Unatakiwa kumpa mtu notisi lakini haujui anakoishi, hauna pa kumpata, au unajua anakoishi lakini anakukwepa.

Wakati mwingine ukienda kwake haufunguliwi mlango au hata ukifunguliwa unaambiwa hayupo. Au yupo umemuona lakini anakataa kabisa kupokea notisi au kuisaini.

Unafanya nini katika mazingira kama hayo na sheria inasemaje?

Kumbuka notisi zinazoongelewa hapa ni zile zinazotokana na masuala ya ardhi. Mfano, notisi ya kuondoka katika pango, notisi ya kusitisha mkataba, notisi ya kujitoa katika mauzo ya ardhi, notisi ya kumtaka mwenye nyumba kufanya jambo fulani, notisi ya kutaka kunadisha ardhi, n.k.

 

1. Nini ufanye?

Nini ufanye, inategemea na ardhi husika iko wapi. Ikiwa ardhi husika ipo kijijini zipo taratibu zake na ikiwa ni maeneo ya mijini halikadhalika zipo taratibu zake.

 

(a) Kwa ardhi za mijini

Kifungu cha 169 (b) cha Sheria ya Ardhi kinaeleza nini ufanye katika mazingira ya notisi kama hayo.

Kinasema, kwanza, ikiwa anafahamika anapoishi lakini hajitokezi, basi notisi hiyo itabandikwa nje ya ardhi hiyo. Kama ni nyumba, notisi itabandikwa kwenye mlango au ukutani kwa nje.

Maana yake, utabandika sehemu anakoishi huyo mtu au kwenye eneo la mgogoro au sehemu zote mbili.

Pili, inaruhusiwa pia kubandika notisi kwenye ofisi ya serikali za mitaa. Lakini hili ni chaguo la pili baada ya lile la kwanza kushindikana.

Na iwe ni ofisi za serikali za mtaa ule ambamo mtu huyo anaishi au mtaa ambao ardhi husika ipo.

Tatu, ni kuweka tangazo la notisi kwenye vyombo vya habari hasa magazeti. Hii ipo Kifungu cha 168 (1) (b) cha Sheria ya Ardhi. Waweza kuweka kwenye gazeti moja au zaidi.

Suala la msingi ni kuwa gazeti hilo liwe linafika eneo mtu huyo anapoishi. Isiwe ardhi iko Tanzania halafu ukatoa notisi kwenye gazeti la Uganda.

 

(b) Kwa ardhi za vijijini

Utaratibu wa kutoa notisi kwa mtu ambaye hajulikani alipo au anayekataa/kukwepa kupokea notisi kwa ardhi za vijijini hautofautiani sana na huu hapo juu wa ardhi za mijini.

Isipokuwa kwa ardhi za vijijini, inaongeza namna nyingine moja, kuwa notisi inaweza kutangazwa au kusomwa kwenye mkutano wa kijiji.

 

2. Notisi kuwa katika maandishi

Ni muhimu kujua kuwa notisi yafaa iwe katika maandishi. Iwe katika maandishi yenye lugha ambayo mhusika anaifahamu.

Lakini pia iwe imeandikwa kwa maandishi ambayo yanaweza kusomeka na kueleweka kwa urahisi.

Notisi ambayo haipo katika uandishi na mpangilio mzuri wa kusomeka, inampa nafasi mhusika kujitetea kuwa hakuelewa notisi ilimaanisha nini.

 

Kuhusu sheria za ardhi, mirathi, makampuni, ndoa n.k, tembelea SHERIA YAKUB BLOG.

546 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!