Jinsi kitambi kinavyoathiri nguvu za kiume, afya

Unajitazama katika kioo, lakini unachukizwa! Unachukizwa na mwili wako mwenyewe. Huna la kufanya, unabaki kuhuzunika tu.

 

Tumbo! Tumbo!

Naam, tumbo lako linaonekana kutuna na kutengeneza mkunjo. Linaonekana linaweza kuchukua muda mrefu katika hali hiyo, inaweza kuwa miezi au miaka; au linaweza lisiishe kabisa!

 

Licha ya kuwa tumbo kubwa linaweza kuufanya mwili kuwa na mwonekano mbaya usiopendeza, kwa hakika madhara yake kiafya ni makubwa zaidi kuliko ubaya wa sura yenyewe.

 

Katika lugha yetu ya Kiswahili, mafuta ya tumboni hujulikana kama “kitambi.” Majina yanayotumika mitaani kukiita kitambi ni pamoja na tumbo la mtungi, kishikio cha mapenzi, tairi la akiba, tumbo la bia, friji, nakadhalika.

 

Kwanini watu walipachika majina kama hayo?

Katika miongo michache ya nyuma hapa Tanzania na kwingineko duniani, kwa kutoelewa, baadhi ya watu walivitazama vitambi kama dalili ya ustawi mzuri wa maisha, na ndiyo sababu ya kuvipachika majina ya ziada.

 

Katika miaka ya hivi karibuni, watu wengi wametambua kitambi ni tatizo kubwa la kiafya. Utawaona wako katika kumbi za michezo ya mazoezi ya viungo (gym), wengine wakiwa katika utaratibu maalumu wa chakula (dieting); na wengine wakiwa katika programu za tiba kupunguza mafuta mwilini, na ikiwezekana kuyaondoa yote. Hata hivyo, wapo baadhi ya watu bado wanafanya utani na mafuta!

 

Ukweli wa mambo ni kwamba kitambi hakina utani! Ukileta utani katika mafuta ya tumboni, basi muda si mrefu utagonga hodi katika chumba cha daktari ukiwa tayari na kisukari (TYPE 2), au ugonjwa wa moyo, au kupooza, au saratani, au shinikizo la damu la kupanda (High Blood Pressure), au matatizo ya kibofunyongo, au ugonjwa wa ini (cirrhosis), huku kuishiwa nguvu za kiume ikiwa ni jambo linalokwenda bega kwa bega na kitambi.

 

Je, hapo utaendelea kufanya utani na kitambi? Bado utaita tumbo la bia? Au majina kadha wa kadha? Hakika utakiita ni tumbo la kifo!

 

Hayo si mafuta mazuri kabisa, wala ya kutania na kuyachekea! Ukiyafungulia mlango na kuyaruhusu yaweke maskani tumboni mwako, ni sawa na kuruhusu nyoka kukaa chumbani kwako. Hatima yake ni nini? Bila shaka ni kukung’ata! Kama zisipofanyika juhudi za haraka kuidhibiti sumu ya nyoka huyo, basi matokeo yaweza kuwa kifo! Kitambi pia ni vivyo hivyo.

 

Mafuta mengi yanapokuwa mwilini huleta tatizo. Lakini mafuta haya ya tumboni yana hatari kubwa zaidi hata kama ni madogo. Baadhi ya watu, kwa kutojua madhara ya vitambi, huchukulia mambo kwa wepesi, husema, “Tumbo langu ni dogo tu, ni kama halipo vile.” Kwa mtazamo wao, ni kwamba wanaweza kunusurika na madhara ya kitambi.

 

Ni kweli kwamba watu wanatofautiana ukubwa wa matumbo. Kuna ambao matumbo yao ni madogo, au ndiyo yanaanza. Kuna wengine ni makubwa kiasi, na wengine makubwa zaidi kiasi ambacho huwafanya kupata taabu katika kufanya kazi mbalimbali.

 

Lakini, ukweli wa mambo ni kwamba mafuta ya tumboni yanaweza kukuletea maradhi, hata kama huna uzito mkubwa au huna tumbo kubwa.

