Taarifa hii imetumia takwimu za shehena ya mizigo iliyopitia bandari ya Dar es Salaam kwa kipindi cha miaka miwili, Mwaka 2014 na 2015. Aidha, uchambuzi wa kina umefanyika kwa kipindi cha mwezi Julai hadi Aprili katika Mwaka wa Fedha wa 2015/2016 ikilinganishwa na shehena kama hiyo kwa Mwaka wa Fedha wa 2014/2015.  Sambamba na tathmini ya mizigo, tathmini ya mwenendo wa ukusanyaji wa ushuru wa forodha katika kipindi husika imefanyika.

Tathmini hii pia imelinganisha uchambuzi linganifu (comparative analysis) juu ya mwenendo wa uingiaji wa shehena za mizigo katika bandari ya Dar es Salaam na Mombasa ili kubaini ulingano wa ufanisi (Comparative performance) na athari za kikanda na dunia kwa ujumla.  

Matokeo ya mchanganuo huu utasaidia kubaini sababu za muda mrefu (underlying factors) na muda mfupi (immediate factors) ambazo kwa namna moja au nyingine zimechangia katika kushuka kwa shehena ya mizigo inayoingia nchini kupitia bandari ya Dar-es-Salaam.

•        Shehena za mizigo inayoingia nchini kupitia bandari ya Dar es salaam

Bandari ya Dar es Salaam inahudumia zaidi ya asilimia 90 ya shehena yote ya mizigo inayoingia nchini kwa matumizi ya ndani (Imports) na shehena  zinazokwenda nchini za jirani (Transit) kama vile Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Rwanda, Burundi, Uganda, Malawi na Zimbabwe.

2.1 Mwenendo wa shehena kwenye Kontena, 2014/15 – 2015/16

Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita shehena ya mizigo kwenye Kontena katika bandari ya Dar es Salaam imepungua kutoka kontena 196,620 mwaka 2014/15 hadi kufikia kontena 171,863 mwaka 2015/16. Katika kipindi cha miezi Julai 2015 hadi Aprili 2016, shehena ya mizigo iliyoingia katika bandari ya Dar es salaam ilipungua kutoka kontena 16,762 mwezi Julai 2015 hadi kufikia kontena 16, 235 mwezi Aprili 2016 sawa na upungufu wa asilimia 3. Ukilinganisha na shehena ya mizigo iliyoingia bandarini kwa kipindi kama hicho mwaka uliopita, shehena hii ilipungua kwa asilimia 13 kama inavyooneshwa katika Jedwali na. 1a pamoja na Grafu na. 1a.

 

Jedwali na 1a: Shehena za Kontena kwa Kipindi cha 2014/15 – 2015/16

 

2.2 Mwenendo wa Shehena za Magari, 2014/15 – 2015/16

 

Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita shehena ya mizigo ya magari yaliyopokelewa katika bandari ya Dar es Salaam imepungua kutoka magari 107,482 mwaka 2014/15 hadi kufikia magari 93,635 mwaka 2015/16. Katika kipindi cha miezi Julai 2015 hadi Aprili 2016, shehena ya magari iliyoingia katika bandari ya Dar es Salaam ilipungua kutoka magari 12,428 mwezi Julai 2015 hadi kufikia magari 7,780 mwezi Aprili 2016 sawa na upungufu wa asilimia 37. Ukilinganisha na idadi ya magari yaliyoingia bandarini kwa kipindi kama hicho Mwaka uliopita, shehena hii ilipungua kwa asilimia 13 kama inavyooneshwa katika Jedwali na. 1b.

 

Jedwali na 1b: Shehena ya Magari kwa kipindi cha 2014/15 – 2015/16

 

2.3   Mwenendo wa shehena  za Kontena kwa Nchi ziendako, 2014/15 – 2015/16

Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, shehena ya mizigo ya kontena imepungua kutoka kontena 196,620 mwaka 2014/15 hadi kufikia kontena 171,863 mwaka 2015/16, sawa na asilimia 13.

