Tunakosea kuwasifu wakwapuzi

 

Mei 16, mwaka huu Chama cha Wanataaluma Wakristo Tanzania (CPT) ambacho ni chama cha kitume ndani ya Kanisa Katoliki kiliandaa kongamano la kumbukizi ya miaka 20 ya kifo cha Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Dhamira ya kongamano ilikuwa Maendeleo Jumuishi na yenye kujali ustawi wa maisha ya wananchi. Mada mbalimbali zilijadiliwa. Mada mbalimbali zilitolewa. Mwenyekiti wa CPT, PROFESA BEDA MUTAGAHYWA; na Mchumi PASCHAL ASSEY, walikuwa miongoni mwa washiriki. Yafuatayo ni baadhi ya waliyozungumza. ENDELEA…

 

Profesa Mutagahywa

Mapendekezo yetu yanahusu maendeleo yaliyojikita kwa watu (People Centered Development). Hili ni suala ambalo Mwalimu Julius Kambarege Nyerere alilizungumzia sana, aliliishi na alijaribu mikakati mbalimbali kuhakikisha maendeleo tunayoyatafuta siyo ya vitu, bali ni ya watu.

CPT imeliangalia hili suala kwa muda mrefu tangu mwaka 2015 – tumejadiliana na mwishowe tukaamua kwamba ili tuyatoe haya tunayojadiliana kwa watu tuwe na forum [jukwaa] la leo. Kuna kitabu kikubwa ambacho tutakitoa kwa jamii ili kufuatilia mantiki tuliyogundua katika kuangalia suala hili la maendeleo yaliyojikita kwa watu kutokana na urithi tulioupata kutoka kwa Mwalimu Nyerere.

Tunasema kwamba maendeleo yaliyojikita kwa watu lazima tuangalie kwa pande mbili zifuatazo: Mosi, ni kufanya watu wenyewe waweze kujiletea maendeleo pamoja na kufungua uwezo wao walionao kwa kutatua matatizo na changamoto wanazokumbana nazo katika maisha.

Binadamu, kwa imani na kwa uhalisia tunajua tunao uwezo wa asili. Mungu ametuumba uniquely na ametupa vipaji ambavyo bahati mbaya vingine vinaozea humo, tunavipeleka makaburini bila kuvitumia. Kwa hiyo binadamu tunao uwezo kwa asili yetu; swali ni namna gani tufungue uwezo huo mkubwa kwa mtu binafsi na jamii kwa jumla – mambo yapi yanatakiwa kufanyika.

Pili, kuna kila sababu ya kuwezesha kuwapo kwa maadili mema katika jamii; na kutoacha kupongeza tabia mbaya zinazofanywa na vijana au watu mbalimbali katika jamii.

Profesa Mutagahywa anatoa mfano kwamba kumeibuka tabia ya kusifu wakwapuzi wa fedha za umma kwa kuwaona ni wajanja, na waadilifu wasiojihusisha na dhambi hiyo wakionekana kuwa ni watu waliozubaa.

“Wakwapuzi wanaonekana ndio wajanja, hii si sahihi. Kupunguza umaskini ni kuweka malengo yanayotekelezeka na kwa kushirikisha walengwa. Umaskini hauwezi kumalizwa kwa kusubiri mkuu wa wilaya, mkuu wa mkoa ili waseme nini cha kufanya,” anasema.

Anasema mapambano ya kweli ya kuutokomeza umaskini yatafanikiwa endapo kutaandaliwa malengo na kuifanya mipango iwe ya watu wenyewe na kwa maeneo husika.

Kwa mtazamo wake, anasisitiza umuhimu wa kubadilishwa kwa muundo wa Serikali za Mitaa ili kuwawezesha watu wajue wana wajibu wa kupambana na kujiondoa kwenye umaskini.

“Watu wawezeshwe ili wawe na shauku ya kufanya mabadiliko wao wenyewe kulingana na rasilimali na mazingira walimo,” anasema.