 

Kwa nini mafuta ya tumboni yalete maradhi? Yana uhusiano gani na maradhi? Kwa nini yapunguze nguvu za kiume? Haya ni baadhi ya maswali ambayo yanaweza kugonga katika akili ya msomaji.

 

Ukweli ni kwamba tumbo kubwa ni matokeo ya mafuta mengi mno yaliyoweka makazi yake tumboni au fumbatio (abdomen); kitabibu yanajulikana kama, “visceral fat.” Mafuta hayo huzonga na kudhuru figo, ini na viungo vingine tumboni na kuharibu utendaji kazi wa viungo hivyo, na kuvuruga utendaji wa homoni.

 

Ni mafuta ambayo huleta madhara makubwa katika mishipa yako ya damu. Seli za mafuta hayo huzalisha homoni na sumu ambazo huathiri afya na tabia yako.

 

Lakini, kabla hatujaenda kuangazia kwa undani uhusiano wa kitambi na magonjwa mbalimbali ukiwamo upungufu wa nguvu za kiume, ambao ndiyo kilio cha wanaume wengi wenye vitambi, kwanza ni muhimu tufafanue kwa ufupi aina za mafuta yaliyo tumboni.

 

Tumboni kuna mafuta ya aina mbili. Kwanza ni mafuta yanayotokea chini ya ngozi ya tumbo. Haya unaweza kuyagusa kwa nje kwa kufinya ngozi ya tumbo. Mafuta haya hayana madhara yoyote na yana msaada mkubwa kwa viungo vilivyo ndani ya tumbo, hukaa kama mto (cushion) kwa viungo kujiegemeza. Kitabibu mafuta haya huitwa “Subcutaneous fat.”

 

Aina ya pili ya mafuta, ni mafuta ambayo kitabibu huitwa “Visceral fat.” Haya hukaa ndani kabisa ya tumbo, hujitengenezea makazi yake karibu kabisa na ini na viungo vingine tumboni. Mafuta haya ndiyo tatizo na chanzo cha matatizo mengi ya kiafya katika mwili wako, na ndiyo mafuta tunayokwenda kujadili madhara yake katika makala haya, sababu ya kutokea kwake na ufumbuzi wake.

 

Kisukari

Moja ya madhara ya kitambi ni kwamba huweza kumsababishia mtu ugonjwa wa kisukari kwa urahisi zaidi. Kwa sababu mafuta ya kitambi kwa ujumla huzonga viungo ambavyo husaidia kurekebisha sukari ndani ya damu.

 

Wakati insulini inapolielekeza ini kuhifadhi sukari ya akiba kwa ajili ya nishati ya baadaye, ini lililozongwa ndani tishu za mafuta hushindwa kuitikia ipasavyo. Matokeo yake, sukari huweza kuanza kujazana ndani ya mishipa ya damu na hivyo kuleta madhara makubwa katika viungo na kukaribisha ugonjwa wa kisukari.

 

Hali hiyo kitabibu huitwa “insulin resistance” ambapo seli za mwili hugoma kukubali homoni ya insulini. Insulini ni homoni ambayo hutolewa na seli za kongosho zijulikanazo kama ‘beta cells.’ Hizi seli hutawanyika katika kongosho lote katika vishada vidogo vidogo vinavyojulikana kama visiwa (islets) vya Longerhans. Kazi kubwa za insulini huelekezwa kwenye umetaboli wa usimamizi wa kabohaidreti (sukari) na wanga, mafuta na protini.

 

Insulini pia hurekebisha kazi za seli za mwili, ikiwa ni pamoja na ukuaji. Insulini ni muhimu sana kwa matumizi ya mwili kama nguvu. “Insulin resistance” ni hali ambayo seli za mwili hugoma kukubaliana na insulini. Hii inaweza kuwa ni hali ya kawaida kama kiwango cha insulini kimepunguzwa. Matokeo yake viwango vikubwa vya insulini huhitajika ili insulini kufanya kazi yake vizuri.

 

Hivyo, kongosho hufidia kwa kujaribu kutoa insulini zaidi. Mgomo huu hutokea katika mwili kuitikia insulini yake yenyewe (endogenous) au pindi insulini inapokuwa inaingizwa kwa sindano (exogenous).

