Kati ya miaka 300,000 hadi 250,000 iliyopita zana kubwa za mawe zijulikanazo kama acheulian zilianza kupotea katika maeneo ya akiolojia ya Afrika. Nafasi yake ikichukuliwa na aina mpya ndogo ndogo na saizi ya kati. Ukamilisho wa zoezi hili unamaanisha mwanzo wa muhula mpya wa kifunsi uliosambaa bara zima uitwao Muhula wa Kati wa Zana za Mawe (M.S.A).

M.S.A ilirudisha shauku ya kubangua mawe kupata vipande na kwa uangalifu kuvitengenezea kingo zenye makali ili kuwa na aina ya zana kama ukombo na ncha za silaha za kurusha.

Pamoja na shauku hii, kulikuwa na uunganishaji wa ufunsi wa matayarisho ya sehemu ya kubangua (ufundi wa ki-Levallois). Ufundi huu wa kuvunja mawe ulijumuisha hatua kadhaa za maandalizi kwenye jiwe linalotarajiwa kubanguliwa ili kupata vipande vyembamba au ncha yenye umbo linalokusudiwa.

M.S.A ina sifa ya kuwa na idadi kubwa ya aina tofauti ya zana zenye ncha zilizofanyiwa maboresho katika maeneo mbalimbali ya Afrika. Kwa mara ya kwanza aina dhahiri ya zana kulingana na eneo zathibitisha uwepo kwa wakati mmoja wa desturi za kiufundi na kimila katika maeneo tofauti.

Umuhimu wa vipande hivi unahusishwa na maendeleo ya teknolojia mpya, na hususan uundaji wa silaha za kuwindia kama mikuki, ncha za mawe zikiunganishwa kwenye mti kupata silaha ya kushambulia kwa kurusha.

Muhula wa mwisho wa zana za mawe

 Miaka 60,000 iliyopita, hatua ya mwisho ya chimbuko la teknolojia ya zana za mawe Afrika ilianza – kipindi kijulikanacho kama Muhula wa Mwisho wa Mawe (L.S.A).

Miaka hii imehusishwa na maendeleo ya tabia za mwanadamu wa sasa (Homo sapiens). Teknolojia mpya ya kupasua mawe iitwayo teknolojia ya ubapa ilianzishwa, ikiwezesha mfumo wa kutengeneza zana nyembamba sana na bapa. Hivi vipande bapa vilibadilishwa kuwa aina mbalimbali za zana ndogo na nyepesi, zilizochukua nafasi ya zile zilizokuwapo awali za ncha za mawe.

Mtindo huu wa kupasua mawe ulileta mabadiliko makubwa katika matumizi ya zana za mawe na kubadili mtazamo wa zana hizi kutoka aina rahisi ya zana zinazoweza kubadilishwa kwa haraka na kuwa zana changamano zilizounganishwa kiufundi.

Kipindi hiki tunazo kumbukumbu za kiakiolojia za vitu vilivyotengenezwa kwa miti na mifupa. Uboreshaji endelevu wa mbinu za uwindaji na ulaji wa wanyama maalumu ulisababisha ongezeko la watu katika baadhi ya maeneo pamoja na kuanza kwa mitandao mikubwa ya uhusiano wa kijamii na kibiashara wakati wa kipindi hiki.

Jamii zilianza kutambuliwa kupitia aina ya mapambo yao, kama ionekanavyo katika mikufu iliyotengenezwa kwa kutumia shanga za maganda ya mayai ya mbuni, mawe ya thamani na ukaria.

Jiolojia ya Bonde Kuu la Ufa na kuanza kwa uwanda wa nyasi

Bonde Kuu la Ufa ambako Bonde la Olduvai linapatikana, ni bonde lenye urefu wa kilomita 6,000 lililotokana na nguvu za asili za dunia na mojawapo ya kivutio cha kijiografia kinachopamba Bara la Afrika.

Bonde la Ufa lilianza kutokea miaka zaidi ya milioni 30 iliyopita kwa mpasuko wa ardhi uliogawa kipande cha mwamba unaolifanya Bara la Afrika kuwa vipande viwili.

Pande linaloitwa Nubia upande wa magharibi, na pande la Somalia kwa mashariki. Vipande hivi viwili zilianza kujitenga na sehemu iliyobaki kati ikadidimia chini na kufanya bonde kubwa lenye kingo za mteremko mkali sana.

Sehemu ya kusini ya hili bonde ndiko kuna maziwa makuu ya mashariki mwa Afrika kama vile Ziwa Turkana (Rudolf), Tanganyika na Nyasa. Upande wa kaskazini bonde hili liliungana na Bahari ya Hindi likatengeneza Bahari ya Sham.

Vilele vya volkano ni vitu vingine vinavyolipamba Bonde hili la Ufa. Milipuko ya volkano katika Bonde la Ufa ni kitu kinachosababishwa na dosari au athari za mipasuko ya nyufa katika mwamba unaoifanya dunia.

Miamba iliyoyeyuka kwa joto hufuata nyufa zilizopo katika mwamba hadi kutokeza juu ya uso wa dunia. Taratibu, mpasuko katika Bonde hili la Ufa unaendelea kuzama chini, na kama hali hii itaendele kwa kiwango kikubwa, basi huenda Bonde hili la Ufa likafunguka na kuwa tawi jipya la Bahari ya Sham na hatimaye kuigawa Afrika sehemu mbili.

Milipuko ya volkano inayoambatana na kufanyika kwa Bonde la Ufa imeathiri kwa kiasi kikubwa hali ya tabia ya nchi ya mashariki mwa Afrika. Kabla ya kuwepo kwa Bonde la Ufa eneo hili lilikuwa tambarare na hali ya joto na unyevu uliosababisha uwepo wa misitu minene. Hali hii ya tabia-nchi iliathiriwa pia na kufanyika kwa Milima ya Himalaya, kaskazini mwa Bara la Hindi.

Bonde la Ufa lilipoendelea kukua, vilele vikubwa vya volkano vya kufikia hadi mwinuko wa mita 4,000 hadi 5,000 vilitokea kutokana na milipuko ya miamba chini ya ardhi pamoja na miinuko ya mwinuko wa miamba uliotokana na mpasuko na mtikisiko wa dunia.

Vilisababisha mlolongo wa milima uliokinga pepo zenye mvuke ziletazo mvua kutoka Bahari ya Hindi. Hali hii ilisababisha tabia-nchi kuwa kame, kupungua kwa vipindi vya mvua, misitu na kufanya hali ya uwanda wa nyasi.

Tangu kufanyika kwa Bonde la Ufa, mmomonyoko wa udongo umejaza udongo kutoka maeneo tofauti ya kingo zake na kutengeneza mazingira tofauti. Mfano, mazingira ya maziwa, mabonde ya mito na kadhalika.

Udongo huu uliokusanywa na nguvu za asili umejumuisha mabaki ya mifupa ya wanyama wakiwamo wanadamu walioishi maeneo hayo, ukitengeneza maeneo yenye umuhimu wa tafiti za mabaki ya wanyama wa kale tunayochimbua hivi sasa. Mmomonyoko wa ardhi unaosababishwa na mito na maji ya mvua husaidia kufichua masalia hayo.

By Jamhuri