Serikali ya Awamu ya Tano sasa imekamilisha safu yake ya watumishi wa kuiendesha, Rais John Magufuli alichukua muda wa wiki/miezi kadhaa kabla hajateua wasaidizi wake na kuunda Baraza lake la Mawaziri.

Baada tu ya kujenga Serikali yake kwa kuteua Mawaziri na Naibu Mawaziri akageukia kupanga safu ya wasaidizi wa kisiasa. Hapo akateua wawakilishi wake katika mikoa na wakuu wa kumwakilisha katika wilaya. Wateule wote hao wakala viapo vyao vya utii pale Ikulu na kisha wakala viapo vya maadili ya uongozi kwa Kamishna wa Maadili ya Uongozi wa Umma, Jaji Salome Kaganda.

Baada ya kuridhika amepata wawakilishi wake mikoani na wilayani, sasa Rais akageukia kuteua watendaji wa Serikali yake mpya. Ndipo aliteua waendeshaji wa Serikali wa Mikoa kiutawala wa Serikali Kuu. Hawa ndio tunawaita ma-RAS yaani ma -Regional Administrative Secretaries. Nao wakaapa na kuahidi kutenda kazi zao kwa mujibu wa maadili ya uongozi wa Taifa letu.

Alipokamilisha safu hii ya watendaji akamalizia mapema mwezi wa Julai kuteua watendaji wakuu wa Serikali za Mitaa. Hapo sasa akawachambua kwa uangalifu wasomi na kuwabebesha zigo la kuendesha Serikali katika Majiji, Miji na Halmashauri za Wilaya. Watendaji hawa ndio Wakurugenzi wa Majiji, Miji na Halmashauri za Wilaya. Wanajulikana kama Wakurugenzi wa Majiji (City Directors), Wakurugenzi wa Manispaa (Municipal Directors) na Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya (District Executive Directors – DED).

Hawa ndio wateule wake wa mwisho walioapishwa pale Ikulu, Julai. Mheshimiwa Rais alitumia nafasi hii kuwaasa wateule wasomi hawa kuwa waende wakatende kazi zao kwa ufanisi mkubwa. Walikuwa wasomi na waliteuliwa baada ya uchunguzi mkubwa (proper scrutiny) kielimu, kimaadili na kwa utendaji kazi wao. Akawaagiza kwenda kuwatumikia wananchi wanyonge ambao kwa maoni yake (Mkuu huyu wa nchi) wametaabika sana na kuwa na kero nyingi na za muda mrefu. Aliwataka Wakurugenzi hao kwenda kuwapunguzia wananchi hizo KERO zao.

Moja ya jukumu alilowaagiza kuanzia Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na sasa Wakurugenzi hawa ambao ndio Watendaji Wakuu, ni kumaliza tatizo sugu lile la wafanyakazi HEWA (Ghost servants) katika Serikali. Hili mimi ninaliita ni donda ndugu katika Serikali yenye utawala bora na lilimpotezea kazi mkuu mpya mmoja wa wateule wa Rais katika Mkoa wa Shinyanga.

Mawaziri wote ni wasomi. Kuna maprofesa, madokta, mainjinia na kadhalika. Wakuu wa mikoa ni wasomi na majenerali wa majeshi ya ulinzi na usalama. Ma-RAS wote ni wasomi na makamishna wakuu wa Polisi, sasa wanafuata hawa Wakurugenzi wa Majiji, Miji na Halmashauri za Wilaya- nako wote ni wasomi.

Hapo inatokeaje kuwapo watumishi hewa katika Serikali yetu huku watumishi waliopo kama wahasibu, maafisa utumishi nao ni wasomi? Nini kinakosekana katika utumishi wa umma? Kikigundulika hicho, watumishi hewa hawatakuwapo. Baada ya kutafakari na kujiuliza maswali kadhaa nikaona niombe msaada kutoka kwa wenzangu kuelimisha umma. Nani msomi? Je, kila msomi ameelimika? Nini maana ya KUELIMIKA? Uwazi na ukweli wenu wasomaji utasaidia.

Nchini tunao wasomi wengi mno. Sina uhakika kama tunao waelimika wengi pia. Kule Kagera wasomi kwa jina la utani mitaani wanaitwa akina “NSHOMILE” ni watu waliokwenda shuleni wakapata ujuzi fulani.

Hivyo wanatofautishwa na wale wasiobahatika kwenda shule na kupata huo ujuzi. Si hivyo tu, bali hapa nchini kumezuka ka-dharau ka-aina fulani. Wale wote ambao kwa mfumo wetu wa elimu hawakubahatika kupata elimu ya Ssekondari, hawa kilugha ya mitaani wanaitwa akina “UPE”. Tunajua maana ya neno hili UPE.

Kuna kipindi fulani alitokea Mbunge wa Temeke akiitwa Kihiyo. Basi sijui ilitokeaje huko mahakamani akashindwa kuelewa mambo au alitoa vyeti feki hata sikumbuki vema. Kuanzia hapo likazuka jina kwa watu wasiojua mambo au hawakuwa na elimu ya kutosha waliitwa “VIHIYO”. Wapo baadhi ya vijana wanasoma shule bado hawaambui chochote nchini mwetu. Wote wasiojua kusoma kule shuleni wanaitwa “VILAZA” (yaani mbumbumbu hawajui kitu).