 

Katika “insulin resistance” kongosho hutoa insulini zaidi na zaidi hadi kufikia wakati sasa haliwezi tena kutoa insulini ya kutosha kwa ajili ya mahitaji ya mwili, hivyo sukari ndani ya damu hupanda.

 

Mshtuko wa moyo

Kitambi kina urafiki mkubwa na ugonjwa wa moyo. Pindi unapokula chakula, kiwango chako cha insulini ndani ya damu hupanda. Kadiri sukari inavyopanda, ndivyo pia insulini nyingi inavyotolewa na kongosho ili kuendelea kuifanya sukari isipande juu zaidi.

 

Mara tu baada ya insulini kufanya kazi yake ya kushushua viwango vilivyopanda vya sukari, ini huondoa insulini kutoka ndani ya damu. Hata hivyo, mafuta yaliyo ndani ya mikondo ya ini, huzuia na kukinza seli za ini kuondoa insulini kutoka katika mikondo ya damu.

 

Kwa hali hiyo, watu ambao hutunza mafuta mengi tumboni, wajue pia hutunza mafuta mengi katika maini yao, hali ambayo mafuta hayo huzuia ini kuondoa insulini ndani ya damu na hivyo kusababisha kiwango kikubwa cha insulini.

 

Ni kwamba unahitaji insulini kuzuia viwango vya sukari ndani ya damu kupanda juu, lakini insulini nyingi hubana mishipa ya ateri na kusababisha mshtuko wa moyo.

 

Vyakula vya mafuta na ukosefu wa mazoezi husababisha ongezeko la uzito. Hali hii huzifanya njia katika mishipa ya damu kuwa myembamba zaidi na kukakamaa, matatizo ambayo hujulikana kitaalamu kama  ‘atherosclerosis au arterioscloris.’ Huu ni mchakato wa kunenepa na kukamaa kwa kuta za ateri kubwa na ateri za ukubwa wa kati.

 

“Arterioscloris” ni hali ambayo husababisha kutokea kwa maradhi ya ateri za moyo (coronary artery), ikipelekea kwenye ugonjwa wa moyo unaosababisha maumivu kifuani (angina) na mshtuko wa moyo, kupooza, na maradhi ya mishipa ya damu. Hii hutokana na lehemu (cholesterol) na baadhi ya vitu kujijenga katika kuta za mishipa ya damu.

 

Kama ujenzi huo wa lehemu utatokea katika mishipa mikubwa ya ateri karibu na moyo itasababisha mshtuko wa moyo, na kama itatokea katika mishipa midogo ya damu inayokwenda kwenye uume, kama tutakavyoeleza baadaye, itasababisha kushindwa kusimama kwa uume. Hali hii ya kushindwa kusimama kwa uume, kitabibu ni dalili ya tahadhari ya awali ya matatizo ya moyo.

 

Vipengele vinavyoweza kusababisha “arterioscloris” ni pamoja na “insulini resistance,” lehemu mbaya (LDL), shinikizo la damu la kupanda (HBP), uvutaji sigara, na kisukari.

 

Mshtuko wa moyo mara nyingi hutokea pindi damu inapoganda na hivyo kuziba mtiririko wa damu kupitia ateri ya moyo (coronary artery). Huu ni mshipa wa damu unaojaza damu inayokwenda sehemu za misuli ya moyo. Mtiririko wa damu ulioingiliwa unaweza kudhuru au kuharibu misuli ya moyo.

 

Mshtuko wa moyo pia huitwa ‘myocardial infarction.’ Ni ugonjwa ambao mtu anaweza kujikuta katika hatari kubwa. Hii ni kwa sababu mara nyingi watu huchanganya dalili zake kwa kuziona ni za ugonjwa mdogo na hivyo kuchelewa kupata matibabu.

 

Watu wenye vitambi wako katika hatari kubwa ya kupata matatizo ya moyo kuliko watu ambao hawana vitambi.

 

Simu: 0766 431675, 0656 620725


 

1517 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!