Hongera sana ndugu wasomaji wa JAMHURI kwa kuuanza Mwaka Mpya wa 2013. Wiki kadhaa huko nyuma tulichapisha makala katika safu hii iliyokuwa na makosa katika kichwa cha habari, hivyo kuleta usumbufu wa kimantiki kwenu wasomaji.

Kichwa hicho kilichokosewa kilisomeka hivi: “Wafanyabiashara wanapaswa “kuolewa bongo zao”. Tunapoanza Mwaka Mpya nimeona ni busara niirudie makala ile katika maana na dhana niliyoikusudia.

Novemba 11, 2012 nilikuwa mmoja ya watu waliohudhuria semina ya biashara na ujasiriamali katika ukumbi wa Matumaini Centre, Sabasaba mjini Iringa. Semina hii iliendeshwa na mtaalamu na mshauri wa kimataifa wa masuala ya biashara na ujasiriamali, Perecy Ugula, kupitia kampuni yake ya Great Opportunity Consulting Limited (GOC Ltd).

 

Semina hii ilidhaminiwa na Benki ya Barclays Tawi la Iringa, kwa ajili ya kuadhimisha siku ya wafanyakazi wa benki hiyo. Waandaaji na wadhamini wa semina hii waliamua kuwafundisha akina mama na vijana wa kikundi cha Matumaini; mafunzo yaliyokuwa na dhima ya ujasiriamali katika mtazamo mpana. Mimi nilibahatika kuwa mmoja wa wageni walioalikwa na kampuni hii ya GOC Ltd katika semina hiyo.

Pamoja na kuwa nimekuwa nikichambua biashara na ujasiriamali katika magazeti, mitandao ya kijamii na kwenye blogs mbalimbali; kiukweli mafunzo niliyoyapata siku ile yamenifungua sana. Namna Mtaalamu huyu anavyofundisha, mbinu anazotumia, mvuto wa uwasilishaji mada zake na uzoefu wake uliotukuka katika ujasiriamali, vyote vilifanya ubongo wangu upate makali mapya.

Kutokana na hayo, nimepata bahati ya kumfahamu mkurugenzi huyu wa GOC Ltd, Ugula na timu yake. Kiukweli wamejipanga kuleta msaada na mageuzi makubwa katika sekta hii ya masuala ya ushauri wa kibiashara na ujasiriamali. Mkurugenzi Ugula ni mhitimu wa masuala ya kilimo kutoka SUA lakini ana mafunzo ya ngazi ya uzamili katika mambo ya uongozi wa ushirika.

Hayo yote tisa; kumi ni kuwa amehudhuria mafunzo ya ujasiriamali ya Umoja wa Mataifa (UN) chini ya Shirika la Kazi Duniani (ILO) na ametunukiwa cheti cha kuwa mkufunzi wa wakufunzi wa ujasiriamali. Katika nyanja ya kimataifa Ugula ni mmoja ya walimu (mentors) wanaowalea wajasiriamali vijana kutoka mataifa zaidi ya 120 duniani.

Malezi hayo yanafanyika kupitia mtandao wa YenMarketPlace. Mtandao huu una udhamini na mwongozo kutoka UN. Jambo la kufurahisha ni kuwa mtaalamu huyu na timu yake ya wataalamu, wanafanya biashara na ujasiriamali wakiwa na kampuni na miradi mbalimbali ya huduma na bidhaa.

Hivyo wanafundisha uhalisia na mambo ambayo wao wenyewe wanayafanya. GOC Ltd tayari imeshaendesha semina na mafunzo maeneo mengi hapa Tanzania kwa vikundi mbalimbali, mashirika yasiyokuwa ya kiserikali pamoja na taasisi za kimataifa, ikiwamo Winrock International. Nilipoyajua haya nikatambua kuwa nimekutana na ‘dhahabu’!

 

Ni kutokana na “dhahabu” niliyoibaini katika semina hii; ndipo nikaona si vema nikatawanyika pasipo kumdodosa mtaalamu huyu na huduma yake hii ambayo ni adhimu hapa Tanzania. Kama ambavyo nimekuwa na shauku ya kuwashirikisha wasomaji wetu fursa na mambo mema katika biashara na ujasiriamali; leo nimeona ngoja niwashirikishe fursa hii ya mafunzo na namna yanavyoweza kuboresha biashara zenu.

