Watanzania naona tu wasahaulifu kwa kiwango fulani. Hii tabia inaturudisha nyuma kimaendeleo, maana kila tunapopiga hatua ya kuimarisha Muungano wetu basi kwa ule usahaulifu uliopo tunajikuta tunavutwa kuangukia nyuma hatua kadhaa. Tunabaki tunalumbana na kuchokonoa hili au lile kuhusu Muungano.

 Ninakumbuka tarehe 22 Septemba 1975 tukiwa pale ndani ya ukumbi wa Diamond, kwenye Mkutano Mkuu wa 17 wa Chama cha TANU yaliamuliwa mambo ya kistoria kweli. Katika mkutano ule, Mwalimu alipendekezwa na Chama chake TANU awe mgombea Urais ndipo wakati Mwalimu akipokea uteuzi ule alitoa wazo la kuunganisha vyama vyetu vya siasa  Chama cha TANU na Chama cha ASP.

 Katika kikao kile Mwalimu, alisema haya “….nchi nyingi duniani huwa haziruhusu mtu yule yule kuendelea kuchaguliwa kuwa Rais wa nchi zaidi ya kipindi kimoja au viwili. Kuna hasara nyingi za utaratibu huu hasa kwa nchi kama zetu. Zipo pia nchi ambazo huchagua mtu mmoja kuwa Rais kwa kipindi chote cha maisha yake kama Sultan. Utaratibu huo nao una faida na hasara zake”. Mwalimu akaendelea kusema, “Katiba yetu hairuhusu mtu mmoja achaguliwe kuwa Rais kwa kipindi chote cha maisha lakini inaruhusu mtu huyo huyo aendelee kuchaguliwa kipindi hata kipindi bila ya kuweka kikomo”. (Hotuba ya Mwl. Nyerere Diamond tarehe 22/09/77).

 Pale tulikumbushwa tu kuwa siyo utaratibu mzuri kuchagua kiongozi yule yule mara kwa mara na akatoa sababu za kuridhisha kabisa kuwa ni kweli kwamba wamekuwepo viongozi wenye uwezo mkubwa na vipawa ambao wameendelea kuongoza nchi zao. Hawa basi wameendelea kuchaguliwa kipindi hadi kipindi siyo kwa sababu ya uwezo wao tena ila kwa sababu ya uongozi wao mzuri wa huko nyuma na kwa sababu watu wanaogopa mabadiliko.

 Hapo ndipo Mwalimu aliposema “mabadiliko lazima yaje, maana kiongozi aliyechaguliwa kwa maisha hatima yake atakwenda (mimi naongeza – atatoweka duniani/atakufa) maana uhai una mwisho”.

 Najiuliza viongozi wangapi barani Afrika wanakumbuka hilo la kuwa maisha yana mwisho? Ni viongozi wangapi nchini Tanzania wanakumbuka hilo hata wakabaki wanang’ang’ania uongozi wa kudumu katika vyama vyao vya siasa au katika NGO zile walizozianzisha kwa kisingizo cha hakuna au haonekani mwingine wa kuweza kufanya hayo ayafanyayo?

 Huo ni usahaulifu na unatupata sisi viongozi wote tuwapo katika nyadhifa mbalimbali katika vyama au Serikali. Ni dhana potofu kuwa bila ya “mimi”, hiki au kile hakitafanyika. Je, Mungu atakapokuita nani atachukuwa mahali pako na kufanya hayo unayofikiria wengine hawawezi kuyafanya? Huko ni kujifikiria zaidi kuliko kulifikiria Taifa. Ni kujidanganya tu maana duniani hakuna anayeweza kuitwa “INDISPENSABLE” wa lazima kabisa.

 Kikao kile cha pamoja cha viongozi wa TANU na AFRO kilikuwa cha vyama viwili kwa mujibu wa Katiba ya nchi yetu, inasema wazi, “Nchi yetu ni ya Chama kimoja, na Katiba yetu ni ya Chama kimoja (Katiba ya muda ile ya 1965). Hapa Katiba ile ilizungumzia kuwa ni nchi ya Chama kimoja wakati vilikuwepo vyama viwili (kimoja TANU kwa sehemu moja ya Jamhuri na kingine ASP kwa sehemu nyingine ya Jamhuri) Mwalimu alikosoa DOSARI ile kuwa haikuwa ndogo.

 Kuanzia hapo Mwalimu alileta wazo kuwa sasa umefika wakati wa kufikiria jinsi ya kuondoa dosari ile. Hapa inafaa ninukuu maneno halisi ya Mwalimu; alisema, “mimi naamini kabisa kwamba tutaisaidia nchi yetu kuimarisha umoja wake na mapinduzi yake na hivyo kuwa na uwezo mkubwa na kusaidiana kuleta umoja na mapinduzi ya Afrika ikiwa bila kusita tena tutaviunganisha vyama vyetu na kuwa na chama kimoja cha mapinduzi”.

