Rais John Magufuli, alipoapishwa kuongoza Taifa letu, nilisema endapo sheria za nchi zitatambuliwa, kuheshimiwa na kusimamiwa, kazi yake ya kuongoza haitakuwa ngumu.

Kweli, siku chache baada ya kuingia madarakani, yapo mambo mengi mazuri aliyoyafanya kwa nia moja tu ya kuirejesha nchi kwenye mstari ili safari yetu ya maendeleo iweze kuendelea vema.

Rais Magufuli, kwa hulka na kasi yake kwenye masuala ya uongozi, alikuwa mkata kiu ya Watanzania waliokwishaanza kukata tamaa kwa uongozi uliopita.

Mwenyezi Mungu, ana mipango yake. Alipomuumba mwanadamu, akamwekea kitu kinaitwa “kusahau”. Baada ya Rais Magufuli, kuanza kushughulikia kero zilizoiumiza nchi, tayari wamejitokeza watu kadhaa kumkosoa, kumdhihaki na hata kumtukana!

Leo Rais Magufuli, anaonekana dikteta kuliko madikteta wote waliowahi kuongoza nchi yetu! Anaitwa dikteta kwa sababu amekuja na utaratibu wa kuwapa muda na sehemu za wanasiasa kuendeshea siasa zao!

Leo hayazungumzwi ya wakati uongozi wa Mzee Benjamin Mkapa wala yale ya Komredi Jakaya Kikwete.

Kwa miezi kenda tu, Watanzania wameshasahau namna nchi hii ilivyokuwa imekamatwa na majizi kila kona. Kitendo cha Rais Magufuli, kuamua kupambana kwa vitendo na wezi, wahujumu na mafisadi, tayari kimetafsiriwa kuwa ni udikteta.

Kwa miezi tisa, Watanzania wameshasahau namna uchumi wa nchi yetu ulivyokuwa umeshikwa na genge la wafanyabiashara wachache walioamua kuratibu kodi za nchi!

Mwaka haujatimia, tayari Watanzania wameshasahau namna watoto wa wakubwa waliotoka madarakani walivyoamua mambo kana kwamba ndio waliokuwa wenye hati miliki ya nchi hii. Wale waliopeana zabuni katika mashirika mbalimbali hadi kwenye vyombo vya ulinzi na usalama kwa sababu tu wana uhusiano na Ikulu, leo wanaposhughulikiwa tunamuona Rais Magufuli, nji dikteka ambaye baadhi yetu tunadiriki kusema hata picha yake haifai kuwekwa ukutani!

 

Juzi, tumesikia katika Wilaya ya Kahama-wilaya moja tu, ikiwa na wanafunzi hewa 29,000! Shilingi milioni zaidi ya 200 zilitafunwa na genge la wateule! Hiyo ni wilaya moja kati ya wilaya zaidi ya 130 nchi nzima.

Wanafunzi hewa ni mbali kabisa na watumishi wa umma hewa ambayo mara ya mwisho tumeambiwa wameshabainika zaidi ya 15,000 nchini kote. Idadi hii inadhamiwa kuwa ni ndogo. Fukuafukua ikiendelea, itaongezeka.

Rais Magufuli, hajamaliza mwaka lakini tayari ameshabaini na kufunga mianya mingi ya upotevu wa fedha za umma kupitia zabuni na michongo mbalimbali.

Lakini ni kwa miezi hii tisa ambayo hata wanahabari wameshaona wanaonewa kuliko wakati wowote ule! Tayari wameshafuta kwenye kumbukumbu zao namna wenzao walivyopigwa wakati na kufurushwa kwa mabomu ya machozi na maji ya kuwasha wakati wakiwa kazini.

Wameshasahau kabisa namna Daudi Mwangosi alivyouawa kwa bomu la kutoa machozi. Hawana taarifa zozote za kutekwa, kupigwa na kutolewa jicho kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania, Absalom Kibanda.

Leo hii hakuna anayekumbuka namna Dk. Stephen Ulimboka alivyotekwa na kupigwa na ‘watu wasiojulikana’. Hadi leo waliofanya matukio hayo mawili, eti hawajulikani!

 Kuna wanahabari waliofunguliwa mbwa, wakang’atwa na wengine wakifungwa jela kwa sababu tu wameandika habari za polisi na watendaji waonevu. Haya hayasemwi kabisa, isipokuwa anaandamwa Rais Magufuli, na kutajwa kuwa ni dikteta kwa miezi yake kenda madarakani.

Sitaki kurejea mengi, lakini ilivyo sasa ni kama watu wanalazimishwa kuamini kuwa wanasiasa katika nchi hii hawakuwahi kukutana na msukosuko wowote ule, isipokuwa kwa awamu hii ya Rais Magufuli.

Tunaaminishwa kuwa wanasiasa wanaswekwa rumande miaka hii, lakini huko tulikotoka kina James Mapalala, Maalim Seif Sharif Hamad, Juma Duni Haji, Kasanga Tumbo, Bibi Titi Mohamed na wengine wengi hawakuwahi kuonja jela!

Makabwela katika nchi hii walifika hatua ya kuonekana kama wanyama tu pindi walipofuata huduma za jamii katika hospitali, Tanesco na katika ofisi zote za umma. Ndani ya miezi tisa kuna nidhamu inarejeshwa ili mwananchi awe wa thamani mbele ya watumishi wa umma. Haya hatuyaoni. Tumekazania udikteta wa Rais Magufuli.

