Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Kajubi Mukajanga, ametoa changamoto mpya kwa waandishi wa habari nchini.

Kajubi anasema mwandishi anaweza kufanya afanyavyo au zinaweza kutungwa sheria nzuri za kila aina isipokuwa kwa kila hali, ni lazima mwandishi azingatie maadili ya kazi yake anayoifanya.

Kauli ya Kajubi imetolewa katika kipindi ambacho usalama wa wanahabari nchini unaonekana kuwa tete, na kwamba MCT wamefikia hatua ya kuanzisha mafunzo ya usalama kwa wanahabari.

Hivi karibuni yamefanyika mafunzo ya aina hii kwa wanahabari waliopo mikoa ya kusini mwa Tanzania. Mafunzo haya yamefanyika mkoani Mbeya.

Idda Mushi, Mwenyekiti wa Morogoro Press Club, anasema mafunzo hayo ni mazuri lakini ipo haja ya kuyakutanisha makundi matatu ambayo ni wamiliki wa vyombo vya habari, wahariri na waandishi wa habari kwa kuwa wakati mwingine wote wanakiuka maadili, hivyo yafaa kuwekana sawa.

Naye Brandy Nelson, Mweka Hazina wa Mbeya Press Club, akiwa katika mafunzo ya siku mbili yahusuyo uandishi wa habari katika mazingira hatarishi, yaliyoandaliwa na MCT na kufanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Paradise, Septemba 16 hadi 17, mwaka huu, jijini Mbeya, alimwomba mwezeshaji, Beda Msimbe, au Lilian Timbuka wamweleze misingi ya uandishi bora.

Mwezeshaji Msimbe alisema waandishi hapa nchini wanapaswa kufahamu kwamba hadi kufikia Machi, mwaka huu, Tanzania imeingizwa kwenye orodha ya nchi duniani ambazo waandishi wake wanafanya kazi katika mazingira hatarishi.

Anasema ipo haja kwa waandishi kufahamu viashiria vya mazingira ya hatari kwa lengo la kujinusuru na madhara mbalimbali wanayoweza kupata wakiwa kazini au mahali popote.

 

Ni hatari kwa mwandishi kuchelewa kufika katika eneo hatarishi na kuchukua taarifa bila kufanya uchunguzi wa namna atakavyoweza kutoroka katika eneo hilo, endapo tatizo linaibuka, anasema.

Kwa mazingira ya sasa nchini, mwandishi anapaswa kufika eneo la tukio kama kwenye migogoro au wananchi wameamua kupambana kama ilivyotokea katika mgogoro wa gesi Mtwara, saa mbili kabla, kwa nia ya kusoma mazingira na kujua endapo askari wataamua kuzima maandamano au mapambano watatokea upande gani na wewe [mwandishi] utapita wapi kujiokoa.

“Simaanishi waandishi muwe waoga, la hasha, bali waandishi msidanganyike kwamba kufia kwenye kazi ni ufahari au ndiyo ujasiri, si kweli kwani ‘dead body never tells the story’ (marehemu haandiki habari), lakini pia hakuna kitu kinachozidi thamani ya uhai,” anasema Msimbe.

Anaeleza haja ya waandishi kupitia mafunzo ya mgambo au Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ili waweze kuwa mahiri katika kufanya kazi kwenye mazingira hatarishi, lakini pia kuwa na mbinu za kijeshi zitakazomwezesha mwandishi kujua viashiria vya hatari na namna ya kuviepuka.

Anafafanua vitendo vinavyovuruga maisha ya mtu vinazaa matatizo kwa waandishi wasiozingatia maadili ya kazi yao, kwa sababu watakuwa wameibua chuki na hasira zilizopitiliza kwa wadau hao iwapo wataviripoti bila kuchukua tahadhari.

Lilian Timbuka anasema; ‘Maadili ya uandishi wa habari’  ndiyo nguzo zinazoshikilia uandishi salama na wenye manufaa kwa jamii.

Alisema maadili kwa mwandishi yeyote aliye katika nchi ambazo waandishi wake wanafanya kazi kwenye mazingira hatarishi kama Tanzania, ni kinga ya kutopata madhara kwa asilimia 99.

Anafafanua kuwa katika maadili kuna vitu vingi, lakini vya msingi zaidi ni kusimamia ukweli, kutopendelea, kuhoji pande zote zinazohusika na tukio, usahihi, ufasaha wa tukio, kupunguza ukali wa maneno au lugha na kuepuka rushwa.

Pia utashi wa akili wa kutambua kuwa kuna habari nyingine inaonekana nzito au kubwa, lakini ikiwa inahatarisha usalama wa nchi, kuchochea migogoro, au haina faida kwa jamii mwandishi unaiweka kando.

Lilian anasema kwa kufanya hivyo, mwandishi atakuwa katika mazingira salama wakati wote, kwani huo ndiyo unaitwa uandishi wa habari wa kuzingatia maadili.

Anasisitiza kuwa waandishi walio wengi nchini wanafanya kazi bila kuangalia au kusoma ishara za nyakati, ambazo zinawaingiza katika matatizo mazito yakiwamo ya vifo pengine kwa kutojua au kwa makusudi.

Lakini pia anasisitiza kuwa waandishi wanaporipoti habari katika mazingira hatarishi, ni muhimu kuzingatia jinsia kwani kuna uwezekano mkubwa ukakosa ukweli wa jambo kutokana na kutoyahoji makundi maalum kama vile wanawake, vijana, walemavu, watoto, wazee, wajane na watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi.

Akihitimisha, Msimbe anasema maadili ni kinga kwa mwandishi, hivyo ni vyema kuyazingatia kikamilifu kila siku kama yanavyozingatiwa maandiko matakatifu na kile kinachoaminiwa na wapagani.

Alisisitiza waandishi kuacha kuandika habari zinazowaweka katika mazingira hatarishi, hasa tunapoelekea kwenye kampeni za uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2014 na Uchaguzi Mkuu 2015.

Anasema waandishi waache kuwa wanazi wa vyama vya siasa, kutopokea na kuomba rushwa, kutojifanya maafisa Usalama wa Taifa na ‘mainfoma’ wa polisi, kwani anayeepuka vitendo hivyo anakuwa na uzito na kuheshimiwa katika jamii anayowajibika kwake.

[email protected]

By Jamhuri