 “Nina hakika kwamba pamoja na mengineyo pia na kwa sababu ya yote hayo niliyosema wakati umefika vyama vyetu vifikirie kutoweka na badala yake tuwe na chama kimoja kipya cha kujenga Tanzania mpya. Tulikuwa na Tanganyika na Zanzibar sasa tunayo TANZANIA” (KUZALIWA KWA CCM  na Ali A Mohamed uk. 14 ibara ya kwanza).

 Mwalimu alihitimisha kwa kusema kwamba tukipenda, kama walivyopenda wenzetu kwa wakati wao, vyama vyetu viwili vinaweza kuungana vikazaa chama kimoja cha mapinduzi kiongoze nchi moja ya Mapinduzi.

 Siyo wengi wa wasomaji wa makala hii wanalijua hili, maana 1975 pengine walikuwa hawajazaliwa au walikuwa katika shule za msingi, kwa hali hiyo wasingaliweza kujua namna TANU na AFRO vyama vilivyoleta Uhuru (Bara) na Mapinduzi (Zanzibar) vilivyokuja kuungana na ikatokea CCM inayotawala hivi sasa.

 Baadhi ya wanasiasa wetu leo hii wanauliza Bungeni – “ziko wapi hati za Muungano? Ziletwe Bungeni tuzione”. Wanadai wananchi hawakushirikishwa, ndiyo maana Muungano huu una mapungufu mengi na hivyo unalalamikiwa. Wenyewe wanaita mapungufu hayo kama “kero  za Muungano”. Kwa usahaulifu wa kile wazee wetu walikuwa wanakitenda nianzie pale vyama vilipoungana. Je, wananchi walishirikishwa? Waliridhia?

 Ndiyo maana nimeanza kwenye ule Mkutano Mkuu wa 17 wa TANU Septemba 22, mwaka ule wa 1975 na mkutano ule ulihitimishwa tarehe 31 Septemba mwaka 1975.

 Mkutano ule ndio ulitoa kama moja ya maazimio yake lile Azimio la kuunganisha vyama vya TANU na ASP na kuwa na chama kimoja kipya cha Mapinduzi ili kiweze kuongoza Taifa hili la Tanzania.

 Wenyeviti wa vyama vya TANU na ASP walichukuwa hatua za busara na sahihi kuwaelewesha wanachama wao juu ya hilo Azimio la Kuunganisha Vyama. Nakumbuka Mwalimu kwa upande wa TANU alitamka hivi, “kama hatuaminiani mpaka sasa basi labda wafufuke Mitume ndiyo watufanye tuamini”. Hii inamaanisha kuwa wananchi wamefikia hatua ya ukomavu wa kisiasa na walikuwa na hali sasa ya kuaminiana – wabara na wazanzibari.

 Tarehe 23 Septemba 1975 katika mkutano ule ule Ndugu Jumbe, ambaye alitoa hotuba ndefu siku hiyo alitoa historia fupi ya Zanzibar, Tanzania Bara, Muungano wa Jamhuri ya Tanzania na Katiba ya Muungano na akasema kwamba kama vyama viwili vikiunganishwa kwa njia sahihi na makini, Muungano wake ungesaidia maslahi ya Watanzania na Bara la Afrika kwa jumla.

Mwaka 1976, mwezi wa Januari TANU iliitisha kikao cha Halmashauri Kuu kujadili namna wananchi watakavyoshirikishwa kutoa maamuzi katika jambo hili la kuunganisha vyama vya siasa – TANU na ASP. Ikaamriwa matawi yote ya TANU nchini walijadili na ifikapo mwezi Aprili tarehe 30, 1976 matawi ya TANU Bara yawe yamepeleka maamuzi ya wanachama Makao Makuu Dodoma ili chama kitoe uamuzi.

 Kule Visiwani Rais wa ASP, Sheikh Jumbe alianzia Kisiwani Pemba katika Mkutano wa Halmashauri Kuu ya ASP tarehe 8 Februari 1976 na akawaambia wajumbe kuwa umefika wakati sasa kwa ASP Visiwani kutoa maamuzi yao juu ya suala la kuunganisha vyama vya TANU na ASP Mzee Jumbe alilisitiza kuwa uamuzi utolewe na wana ASP wote wenye KADI za Chama. Aliwataka wajumbe wafikirie maslahi ya wananchi. Basi mawazo yote yakusanywe kutoka matawini, Wilayani mpaka Mkoani.

1208 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!