BODI mpya ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) imesimamisha wakurugenzi 16 ili kupisha uchunguzi wa tuhuma mbalimbali zinazowakabili.

Idadi hiyo, pamoja na wengine saba waliosimamishwa awali, inafanya idadi ya wakurugenzi waliosimamishwa TPA ifike 23 tangu, Dk. Harrison Mwakyembe, awe Waziri wa Uchukuzi.

 

Kwa miaka mingi TPA imekuwa miongoni mwa mashirika ya umma yanayonuka rushwa, uzembe, uonevu, wizi, uhujumu uchumi na sifa nyingine nyingi za aina hiyo.

 

Tunatambua adha ya kusimamishwa kazi, lakini katika hili, tunapenda kuungana na Bodi ya TPA pamoja na uongozi thabiti wa Dk. Mwakyembe. Waziri huyu amekuwa mfano wa kuigwa miongoni mwa mawaziri wengi katika Serikali hii ya Awamu ya Nne.

 

Kwa maneno mengine ni kwamba kumbe tukiamua, tunaweza kabisa kuibadili nchi yetu. Wakurugenzi waliosimamishwa TPA bado ni watuhumiwa. Lakini tutakuwa watu wa ajabu kabisa kudhani kwamba kinachowakabili ni tuhuma tu. Akili ya kawaida inatufanya tuamini kuwa kama si wote, basi miongoni mwao kuna wala rushwa, wezi na wazembe.

 

Tunasema hivyo tukirejea utendaji kazi wa TPA pamoja na makusanyo yanayotokana na vyanzo mbalimbali bandarini. Tangu Waziri Mwakyembe apitishe utaratibu wa fedha za malipo za TPA zilipwe benki, kuna habari kwamba makusanyo yamepanda kutoka Sh bilioni 28 kwa mwezi hadi Sh bilioni 40 kwa muda huo! Hili ni ongezeko la Sh bilioni 12 ndani ya mwezi mmoja.

 

Je, kabla ya utaratibu huu, fedha hizo zilikwenda wapi? Je, ni kweli kwamba ziliishia mifukoni na matumboni mwa wakurugenzi hawa pamoja na wafanyakazi wasio waadilifu? Katika mazingira ya aina hii, haitoshi tu kuiachia Mahakama kuwashughulikia watu hawa. Lazima Serikali ianze uchunguzi wa mali zao ili kubaini wingi na uhalali wake kwa watuhumiwa wote.

 

Kuwasimamisha kazi tu na kuacha wakiendelea kufaidi mali za wizi ambazo ni za Watanzania wote, hakusaidii kabisa kurejesha maadili miongoni mwa watumishi wa umma. Wakati umefika sasa wa kuzitambua mali zao na kujua namna walivyozipata, na namna wanavyolipa kodi. Watakaoshindwa kutoa maelezo ya kuridhisha juu ya ukwasi wao, mali zao zitaifishwe na ikiwezekana ziwasaidie yatima ambao wanataabika sana .

 

Tunachukua fursa hii kuipongeza Bodi ya TPA, na sana sana kumpongeza kwa namna ya kipekee, Dk. Mwakyembe kwa ujasiri wake wa kufumua mtandao wa wizi na ufisadi uliopindukia ndani ya vyombo anavyoviongoza.

 

Hata hivyo, Dk. Mwakyembe pamoja na Bodi wao wenyewe hawawezi kufanikiwa kama jamii nzima ya wapenda nchi itawaacha bila kuwaunga mkono. Ni wajibu wa kila mzalendo kujitokeza kuwaunga mkono viongozi wa aina hii wanaothubutu na kufanikiwa kuleta mabadiliko.

 

Watanzania wameibiwa sana . Wamenyonywa sana . Wametaabishwa kwa muda mrefu. Uwezo wa kuondokana na uonyonge huu wa kukomesha kuibiwa, kunyonywa na kutaabishwa tunao wananchi wenyewe. Kila mmoja katika nafasi yake ashiriki kuwapa ushirikiano viongozi wetu ili tuione Tanzania mpya yenye neema na usawa kwa kila Mtanzania. Hongereni sana Bodi ya TPA na Dk. Mwakyembe.

 

 

1050 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!