2-+mulongo+(kulia)+mwambeneMahakama Kuu Kanda ya Mwanza kitengo cha Ardhi imetoa uamuzi wa kubomolewa jengo la biashara lililopo mbele ya kiwanja Na 14 kitalu E Nyegezi kilichopo maeneo ya Mkolani eneo ambalo limetengwa na Halmashauri ya Jiji la Mwanza kwa ajili ya ujenzi wa viwanda katika barabara kuu itokayo jijini kuelekea Shinyanga ili kupisha ujenzi wa kituo cha mafuta.


Katika rufaa hiyo ambayo ilipewa Namba 66 ya Mwaka 2014, ilitokana na mwomba rufaa, Johas Faustine dhidi ya Cerdic Lema aliyedai mbele ya mahakama hiyo ya kutaka jengo lake la biashara lililoko kiwanja Nambari 14 kitalu E Nyegezi lisibomolewe ili kupisha ujenzi wa kituo cha mafuta.


Faustine anayetetewa na Wakili Shirima, alidai analimiliki kihalali ardhi ambayo alijenga jengo hilo sababu ambayo ilipingwa na Wakili Anthony Nasimire, kutoka kampuni ya Nasimire & Company Advocates kwamba mwomba rufaa hakuweza kuwasilisha vielelezo vyovyote muhimu vinavyoonyesha kuwa kiwanja hicho ni mali yake na kuiomba mahakama kubomoa jengo hilo ambalo limejengwa kinyume na taratibu za mipango miji.


Katika uamuzi wake, Jaji A.N. Sumari alitoa amri ya kuvunjwa jengo hilo ili kupisha njia ya uwazi ambayo Lema ataitumia baada ya ujenzi wa kituo cha mafuta kukamilika.
Kadhalika baada ya uamuzi huo, Faustine mara moja alipelekea malalamiko yake kwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo ili kunusuru jengo lake lisibomolewe ili kupisha ujenzi wa kituo cha mafuta.


Akizungumza na baadhi ya wananchi kuhusiana na sakata hilo RC Mulongo anasema kuwa jengo hilo haliwezi kubomolewa kwa amri ya mahakama na kumuagiza Ofisa Mtendaji wa Kata ya Mkolani kutoidhinisha barua zozote ambazo zitatoka mahakamani kwa ajili ya kutekeleza amri hiyo.
Anasema kuwa suala hilo ataweza kulishughulikia ili muafaka upatikane na kusema kuwa litakuwa limepatiwa ufumbuzi ndani ya wiki mbili kuanzia Aprili 18 mwaka huu kauli ambayo ilipingwa na mjibu rufaa Lema ambaye alidai kuwa hakutendewa haki kwa madai kuwa hakuna kiongozi ambaye yuko juu ya sheria.


Naye Wakili Nasimire kutoka Kampuni ya Nasimire & Company ya jijini Mwanza, wakati akiongea na gazeti hili kwa njia ya simu, anasema kuwa uamuzi wa mahakama uko pale pale na kwamba jengo hilo litaweza kubomolewa wakati wowote kuanzia sasa kwa madai kuwa hiyo ni amri ya mahakama na siyo ya mlalamikiwa.


Awali, jengo hilo wakati likianza kujengwa, uongozi wa jiji la Mwanza kupitia barua yenye kumb. Na MCC/E60/615/11/32/TPB ya Aprili, 2013 iliyosainiwa na Thobias Bujiku kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, ulimwandikia Faustine ya kusitisha ujenzi huo lakini alikaidi amri hiyo.
Kipengele cha barua hiyo kinasema, “Kwa mujibu wa kifungu cha 124 cha kanuni za Serikali za Mitaa (Local Government Urban Authorities Development Control) iliyotangazwa kwenye Gazeti la Serikali Na 242 ya mwaka 2008, uendelezaji wowote katika maeneo yaliyopangwa au kupimwa unapaswa kuwa na vibali vya halmashauri.”


Ukaguzi uliofanyika Aprili, 12, 2013 umebaini kwamba umejenga katika eneo lililopimwa bila kuwa na vibali vya ujenzi (Building Permit). Hivyo basi, kwa mujibu wa sheria tajwa hapo juu, ujenzi katika eneo hilo umefanywa kinyume cha sheria na ujenzi huo umefanyika katika eneo la hifadhi ya barabara,” kimeeleza kipengele cha barua hiyo.


Pia barua ya Katibu Mkuu, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Patrick Rutabanzibwa, katika barua yake yenye Kumb. Na CA.205/329/01.C/108 ya Agosti 6, 2013 alimwandikia Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza na kumwelekeza jengo hilo kuvunjwa kutokana na kujengwa katika hifadhi ya barabara jambo ambalo halikutekelezwa.


“Wizara itafurahi kupata taarifa ya kubomolewa kwa jengo lililotajwa mapema iwezekanavyo na maelezo kuhusu sababu za kuchelewa kumchukulia hatua mwendelezaji haramu wa jengo hilo, ambaye aliandikiwa notisi ya Aprili 17, 2013,” inaeleza sehemu ya barua hiyo.
Anasema kwamba kuchelewa kuchukua hatua kunaendelea kusababisha hasara kwa pande zote, yaani Halmashauri, wananchi wa jiji wanaotii sheria na taifa kwa ujumla.

By Jamhuri