Kwa kipindi cha Mwezi Julai 2015 hadi Aprili 2016 jumla ya kontena 171,863 yalipokelewa katika bandari ya Dar es Salaam, kati ya hayo asilimia 71.5 ambayo ni makontena 122,842 yalikua ni kwa matumizi ya ndani (home use), asilimia 10.7 ambayo ni makontena 18,458 yalipelekwa Rwanda, asilimia 7.4 sawa na makontena 12,660 yalipelekwa Zambia, asilimia 7.0 sawa na makontena 12,014 yalipelekwa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), asilimia 2.6 sawa na makontena 4,525 yalipelekwa Burundi, asilimia 0.5 sawa na makontena 824 yalipelekwa Malawi na asilimia 0.3 sawa na makontena 540 yalipelekwa nchini Uganda.

Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, shehena za mizigo ya kontena iliyopokelewa kwa ajili ya matumizi ya ndani imepungua kutoka kontena 138,616 mwaka 2014/15 hadi kufikia kontena 122,842 mwaka 2015/16, sawa na asilimia 11. Kwa kuwa sehemu kubwa ya mizigo iliyopokelewa na bandari ya Dar es Salaam hubaki nchini hivyo imekua na madhara kidogo kwenye makusanyo ya ushuru wa forodha. Ukilinganisha kontena zinazopitia  bandari ya Dar es Salaam kwenda nchi jirani (transit) idadi ya makontena yanayokwenda Rwanda yameongezeka kwa asilimia 16 kutoka makontena 15,867 mwaka 2014/15 kufikia makontena 18,458 mwaka 2015/16 wakati makontena yaendayo Zambia na Burundi yamepungua kwa asilimia 30 kutoka kontena 18,169 (Zambia) na 6,466 (Burundi) mwaka 2014/15 hadi kufikia kontena 12,660 (Zambia) na 4,525 (Burundi) Mwaka 2015/16. Kontena ziendazo DRC zimepungua kwa asilima 25 kutoka kontena 15,927 mwaka 2014/15 hadi kufikia kontena 12,014 mwaka 2015/16. Wakati makontena yaendayo Malawi yamepungua kwa asilimia 16 kutoka makontena 983 mwaka 2014/15 mpaka 824 mwaka 2015/16, makontena yaendayo Uganda pia yamepungua kwa asilimia 9 kutoka kontena 592 mwaka 2014/15 hadi kontena 540 mwaka 2015/16 kama inavyooneshwa kwenye Jedwali na. 2a.

 

Jedwali na. 2a: Shehena  za Kontena kwa Nchi Ziendako, 2014/15-2015/16

Chanzo: Idara ya Ushuru na Forodha, Mamlaka ya Mapato Tanzania

 

2.4    Mwenendo wa shehena za Magari kwa Nchi yaendako, 2014/15 – 2015/16

Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, shehena ya magari yaliyopokelewa katika bandari ya Dar es Salaam imepungua kutoka magari 107,482 mwaka 2014/15 hadi kufikia magari 93,635 mwaka 2015/16, sawa na asilimia 13.

Kwa kipindi cha Mwezi Julai 2015 had Aprili 2016 jumla ya magari 93,635 yalipokelewa katika bandari ya Dar es Salaam, kati ya hayo asilimia 45.5 ambayo ni magari 42,601 yalikua ni kwa matumizi ya ndani (home use), asilimia 21.2 ambayo ni magari 19,843 yalipelekwa Zambia, asilimia 11.7 sawa na magari 10,943 yalipelekwa DRC, asilimia 11.3 sawa na magari 10,582 yalipelekwa Malawi, asilimia 5.6 sawa na magari 5,250 yalipelekwa Rwanda, asilimia 3.9 sawa na magari 3,619 yalipelekwa Burundi na asilimia 0.9 sawa na magari 797 yalipelekwa nchini Uganda.

Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, idadi ya magari yaliyoingia bandarini kwa ajili ya matumizi ya ndani imepungua kutoka magari 46,519 mwaka 2014/15 hadi kufikia magari 42,601 mwaka 2015/16, sawa na asilimia 8. Ukilinganisha idadi ya magari yaliyopitia bandari ya Dar es Salaam katika kipindi husika, kiasi cha magari yaliyopelekwa Rwanda kiliongezeka kutoka magari 3.499 mwaka 2014/15 hadi magari 5,250 sawa na asilimia 50, magari yaliyopelekwa Burundi yaliongezeka kwa asilimia 19 kutoka magari 3,034 mwaka 2014/15 hadi magari 3,619 mwaka 2015/16, kiasi cha magari ya Uganda kiliongezeka kwa asilimia 18 toka magari 674 mwaka 2014/15 hadi magari 797 mwaka 2015/16, idadi ya magari yaliyokwenda Malawi iliongezeka kwa asilimia 14 toka magari 9,323 mwaka 2014/15 hadi kufikia 10,582 mwaka 2015/16. Hata hivyo, idadi ya magari yaendayo Zambia ilipungua kwa asilimia 40 kutoka magari 33,146 mwaka 2014/15 hadi magari 19,843 mwaka 2015/16 wakati magari yaendayo DRC yalipungua kwa asilimia 3 toka magari 11,290 mwaka 2014/15 hadi 10,943 mwaka 2015/16 kama inavyooneshwa katika Jedwali na. 2b na Grafu na. 2b. Kiasi kikubwa cha magari kilichopungua ni magari yaendayo Zambia na DRC.

 

• Ukusanyaji mapato kwa kipindi cha Julai 2015 – APRILI, 2016

3.1    Mapato ya Idara ya Forodha Kwa Ujumla, 2014/15 – 2015/16

Katika kipindi cha miezi kumi ya mwaka wa Fedha 2015/16 mapato halisi ya kodi idara ya Forodha, Tanzania Bara, yalifikia Shilingi za Kitanzania milioni 4,358.7 ukilinganisha na lengo la kukusanya Shilingi za Kitanzania milioni 4,416.2 sawa na asilimia 98.7 ya lengo kama inavyooneshwa katika Jedwali na. 3a. Makusanyo haya ni sawa na ongezeko la asilimia 29.3 ukilinganisha na makusanyo yaliyofikiwa katika kipindi kama hiki katika mwaka wa fedha 2014/15, ambayo ni sawa na Shillingi za Kitanzania milioni 3,371.6.

 

Jedwali Na. 3a:      Mapato ya Idara ya Forodha kwa Mwaka 2014/15 – 2015/16

3.2   Mapato Yatokanayo na Uingizaji wa Mizigo Bandarini, 2014/15 – 2015/16

Katika kipindi cha mwaka 2015/16 bandari ya Dar es Salaam iliingiza kiasi cha Shilingi za Kitanzania milioni 14,018.5. Kiasi hicho ni sawa na asilimia 1.3 pungufu ya kiasi ambacho bandari iliingiza kwa mwaka 2014/15, ambacho ni Shilingi za Kitanzania milioni14,196.8 kama inavyooneshwa katika Jedwali na. 3b na Grafu 3b.

• Ulinganifu wa mwenendo wa shehena za mizigo kupitia bandari ya Mombasa na bandari ya Dar es Salaam.

• Shehena ya Kontena Zipitazo Bandari ya Mombasa, 2014/15-2015/16

Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita shehena ya mizigo kwenye Kontena katika bandari ya Mombasa imepungua kutoka kontena 85,692  mwaka 2014/15 hadi kufikia kontena 77,085 mwaka 2015/16. Katika kipindi cha miezi Julai 2015 hadi Machi 2016, shehena ya mizigo iliyoingia katika bandari ya Mombasa ilipungua kutoka kontena 94,344 mwezi Julai 2015 hadi kufikia kontena 77,085  mwezi Machi 2016 sawa na upungufu wa asilimia 18.3. Ukilinganisha na shehena ya mizigo iliyoingia bandari ya Mombasa kwa kipindi kama hicho mwaka uliopita, shehena hii ilipungua kwa asilimia 1.0 kama inavyooneshwa katika Jedwali na. 4a pamoja na Grafu na. 4a.

