*Kila mjumbe wa Tume analipwa Sh milioni 294

*Waziri Chikawe asema hizo wanalipwa ‘vijisenti’

*Hofu yatawala kama posho nono hazitawapofusha

*Jaji Warioba, Profesa Baregu wapata kigugumizi

 

Tume ya Mabadiliko ya Katiba inayoongozwa na Waziri Mkuu (mstaafu) Jaji Joseph Warioba imetengewa mabilioni ya fedha kwa kiwango cha kutajirisha wajumbe wa Tume hiyo ambapo kila mjumbe anapata Sh milioni 294 ndani ya mwaka mmoja.

Mgawanyo wa bajeti hiyo ndio suala zito zaidi. Kwa hali ya sasa, karibu asilimia 40 ya bajeti ya Tume hiyo inakwenda kwenye posho pekee. Kila mjumbe kati ya wajumbe wote 34 atalipwa kati ya Sh 280,000 hadi 450,000 kwa siku mpaka kazi hiyo itakapokamilika.

 

Posho ya uwajibikaji (responsibility allowance) wanayolipwa wajumbe ni kati ya Sh 50,000 hadi 150,000; posho ya vikao (sitting allowance) ni kati ya Sh 150,000 hadi Sh 200,000; posho ya siku Sh 80,000.

 

Wajumbe wa kawaida wa tume hiyo kwa mujibu wa mchanganuo wa bajeti, watalipwa posho ya Sh 450,000 kwa siku, lakini Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Tume fungu lao ni kubwa zaidi ambalo limeongezewa viburudisho na takrima.

 

Taarifa za uchambuzi wa posho hizo zinaonesha kuwa, kila mjumbe kuanzia mwaka wa fedha wa Julai 2012 hadi Julai 2013, atakusanya zaidi ya Sh 294 milioni.

 

Pamoja na kuhakikishiwa kuwa na ukwasi mkubwa, pia wametengewa Sh milioni 10 kwa ajili ya matibabu kwa wale ambao wameelezwa kuwa hawapo kwenye utaratibu wa kugharamiwa tiba na serikali.

 

Dau kubwa ambalo lipo kwenye bajeti hiyo ni kutengwa Sh 250 milioni zinazodaiwa zitatumika kwa ajili ya usafi na ulinzi wa ofisi za Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

 

Wajumbe hao 34 kutoka Bara na Visiwani wametengewa Sh 10 milioni kugharamia mazishi na kuwasafirisha wajumbe wa Tume hiyo ikitokea mjumbe akafariki dunia wakati wakiwa kwenye mchakato wa kukusanya maoni.

 

Ukiacha Jaji Warioba, wajumbe wengine wanaolipwa kiwango kinachotajwa na baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kiuchumi kuwa ni kufuru ni Makamu wake Jaji Mkuu (mstaafu) wa Tanzania, Agustino Ramadhan.

 

Ukiacha Jaji Warioba (Mwenyekiti) na Makamu wake, Jaji Ramadhani, wajumbe wengine 15 kutoka Bara la 15 kutoka Zanzibar ndio wenye kuogelea katika ukwasi huo, wakisaidiwa na Katibu wa Tume na Msaidizi wake.

 

Wajumbe kutoka Tanzania Bara ni Prof. Mwesiga L. Baregu, Riziki Shahari Mngwali, Dk. Edmund Adrian Sengodo Mvungi, Richard Shadrack Lyimo, John J. Nkolo, Alhaj Said El- Maamry na Jesca Sydney Mkuchu.

 

Wengine ni Prof. Palamagamba J. Kabudi, Humphrey Polepole, Yahya Msulwa, Esther P. Mkwizu, Maria Malingumu Kashonda, Al-Shaymaa J. Kwegyir (Mb), Mwantumu Jasmine Malale na Joseph Butiku.

 

Wajumbe wengine walioukwaa ukwasi huo kutoka Zanzibar ni Dk. Salim Ahmed Salim, Fatma Said Ali, Omar Sheha Mussa, Raya Suleiman Hamad, Awadh Ali Said, Ussi Khamis Haji na Salma Maoulidi.

 

Pia wamo Nassor Khamis Mohammed, Simai Mohamed Said, Muhammed Yussuf Mshamba, Kibibi Mwinyi Hassan, Suleiman Omar Ali, Salama Kombo Ahmed, Abubakar Mohammed Ali na Ally Abdullah Ally Saleh.

 

Ukiacha maafisa wengine wa Tume hiyo, wenye kufaidi posho hizo nono ni pamoja na Katibu wa Tume Assaa Ahmad Rashid na Naibu Katibu Casmir Sumba Kyuki. Kyuki alikuwa Mkurugenzi katika Wizara ya Sheria na Katiba kabla ya kuteuliwa kuwa Naibu Katibu.

 

Tume hiyo yenye wajumbe 32, Katibu na Katibu Msaidizi, imetengewa Sh bilioni 39.5 kwa mwaka wa fedha 2012/13.

