Tumemaliza wiki mbili sasa tangu litokee tukio la kinyama la kumteka, kumpiga na kumuumiza vibaya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk. Stephen Ulimboka. Tangu litokee tukio hili baya na la kinyama, mjadala umekuwa mkali na yameibuka maneno ninayoamini yanapaswa kupatiwa majibu na uchunguzi huru.

Nadhani kwa kuwa hii ni mara yangu ya kwanza kuandika rasmi katika mada hii kwa njia ya uchambuzi, nichukue fursa hii kuwapa pole madaktari wote nchini kwa masahibu yanayowapata, lakini pia niwape pole Watanzania kwa ujumla si tu kwa sababu matibabu yamesitishwa katika hospitali nyingi za umma, bali pia kutokana na utamaduni huu mpya na wa kinyama wa kutekana.

Sitanii, kuna kitendawili kikubwa juu ya nani hasa aliyemteka Dk. Ulimboka. Mwanzo alituhumiwa Kamishna Msaidizi wa Polisi, Ahmed Msangi, kuwa ndiye aliyemteka na kumuumiza. Zilisambazwa meseji kwamba alipokwenda kumhoji Dk. Ulimboka yeye alimtaka amrejeshee simu yake na wallet alivyompora.

Binafsi nilihojiana na Msangi kisha nikahojiana na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI), Profesa Lawrence Museru, kuthibitisha aliyoniambia Msangi. Nilichokipata ni maelezo kwamba maneno yanayosemwa kuwa Msangi aliambiwa arejeshe wallet na simu yalichakachuliwa bali uhalisia Dk. Ulimboka alimwambia Msangi kuwa waliomteka walimwibia simu na wallet yake. Basi.

Baada ya hapo, nimeshuhudia mnyukano uliozimwa na Spika wa Bunge, Anne Makinda, bungeni. Mbunge wa Viti Maalum, Injinia Stella Manyanya na  Mweka Hazina wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mwigulu Mchemba walikuwa wakinyukana na John Mnyika. Wakubwa hawa walikuwa wakituhumiana kuwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeshiriki kumteka Dk. Ulimboka na kinahamasisha mgomo. Mnyika alikuwa akikanusha.

Wakati hayo yakiendela, baadhi ya wabunge wakawa wananipigia simu na kuniambia kuwa Dk. Ulimboka alipigwa na madaktari wenyewe. Nilihoji iweje apigwe na madaktari? Maneno niliyoambiwa ni haya: “Kabla ya mgomo wa madaktari kuanza Dk. Ulimboka alikuwa anatumia simu ya Nokia kitochi. Baada ya mgomo akaanza kutumia Blackberry. Tena si simu moja, bali Blackberry tatu kwa wakati mmoja. Blackberry inauzwa si chini ya 1,500,000.

“Kilichowasikitisha wengi, ikaonekana ana gari mpya anatembelea na wengine wakasema alikuwa amenunua kiwanja. Kibaya zaidi sauti yake ya kutetea madaktari ikawa inaendelea kufifia kila siku zinavyopita, huku akikutana mara nyingi na viongozi wa polisi na usalama wa taifa.” Kauli hii ilinitisha kidogo na nikahoji iwapo kuna wasiwasi mikutano hiyo imezaa matunda ya yeye kumiliki vifaa vya kisasa kama simu na gari. Jibu nililoambiwa ni: “Kuna uhusiano wa karibu.”

Baada ya kauli hiyo, nikapata hadithi nyingine, kwamba pale Muhimbili ingawa Dk. Ulimboka alikuwa hafanyi kazi za kitabibu kutokana na kutokuwa na leseni, kuna mgonjwa aliyefikia mikononi mwake akashindwa kumpa huduma nzuri, hivyo mgonjwa yule akafariki na ndugu wakaamua kulipiza kisasi. Nikasema wao walijuaje? Mmoja akanijibu hivi: “Ndugu walitoa maneno makali hapo hospitalini MOI baada ya tukio.”

Maneno na tuhuma hizi zinatisha. Kwanza ikumbukwe mtuhumiwa namba moja baada ya hili tukio lilivyozuka alikuwa ni Serikali kupitia polisi. Leo idadi ya watuhumiwa wa kumteka Dk. Ulimboka imeongezeka. Wanaingizwa madaktari, ndugu wa wagonjwa na zinaibuliwa tuhuma mpya za vyombo nyeti vya dola – Usalama wa Taifa la Polisi – kushiriki kufanya dhambi ya kutoa rushwa!

Sitanii, hapa tulipofika ni pabaya. Uvumi huu tunaweza kuendelea kuupuuza lakini una madhara makubwa. Tanzania kama nchi siku zote hatukuwa tukiishi kwa uvumi. Nchi yetu imekuwa ya amani kitambo na tumelelewa katika msingi imara wa kusema ukweli. Kanuni ya TANU iliyokuwa ikisema: “Nitasema kweli daima fitina kwangu mwiko,” sasa inapotea kwa kasi.

