KONA YA AFYA

Vidonda vya tumbo na hatari zake (11)

Katika sehemu ya kumi, Dk. Khamis Zephania alifafanua maumivu ya vidonda vya tumbo, tofauti ya vidonda hivyo na vile vya duodeni, sababu za kutosagika kwa chakula na mtu kupungua uzito. Sasa endelea…

Tumbo kujaa gesi: Vidonda vya tumbo huweza kusababisha gesi. Tumbo kufura ni moja ya dalili kubwa za vidonda vya tumbo, na kufura kuna uhusiano mkubwa na gesi nyingi iliyozidi tumboni.

 

Kuna uhusiano gani kati ya gesi na vidonda vya tumbo? Vidonda vya tumbo hutokea kwa sababu asidi ambayo huzalishwa na tumbo haina uwezo wa kuvunjavunja chakula ambacho kipo tayari tumboni, na hivyo asidi hiyo hudhuru kuta za tumbo wakati inapokuwa inazunguka.

 

Hali hii husababisha tundu kutokea katika kuta hizi na hivyo kuzidi kuzuia usagaji wa chakula ambacho kimeingizwa ndani ya mwili. Matokeo ya chakula hiki ambacho hakikusagwa ni kuhisi gesi ghafla kutoka nje mdomoni katika hali ya kubeua.

 

Hapa tuingie ndani kidogo juu ya gesi kwa sababu watu wengi wana gesi na wamekuwa hawajui chochote juu ya tatizo hili.

 

Kila mtu ana gesi tumboni na huiondoa kwa kupiga mbweu au kutoa upepo kupitia rektamu.  Hata hivyo, watu wengi wanadhani wana gesi nyingi ilhali kwa ukweli wana kiwango cha kawaida. Watu wengi huzalisha takriban painti 1 hadi 3 za gesi kwa siku  na kutoa gesi takriban mara 14 kwa siku.

 

Gesi hutengenezwa kwa mvuke usio na harufu, carbon dioxide, oksijen, naitrojeni, haidrojeni na wakati mwingine methani (methane). Harufu mbaya ya gesi (kujamba) hutokana na bakteria ndani ya utumbo mkubwa ambaye hutoa kiwango kidogo cha gesi yenye sulphur.

 

Ingawa kuwa na gesi ni hali ya kawaida, hata hivyo inaweza kuleta usumbufu na kukosesha raha. Kufahamu sababu, njia za kuondosha dalili na matibabu husaidia kuleta nafuu.

 

Nini husababisha gesi?

Gesi katika viungo vya njia ya mmeng’enyo wa chakula (ambavyo ni umio, tumbo, utumbo mdogo na utumbo mkubwa) hutokana na vyanzo viwili: Kumeza hewa, kuvunjwavunjwa vyakula ambavyo havikumeng’enywa.

 

Kumeza hewa: Kumeza hewa (gerophagia) ni sababu kubwa ya gesi tumboni. Kila mtu humeza kiwango kidogo cha hewa wakati anapokuwa anakula na kunywa.

 

Hata hivyo, kula au kunywa kwa haraka, kutafuna jojo, kuvuta sigara au kuvaa meno bandia yaliyolegea huweza kusababisha baadhi ya watu kuingiza hewa zaidi tumboni. Kupiga mbweu na kuteuka ni njia ambayo hewa iliyomezwa huondolewa tumboni.

 

Gesi inayobaki huingia ndani ya utumbo mdogo na kusharabiwa (kufyonzwa). Kiwango kidogo husafiri na kuingia katika utumbo mkubwa kwa ajili ya kutoka kupitia haja kubwa.

 

Tumbo pia hutoa carbon dioxide pindi asidi ya tumbo na bicarbonate vinapochanganyika, lakini sehemu kubwa ya gesi hii husharabiwa katika mikondo ya damu na hivyo haiingii katika utumbo mkubwa.

 

Vyakula visivyomeng’enywa: Hii ni hali ambayo mwili unakuwa hausagi na kufyonza baadhi ya kabohaidreti, sukari, wanga, nyuzinyuzi zilizo kwenye vyakula vingi ndani ya utumbo mdogo kwa sababu ya ukosefu wa baadhi ya vimeng’enya.

 

Baadaye vyakula hivi ambavyo havikumeng’enywa hutoka ndani ya utumbo mdogo na kuingia katika utumbo mkubwa, mahala ambapo bakteria wasio na madhara husaga chakula, wakizalisha haidrojeni, na carbon dioxide.

 

Takriban theluthi moja ya watu wote huzalisha methane. Kisha gesi hizi hutoka kupitia rektamu. Mtu ambaye hutoa methane atatoa choo ambacho huelea ndani ya maji.

 

Tafiti hazijatambua ni kwa nini watu wengine hutoa methane na wengine hawatoi. Vyakula vinavyosababisha gesi kwa mtu mmoja vinaweza visisababishe gesi kwa mtu mwingine. Sehemu kubwa ya vyakula vyenye kabohaidreti vinaweza kusababisha gesi; vyakula vyenye mafuta na protini husababisha gesi kidogo.

 

Hivi ni vyakula ambavyo husababisha gesi tumboni: Sukari; sukari zinazosababisha gesi ni raffinosa, lactose, fructose na sorbitel. Raffinose: Maharage yana kiwango kikubwa cha sukari changamano (complex sugar) hii. Kiwango kidogo hupatikana katika kabichi, brokoli, asparagasi na baadhi ya mboga za majani na nafaka zisizokobolewa.

Itaendelea