Msanii Rajab Abdul Kahali, maarufu kwa jina la ‘Harmonize, hatimaye ameandika rasmi kwa kundi la Wasafi Classic Baby (WCB) akitaka kuvunja mkataba wake na kuanza maisha mengine nje ya lebo hiyo.

Akizungumza na runinga ya Wasafi, Ofisa Mtendaji Mkuu wa WCB, Sallam SK (alias Mendez) amesema msanii huyo ameandika rasmi kwa kundi hilo akisema anataka kujiondoa.

Sallam amesema kwamba kwa sasa moyo wa msanii huyo haupo tena na WCB na ameitisha mkutano na usimamizi wa WCB katika harakati yake ya kukubaliana na hatua hiyo.

“Harmonize kwa sasa moyo wake haupo WCB, kimkataba bado yupo. Kwa nini ninasema hivyo? Harmonize ameshatuma barua ya maombi ya kuvunja mkataba na yuko tayari kupitia vipengele vyote vya sheria kusitisha mkataba wake na ni kitu ambacho tumependezwa nacho. Yeye mwenyewe ameridhia na ameomba kikao na uongozi,” amesema Sallam.

Amesema msanii huyo wa wimbo ‘My Boo’ bado yumo katika mkataba wa WCB na kusisitiza kwamba ingekuwa heri iwapo Harmonize angetoka bila kuzua balaa.

“Sisi kama taasisi tuko radhi kwa kile ambacho ataamua, hatuwezi kupinga chochote. Akiamua kufuata maelezo hayo ana baraka asilimia 100 za Wasafi na akitaka kushirikiana na Wasafi wakati wowote tuko wazi. Unajua unapoondoka kwa mazingira mazuri inasaidia uhusiano,” amenukuliwa Sallam.

Kwa mujibu wa Sallam, tangazo hilo kwamba Harmonize amejiondoa rasmi WCB litatangazwa rasmi baada ya mchakato wote huo kufuatwa na kukamilishwa.

Sallam amesema katika tamasha la Wasafi lililofanyika mjini Mwanza, Harmonize alitumia usafiri binafsi kufanya baadhi ya mambo yaliyotoa tafsiri kwamba amejitenga.

“Hata hivyo tumependezwa na hatua yake kwa sababu labda kuna vitu ameona akivifanya atafika mbali,” amesema Sallam.

Maudhui ya Wasafi festival ni umoja, msanii akiamua kuacha kuambatana na wasanii wenzake ambao wapo katika tamasha ni kwenda kinyume.

Meneja huyo amewaomba radhi wasanii wote walioshiriki tamasha la Mwanza kutokana na Harmonize kufanya jambo hilo na kwamba uongozi wa Wasafi haukuwa na taarifa.

806 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!