Pengine nitangulie kusema mambo mawili kuhusu ukienyeji wetu katika biashara na uzoefu kutoka kwa wenzetu. Wafanyabiashara wengi wa Tanzania tumekuwa tukifanya biashara kwa mazoea, kwa kienyeji na kubahatisha kwingi. Hatuna mbinu wala mafunzo ya kitaalamu kwa ajili ya kuendesha biashara zetu kwa tija.

Mambo ni tofauti kwa wafanyabiashara na wajasiriamali wenzetu waliopo katika nchi zilizoendelea. Hata majirani zetu Wakenya wametuzidi katika utamaduni huu wa kuhudhuria semina, warsha, makongamano ama matamasha mara kwa mara kujipatia mbinu mpya za kibiashara. Unapohudhuria semina, makongamano ama warsha hizi unapata wasaa wa kupata mbinu mpya.

Ilipomalizika semina hii nikamfuata mtaalamu huyu nikamweleza kwamba kuna wasomaji wetu waliotapakaa nchi nzima, ambao kila wiki wanafuatilia Anga za Uchumi na Biashara. Kiu ya wengi imekuwa ni kupata semina na maarifa ya ujasiriamali na biashara ambayo yatawatoa hatua moja kwenda nyingine.

Baada ya kumueleza haya Ugula, alinieleza kuwa kampuni yake ina majibu ya hitaji langu na la wasomaji wetu. Akatanabaisha kuwa madhumuni ya GOC Ltd ni kutoa huduma za ushauri wa kijasiriamali na programu za aina zote ziendanazo na biashara na miradi ya maendeleo.

 

Akanieleza kuwa wamekusudia kuziba ombwe la ukosefu wa maarifa, ujuzi, kanuni na mikakati endelevu miongoni mwa wafanyabiashara, taasisi za kimaendeleo, serikali pamoja na vikundi vingine vya kiuchumi zikiwamo SACCOS, FBOs na NGOs. Pia akanisisitiza kuwa kampuni yake imelenga kuwasaidia mtu mmoja mmoja, wale wote wenye kiu ya kufanikiwa kupitia ujasiriamali, wahitimu kutoka ngazi za elimu zote vikiwamo vyuo vikuu na makundi yanayojishughulisha na kuzisaidia jamii.

 

Katika kufuatilia machapisho yao, nikagundua GOC Ltd ni kampuni iliyokuja Tanzania kwa wakati husika. Nafahamu ombwe la maarifa lililopo miongoni mwa wajasiriamali wa nchi hii kutokana na namna wanavyonipigia simu, kuniandikia ujumbe wa simu na kompyuta pamoja na kukutana nami.

Wapo baadhi ya wasomaji ambao hufanikiwa kukutana nami; lakini ninapowasikiliza shida zao kuna wengine huwa nashindwa hata nianzie wapi kuwasaidia kutokana na ukosefu mkubwa wa kujitambua, kujiamini na imani kwa biashara zao. Mbinu za useminishaji nilizokutana nazo kwa Perecy Ugula na kampuni yake ya GOC Ltd vinatoa majibu mengi kama si yote kati ya yale yanayohitajiwa na wajasiriamali wengi.

Kwa kuwa maono ya kampuni hii ni kuwafikia na kufanya kazi na maelfu ya wadau wa maendeleo kwa njia ya ushauri wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii; huduma zao zimejielekeza katika maeneo matatu makubwa. Mafunzo maalumu ya elimu ya ujasiriamali ambayo yanalenga kujenga uwezo, uthubutu na ushindani katika biashara, huku mbinu zenye viwango na ithibati ya Umoja wa Mataifa vikiwa vinatumika.

 

Huduma nyingine ni mafunzo na karakana (workshops) za kibiashara zinazolenga kutumbukiza maarifa ya kibiashara katikati ya watu ambao ni wazoefu na wale waliokwishaanza biashara. Ni katika huduma hii ya pili ndipo wanapoendesha usajili wa biashara na michanganuo ya miradi.

Pia wanasaidia uandishi wa michanganuo ya kibiashara kwa ajili ya kuombea mikopo katika benki na mbinu za kubaini, kuibua na kutumia fursa za kibiashara. Suala la ongezeko la thamani, kutafuta masoko na usimamiaji wa biashara ni mambo yaliyojumuishwa humu.

