Mkuu huyo wa mkoa alifanya ziara hiyo baada ya kupata malalamiko kutoka kwa Mkurugenzi wa kituo hicho, Dk. Chacha, dhidi ya Serikali ya Wilaya ya Tarime, akidai haishiriki kuchangia gharama za mahitaji ya watoto kituoni hapo, hususan mahitaji ya matibabu.


Dk. Chacha anadai kuwa amekuwa akiomba msaada wa madaktari kwa ajili ya kituo chake bila mafanikio, hivyo akamwomba Mkuu huyo wa Mkoa amsaidie kupata msaada wa madaktari, dawa na walimu. Ingawa katika hotuba yake, Tuppa hakujibu ombi hilo la Dk. Chacha, ila aliishia kumpongeza kwa kurudi kuwekeza nyumbani (Tanzania).


Mara baada ya hotuba ya Mkuu huyo wa Mkoa, ilizuka minong’ono miongoni mwa wananchi ikimlenga Dk. Chacha. Mmoja alisimama na kuhoji: “Dk.Chacha anaombaje msaada serikalini wakati anasaidiwa na wafadhili wa Kizungu kuendesha kituo?

 

Alisema: “Isitoshe zahanati ya kituo chake imechangiwa na nguvu za wananchi lakini cha ajabu wanakijiji hutozwa gharama kubwa za matibabu kinyume cha makubaliano yaliyopo, lakini pia Dk. Chacha hana uhusiano mzuri na wananchi wa Kijiji cha Ntagacha.”

 

Malalamiko hayo yalimsukuma mwandishi wa makala hii kurudi kijijini Ntagacha siku chache baadaye, ili kupata ukweli baina ya wananchi na mmiliki huyo wa kituo hicho cha watoto yatima.


Petro Daudi ni Mwenyekiti wa Kitongoji cha Komeserere katika Kijiji cha Ntagacha. Anasema; “Dk. Chacha alifika kijijini hapo kwa ‘style’ ya ajabu, ambayo baadaye iligundulika ilikuwa ni ulaghai wa kutaka kupewa ardhi ya kuendeshea uwekezaji wake huo.

 

“Wananchi wakampatia maeneo ya ardhi kwa gharama ndogo wakiamini amekuja kusaidia wanakijiji, kumbe zilikuwa ni mbinu za kututeka akili tukafanya kila alichokitaka tukijua ni mtu mwema kumbe ni mlaghai,” anasema.


Daudi anasema vitendo vya Dk. Chacha kuchimba visima sita na kukarabati madaraja mawili, viliwashawishi wanakijiji na kumwona ni mtu mwema na mwenye nia ya kuwaletea maendeleo lakini matokeo yamekuwa tofauti na matarajio yao.

 

“Kwa jinsi alivyokuja mwanzoni kila mwananchi alimpenda, kumbe alikuwa chui aliyevaa ngozi ya kondoo akisema wanakijiji watasaidiwa na kituo kitakuwa cha kulea watoto yatima, lakini ametumia eneo hilo kuanzisha shule ya kusomesha hadi watoto wa matajiri kwa gharama kubwa,” anasema Daudi.


Mwalimu wa kituo hicho aliyeomba kutotajwa jina, alisema kituo hicho kinatoa elimu ya awali na msingi, na kwamba kwa sasa kina wanafunzi waliotarajiwa kuhitimu darasa la saba mwaka huu.


Kituo hicho kinasadikika kuwa na jumla  ya wanafunzi 416 na walimu 15. Inaelezwa kwamba kwa sasa kimeelekeza nguvu kubwa katika kutoa elimu, ambako watoto 101 wanasoma bure na 315 kutoka maeneo mbalimbali nchini wanalipiwa ada na wazazi/walezi wao.


Mkazi mwingine wa kijiji hicho, Omary Bakari, anasema Dk. Chacha hana uhusiano na wanakijiji na kwamba watu wengi walioajiriwa kufanya kazi kituoni hapo wanatoka nchi jirani ya Kenya, hali isiyowanufaisha wenyeji.


“Mwekezaji anapowekeza anapaswa kuwanufaisha wananchi wanaomzunguka katika masuala ya elimu, afya, maji, barabara na ajira lakini katika kituo hiki kati ya walimu 15 waliopo Mtanzania ni mmoja, wengine wote ni Wakenya.


“Wahudumu na wapishi ni Wakenya, inamaana Tanzania hawajui kupika? Kwanini walimu wote watoke Kenya wakati Tanzania tuna walimu wengi wasomi au nao hawajui Kingereza? Huyu ni mtu wa namna gani asiyethamini wa kwao?” anahoji Bakari.