 4.2   Mwenendo wa shehena  za Kontena katika Bandari ya Mombasa kwa Nchi ziendako, 2014/15 – 2015/16

Kwa kipindi cha Mwezi Julai 2015 had Machi 2016 jumla ya kontena 280,107 yalipokelewa katika bandari ya Mombasa, kati ya hayo asilimia 71.6 ambayo ni makontena 200,646 yalikua ni kwa matumizi ya ndani (home use), asilimia 21.7 ambayo ni makontena 60,684 yalipelekwa Uganda, asilimia 2.8 sawa na makontena 7,722 yalipelekwa South Sudan, asilimia 1.4 sawa na makontena 3,893 yalipelekwa DRC, asilimia 1.3 sawa na makontena 3,611 yalipelekwa Tanzania, asilimia 1.1 sawa na makontena 2,976 yalipelekwa Rwanda, asilimia 0.1 sawa na makontena 228, 174, 167 yalipelekwa nchini Somalia, Ethiopia na Burundi na asilimia 0.0 sawa na makontena 6 yalipelekwa nchini Zambia.

Kama ilivyo kwa bandari ya Dar es Salaam, katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, shehena ya mizigo ya kontena katika bandari ya Mombasa imepungua kutoka kontena 292,926 mwaka 2014/15 hadi kufikia kontena 280,107 mwaka 2015/16, sawa na upungufu wa asilimia 4 kama inavyooneshwa kwenye. Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, shehena za mizigo ya kontena iliyopokelewa kwa ajili ya matumizi ya ndani ya Kenya imeongezeka kutoka kontena 187,016 mwaka 2014/15 hadi kufikia kontena 200,646 mwaka 2015/16, sawa na asilimia 7. Idadi ya makontena yanayokwenda Uganda imepungua kutoka makontena 75,253 mpaka makontena 60,684 sawa na asilimia 21.7, South Sudan yamepungua kwa asilimia 47 kutoka makontena 14,563 mwaka 2014/15 kufikia makontena 7,722, kontena ziendazo Rwanda  zimepungua kwa asilima 37 kutoka kontena 4,703 mwaka 2014/15 hadi kufikia kontena 2,976 mwaka 2015/16. Wakati makontena yaendayo DRC yamepungua kwa asilimia 30 kutoka makontena 5,573 mwaka 2014/15 mpaka 3,893 mwaka 2015/16, makontena yaendayo Tanzania pia yamepungua kwa asilimia 19 kutoka kontena 4,448 mwaka 2014/15 hadi kontena 3,611 mwaka 2015/16, Kontena ziendazo Burundi  zimepungua kwa asilima 75 kutoka kontena 668 mwaka 2014/15 hadi kufikia kontena 167 mwaka 2015/16, Kontena ziendazo Somalia  zimepungua kwa asilima 67 kutoka kontena 699 mwaka 2014/15 hadi kufikia kontena 228 mwaka 2015/16. Kontena ziendazo Ethiopia na Zambia zimeongezeka kwa asilimia 100 toka kontena 0 na 3 mwaka 2014/15 mpaka kontena 174 na 6 mwaka 2015/16 (Jedwali na. 4b).

• Sababu za upunguaji wa shehena za mizigo katika bandari ya Dar es Salaam.

Sababu  za kupungua kwa shehena ni pamoja na hizi zifuatazo:-

• Miundombinu hafifu

• Uwingi wa tozo katika bandari yetu ikilinganishwa na bandari jirani

• Kuanzishwa kwa Himaya ya Forodha ya pamoja

• Sheria kali za matumizi ya barabara

• Ushindani wa kibiashara

 • Miundo Hafifu 

Miundombinu hafifu ya usafirishaji hasa kwa njia ya reli huwalazimisha wateja kusafirisha mizigo yao kwa njia ya  barabara  tu. Mizigo huchukua muda mrefu kumfikia mteja na pia husababish gharama. Mizigo inayosafirishwa kwa njia ya barabara huchukua muda mrefu kumfikia mteja kutokana na vikwazo mbalimbali vilivyopo barabarani na mipakani. Kuimarika kwa miundombinu ya  nchi jirani  hasa Msumbiji        kumewavutia baadhi ya wateja hasa  kutoka nchi za Zambia na Malawi, kutumia zaidi bandari ya Beira na Nacala.

