Kampuni ya uchimbaji madini – Acacia Gold Mine, imetoa notisi ya kutaka kujiondoa kuidhamini klabu ya Stand United ya mkoani Shinyanga, kutokana na mgogoro unaoendelea kufukuta klabuni hapo.

Acacia Gold Mine, imetangaza kuvunja mkataba wa udhamini huo endapo klabu hiyo itashindwa kumaliza mgogoro huo ambao umedumu kwa muda mrefu. Mdhamini huyo ametoa notisi ya miezi mitatu.

Mkataba baina ya Acacia Gold Mine na klabu ya Stand United wenye thamani ya shilingi bilioni 2, ulioingiwa msimu wa 2015/16, ulitakiwa kudumu kwa misimu miwili ya ligi. 

Kutokana na udhamini huo, klabu ya Stand United ilikuwa ni moja kati ya klabu bora kutoka Kanda ya Ziwa, huku udhamini huo ukishindana kwa karibu na klabu kubwa za Simba na Yanga.

Klabu ya Stand United imemaliza ligi ya msimu uliopita wa 2015/2016 ikiwa katika nafasi ya tisa kati ya klabu 14 zinazoshiriki Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL).

Udhamini huo umesaidia kuifanya klabu iweze kufanya vizuri katika michezoyake, pamoja na kuboresha programu mbalimbali za timu na kuendeleza vipaji pamoja na utawala.

Azma ya kujitoa iliyotangazwa na mdhamini Acacia Gold Mine, ni ishara mbaya kwa timu hiyo kuelekea kuanza kwa msimu mpya wa Ligi Kuu 2016/17, hali hiyo itasababisha klabu hiyo kubaki na fedha za mdhamini wa Ligi Kuu Vodacom Tanzania pamoja Televisheni ya Azam aliyenunua haki za matangazo.

Akizungumza na JAMHURI, msemaji wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Alfred Lucas, anasema mgogoro huo umetokana na fedha iliyomwagwa na mdhamini katika klabuhiyo.

Anasema mgogoro huo umekuwa mkubwa na unaonekana kukosa suluhu kutoka kwa viongozi wa shirikisho hilo, pamoja na wadau wengine wa mchezo wa soka.

“Ni masikitiko makubwa pia aibu kwa soka la Shinyanga kama wataendelea kutanguliza maslahi binafsi na kushindwa kutanguliza maendeleo ya soka na kuiacha klabu irudi ilikotoka,” anasema Lucas.

Anasema ushauri shirikisho kwa pande zinazosigana ni kukaa pamoja na kuelewana kwa manufaa mapana ya wapenda soka wote ndani na nje ya mkoa huo kwa lengo la kuiokoa klabu yao.

Anasema kupitia fedha ya udhamini, Acacia wangeweza kuchangia katika mambo mengine ya kijamii, lakini waliamua kuwekeza katika soka, hiyo itaacha doa kwa wadau wengine ambao walikuwa na nia ya kuwekeza kwenye soka.

Msemajiwa Stand United, Deo Kaji, anasema Acacia iliona umuhimu wa kuwekeza kiasi kikubwa cha fedha kwa lengo la kutaka kuinua kiwango cha soka katika Mkoa wa Shinyanga, ndoto ambayo inaelekea kuyeyushwa na baadhi ya watu wachache kwa ajili ya maslahi yao.

“Ni kweli mdhamini ametoa angalizo la miezi mitatu lakini hata kabla ya miezi hiyo kwisha tayari kuna utulivu wa hali ya juu na tunajiandaa na pambano letu la kufungua ligi dhidi ya Mbao FC kwenye Uwanja wa Kambarage Shinyanga,” anasema Kaji.

Anasema Stand United inajitahidi kufanya kila linalowezekana kuokoa mkataba baina yao na Acacia, vinginevyo klabu hiyo inaweza kujikuta inarudi ilikokuwa miaka ya nyuma.

“Ni aibu ndani ya Mkoa wa Shinyanga, sisi viongozi kuichimbia kaburi klabuyetu…tena kwa kuangalia maslahi binafsi, bila ya kuangalia hatima ya soka letu ndani ya mkoa na Taifa lote kwa ujumla,” anasema Kaji.

Anasema kuna haja ya viongozi wa klabu hapa nchini kutumia fedha za wadhamini kusaka vipaji, kuliko fedha hizo kugeuka kuwa vyanzo vya migogoro na kuendelea kulididimiza soka. 

Anasema migogoro inayotaka kuipoteza klabu ya Stand katika ramani ya soka hapa nchini haina budi kupigwa vita na watu wote wenye nia ya dhati ya kuliona soka la Tanzania likipiga hatua.

1168 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!