Sababu za kupungua nguvu za kiume -5


Wiki iliyopita, Dk. Khamisi Ibrahim Zephania alizungumzia kwa kina homoni ya kiume na umuhimu wake katika tendo la ndoa. Sasa endelea kumfuatilia zaidi…

Panahitajika ubongo, neva, homoni, mishipa ya damu, tezi [glands], utendaji mzuri wa figo, ini, baadhi ya misuli na viungo chungu nzima ndani ya mwili kama tutakavyoona katika makala zetu za mbele.

Nukta muhimu hapa unayopaswa kuzingatia ni kuwa mtu anayepungua nguvu za kiume ina maana kwamba kuna seli, au tishu, kiungo au viungo, mfumo au mifumo ndani ya mwili wake kimeshindwa au vimeshindwa kufanya kazi katika utaratibu wake wa kawaida.

Au kuna matukio ya vitendo kama vile mpwito neva [nerve impulses] zinazokwenda kwenye ubongo, uti wa mgogo, eneo linalozunguka uume hazifanyi kazi vizuri. Mpwito neva ni mchuruziko wa mawimbi madogo madogo sana ya kemikali-umeme kutokana na  urefu wa neva, hivyo kuwezesha sehemu moja ya mwili kuwasiliana na nyingine.

Au kuna mwitiko dhaifu wa misuli, au kuna dosari katika tishu za utembe [fibrous tissues]. Hizi ni tishu ambazo kwa kawaida huwa na seli ndefu na nyembamba. Au huenda kuna dosari katika mishipa ya vena na ateri na pia iliyo karibu na Corpora cavernosa.

Au huenda kuna matatizo mengine kadha wa kadha.

Kama mtu atakwenda kwa daktari mwenye utaalamu na kumlalamikia, “Nimepungua nguvu za kiume!” Daktari atachunguza mzunguko wa damu, mfumo wa neva, mfumo wa mkojo, homoni na kemikali na utendaji wa viungo vingine.

Daktari atamhoji kuhusu afya yake kwa ujumla, historia yake, mtindo wake wa maisha na kazi zake. Kisha atamfanyia vipimo ili kugundua kiini cha tatizo.

Baada ya kubaini chanzo cha tatizo, daktari atampa mgonjwa dawa zinazokwenda kutibu chanzo cha tatizo.

Mathalan, tatizo laweza kubainika kuwa mgonjwa ana tatizo la kutanuka kwa tezi-dume [prostate gland], hivyo daktari atampa dawa za kurekebisha hiyo tezi au atashauri upasuaji kulingana na hali au ukubwa wa tatizo.  Au mgonjwa anaweza kuwa ana tatizo la homoni mwilini [hormonal imbalance], daktari atampa dawa za kurekebisha tatizo hilo na kadha wa kadha.

Hivyo, utaona hapa kuwa kutanuka kwa tezi-dume, tatizo linalojulikana kama Benign Prostate Hyperplasia [BPH] au Benign enlargement of the prostate [BEP] au Adenofibromyomatous hyperplasia na Benign prostatic hypertrophy ndiyo ugonjwa, ambapo moja ya dalili zake ni kufika kileleni haraka kama tunavyokwenda kuliona tatizo hili kwa mapana zaidi katika makala za mbele.

Au katika mfano wetu wa pili, tatizo la homoni [hormonal imbalance] ndiyo ugonjwa, baadhi ya dalili zake ni kukosa hamu ya tendo la ndoa, kukosa msisimko wa mapenzi na uume kusimama kwa ulegevu.

Orodha ya matatizo yanayosababisha kupungua nguvu za kiume ni ndefu, nimesema yanafika 100, na hata zaidi ya 100! Tutaona baadaye mbele katika makala haya.

Hivyo, wauza dawa za nguvu za kiume inawapasa wasome, wapate walau A, B, C, siyo kuwaibia watu vijisenti vyao kwa matibabu ambayo hayatawasaidia.

Haiwezekani na haingii akilini, huyu aishiwe nguvu za kiume kutokana na kupungua kwa kemikali ya nitric oxide ndani ya damu, na yule apungue nguvu za kiume kutokana na tatizo la prostate ati wote watibiwe kwa dawa ya aina moja. Jambo hilo litakuwa siyo kweli kabisa!

Kama nilivyokwishaeleza, kupungua nguvu za kiume ni dalili ya ugonjwa. Ikiwa mtu atakimbilia kubugia dawa ili kujitibu bila kuangazia matibabu kwenye chanzo cha tatizo, basi mtu huyo atakuwa ni sawa na amekimbilia kutibu dalili ya ugonjwa na ugonjwa utabaki palepale.  Anachoweza kupata ni unafuu wa muda mfupi sana, lakini baadaye hali itaendelea vilevile; na hata inaweza kuwa mbaya zaidi.

Mfano, watu wengi wamekuwa wakifika katika kliniki yangu kutibiwa nguvu za kiume na wengine kunipigia simu na kudai walikwishatumia Viagra au dawa zinazofanana na Viagra kiutendaji. Nitaeleza kwa kirefu madhara ya Viagra katika makala za mbele, lakini hapa nieleze kwa ufupi sana.

 

Viagra siyo matibabu ya nguvu za kiume hata kidogo. Haiendi kutibu chanzo cha tatizo. Inachofanya ni kulazimisha damu iingie katika uume na ikae humo kwa kusisimua nitric oxide. Hatari yake ni kuwa vitu ambavyo ni vigonjwa ndani ya mwili vitalazimishwa  kufanya kazi katika hali hiyo hiyo ya ugonjwa, hatimaye baadaye havitafanya kazi kabisa.

Ni kama mtu mgonjwa, tuseme anaugua malaria, pengine yuko taabani, unamlazimisha abebe debe la mahindi. Anaweza kujikongoja akafaulu mara ya kwanza lakini baadaye anaweza kushindwa kabisa, na hata anaweza kufa! Hii ndiyo maana watumiaji wengi wa Viagra, baadaye huja wakilalamika, “Mambo yamekuwa mabaya zaidi!”


3271 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!