 • Uwingi wa tozo katika bandari yetu ikilinganishwa na bandari jirani

Uwingi wa tozo (charges) katika bandari ya Dar es Salaam: Malalamiko ya wateja yamejikita hasa katika maeneo     yafuatayo:-

• “Warehouse rent” inayotozwa na TRA pamoja na “Storage charges” zinazotozwa na TPA kwa mzigo huohuo.       

• Sheria ya ongezeko la thamani (VAT) kwa mizigo ya nchi jirani ambapo bandari zingine hazitozi kodi      hiyo.

• Gharama kubwa zinazotozwa na Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa mizigo wanayokagua ambapo zilipanda kutoka Dola 100 ya kimarekani kwa mzigo wote hadi kufikia Dola 1 kwa tani ndani ya muda mfupi.

 • Vibandiko vya SUMATRA (Stickers): SUMATRA ilikuwa ikitoza Sh. 7,000/= kwa ajili ya “sticker” kwa mwaka, kwa sasa imefikia Sh. 120,000/= kwa mwaka.

• Usalama mdogo njiani wakati wa kusafirisha mizigo ya thamani kubwa Kama Shaba na kuongeza gharama za ulinzi inapokuwa njiani: Kwa mizigo inayopitia bandari ya Dar es Salaam, gharama hizo hulipwa na mteja wakati kwa mizigo inayopitia katika bandari za Afrika ya Kusini, gharama hizo hulipwa na msafirishaji.

 Tozo hizi zote huongezeka katika gharama za kawaida na kusababisha bandari yetu kuwa ghali.

• Kuanzishwa kwa Himaya ya Forodha ya pamoja

Kuanzishwa kwa himaya moja ya Forodha (Single Customs Territory) kumelazimu kodi kwa ajili ya mizigo ya nchi jirani kutozwa hapa nchini kabla haijaondoshwa bandarini. Mfumo huu haupendwi na wafanyabiashara wa kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ambao wangependa kulipia kodi hizo baada ya mzigo kufika katika nchi yao Kama wanavyofanya kwa mizigo inayopitia bandari zingine ambazo hazitumii mfumo wa ‘Single Customs Territory’.

• Sheria kali za matumizi ya barabara nchini

• Kutoruhusu matumizi ya magari makubwa ya inter-links: Nchi jirani za Kusini mwa Afrika ikiwemo Zambia, zinaruhusu matumizi ya magari hayo hivyo kutoa wigo mpana kwa mteja kusafirisha mizigo yake kupitia katika bandari zingine ambazo zimaruhusu Magari aina zote.

•Udhibiti wa kupindukia unaofuatiwa na kuwepo kwa vituo vingi vya ukaguzi kwa maana ya mizani na vya Polisi. Vituo hivyo huwachelewesha wateja na kuwasababishia gharama kubwa za usafirishaji kupitia bandari ya Dar es Salaam.

• Utitiri wa “Regulatory agencies” ambao huchelewesha uondoshaji wa mizigo bandarini na kuongeza gharama kwa wateja.

• Ushindani wa kibiashara

Kuongezeka kwa ushindani wa kibiashara ambapo mgawo wa shehena (traffic share) kupitia bandari ya Dar es Salaam umekuwa ukipungua ikilinganishwa na mgawo wa nchi jirani (Ona Jedwali Na. 5).

 

I SHINDANI:

 

HITIMISHO

6.1  Sababu nyingi zinazosababisha kupungua kwa mzigo kupitia bandari ya Dar es Salaam ni za muda mrefu na zilishajadiliwa katika maeneo mbalimbali na mapendekezo kadhaa kutolewa kwa taasisi husika. Matokeo ya kuchelewa kuchukua hatua         stahiki kwa wakati muafaka ni kupungua kwa shehena inayopitia katika bandari ya Dar es Salaam.    