Huduma ya tatu wanayoifanya ni kutoa huduma za ushauri kwa kadiri ya mahitaji maalumu ya wahitaji. Hapa ndipo waliponivutia sana; yaani ninyi kama ni kundi la wafanyabiashara, kikundi, VICOBA, ROSCAs ama SACCOs mnaweza kuwaita wataalamu hawa na kisha mkasema matatizo yenu halafu wao wakaandaa semina ama kifurushi cha mchanganuo unaojibu matatizo yenu kwa upana na usahihi.

 

Katika semina ile tulifundishwa mambo mengi mazuri lakini kuna jambo mkufunzi huyu alitupatia washiriki; ambalo liliniacha hoi na nikajiona kumbe ningali na ujinga mwingi katika biashara. Mkufunzi alitutaka washiriki tukae katika makundi matatu na tushikane mikono. Kisha akatuagiza kila mtu atulie kwa dakika kumi atafakari jambo lolote ambalo atalifanya ndani ya dakika tano.

Dakika kumi zikaisha na kila mmoja akatakiwa kufanya alichokifikiria. Wengine wakaanza kuhamisha viti, wengine wakakusanya chupa za maji, wengine wakaenda uani, wengine wakaanza kupigana picha; ilimradi tu ilikuwa vurugu ukumbini. Baadaye akachagua watu watatu waeleze nini waliwaza kukifanya na kama wamefanikiwa ama la!

Wa kwanza akasema alipanga kwenda uani (na amefanikiwa). Wa pili alipanga kupiga picha (na amefanikiwa). Wa tatu alipanga kukusanya chupa za maji (na amefanikiwa). Wa nne alipanga kupata namba ya mmoja wa washiriki (na hajafanikiwa). Katika mjadala uliofuatia majibu hayo ndipo mkufunzi alipotufumbua akili namna Watanzania tunavyoishi nusunusu tukiwa hatuna malengo yenye tija na yanayoelezeka.

Mathalani akaeleza kuwa mtu unaposema unataka kupiga picha; je, nani kakutuma? Unapiga kwa malengo gani na nani atakulipa ama kuinunua? Unasema unataka kukusanya chupa za maji, ili iwaje? Unazipeleka wapi na ni nini kimekusukuma kufanya unachofanya?

 

Awali jambo hili lilionekana kuwa la kitoto lakini udadavuzi wa mkufunzi huyu ulifanya kila mshiriki kukiri kuwa atakwenda kufikiria upya kuhusu biashara yake na maisha yake kwa ujumla. Ilidhihirika kuwa Watanzania wengi tunafanya mambo bila kuwa na picha kamili ya tunakokwenda na mafanikio tunayoyatafuta.

 

Kwa mfano, kama una biashara ya duka; hivi umeshawahi kujiuliza utafanyaje siku ukiamka asubuhi na kukuta duka lote limeungua? Je, kwa miaka mingapi ijayo utaendelea kuifanya biashara hiyo ya duka? Je, kama ukifariki leo umemwandaa nani kuhakikisha duka lako si tu linaendelea bali pia linakua?

 

Nimeendelea kuwasiliana na mkurugenzi huyu na timu yake ya GOC Ltd, kuangalia uwezekano wa kuzipeleka huduma zao kwa Watanzania wengi zaidi na zaidi. Bahati nzuri ni kuwa wameniruhusu kumuunganisha mtu yeyote, kikundi, taasisi ama asasi yoyote itakayokuwa na uhitaji wa huduma zao.

Kwa maana hii ninafurahi kuwajulisha wasomaji wa Anga za Uchumi na Biashara kuwa sasa popote ulipo, unaweza kuwasiliana nami kwa ajili ya msaada na ushauri wa kibiashara na kiujasiriamali kupitia kampuni hii ya GOC Ltd. Wafanyabiashara, wajasiriamali na Watanzania wote ni wakati wa kuamka na kuchangamkia fursa za kunolewa bongo zetu ili kupiga hatua ya kimaendeleo.

 

Sote tunahitaji ushindi wa kiuchumi.

 

[email protected], 0719 127 901



By Jamhuri