Tunatembeza fitina usipime. Kwa sasa wengi tunazungumza tunayoona yana maslahi katika kufanikisha malengo yetu. Tunapofika mahala pa kutuhumiana kwa kiwango hiki bila majibu, hakika nawaambia tunaweza kuwa hatujijui. Hatujijui tumefikaje hapa. Tulipofikia ni ishara ya kuchanganyikiwa na maisha. Wabunge wamechanganyikiwa, madaktari wamechanganyikiwa na wananchi ndiyo usiseme.

Mitaani maisha yamekuwa magumu. Nilikuwa namwambia rafiki yangu kuwa ukiona deni la Serikali linakua na kufikia Sh trilioni 22 maana yake ni kwamba Watanzania wengi wamefanya kazi hawajalipwa, hivyo madeni mitaani ni mengi mno. Madeni yakiishakuwa mengi na utamaduni tuliojiwekea wa kila siku kuishi kwenye sherehe, ujue taifa linaelekea kuanguka kama ilivyoanguka dola ya Warumi.

Nchi yetu leo tunaendekeza michango ya harusi, tena kwe nyodo ukichanga chini ya Sh 50,000 unapewa kadi ya ‘asante’. Nchi yetu hii hii, tumeendekeza sherehe za kuzaliwa (birthday party), nchi yetu hii tuna matumizi makubwa kuliko kipato chetu. Hii ndiyo maana baa na nyumba za wageni zinazidi kuongezeka kila kukicha.

Hii maana yake nini? Ni rahisi tu. Huwezi kupata muda wa kuzalisha wakati upo kwenye sherehe. Kwa yeyote aliyepata kufanya sherehe anajua maana yake. Ukifanya sherehe tu nyumbani, ikiisha unakuwa umetingwa na madeni, maana muda wa kuzalisha unakuwa unasherehekea na hivyo kutumbua akiba uliyoikusanya kwa jasho kubwa.

Hatimaye inakuwaje? Haya ndiyo yaliyowaangusha Warumi. Katika Jiji la Athens, inaelezwa kuwa wenyeji walikuwa 95,000, watumwa, vijakazi na wageni walikuwa 365,000. Hii maana yake ni kwamba karibu kila Mrumi mmoja alikuwa na vijakazi watatu. Wakaishia kugida ulabu, watumwa wakaunganisha nguvu na kuwapindua.

Sisemi falsafa hiyo ndiyo inayotunyemelea hapa nchini, la hasha, ila si vibaya kutabiri. Ni ukweli ulio wazi kuwa madaktari wanadai posho na mishahara mikubwa zaidi. Ni ukweli kwamba Tanzania tumeishi maisha ya kushona suti na tumetumia hadi senti ya mwisho. Ni ukweli kwamba deni la taifa limekua kwa kasi hadi Sh trilioni 22 kutoka wastani wa Sh trilioni 10 mwaka 2009. Hii maana yake nini? Tunaelekea wapi? Jibu mwenyewe.

Katika familia mnapofikia mahala hakuna fedha lawama zinaongezeka. Ndipo baba mwenye nyumba hupata fursa ya kukagua na kubaini matumizi mabaya ya chumvi. Kati ya bidhaa zote katika familia chumvi ni kiungo cha mwisho kugombaniwa. Ukiona familia inaanza kupigizana kelele kwa matumizi mabaya ya chumvi, basi ujue tatizo ni kubwa kuliko mnaloliona.

Sitanii, leo tumefika pabaya. Tukio la Dk. Ulimboka limefungua vidonda vibichi. Kila mtu ana maumivu. Tumeanza kusambaza umbea na maneno yasiyothibitika, kwa sababu wengi tumekata tamaa. Tumeanza kutuhumiana bila ushahidi na hatimaye kufikishana katika kuhujumiana. Hapa ninachodhani polisi au serikali inapaswa kupima upepo.

Wapime upepo na kuitisha uchunguzi utakaoaminika. Kamisheni ya uchunguzi, hata kama umeishaanza, ijumuishe wawakilishi wa madaktari, waandishi wa habari, viongozi wa dini, wanasheria, mashirika ya haki za binadamu na kada ya watu mmoja mmoja wanaoaminika na kuheshimika katika jamii. Nasema tukio hili si dogo hata chembe, tusilipuuze.

Ujasiri alioupata huyo aliyemtenda Dk. Ulimboka, asipodhibitiwa leo hatapata shida kutumia uzoefu huo kesho kufanya jambo baya zaidi. Kwa sasa daktari huyu yuko hospitalini anapigania moyo kama taarifa zinavyoeleza, nami namuombea kwa Mungu aponea haraka.

Mwisho ni hili nisilotaraji kama madaktari watalipenda sana. Naamini hakuna daktari aliyeshuka kutoka mbinguni kama Malaika Gabriel. Nyote mnaujua uwezo wa Serikali yetu kwa sasa. Tukijenga tabia ya kutaka kumkamua lita 20 ng’ombe aliyekauka maziwa kwa kuwa ana mimba tutakata chuchu. Ni heri tuvute subira, ikibidi tumuongezee mashudu kwa njia ya kulipa kodi zaidi, kudai risiti kila tunaponunua bidhaa na ng’ombe akizaa, basi tuandae madumu ya kuhifadhi maziwa.

Mungu ibariki Tanzania.

 


1293 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!