Kuzuia mwanandoa kuuza ardhi ya familia

Kuna wakati katika maisha ya ndoa, mmoja wa wanandoa anaweza akataka kuuza au kubadili jina la nyumba ama  kiwanja bila ridhaa ya mwenzake ilhali nyumba hiyo ni ya familia.

Lakini pia nje ya hilo kuna mazingira ambayo mtu anaweza kuwa si mwanandoa lakini mwenye masilahi katika nyumba au  kiwanja cha mtu fulani na anataka kuzuia nyumba ama kiwanja hicho kisibadilishwe jina au kisiuzwe. Kisheria jambo hilo linaruhusiwa na huitwa zuio (caveat).

Hili si zuio la kwenda mahakamani kama mazuio tuliyoyazoea. Hili ni zuio jingine kama nitakavyolieleza. Aidha, kuzuia hati isibadilishwe kimsingi ni sawa na kuzuia nyumba isiuzwe.  Hii ni kwa kuwa hakuna namna ambayo mnunuzi anaweza kununua kitu ambacho hakiwezi kubadilika na kuingia katika jina lake.

Ikiwa mke ana wasiwasi kuwa mume anaweza kumzunguka na kuuza mali ya familia au mume ana wasiwasi juu ya uwezekano wa mke kuuza, basi wanayo ruhusa ya kuweka zuio ili hati ya nyumba isibadilishwe.

Kuzuia hati isibadilishwe

Mke au mume, mmoja  anaweza kuweka kizuizi katika nyumba ya ndoa (matrimonial home) iwapo kuna dalili kuwa mmiliki aliyeandikishwa anaweza kuiuza au  kuiweka rehani bila ya ridhaa ya mwingine.

Mara nyingi migongano katika familia inapoanza mmoja kati ya wanandoa hukimbilia kuuza baadhi ya mali kwa aidha, kumkomoa mwenzake au sababu nyingine yoyote. Kwa hiyo ili kuliepuka hilo unapogundua kuwa kuna uwezekano huo, basi sheria imekuruhusu mwanandoa kuweka zuio ili hati isibadilishwe, hivyo kuepuka kuuzwa kwa mali.

Maombi yawasilishwe wapi?

Mamlaka za ardhi ni mamlaka ambazo hutakiwa kupelekewa maombi haya ya zuio. Mara nyingi mamlaka za ardhi huwa zipo katika ofisi za wilaya au  manispaa katika mkoa wako isipokuwa kwa walio Dar  es Salaam, maombi hupelekwa makao makuu  pale Wizara ya Ardhi kama ni hati.

Zuio huandaliwa vipi?

Maombi haya si maombi kama maombi mengine yalivyo. Maombi haya ni maombi ya kisheria na huandaliwa katika ofisi za wanasheria na hupelekwa yakiwa na muhuri wa mwanasheria. Katika maombi hayo mwombaji hueleza jina lake  kwa urefu, anuani yake, uhusiano wake na yule ambaye jina  lake ndilo liko kwenye hati ya anayemwekea zuio huku akieleza sababu za msingi kwa nini anataka kuzuia hati isibadilishwe.

Nyaraka za kuambatanisha

Kwanza, picha mbili  za mwombaji huku kila picha moja ikibandikwa kwenye nyaraka moja.

Pili, risiti za malipo ya ada ya usajili. Maombi haya hulipiwa kiasi cha  fedha lakini si kikubwa sana, kwa hiyo lazima uambatanishe na risiti za malipo.

Tatu, mwombaji aambatanishe vielelezo vinavyompa haki juu ya kiwanja husika kwa mfano cheti cha ndoa, mkataba wa mkopo na mengine ya aina hiyo. Kwa leo ni hayo.

Kuhusu sheria za ardhi, mirathi, masuala ya kampuni au ndoa tembelea SHERIA YAKUB BLOG.