NAANDIKA makala hii nikiwa jijini Manchester kwa shughuli maalumu ya kimichezo, nikiwa mdau kiasi. Naandika nikiwa bado na tafakari nzito na hofu juu ya hali ya vyombo vya habari vya Uingereza huko tuendako.


Hii inatokana na kazi na ripoti iliyotolewa na Jaji Leveson, ikionekana kushambulia vyombo vya habari kwa kiasi kikubwa na kutaka serikali ividhibiti.

Hofu yangu si juu ya nchi hii sana, lakini mrejesho wake katika nchi zetu, hasa Tanzania yetu. Udhibiti ukiwekwa hapa leo, najua kesho ‘waheshimiwa’ wataamka na kutaka kufotokopi kilichoamuliwa hapa.


Lord Leveson katika ripoti yake aliyoandaa baada ya kazi ndefu na mahojiano na watu mbalimbali, akiwamo Waziri Mkuu, David Cameron, anataka media ifungwe gavana.


Cameron hakupokea kwa furaha wala bashasha ripoti hiyo, na mpaka sasa anaonyesha kwamba kuna tatizo na kwa kweli linamuumiza ndani kabisa ya moyo wake.


Cameron ni mtu huru sana, anayependa uhuru sana pia kwa watu wengine, hasa wanahabari, kwa hiyo kimsingi hakubaliani na kuvifunga vyombo hivyo gavana.


Alionyesha mshituko wake punde baada ya Jaji Leveson kutoa ushauri wake, na Cameron hakuogopa kujikuta amesimama mwenyewe.


Naibu Waziri Mkuu, Nick Clegg pamoja na wengine ndani ya Conservative wanataka hatua zichukuliwe kudhibiti media, lakini Cameron bado anasema hapana.


Wapinzani nao, wakiongozwa na Ed Miliband wameshaweka wazi msimamo kwamba lazima vyombo vya habari vidhibitiwe, kwa hiyo Cameron amejiweka eneo hatari, lakini amesimamia ukweli.


Waziri mkuu hakuishia kwenye kuzungumzia ripoti juu juu tu, aliwaita wahariri wakuu, ambapo jumla walikuwa kama 19 hivi, wakaketi pale 10 Downing Street kujadili mustakabali wa vyombo vyao na wao wenyewe.


Lakini Cameron kwa alivyobanwa, hana namna isipokuwa kukubali, japo kwa shingo upande kuunda chombo huru cha kusimamia media.


Alipokutana nao, Cameron aliwaambia kwamba muda unawatupa mkono na wasipochukua hatua, watakuja kuumia wenyewe.


Alitaka wenyewe wahariri watoe mapendekezo kwa hoja kuntu juu ya jinsi ya kuunda chombo kisichoonea wala kupendelea, ili kusimamia mambo ya magazeti.


Yote haya yamesababishwa na yale mambo ya udukuzi wa simu za watu aina mbalimbali kupata habari za magazeti, kazi iliyofanywa kitambo kidogo.


Hiyo ni kinyume cha sheria na wakati mwingine maadili. Hata hivyo, kuna saa unaangalia udukuzi ulivyofanyika, unaishia kusema potelea mbali sheria ni nini, bora wamedukuzi kukomesha michezo michafu ya watu wanaojidai ndio wenyewe duniani.


Cameron anasema anahofia kuanza kudhibiti uhuru wa habari, jambo ambalo ni kinyume na utamaduni wa miaka na miaka hapa Uingereza.


Wapo wanaosema ushauri wa Lord Leveson una baadhi ya vipengele ambavyo vikitekelezwa vitakuwa vimekiuka Katiba na baadhi ya sheria za Uingereza.


Waziri wa Nchi (Sera), Oliver Letwin alizungumza na wahariri kwa muda mrefu, baada ya Cameron kuanza nao kwa dakika 20 hivi akieleza yaliyokuwa yamemkwama kifuani pake, asivyopenda kuidhibiti media.


Lakini Letwin akasema kwamba wanaanza kufanyia kazi mapendekezo ya Leveson na kwamba mdhibiti wa habari naye atakuwa anaratibiwa na chombo kingine.

Haya, tusubiri maana tunaambiwa si ajabu mdhibiti mpya na huru akawa tayari amewekwa kabla ya Krismasi aanze kazi yake.

Tuwasiliane kwa leejoseph2@yahoo.com


 

 

 

5077 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!