Vidonda vya tumbo na hatari zake (9)

Katika sehemu ya nane ya makala haya, Dk. Khamis Zephania alizungumzia pamoja na mambo mengine, madhara ya kazi za usiku, makundi ya damu na uhusiano wa vidonda vya tumbo. Sasa endelea na sehemu hii ya tisa…

Dalili za vidonda vya tumbo

Si kawaida watu kuwa na vidonda vya tumbo na kusiwe na dalili. Dalili za vidonda vya tumbo hutofautiana baina ya mtu na mtu. Watu wengi hawajui kabisa kama wana vidonda vya tumbo, isipokuwa kama ghafla watajiona wakitapika damu, wengine huhisi maumivu au mchomo katika sehemu yao ya juu ya tumbo (fumbatio).

Baadhi ya wagonjwa hukuta kwamba wanapokula kwa hakika husaidia kuondoa tabu kwa muda. Wengine hukuta kuwa wanapokula ndiyo hufanya hali kuwa mbaya zaidi. Vinywaji vya striki, vyakula vya moto na vya kusisimua vinaweza kufanya maumivu kuwa makali zaidi.

 

Hata hivyo, ni muhimu kujua kuwa watu wengi wenye maumivu ya tumbo siyo kwamba wana vidonda vya tumbo.

 

Mgonjwa wa vidonda vya tumbo anaweza kuonesha baadhi ya dalili zifuatazo: Kichefuchefu, kutapika, kuhisi mchomo ndani ya tumbo (abdomen), maumivu ndani ya kifua, kupiga mbweu mara kwa mara, kukosa hamu ya chakula, kupungua uzito, damu ndani ya mavi au matapishi, kutosagika chakula tumboni na kiungulia.

 

Maumivu: Ni hisia za mwili zisizo nzuri ambazo mwili hupata ikiwa ni dalili ya tahadhari kwamba mwili umedhuriwa.

 

Vidonda vya tumbo vinaweza kuleta dalili zisizo kali sana zinazofanana na kiungulia au maumivu makali yanayosambaa sehemu yote ya juu ya mwili. Maumivu haya kwa kawaida hutokea ndani ya fumbatio, lakini mara nyingi maumivu yanaweza kuhisiwa kifuani. Wakati mwingine maumivu hutambaa hadi kwenye mgongo; hizi ni dalili za hatari.

 

Maumivu huja takriban dakika 30-120 baada ya kula au katikati ya usiku tumbo linapokuwa tupu. Katika muda huu, juisi ya asidi ya tumbo ni rahisi zaidi kuchoma miishilio ya neva isiyo na kinga. Mara nyingi, maumivu huisha baada ya kula au kunywa kitu au kutumia kizima asidi ili kuzimua asidi ya tumbo.

 

Hata hivyo, dalili zinaweza kutofautiana kutokana na mahala kidonda kilipo, uwepo wa matatizo mengine na pia kutokana na umri wa mtu. Kwa mfano, wagonjwa wa kisukari, watoto na wazee wanaweza wasiwe na dalili kabisa. Kwa watu kama hawa, vidonda hutambuliwa pale matatizo makubwa yanapotokea. Pia hata watu ambao vidonda vyao vilivyosababishwa na NSAIDs wanaweza kuchukua muda mrefu dalili zao kujitokeza.

 

Pia, dalili za vidonda vya tumbo vya duodeni na vile vya ndani ya tumbo hufanana, isipokuwa tofauti ni wakati ambao maumivu hutokea (hili tutalieleza hivi punde). Maumivu ya vidonda vya duodeni huweza kutokea saa kadhaa baada ya kula chakula (yaani tumbo linapokuwa tupu). Na huweza kupata nafuu (improvement) baada ya kula. Maumivu pia yanaweza kukuamsha mara kwa mara katikati ya usiku.

 

Maumivu ya vidonda vya tumbo (gastric ulcers) hutokea muda mfupi tu baada ya kula (wakati ambao chakula bado kiko tumboni).

Maumivu ya tumbo husababishwa na nini?

Husababishwa na kidonda na kuzidishwa na asidi ya tumboni inayokuja kukutana na kidonda. Maumivu pia yanaweza kusababishwa na kujengeka kwa gesi na kufunga choo.  Licha ya kuwa maumivu ya tumbo ni dalili ya kwanza, maumivu mengi ya tumbo si makali sana. Hata hivyo, vidonda vya tumbo hutofautiana na vidonda vya duodeni (duodenal ulcer). Hapa tutazame kidogo tofauti zao:

 

Vidonda vya duodeni: Vidonda vya duodeni vinaweza kusababisha maumivu, mchomo, maumivu kama ya njaa katika sehemu ya juu ya fumbatio, chini kidogo ya mfupa wa kidari (breastbone).

 

Maumivu yana kawaida ya kutokea au kuwa makali zaidi pale tumbo linapokuwa halina chakula, mara nyingi saa mbili mpaka saa tano baada ya kula.  Tabia nyingine ya dalili ya vidonda vya duodeni ni maumivu ambayo huweza kutokea wakati wa katikati usiku, wakati ambao utemaji wa asidi na uzalishaji huenea zaidi sehemu yote.

 

Pia, vidonda vya duodeni vina tabia ya kutoweka kwa majuma au hata miezi bila sababu ya kueleweka. Takriban nusu ya watu wenye vidonda vya duodeni wana aina moja za kusumbuliwa, kuchoma, kuuma, kujihisi njaa. Maumivu ni makali kidogo, au makali kiasi.

 

Kwa watu wenye aina hii ya vidonda, mara nyingi maumivu hayapo wakati wa kuamka lakini hutokea wakati wa asubuhi ya katikati. Kunywa maziwa au kula chakula (vitu ambavyo huzuia asidi ya tumbo) au kutumia dawa za kuzima asidi (antacids) hupunguza maumivu, lakini maumivu hayo yana tabia ya kurudi baadaye ndani ya saa 2 au 3.

 

Vidonda vya tumbo: Dalili za vidonda vilivyo katika mfuko wa chakula, marginal na stress, tofauti na zile za utumbo hazifuati mtindo wowote. Maumivu kutoka katika vidonda hivi yana kawaida ya kutokea mara tu baada ya kula.

 

Maumivu ya vidonda hivi pia yana kawaida ya kutokubali kwa ufanisi mzuri vizima asidi na baadhi ya dawa. Kula hakusaidii kuondoa maumivu ila huyaongeza.  Tofauti na vidonda vya duodeni, maumivu ya vidonda vya tumbo hayaishi mara yanapoanza.

 

Kipengele kingine kinacholeta tofauti ni kwamba wakati katika vidonda vya tumbo, maumivu huongezeka haraka baada ya mlo, katika vidonda vya duodeni inaweza kuchukua saa 2-3.

 

Mtu anaweza kuuliza; “Kwa nini kuna maumivu kufuatia chakula?” Hii hutokana na uchocheaji wa utemaji wa asidi inayotiririka kwenye kidonda na kuchochea kipokezi cha maumivu. Katika vidonda vya duodeni, huchukua takriban saa mbili 2-3 asidi kufika katika eneo la kidonda.

 

Itaendelea


By Jamhuri