Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) limethibitisha kupokea malalamiko kutoka kwa Shirikisho la mchezo huo nchini Malawi (FAM), kuhusu matamshi yaliyotolewa na Kocha wa Nigeria, Stephen Keshi, yanayohusishwa na ubaguzi wa rangi.

Kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), FIFA imesema kuwa kwa sasa hakuna taarifa yoyote itakayotolewa juu ya sakata hilo hadi uchunguzi utakapokamilika.

 

FAM imedai kuwa Keshi alitoa matamshi ya ubaguzi dhidi ya kocha wake, Tom Sainfiet, ambaye ni raia wa Ubelgiji.

 

Katibu Mkuu wa FAM, Suzgo Nyirenda, ameiambia BBC hivi karibuni kuwa matamshi ya ubaguzi kama hayo hayafai kwenye michezo katika dunia ya sasa.

 

”Tunahisi hili ni kama shambulio dhidi ya kocha wetu na tutamtetea kwa hali na mali bila kuzingatia uraia wake na rangi ya ngozi yake.

 

”Tumetuma ushahidi wa yale Keshi aliyoyasema na tunatarajia kuwa FIFA itachukua hatua kali dhidi ya kocha huyo wa Nigeria,” alisema Nyirenda.

 

Kesi hiyo inahusiana na matamshi ambayo Keshi aliyatoa kufuatia wito wa Malawi wa kuhamisha mechi yao ya kufuzu kucheza Kombe la Dunia mwaka 2014 kutoka mji wa Calabar kutokana na sababu za kiusalama.

 

mahojiano na runinga moja ya Uingereza, Keshi alisema, ”Nafikiria kuwa kocha huyo wa Malawi ni mwendawazimu.”

 

”Ikiwa anataka kuongea na FIFA, basi lazima arejee kwao nchini Ubelgiji. Yeye siyo mtu wa Afrika, ni Mzungu mweupe, lazima arudi kwao Ubelgiji,” alisema Keshi.

 

Maofisa wakuu wa FAM na kocha huyo hawajasema lolote kuhusiana na madai hayo ya kocha wa Malawi, Saintfiet, na FAM.

 

Mechi hiyo kati ya Malawi na Nigeria mjini Calabar itaamua nani atafuzu kwa raundi ya mwisho ya mechi ya kufuzu kwa fainali hiyo barani Afrika.

 

Mabingwa hao wa Afrika wanahitaji kutoka sare ya aina yoyote ili kufuzu ilhali Malawi inahitaji ushindi ili isonge mbele.

By Jamhuri