1. LESENI HUTOLEWA KWA NAMNA MBILI

Unapohitaji leseni ya kutafuta madini unapaswa kujua kuwa leseni hizi hutafutwa kwa namna mbili tofauti. Kwanza kwa maombi maalum na pili kupitia zabuni. Sheria mpya ya madini Sheria namba 14 ya 2010 ndiyo kiini cha makala hii.

 

2. LESENI KWA MAOMBI MAALUM

Kwa maombi maalum ni hatua ya kawaida ya kuomba kama unavyoweza kuomba kazi au zabuni yoyote ambayo haijatangazwa na Serikali.

Hatua hii huja baada ya mjasiriamali kuliona eneo la madini na kuamini kuwa anaweza kuwa sehemu ya biashara ya eneo hilo.

Maombi hufanywa katika fomu maalum ambazo hupatikana kwa Kamishna wa Madini. Makamishna wa Madini hupatikana hata wilayani au mikoa na hivyo inategemea ni sehemu ipi unataka kutafuta hayo madini.

Kubwa ni kuwa kuna utata kwa kutumia wilaya au mkoa husika katika kupata fomu hiyo kwa ajili ya kutuma hayo maombi.

 

(a) ILI KUPATA LESENI SIYO LAZIMA UMILIKI KAMPUNI

Ipo dhana inayofifisha jitihada za baadhi ya wajasiriamali wenye ndoto na biashara hii kwa kudhani kuwa leseni hutolewa kwa kampuni tu, tena kampuni kubwa. Hii si kweli kwani hata mtu binafsi anaweza kuomba leseni. 

Hii ni kwa mujibu wa kifungu cha 28 (1) cha Sheria ya Madini. Kwa hiyo, inafaa sana kueleweka kuwa suala la utafutaji wa madini halihusu kampuni bali hata watu binafsi wanaweza kuomba leseni hizo na kupata.

 

(b) TAARIFA ZIPI ZINAHITAJIKA KWA MTU BINAFSI NA KAMPUNI

Unapotuma maombi ukiwa kama mtu binafsi utatakiwa kuainisha majina matatu kamili, uraia wako, anuani ya posta ikiwa ni pamoja na anuani kamili ya makazi, sambamba na hilo iandaliwe picha ya sasa ya pasipoti. 

Na kama ni jina la kampuni kitahitajika cheti cha usajili, majina ya wakurugenzi na uraia wao. Pia kwa wote mwombaji binafsi au kampuni atatakiwa kuainisha aina ya madini anayoomba kutafuta, ikiwa ni madini ya malighafi ujenzi, madini ya viwandani, almasi, madini chuma n.k.

 

3. LESENI KWA ZABUNI

Maombi kwa njia ya zabuni yameainishwa katika kifungu cha 29 (1) cha Sheria ya Madini.

Mchakato wa kawaida wa kumtafuta mzabuni ndiyo utakaohusishwa katika maombi haya. 

Mamlaka husika zitatangaza zabuni na washindani watajitokeza kwa njia ya maombi. Hapa maombi yataandaliwa kwa kufuata utaratibu wa jumla utakaokuwa umeelekezwa kwenye tangazo la zabuni hiyo. 

Kwa mujibu wa kifungu hicho, maombi yatawasilishwa kwenye bodi ya ushauri wa madini.

Bodi ya ushauri wa madini ni chombo kinachoanzishwa na kifungu cha 23 (1) ambacho jukumu lake kubwa ni kumshauri waziri mwenye dhamana ya madini masuala yanayohusu madini. 

 

4. WAJIBU KWA ALIYEPATA  LESENI

(a) Kwanza ni kuanza utafutaji wa madini mapema ndani ya miezi mitatu tangu kupata leseni.

(b) Kuzingatia mpango wa utafutaji ulioainishwa kwenye leseni, na

(c) Utafutaji usiwe chini ya kiwango kwa mujibu wa leseni husika.

 

Kuhusu sheria za ardhi, mirathi, kampuni, ndoa n.k, tembelea SHERIA YAKUB BLOG.

By Jamhuri