hussein-sharrif-Casillas + Ngasa

 

Kocha Mkuu wa Simba ya Dar es Salaam, Goran Kopunovic, amekaa na kipa wa timu hiyo, Hussein Sharrif 'Casillas', na kumwambia hana budi kukaza msuli ili aanze kukaa golini kulinda lango kama zamani.
  “Ndiyo, nimekaa naye na kumweleza Casillas ajitahidi,” anasema Kopunovic alipozungumza na mwandishi wa habari hizi mwishoni mwa wiki iliyopita. Amesema kwamba kipa huyo ana nafasi bado.


  “Kujituma ndiyo mbinu pekee itakayomfanya Casillas acheze kikosi cha kwanza, kwani kinyume na hapo hataweza kupata nafasi, maana wenzake wanajitahidi,” anasema kocha huyo akizungumzia makipa wengine ambao ni Ivo Mapunda, Manyika Peter, Denis Richard.  
  Kocha huyo anasema juhudi za Casillas lazima zitekelezwe sasa kwa kuwa zimebaki mechi chache kabla ya pazia la msimu wa Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL) halijafungwa. Ligi Kuu Tanzania Bara inatarajiwa kufikia tamati Mei, mwaka huu.
 
 Katika taarifa nyingine kuhusu wachezaji mahiri nchini, uongozi wa Yanga umefuta mipango ya nyota wake, Mrisho Ngassa, aliyetangaza kuitema timu hiyo mwishoni mwa msimu huu. Wamesema katu hawana mpango wa kumtema.
  Mwishoni kwa wiki iliyopita, Ngassa alinukuliwa akisema kuwa huu ndiyo msimu wake wa mwisho kuichezea timu hiyo ya Jangwani na kusema kuwa anatamani kwenda kucheza katika timu za Afrika Kusini, DR Congo na Qatar.
 
 Hali imekuwa tofauti kwa Yanga baada ya Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Yanga, Jerry Muro kusema kuwa Yanga bado ina mpango wa kukaa chini na Ngassa kujadili kumuongezea mkataba.
  “Msione tupo kimya licha ya Ngassa kutamka vitu vingi, bado tuna mpango wa kukaa naye meza moja ili kujadili mkataba mpya na hatujakata tamaa ya kumbakiza kwa kauli alizotoa za kutaka kuondoka, lengo letu tuwe naye kwani ana mchango mkubwa kwenye timu,” anasema Muro.
  Mkataba kati ya Ngassa na Yanga unaisha mwisho wa msimu huu wa Ligi Kuu Bara, lakini amekuwa hana furaha na klabu hiyo kutokana na deni la Sh milioni 45 analodaiwa na benki moja alikokopa kulipa deni alilokuwa anadaiwa na Simba.

2417 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!