Profesa Mutagahywa anazungumzia suala la uzalishaji mali: “Ushiriki wa dola kwenye uzalishaji mali hauna budi kubadilika. Ilivyo sasa ni kuwa uchumi unaendeshwa kwa maagizo kutoka juu [kwa viongozi] kwenda chini [kwa wananchi]. Hapa tunapaswa kuangalia ili kuifanya nafasi ya dola iwe kuwezesha juhudi za uzalishaji kupitia vikundi na watu binafsi. Tuwe na uchumi shirikishi. Watu watafute maendeleo yao badala ya kuletewa. Tuwe na sera zinazotekelezeka zinazolenga kuwakomboa maskini ambao ndio wengi.”

Anasema maendeleo ya kweli ya wananchi wa hali zote hayana budi kuwa katika mfumo unaohakikisha kila mmoja anakuwa na ulinzi wa hifadhi za jamii.

“Huduma za kifedha sasa zinaangalia faida zaidi. Tujiulize, fedha za mifuko ya jamii zinaelekezwa wapi? Jamii inapaswa ihadharishwe ili iwe na mshikamano. Jamii ikikosa sifa hizi itapata hasara kubwa. Tunahitaji sheria madhubuti kwa ajili ya masilahi ya wote,” anasema.

Anashauri hifadhi ya jamii iwe ni kwa jamii nzima badala ya utaratibu wa sasa ambako wanufaika ni wale wanaochangia kwenye mifuko ya hifadhi; kwa kuzingatia kuwa asilimia 28.1 ya idadi ya watu wote nchini ni maskini.

“Hifadhi za jamii iwe pia kwa wote ambao hawawezi kuchangia wenyewe. Hili litawezekana tu endapo wadau wote watashirikishwa,” anasema.

Kwa upande wa huduma za kifedha, anaona kwa sasa taasisi nyingi zinalenga zaidi kupata faida, na kwa sababu hiyo ni idadi ndogo ya wananchi wanaopata huduma za kibenki. “Hakuna kizuizi kwa watu wa kawaida kuweka nguvu zao pamoja na kupata huduma za kifedha? Kwanini hili halifanyiki? Kwanini watu hawawezeshwi ili waondokane na umaskini?” anahoji.

Kwa mtazamo wake, anaona hili ni tatizo la kibinadamu linalopaswa kutafutiwa na kupatiwa ufumbuzi kwa kulenga kuwawezesha watu kujitambua na kuondoka kwenye lindi la umaskini.

Paschal Assey

Mchumi Assey anaanza kwa kunukuu: “Inabidi tuachane na uchumi unaojali zaidi ukwasi kuliko ustawi wa jamii. Hii ina maana ya kutoka kwenye uchumi wa mapato na faida kutokana na biashara ya kubabaisha na kubahatisha, tuwe na uchumi unaowekeza katika rasilimali watu kwa kutengeneza ajira na kuendeleza uwezo wa watu…Kuamsha uwezo wa watu, kuamsha vipawa vyao ili waweze kujinusuru katika umaskini.”

Mfumo wa fedha: Hizi ni taasisi za soko mitandao na miundombinu inayoondosheka na isiyoondosheka ambayo inawezesha mtoaji wa huduma za fedha na kufanya malipo kati ya wachuuzi wa jumla na wa rejareja.

“Taasisi ambazo tunazungumzia ni mabenki, kampuni za bima, mifuko ya ustawi wa jamii [usalama wa jamii], huduma ndogo za fedha, vyama vya ushirika na soko la mitaji. Huo mfumo ukifanya kazi vizuri unaweza kutoa huduma ili uchumi uweze kukua.

“Tujiulize, je, taasisi hizi zinatoa huduma kwa wengi kwa maana ya mikopo, kuwezesha malipo kufanyika kwa urahisi na huduma nyingine kwa gharama zinazobebeka ambazo wapata huduma wanaziweza? Je, mfumo unachochea ulimbikizaji wa mali na mapato kwa watu wachache? Je, mfumo unachochea utu wa pesa kama pesa, tofauti na kuona kama chombo cha kubadilishana thamani na kielelezo cha thamani ya mali? Je, huo mfumo unachangia vipi kutokomeza umaskini? Haya ni maswali ambayo ningewaomba tutafakari kwa pamoja.”

