Serikali imetakiwa kuboresha mipangilio ya ulipaji kodi ikiwamo kuondoa tozo zisizokuwa za ulazima, ili kutengeneza mazingira rafiki kwa wawekezaji pamoja na kuepuka kupungua kwa mzunguko wa fedha.

Akifanya mahojiano maalumu na JAMHURI, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe mkoani Morogoro, Professa Prosper Ngowi, anasema kukosekana kwa fedha katika mzunguko kunatokana na mpangilio wa sera za ulipaji kodi.

Prof. Ngowi ambaye ni mchumi, anasema kuwa mzunguko mdogo wa fedha inachangiwa kwa kiasi kikubwa na utozwaji wa kodi za aina nyingi na kusababisha wafanyabiashara kubaki na fedha kidogo mkononi mwao.

Anabainisha kuwa uwepo wa riba kubwa katika benki, ni miongoni mwa vikwanzo kwa wafanyabiashara wa sekta binafsi kwa kukosa ushawishi wa kukopa kutokana na ukubwa wa gharama ya ukopaji.

“Uwepo wa hali hii inakuwa vigumu kuwa na mzunguko mzuri wa fedha, kwani wafanyabiashara inawapa wakati mgumu kwenda kukopa benki kwa ajili ya kuendeleza uwekezaji wanaofanya,’’ anasema Prof. Ngowi.

Anasema ingawa Rais John Magufuli ameweza kubainisha  kukosekana kwa fedha kunasababishwa na watu kuficha fedha zao benki, lakini katika hilo linasababishwa kwa kiasi kidogo katika masuala ya uchumi.

Anabainisha kuwa nchi ipo katika mipango ya kufanikisha maendeleo ya uchumi wa viwanda, hivyo ili ifanikiwe kunatakiwa kuwapo kwa mzunguko wa fedha ili wawekezaji wapate fursa ya kuwekeza katika miradi husika. 

“Ili maendeleo yaweze kupatikana kwa wawekezaji, tuwe na mzunguko mkubwa wa fedha ili wateja (Watanzania) waweze kununua bidhaa,” anasema Prof, Ngowi.

Anaeleza kuwa endapo hali hii ikiendelea – ya ukosefu wa fedha katika mzunguko wa biashara – itakuwa changamoto kutimiza malengo ya kuwa na uchumi wa viwanda.

“Endapo hali hii ikiendelea na kuingia kila mahali, kuna uwezekano wa kuwapo kwa mtikisiko wa uchumi, jambo ambalo si zuri, kwani asilimia kubwa ya kumpuni zitashindwa kuzalisha pamoja na kujiendesha na kulazimika kupunguza wafanyakazi,” anasema Prof. Ngowi.

Pia anasema kwamba Serikali itakosa mapato kama ilivyotokea mwaka 2008 katika mtikisiko wa uchumi duniani, hivyo ni jukumu la Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuchukua hatua stahiki.

Anasema sasa (BoT) inatakiwa kutuliza soko kwa kutoa mwongozo na isipofanya hivyo, upo uwezekano mkubwa wa soko kuingiwa na hofu.

“Mfano mzuri Benki ya Twiga imefungiwa na watu wameshindwa kuendesha fedha zao (access), jambo hilo linasababisha baadhi ya watu kuanza kuingiwa na hofu kuwa isije ikatokea katika benki nyingine ambazo wanazitumia, na kuanza kwenda kuzitoa fedha zao,  na mwisho wa siku benki watakosa fedha, jambo ambalo linaleta athari katika uchumi,’’ anasema Prof. Ngowi.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Prof Humphrey Moshi, anasema Rais Magufuli kwa kipindi cha mwaka mmoja ameweza kubadili fikra za Watanzania kufanya jambo fulani kwa mazowea ikiwamo kubana bajeti ya matumizi ya kawaida, ili kuangalia uwezekano wa kupanua wigo wa maendeleo.

Prof. Moshi anasema kuwa hatua hizo ni sehemu ya kujenga mazingira bora ya kutengeneza njia ya kuwa na uchumi imara hapo baadaye.

Anaeleza kuwa Serikali ipo katika mipango ya kutengeneza misingi ya kukuza uchumi kwa kufanya uwekezaji wa kufufua miundombinu mbalimbali ikiwamo reli pamoja na kufanyika maboresho kwa kiasi kikubwa katika Mamlaka la Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA).

Prof. Moshi anasema uwekezaji huo pamoja na kubana matumizi kitaalamu, umechangia kwa kiasi fulani ukosefu wa fedha katika mzunguko wa biashara na kusababisha ugumu katika shughuli za kiuchumi.

Anaeleza kwamba wafanyabiashara wanapaswa kukubaliana na mabadiliko ya hali ya uchumi ili kuweza kuendelea na biashara zao.

“Kama kipindi cha nyuma walikuwa wanapata faida ya asilimia 20, sasa wanatakiwa kukubali kushusha bei ili waweze kuuza hata kama wakipata faida ya asilimia 10. 

Anaendelea kusema, “Mabadiliko yoyote yanapotokea katika utendaji kunakuwa na uwezekano wa hali ya uchumi kubadilika, lakini tunapaswa kukubaliana na hali halisi ili tuweze kusonga mbele,”  anasema Prof. Moshi.

Msomi huyo wa uchumi ameitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutokadiria viwango vikubwa vya kodi kwa lengo la kumridhisha Rais Magufuli na kuonekana wanafanya kazi nzuri, ila wanapaswa kuangalia jinsi ya kuweka mazingira mazuri yatakayomfanya mwekezaji aendelee kufanya biashara hapa nchini.

“Kutofanya hivyo, kunaweza kuwa na wafanyabiashara wachache ambapo itakuwa hasara kwa Taifa ambalo linahitaji kukuza uchumi,” anasema Prof. Moshi.

Anabainisha kuwa ipo kesi inayoendelea kuhusu mfanyabiashara mmoja ambaye awali alikuwa analipa kodi ya Sh milioni 20 kwa mwaka, lakini baada kupandishiwa kodi hadi kufikia milioni 45 ameona bora kuacha kufanya biashara kuliko kutoa kiasi hicho cha fedha.

“Endapo mfanyabiashara akirudisha mzigo tayari TRA watakosa mapato, hivyo ni bora wakafanya kitu ambacho kinaweza kuleta matunda na kuchochea uwekezaji,’’ anasema Prof. Moshi.

Novemba 3 mwaka huu, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiwa katika Bunge la 11 la Bajeti la mwaka 2016/2017, alisema Serikali inaendelea kufanya mazungumzo na TRA ili kutafuta kanuni nzuri ya kodi ambayo itakuwa rafiki kwa wafanyabiashara.

Majaliwa alikiri kupokea malalamiko ya utozwaji wa kodi kwa wafanyabiashara, baada ya kuwa na ongezeko la kodi kwa wadau mbalimbali wa biashara.

Anasema kuwa mfanyabiashara yeyote kama ana malalamiko yoyote, anapaswa kwenda mamlaka husika ili kuangalia jinsi ya kutatua changamoto zinazomkabili katika uendeshaji.

Hata hivyo, anasema kuwa Serikali inaendelea kuwaunga mkono wawekezaji kwa ajili ya kuendeleza fursa na kupanua wigo katika nyanja mbalimbali.

2049 Total Views 6 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!