 

6.2 TPA imekuwa ikifanya maboresho mbalimbali katika utoaji wa huduma ikiwemo ununuzi wa vitendea kazi na matumizi ya mifumo kwenye maeneo ya      ulinzi na usalama, malipo, uhudumiaji wa shehena na meli. Jitihada hizo pekee hazitoshi, ni vema kila mdau akatimiza wajibu wake katika kuboresha huduma za bandari.

Mapendekezo

Ili kuzuia kupungua kwa shehena kupitia Bandari ya Dar es salaam ni vema uamuzi ukafanyika mapema katika maeneo ambayo wateja wetu wamekuwa wakiyalalamikia kama ifuatavyo:-

7.1  VAT kwa mizigo inayokwenda/kutoka nchi jirani iondolewe haraka kwa kuwa sheria hiyo haitumiki katika bandari zingine shindani na inatufukuzia wateja.

7.2  Kurejea upya viwango vya tozo  mbalimbali vinavyolalamikiwa na wateja mfano kutoka tozo ya Dola za Kimarekani 23.00 kwa tani hadi Dola 16.00 kwa tani kwa mzigo wa shaba ili bandari   yetu         iweze kukabiliana na ushindani uliopo. Bandari ya Durban hutoza Dola za kimarekani 17.86 kwa tani wakati bandari ya Walvis Bay hutoza Dola za Kimarekani 21.00 kwa tani kwa mzigo kama huo.

7.3  Makubaliano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya D.R. Congo kuhusu Himaya Moja ya Forodha (Single Customs Territory) yasitishwe kwa kuwa utaratibu huo hauinufaishi Tanzania badala yake unachangia kukimbiza wateja wa Bandari.

7.4 Tozo za “Storage” na “Warehouse rent” zinamtoza mteja mara mbili kwa kitu kile kile. Tozo ya TRA ya “Warehousing rent” iondolewe na kubaki ya TPA inayotokana na huduma ya kuhifadhi mzigo.

7.5  Shehena ya mafuta ya nchi jirani inayopitia katika ya Bandari ya Dar es Salaam, hupewa siku 30 iwe imeondoshwa kutoka nchini ambapo baada ya siku hizo mzigo huo unakuwa “localized”.  Siku hizo ziongezwe hadi kufikia siku 90 kabla ya  kuwa “localized” kama ilivyo katika Bandari shindani. Hii inatokana na ukweli kwamba, mteja anapokuwa na mzigo mkubwa hawezi kusafirisha mzigo wote kwa muda mfupi kwa kutumia magari ambayo ndiyo njia pekee ya kuaminika kwa sasa.

7.6 Uboreshaji wa reli: Kasi ya uboreshaji wa usafirishaji wa njia ya reli iongezwe kwani ni msaada mkubwa sana katika utendaji kazi wa Bandari. Wateja wakuu kama vile M/S Bakhressa hupitishia mzizigo yao iendayo katika masoko ya Uganda, Rwanda na Burundi katika Bandari ya Mombasa kutokana na kukosekana kwa huduma ya uhakika ya reli kwa upande wa Tanzania.

7.7 Wasafirishaji wa chai na kahawa hasa itokayo katika mikoa ya Kilimanjaro na Arusha hupitishia shehena hiyo katika Bandari ya Mombasa kwa sababu ndiko mnada wa mazao hayo uliko. Mnada wa mazao hayo urejeshwe kama zamani ili kuvutia wasafirishaji hao kutumia Bandari zetu.

7.8 Ili kuondoa malalamiko na matatizo yanayolalamikiwa na wateja kuhusu utendaji kazi wa Bandari Kavu (ICD), TPA iruhusiwe kuendelea na mpango wake wa kuwa na eneo la kuhifadhia mizigo kule Kisarawe.

7.9 Kutokana na hatua zitakazochukuliwa na Serikali, TPA ikishirikiana na wadau wa Bandari ichukue hatua za haraka kuinadi Bandari yetu na kuwaeleza wateja wetu kuwa vikwazo walivyokuwa wanalalamikia vimeondolewa.

By Jamhuri