Watanzania wengi wanaozungumza Kiswahili na waliojaaliwa kupata kiasi fulani cha elimu, huugua ugonjwa ambao moja ya dalili zake ni kuongea au kuandika kwa kutumia zaidi ya lugha moja. Na kwa kawaida, lugha ya pili huwa ni Kiingereza.
  Akifunga Mkutano wa Bunge Septemba 8, 2004, Waziri Mkuu Frederick Sumaye alizungumzia tatizo hili na athari zinazojitokeza za kuzivuruga lugha zote mbili — Kiingereza na Kiswahili.
 Baadhi ya mifano aliyotoa ambayo ilitumiwa na wabunge wakati huo ilikuwa:
“Waziri u-clean your house” (Waziri, safisha nyumba yako)


“Ina-confuse madereva” (Inawachanganya madereva)
“Bajeti hii haina vibrancy, economic growth imekosekana” (Bajeti hii haina uhai, ukuaji wa uchumi unakosekana).
 Siku zote nimekuwa nikiamini kuwa watumiaji wa lugha ya Kiswahili wenye tabia ya kutumia maneno ya Kiingereza ni watu wanaojaribu kuwakoga wale wasiofahamu lugha ya Kiingereza.


  Nimekuwa nikiamini kuwa hakuna sababu ya msingi ya kuchanganya lugha hizi mbili, iwapo nia siyo kuwakoga watu. Hii ndiyo imani yangu, lakini tunafahamu siku zote ugumu wa kuishi wakati wote katika misingi ya imani.
  Nilipoanza kufanya utafiti kwa madhumuni ya kuandika makala hii niliongea na mbunge mmoja nikamwambia:


“Nimepata wazo la kuandika article, kucriticize tabia ya kuchanganya lugha mbili kwenye mazungumzo….”   


Nilisita kidogo kwenye maelezo yangu baada ya kugundua kuwa hata mimi naugua ugonjwa huo huo unaowaathiri baadhi ya Watanzania.
 Katika hiyo sentensi fupi ya Kiswahili nilikuwa tayari nimeshatumia maneno mawili ya Kiingereza, article (makala), na criticize (kukosoa). Labda inabidi kupitia upya msimamo wangu juu ya kuchanganya lugha. Inawezekana kutokea watu wawili ambao hawana kusudio lolote la kukogana kwa ufahamu wao stadi wa lugha ya Kiingereza, lakini wakalazimika kupenyeza maneno ya Kiingereza katika mazungumzo kwa madhumuni ya kurahisisha mawasiliano.
  Mtu mmoja alinipa mfano wa matumizi ya maneno ya Kiingereza ambao unadhihirisha ugumu huu wa kukwepa kuchanganya lugha, ingawa naweza kusema tena kuwa hili ni tatizo linalowakumba zaidi wale waliopata elimu zaidi kidogo kuliko wenzao.


  Yupo mtaalamu alikuwa akielezea mfumo wa kutoa sumu iliyoko kwenye mwili wa binadamu. Alitamka yafuatayo kwa Kiingereza (nitafafanua maana muda si mrefu) “To eliminate poison from the body, you utilize the skin, the lungs, and the digestive system.”
  Aliyenisimulia mfano huu aliendelea kunijulisha kuwa mtaalamu angeitamka hiyo sentensi kwa lugha ya Kiswahili angesema: “Kuondoa sumu kwenye mwili, unatumia ngozi, mapafu….” halafu angekwama kueleza maana ya the digestive system na badala yake angetoa maelezo marefu kuwa ni ule mfumo unaoanzia kwenye mdomo na unaishia kwenye sehemu fulani ya faragha ya mwili wa binadamu.


 Anasema mtu aliyemsikia akitapatapa kutafuta tafsiri sahihi ya the digestive system alimwambia atumie “mfumo wa mmeng’enyo”.
 Juzi nimesikiliza kipindi cha afya kwenye kituo kimojawapo cha redio nchini, na daktari alituma maneno “mfumo wa mmeng’enyo.” Yawezekana kuwa sasa hivi ni maana inayojulikana na watumiaji wengi wa lugha ya Kiswahili, ingawa nina wasiwasi kama leo nikuzunguka Butiama kwa siku nzima nitapata watu wengi wanaofahamu maana hii halisi.
 Nina uhakika mkubwa kuwa wale waliomaliza shule ya msingi mwaka 1972 kama mimi wameanza kusikia hayo maneno wakiwa watu wazima.


