SAID+MAKAPUKuna wakati ili ufanikiwe basi ni vyema kujifunza kwa yule aliyefanikiwa. Mtu aliyefanikwa kwa kumwangalia tu matendo yake unapata funzo.
Unaweza kumwangalia namna anavyoongea, anavyotembea, anavyocheka na namna anavyochagua marafiki, kusikiliza watu na kadhalika na utajikuta umepata funzo kubwa sana hata kama hujakaa naye mezani na kuzungumza naye neno lolote.
Watu waliofanikiwa ni hazina kwa mtu yeyote anayetaka kujifunza. Msimu wa Ligi Kuu nyingi duniani unaelekea ukingoni ambako kule England Chelsea ikijulikana ni bingwa tayari.


Hispania nako Vermaleen akivaa medali  ndani ya uzi wa Barcelona bila kucheza mechi hata moja. Pia hapa kwetu tumeshaanza kusahau tangu Yanga wamekabidhiwa Kombe la Ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Kinachosikika sasa ni tetesi za usajili, huku timu zikipigana vikumbo huku na kule na majina yanayovuma katika usajili yakiwa ni Deus Kaseke wa Mbeya City na Malimi Busungu wa Mgambo JKT wote wanaowaniwa na klabu kongwe nchini za Simba na Yanga.
Katika mwenendo wa Ligi hapa Tanzania, Yanga imechukua ubingwa wake chini ya Kocha wa Kidachi Hans der Pluijm aliyepokea jukumu hilo kutoka kwa Mbrazili Marcio Maximo.


Na kule England, Manchester United imerejea kwenye ‘Top four’ chini ya Mdachi Luis van Gaal baada ya mwaka jana kuishia nafasi ya saba chini ya kocha mzawa David Moyes. Hawa makocha wawili wa Kiholanzi wana mambo kadhaa ambayo yanatupa mafunzo katika soka letu.
 Yanga wakiwa wanalia na kuondokewa na kiungo wao mahiri, Frank Domayo, aliyetimkia Azam hata alipokuja Maximo naye alionesha kuwa kilio hicho hakikwepeki hata kidogo kwa matokeo mabaya uwanjani.
Lakini wakati pengo hili likionekana, Said Juma ‘Makapu’ alikuwa amekaa kwenye benchi au jukwaani na wakati huo Salum Telela anapangwa kama beki wa kulia.


Alipofika Hans der Pluijm aligoma kulia kilio cha Domayo akaangalia kikosi akaona kimetimia na akaamua kumtoa Makapu kutoka jukwaani na kumweka sehemu ya kiungo, huku akimtoa Telela kutoka mbavu ya kulia na kumweka kama kiungo na vilio vikakoma furaha ikarejea kwa vijana wa Jangwani.
Akamtoa Simon Msuva kutoka kuwa mchezaji wa akiba na kumfanya kuwa mchezaji muhimu uwanjani. Kilichotokea wote tumekiona. Mholanzi huyu alimpokea Tambwe aliyetupiwa virago Simba kwa madai ya kushuka kiwango na kumtumia kuchagiza sherehe za ubingwa kwa mabao 13 aliyoifungia klabu hiyo katika mechi za Ligi.


Hapo utagundua kuna kutambua kipaji, kutoa nafasi ya kuonekana kwa kipaji, na kukivumilia mwishowe ubora unaonekana.
Ilihitaji jicho la Kiholanzi kujua kuwa Msuva anayezomewa atakuja kuwa mfalme mpya ndani ya klabu. Ilihitaji roho ngumu ya Kiholanzi kujua galasa Tambwe atakuja kuwa dhahabu na kupiga mabao 13.


Bado ilihitaji weledi wa soka kumvumilia Sherman aliyekuja kuonesha uwezo wa ufungaji mwishoni mwishoni mwa Ligi. Busara ya Kiholanzi pia ndiyo iliyomrejesha Charles Mkwasa ‘Master’ kama kocha msaidizi Yanga kama ilivyotokea kwa Ryan Giggs pale Manchester United.
Ninapotafakari haya kwa hapa nyumbani, huwa sioni tofauti ya Pluijm alivyomfanya Msuva kuonekana mtu muhimu kwenye timu kama ilivyokuwa kwa Ashley Young wa Manchester United.


Bado sioni tofauti ya thamani ya Makapu ilivyoibuliwa pale Jangwani ikilinganishwa na thamani ya Fellain wa Man U ambaye mwanzo wa msimu kila shabiki wa wababe hao wa England, alilaumu kwanini hakuuzwa.
Ligi imekwisha Makapu amekuwa lulu na pale Old Traford hakuna aliye tayari kusikia Fellain anauzwa. Tujifunze walau kwa hawa Waholanzi namna wanavyoweza kuona vipaji na kuvilea maana yawezekana tumeshawapoteza wakina Makapu wengi sana hapa kwetu kwa kukosa jicho, uvumilivu na busara za Kiholanzi.

Baruapepe: [email protected] Simu: 0715 366010

By Jamhuri