Sasa niulize, maafisa wanaokula fedha au mishahara ya watumishi hewa ni mbumbumbu au ni “UPE”, vilaza au ni “vihiyo”? Kama ni hivyo waliajiriwaje katika ofisi zinazoshughulika na fedha?

Mbona ni maafisa wasomi na wana hati kuonesha ukomo wa elimu zao? Mimi ninasema msomi yeyote asiyekuwa mwajibikaji kwa Taifa lake, mbinafsi na mlafi HAKUELIMIKA (he/she is UNEDUCATED”) licha ya kupitia shule na kupata hati ya ukomo wa elimu yake.

Nimekuwa nikitafakari tafsiri sahihi ya maneno haya “KUSOMA” na “KUELIMIKA” yaani kutambua nani mtu msomi na nani mtu aliyeelimika katika nchi hii. Wazo hili linanijia kutokana na “madudu” yanayofanywa na hawa wasomi wa nchi hii katika utumishi wao kwa umma. Sijafanikiwa kupata maelezo sahihi na ya kuridhisha juu ya tafsiri ya usomi na uelimikaji.

Imetokeaje kwa muda mrefu namna hii Serikali yetu kuanzia Awamu ya Kwanza ya Mwalimu Nyerere hadi leo Serikali ya Awamu ya Tano ya Dk. Magufuli wapo watumishi hewa au “maruhani” (kwa kiingereza wanaitwa “ghost servants”) katika Taifa hili?

Si hivyo tu, bali kumekuwapo na utamaduni wa baadhi ya wasomi kutumia hati bandia, yaani vyeti vya kughushi ili wapate kazi wasizostahili kisifa (not merited by virtue of academic qualifications).

Huu udanganyifu katika elimu unatokeaje au niseme unatumika ili iweje? Nani mnufaika wa hali hiyo? Ni Taifa au ni mtu binafsi? Ipo haja Watanzania kumuunga mkono Rais katika kukomesha tatizo hili ambalo linaonesha ukosefu wa elimu. Wahusika licha ya kupata ujuzi na maarifa darasani mimi nasema hawakuelimika hata kidogo.

Enzi zetu zile kwenye miaka ya 1950 huko wakati harakati za siasa zilipoanza Chama cha TANU kilikuja na wimbo wa kuhamasisha wananchi. Tukiimba “Ee TANU YAJENGA NCHI” na kaulimbiu yake ilikuwa “UHURU NA KAZI”. Siku hizi wabongo wengine kwa sababu zao binafsi wamebuni kauli mbiu kejeli kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakitafsiri eti ni “Chukua Chako Mapema”. Ni kweli au ni sahihi tafsiri namna hii?

Hii ilitokeaje? Mimi nakumbuka ilikuwa mwaka ule wa 1982 wakati wa Mkutano Mkuu wa CCM pale katika Ukumbi wa Diamond. Katika uchaguzi ule wa kihistoria na wa kwanza tangu kuundwa kwa CCM kule Unguja Februari 5, 1977 wakajtokeza vijana wasomi kugombea viti katika Halmashauri Kuu ya Chama. Wazee, “veterani” wa Chama hawakutarajia mageuzi ya uongozi katika chama chao wakati ule.

Ikatokea tu katika uchaguzi ule Mkoa wa Ruvuma, kijana Mchumi wa Chuo Kikuu, Osmund Kapinga, alimgaragaza veterani Mzee Reverend Padre Martin Chengula. Kule Mkoa wa Lindi, Bi. Mwalimu Mary Watondoha akampiku au akambwaga veterani maarufu wa Lindi Mzee Sheikh Bashehe Mikidani. Hapo ndipo minong’ono ikaanza kusikika ukumbini mle. Wazee wakataharuki. Vipi, kuna nini ndani ya Chama? Mbona yanakuja mageuzi ya ghafla haya? Hapo ndipo kauli hiyo ya “Chukua Chako Mapema” ya chama kipya ikasikika. Jamaniee sasa tukae chonjo, tukichelewa tutakuta vijana wametupiku. Basi, chama hiki kinatuasa kuchukua chetu mapema kabla hatujaadhirika kama akina Chengula na Bushehe Mikidadi. Kuanzia hapo kukaanza kusikika hili la chukua chako mapema eti ndiyo CCM!

Kuna ukweli kiasi gani juu ya tafsiri hiyo ya CCM- mimi sijui. Nijualo vijana siku hizi hawana uhakika na hali zao za ajira. Basi, wakishaajiriwa tu wanajitahidi kukusanya utajiri kwa haraka haraka. Kwanza wanajipatia runinga, wananunua gari, halafu utaona wanajenga nyumba kule Mbezi, alimradi katika muda mfupi tu wakuwamo kazini huwa wana “assets” kupita kipato chao kinavyoruhusu.

Wakiulizwa wanajibu kimzaha “shauri lako, chukua chako mapema brother. Hizi ni enzi za CCM!” Ulafi wa haraka haraka na kujipatia utajiri namna hii unatisha!

 

>>ITAENDELEA…

By Jamhuri