 Wakati huohuo ufahamu wa neno au maneno sahihi ya kutumia ya Kiswahili haumalizi tatizo la kuelewana kwa urahisi ili mradi watumiaji wa lugha siyo wataalamu wa lugha ya Kiswahili.
 Nashindwa kumtaja mtu hata mmoja ninayemfahamu ambaye atatumia “mfumo wa mmeng’enyo” katika mazungumzo ya kawaida. Anayekutwa na uzalendo huo wa kutumia maneno hayo kwenye mazungumzo atalazimika kutoa maelezo ya ziada kwa wanaomsikiliza ili wamuelewe. Na pengine tutaanza kumsema pembeni kuwa ni mtu anayejaribu kukoga wenzie kwa ufahamu wake mahiri wa lugha ya Kiswahili.
Tukirudi kwa wabunge, inasemekana kuwa nao wanazo hoja za msingi za kuchanganya lugha hizi mbili. Mbunge mmoja aliniambia kuwa kwa sababu ya dakika chache wanazoruhusiwa kuongea bungeni kwa mujibu wa kanuni za Bunge ni vigumu kwa mbunge kuwasilisha hoja zake ndani ya muda unaoruhusiwa na wakati huo huo apewe sifa ya kuongea Kiswahili fasaha.


Pengine ipo hoja ya msingi inayoweza kukubalika juu ya ugumu wa kuongea Kiswahili kilichonyooka pasipo kuchanganya Kiingereza au lugha nyingine za kigeni.
Ni wazi kuwa wanataaluma wetu wengi wanajifunza taaluma zao kwa kutumia lugha nyingine zote unazoweza kufikiria isipokuwa Kiswahili. Naamini kuwa hata wale wataalamu wa lugha ya Kiswahili hutumia lugha ya Kiingereza kupanua uelewa wao wa lugha ya Kiswahili.
 Kwa hiyo, baada ya miaka mingi wakifundishwa kwa lugha ambayo siyo lugha za mama zao, ni vigumu kutegemea watu hao hao wazungumze Kiswahili bila kupachika maneno ya lugha mojawapo ya kigeni.
Nakumbuka kuwa baada ya kusoma na kuishi nchini Canada kwa zaidi ya miaka minne, niliporudi Tanzania mwaka 1985 nilikuwa hata kuota naota kwa lugha ya Kiingereza.


Lakini pamoja na mapenzi yangu yasiyo na mipaka kwa lugha ya Kiswahili, nakiri kuwa wakati mwingine tunalazimika kutumia maneno ya lugha nyingine ya kigeni ili kurahisisha mazungumzo.
Mwaka 2005 nilikuwa najadili mchakato wa kupitisha wagombea ubunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka huo.
Mwanasiasa niliyekuwa naongea naye alikuwa amefanyiwa upasuaji mdogo wa mkono wake katika kipindi ambacho mchakato wa kupitisha wagombea ulikuwa unaendelea ndani ya CCM.


Tuliongelea siasa kwa muda kidogo halafu nikamuuliza, “mkono vipi?” Jibu lake linadhoofisha hoja ya kung’ang’ania matumizi ya Kiswahili peke yake kwenye mazungumzo. Alinijibu kuwa ‘Mkono alikuwa amepita bila kupingwa’.
Mimi nilikuwa nimehamishia mazungumzo kwenye masuala ya afya yake, kumbe yeye alikuwa bado kabaki kwenye mchakato wa CCM na wagombea wake. Yeye, kwa makosa, alielewa kuwa namuulizia Mhe. Nimrod Elirehema Mkono, Mbunge wa Musoma Vijijini, wakati mimi niliulizia hali ya mkono wake.
Bila kukusudia nilijikuta nalazimika kutumia lugha ya Kiingereza kumuelewesha ili kurahisisha mawasiliano.


Inahitajika jitihada ya nguvu kulinda matumizi sahihi ya lugha ya Kiswahili, lakini changamoto zipo, na wanaozikuza changamoto hizi ni wasomi.

By Jamhuri