Azimio la Arusha: Azimio hili lilitangazwa Februari, 1967. Kwa Tanzania iliyotekeleza Azimio la Arusha, malengo yote ya shughuli za kijamii, kiuchumi na kisiasa lazima yahusu maendeleo ya mtu, yaani wananchi; na wananchi wote wa nchi hii.

“Alisema [Mwalimu Nyerere] kujenga utajiri ni jambo jema na inatulazimu kuongeza utajiri wa nchi, lakini utajiri huo utakoma kuwa wa maana pindi ukiacha kumtumikia mtu na kuanza kutumikiwa na mtu. Hii ni falsafa ya Mwalimu na ni falsafa ya Ujamaa tuliyokuwa nayo. Falsafa tuliyonayo kwa sasa ni ipi? Mimi siijui.

“Wakati huo wa Azimio la Arusha taasisi za fedha zilitaifishwa. Ili kutimiza azima hii pamoja na mambo mengine, ililazimika kuwa na mfumo wa taasisi za huduma za fedha kwa kutekeleza falsafa ya Ujamaa na kuondokana na mfumo ambao uliendana na dhana ya ukoloni ya kuzalisha na kusafirisha nje malighafi za nchi kwa ajili ya uchumi wa wakoloni. Hilo ndilo lililokuwa lengo kuu.

“Falfasa hii ilikuwa inatazama ndani zaidi kuboresha maisha ya uchumi kuliko kutegemea uchumi wa nje. Kwa hiyo tulibakiwa na benki moja kubwa ambayo iliitwa National Bank of Commerce (NBC), siyo National Bank of Commerce ya sasa hivi, bali ya wakati ule. Katika mfumo wa fedha ilikuwa na mali karibu asilimia 90. Benki nyingine zilikuwa CRDB, Tanzania Investment Bank (TIB), The Peoples Bank of Zanzibar (PBZ). Taasisi nyingine tulizokuwa nazo ni National Insurance Corporation (NIC), National Provident Fund (NPF) [NSSF], na vyama vya ushirika.”

Kumetokea nini? Assey anasema kuna mfumo wa fedha ambao ulikuwa ubebe uchumi wa kijamaa. Inawezekana mfumo huu haukuweza kukidhi mahitaji ya mfumo wa Ujamaa, na zikatokea shocks, lakini kwa matokeo chanya nchi hii iliweza kujenga viwanda.

“Makampuni ya umma ambayo pamoja na kuchota pesa kutoka Hazina kama ruzuku, mengine yalikuwa yanakwenda vizuri sana. Kulikuwa na viwanda vya nguo, kulikuwa na Kiwanda cha Zana za Kilimo, TEGRI Plastics, na zaidi kulikuwa na kampuni na viwanda 400 ambavyo baadaye vilibinafsishwa.

“Tulikuwa na mfumo wa kodi uliolenga kuleta usawa katika fursa za uzalishaji na mgawo wa pato la taifa. Lakini vilevile kulikuwa na mfumo wa mishahara na masilahi uliolenga kutokuwa na tofauti kubwa za kipato kati ya watu. Hayo malengo yalifikiwa kwa kiasi kikubwa.”

Hata hivyo, Assey anasema kulikuwa na matokeo hasi. Anayataja: “Tulikuwa na benki moja kubwa ya biashara (NBC). Ilikuwa inatoa mikopo kwa mashirika ya umma wakati mwingine bila uchunguzi wa kutosha. Hiyo ikasababisha kuwa na mikopo ambayo hailipiki. “Baadaye ilikuja kuwa offloaded  kwa taasisi moja.

“Kwa kiasi kikubwa kulikuwapo ukosefu wa ushindani. Benki Kuu ilikuwa haifanyi udhibiti wa mabenki kama inavyofanya sasa hivi. Kulikuwapo mfumko wa bei na thamani ya shilingi ilikuwa inaanguka. Wakati tathmini inafanyika mwaka 1989 hii ndiyo iliyokuwa hali na iliundwa Presidential Commission of Inquiry – Mwenyekiti wake alikuwa Charles Nyirabu. Hitimisho moja la ripoti hiyo ilisema mfumo wa fedha ulishindwa jukumu lake la kuchagiza kuwekeza kwa ajili ya kuendeleza uchumi.”

724 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!