Anasema kwamba wafanyakazi wengi wa kituo hicho wanalipwa ujira mdogo, na baadhi yao wamekuwa wakisimamishwa na kufukuzwa kazi ghafla bila sababu za msingi. “Dk. Chacha akikuona tu unaozungumza na Mzungu ujue huna kazi, anahisi kuna kitu unamtuhumu au labda unamwomba msaada Mzungu huyo,” anaongeza Bakari.


Nyamuhanga Chacha ni mdogo wake Dk. Chacha. Naye anamlalamikia kaka yake huyo kwamba alimlaghai na kutwaa ardhi yake bila kumpatia malipo waliyokubaliana.

 

“Kaka alipokuja kutoka Marekani alifikia kwenye nyumba zetu akasema amekuja kumjengea mama nyumba, baadaye akaniomba nihame ili anijengee nyumba, ndipo nikanunua ardhi nyingine yenye ukubwa wa ekari moja kwa gharama ya Sh 300,000 nikajenga nyumba nyangu lakini cha ajabu hadi leo sijajengewa nyumba aliyoniahidi,” anasema Nyamuhanga.


Anasema; “Alitulaghai wanakijiji tukamwachia maeneo yetu tukidhani atatusaidia kumbe hana msaada wowote. Nilikuwa ninamfanyia kazi ya kupalilia mashamba na bustani kwa malipo ya Sh 30,000 kwa mwezi.”


Pia wanakijiji wanamlalamikia Dk. Chacha kwamba anawatoza gharama kubwa za matibabu katika zahanati ya kituo hicho bila kujali kuwa walichangia nguvu kazi katika ujenzi huo.


Mwenyekiti wa Kijiji cha Ntagacha, Steven Kisunte, anasema, “Wanakijiji walisomba mawe, mchanga, kokoto, matofali na maji, wakachimba msingi kwa nguvu zao, lakini baada ya zahanati kukamilika wanatibiwa kwa gharama kubwa. Mtu anatibiwa malaria kwa Sh 4,000 hadi Sh 5,000.”


Kisunte anasema; “Dk. Chacha alikuja kijijini katika sura kama ya kidini hivi, akionesha ni mtu wa msaada. Tulifanya makubaliano ya mdomo hasa ukizingatia ni mzaliwa wa hapa. Lengo la kituo lilikuwa ni kulea na kusomesha watoto yatima bure, lakini sasa kimekuwa mradi wake wa biashara.

 

Ofisa Elimu Wilaya ya Tarime, Emanuel Johnson, anasema hajatembelea City of Hope kwa muda mrefu, lakini akadokeza kuwa Dk. Chacha amekuwa akikiuka taratibu zinazotolewa na uongozi wa wilaya kuhusu uendeshaji wa shule ya kituo hicho.

 

Kwa upande wake, Ofisa Ustawi wa Jamii wa Wilaya ya Tarime, Peter Mwanga, anasema Dk. Chacha amekuwa akikwepa kushirikisha wataalamu wa Serikali katika kupata miongozo halali ya kuendesha kituo chake hicho.


“Tumekuwa tukikorofishana na Dk. Chacha kuhusu kuleta taarifa za kituo chake, hadi sasa hakuna taarifa yoyote iliyofika ofisini kuhusu kituo chake. Nasikitika kusikia kwamba watoto wanalipa ada wakati kilianzishwa kwa madhumuni ya kulea bure watoto yatima, itabidi tukitembelee tena,” anasema Mwanga.


Mkuu wa Mkoa wa Mara, John Tuppa, anasema makubaliano yasiyo ya kimaandishi ni kikwazo cha kumwajibisha mwekezaji anayeshindwa kutimiza ahadi zake kwa wananchi. Hata hivyo, Tuppa anasema Serikali inashughulikia tatizo hilo ikiwa ni pamoja na kuandaa mkataba na uwekezaji wa kituo hicho.


“Tunaandaa utaratibu… tunataka kuingia makubaliano ya kimaandishi na huyu Dk. Chacha tumpe masharti yetu ili anaposhindwa kutekeleza awajibishwe. Tumeshindwa kumbana kwa sababu wananchi hawakufanya naye makubaliano ya kimaandishi, kwa hiyo huwezi kumwajibisha.


“Hata huo msaada wa dawa na wauguzi anaotuomba hadi akubali masharti yetu kama Serikali ili wananchi watibiwe kwa gharama nafuu,” anasema Tuppa.

JAMHURI inaendelea na juhudi za kumtafuta Dk. Chacha aweze kuzungumzia tuhuma hizo zinazoelekezwa kwake.


 

1858 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!