Nayasema haya si kwa sababu naomba uongozi huu ufanye mabaya zaidi ya hayo, la hasha! Nayasema haya katika kuonesha kuwa hiki kitu KUSAHAU ambacho Mwenyezi Mungu, ametuwezesha kuwa nacho, ni kitu cha aina yake. Usipotafakari dhana ya ‘kusahau’ unaweza kuona kila kitu kinachofanywa sasa ni kibaya!

 Hatuungi mkono udikteta kama ambavyo hatuwezi kuunga mkono ubatizo huo kwa kiongozi anayejaribu kurejesha misingi iliyokwishavurugwa katika Taifa letu.

Rais Magufuli ni binadamu. Anaweza kuwa na upungufu wake kama binadamu. Kuna maeneo fulani fulani yawezekana akawa anakosea. Ni wajibu wetu kumsaidia, lakini si haki kujenga taswira ili aonekane ni mtu katili asiyekuwa na chembe ya huruma.

Kwa upande wetu vyombo vya habari tunaiona hatari inayokuja. Ukiacha ya kufungiwa, lakini ya kudumu kabisa soko! Hatupati matangazo. Bila matangazo, ikizingatiwa hatuna ruzuku, magazeti mengi yatakufa. Hili tunaishauri Serikali ilitazamwe kwa jicho la hadhari-mapema kabisa.

Haya ndio mambo tunayopaswa kuyazungumza. Tuwezeshwe tuwe na chombo cha kutuwajibisha kitaaluma pindi tunapokosa kama ilivyo kwa wanasheria, madaktari, makandarasi na kadhalika. Hii funga funga inayofanywa na Serikali si nzuri.

Lakini hiyo haina maana kwamba sasa tuandike au tutangaze hamasa ya vita, nchi iingie kwenye machafuko kwa kigezo cha ‘uhuru wa habari na wanahabari’. Haiwezekani. Hata huko Marekani tunakodai kujifunza demokrasia, hawaruhusu upuuzi huo.

Tanzania haiwezi kujengwa kwa misingi kama ile inayotumiwa na nchi iliyokwishaendelea kama Marekani. Nchi inayohitaji kuendelea, lazima kuna mambo yanayopaswa kutendwa na kiongozi mkuu na wasaidizi wake bila kujali majina gani mabaya watakayopewa.

Kwa mfano, leo hii katika mataifa yaliyoendelea ni nadra kumsikia kiongozi wa nchi akihimiza watu kupenda kufanya kazi. Katika nchi hizo utendaji kazi ni utamaduni! Hapa kwetu tukisema ni demokrasia na haki ya raia kuamua, ama kufanya, au kutofanya kazi, hatuwezi kujikwamua kwenye hali hii dhalili tuliyonayo.

Katika nchi yetu bado kuna watu wanaamini wanapaswa kufanyiwa kazi. Hao ni wale wanaoshinda vijiweni au kwenye safari za kujulia hali ndugu, jamaa na marafiki! Hao lazima wabanwe kwa kutakiwa wafanye kazi. Hili Rais Magufuli, analisisitiza mno; wakati mwingine kwa kunukuu maandiko Matakatifu yanayosema; “asiyefanya kazi na asile”.

Kuwabana watu wapende kufanya kazi ili wapate ujira kulingana na jasho lao, huo ni udikteta mzuri.

Tunalalamika mitaani hakuna fedha. Ndio, fedha zimepungua. Kuna maana gani kuwa na fedha nyingi zinazotokana na ukwepaji kodi, badala ya kuwa na fedha za wastani zinazopatikana kwa njia halali?

Leo walimu wanaandaliwa mazingira mazuri ya kazi. Wanafunzi wanasaidiwa mambo kadha wa kadha kutoka kwenye mfuko wa Serikali. Huduma za hospitali zinaboreshwa. Haya hayawezekani endapo hakuna kodi inayokusanywa.

 Mwalimu Nyerere alisema haya kuhusu kodi: “…Kazi ya utajiri ni kuondoa dhiki, kazi ya mali ni kuondoa dhiki. Lakini serikali yetu inapotaka kupata fedha kidogo za kuondolea dhiki, na matajiri wa Tanzania ndiyo wenye fedha, Serikali yetu haiwaombi. Hivi huwaomba hawa? Hatuwaombi. Tunawatoza kodi. Uende uwaombe matajiri, unapita unawaomba matajiri, watakubali? Wanapigwa kodi; wapende wasipende wanatozwa kodi, asiyelipa tunamtia ndani.

“Njia peke yake duniani ya kuvamia mali ya matajiri, isaidie kuondoa dhiki, ni kuwatoza kodi. Hakuna njia nyingine. Kama mali yenyewe mmewaachia mpaka wakawa nayo, wanatozwa kodi; hawaombwi. Kuomba unaomba zaka! Lakini unaweza kuendesha nchi kwa zaka ya Jumapili?”

Kwa namna mambo yanavyokwenda, kumbe inawezekana kabisa kuifanya nchi yetu kuwa ya kupigiwa mfano mzuri kwa mambo kadha wa kadha. Tumkosoe Rais Magufuli na wasaidizi wake, lakini tusimbeze au kumkatisha tamaa. Ukimsikiliza, unabaini nia njema aliyonayo kwa nchi hii na watu wake.

By Jamhuri