 

Mchanganuo unaonesha kwamba mafungu yaliyotengwa ni posho za vikao ni Sh 9.5 bilioni; posho za madaraka Sh 630 milioni; posho ya kujikumu Sh 4.3 bilioni; nyumba za wajumbe Sh 2 bilioni; ununuzi wa magari mapya wanayoyatumia sasa Sh 9.8 bilioni. Jumla yapo magari 55 mapya na fedha za kugharamia mafuta Sh 4.7 bilioni.

 

Pamoja na kelele za wananchi na wabunge wa Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria, na ahadi ya Waziri wa Sheria na Katiba, Mathias Chikawe, wangefanyia kazi upunguzaji na uwianishaji wa bajeti hiyo, jambo lililofanyika ni kushusha bajeti ya jumla kidogo tu hadi Sh bilioni 35, bajeti ambayo bado ni kubwa ikiwa ni sawa na bajeti ya wizara za kawaida zaidi ya 4. Zipo wizara zinazopata kiasi cha Sh bilioni 8 kwa mwaka mpaka sasa.

 

Ofisi ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba pia inatarajiwa kutumia Sh 256 milioni kugharamia umeme na maji ambapo kila huduma imepangiwa kugharimu karibu Sh 128 milioni, yaani umeme Sh. 127,992,000 kadhalika maji nayo yamepangiwa kugharimu kiasi hicho.

 

Tume hiyo imetengewa posho ya takrima iliyoitwa hospitality services ya jumla ya Sh. 300 milioni huku simu za TTCL pamoja na gharama za nukushi (fax) zikifikia karibu Sh 127 milioni wakati zile za mkononi zitawagharimu walipa kodi zaidi ya Sh 91.2 milioni.

 

Wafanyakazi wa kawaida ambao siyo wajumbe bali ni watumishi wa ofisini watawala, wahasibu, makatibu muhtasi, wafagizi, wataalamu wa kompyuta, madereva na wengine nao wametengewa mafungu kadhaa ikiwemo posho ya kujikimu wakisafiri kiasi cha Sh 4.3 bilioni.

 

Pia wafanyakazi hao ambao watalipwa posho ya Sh. 50,000 kwa siku wametengewa Sh 300 milioni kwa ajili ya kununulia vifaa vya chai ambavyo havikuelezwa ni vitu gani pamoja na vitafunwa.

 

Wachambuzi wengi wanaona kuwa mafao makubwa yanayolipwa kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, pamoja na heshima ya ving’ora katika misafara yao inakuwa kama rushwa ya aina yake na kuwafanya kuabudu kila watakachoambiwa na serikali kuhusu mwenendo wa mchakato wa Katiba Mpya.

 

Waziri Chikawe asema ni vijisenti

Akizungumzia posho hizo, Waziri wa Sheria na Katiba, Mathias Chikawe amesema malipo hayo ni sawa na bure kwa kuwa wajumbe hao wanafanya kazi ngumu.

 

“Hahahahahahahaha!… Brother wale wazee wanajitolea tu. Pale ni kama wanafanya kazi bure tu. Hicho ni kiasi kidogo sana kwao. Wameacha kazi zao nyingi za muhimu na za maana wameamua kutusaidia kupata Katiba mpya.

 

“Angalia, wazee  kama  Mzee Salim (Dk. Salim Ahmed Salim) akiitwa katika kikao kimoja cha Baraza la Usuluhishi analipwa fedha ningi sana kuliko hizi, lakini ameacha hizo fedha amekuja kufanya kazi ya Tume. Waacheni wazee wetu wanafanya kazi kubwa hawapumuziki wamejitoa kufanya kazi ya taifa.

 

“Fedha hii ilipitishwa na Bunge tena wabunge wakasema kuwa ni ndogo wakataka iiongezwe, nikasema wacha tuendelee na hii kwanza tukikwama tutaongeza, lakini ni ndogo mno hii,” amesema Chikawe.

 

Kuhusu malipo hayo kufananishwa na rushwa, Chikawe amesema serikali haina faida yeyote katika Tume hiyo kwani haitoi maoni ya Katiba kwa kuwa maoni  yanatolewa na wananchi kwa Tume kwa kufuata sheria na kanuni za Tume hiyo.

 

Wakati Chikawe akisema hayo mjumbe wa Tume hiyo, Profesa Mwesiga Baregu, ameruka kimanga kuzungumzia malipo hayo kwa madai kuwa yeye si msemaji wa Tume hiyo.

 

“Mie siwezi kuzungumzia bajeti hiyo kwa kuwa sio msemaji wa Tume, bali ni mjumbe tu. Itakuwa bora umuulize Katibu wa Tume na watendaji wake wengine mie siwezi kuzungumzia kama ni kubwa mno au ndogo,” amesema  Profesa Baregu.

 

Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Warioba kwa wiki mbili sasa anatafutwa ofisini kwake bila mafanikio na Ijumaa aliwasiliana na gazeti hili akaagiza apigiwe simu siku ya Jumamosi asubuhi, lakini muda wote kila alipopigiwa hakupokea.

 

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Sheria na Katiba, Pindi Chana, aliliambia Jamhuri kuwa ikiwa malipo hayo yameidhinishwa na Bunge basi hakuna la kuhoji kwani kiasi hicho kilipitishwa kwa uwazi.

 

 

 

 

By Jamhuri