Ushindi wa Dar es Salaam Young Africans (Yanga) wa mabao 3-0 dhidi ya JKT Mgambo katika mashindano ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Jumatano iliyopita, na sare ya bao 1-1 kati ya mabingwa watetezi, Wekundu wa Msimbazi Simba Sports Club ya jiji na Polisi Morogoro siku hiyo, ulizifanya Yanga na Simba kufikisha pointi 23 kila mmoja. Hali ya kulingana pointi ya mahasimu hao wakuu wa soka nchini imeibua msisimko mpya kwa mashabiki wa pande zote.

Tangu ligi hiyo ianze kutimua vumbi msimu huu Novemba 15, Simba imekuwa kileleni kwa muda wote huku ikiinyanyasa Yanga kwa pointi nyingi, wakati fulani zilifika saba. Lakini taratibu, pengo hilo lilianza kupungua hasa baada ya Simba nayo kuanza kucheza mechi zake nje ya jiji la Dar es Salaam na kutoka sare mfululizo.

 

Kabla ya ligi hiyo kuanza, Yanga ililishutumu Shirikisho la Kandanda Tanzania (TFF) kwa kupanga ratiba ya mechi inayoibeba Simba, tuhuma ambazo zilielezwa zinatokana na timu hiyo kupangiwa mechi tano mfululizo kwa kuanzia kucheza nyumbani (kwenye uwanja wa Taifa), huku yenyewe ikianzia mikoani.


Yanga ilianza kwa kupambana na Prisons kwenye uwanja wa Sokoine-Mbeya, zilikotoka suluhu, kisha ikacheza na Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri katika mji kasoro bahari ilikokung’utwa mabao 3-0 na kushika nafasi ya saba katika msimamo wa ligi hiyo.

 

Kufungwa kwa timu hiyo kwa idadi hiyo ya mabao, kulisababisha iporomokee kwenye nafasi ya 13 ikiwa inabebwa na JKT Mgambo peke yake, timu ambayo ndiyo kwanza imeanza kucheza Ligi Kuu ya Tanzania Bara msimu huu katika historia yake.

 

Matokeo hayo ya Yanga yalisababisha aliyekuwa kocha wake, raia wa Ubelgiji, Tom Saintfiet; Katibu Mkuu, Celestine Mwesiga na Msemaji wa Klabu hiyo, Louis Sendeu, watimuliwe huku aliyekuwa kocha mkuu wa timu ya APR ya Rwanda, Mholanzi Ernest Brandts, akipewa mikoba ya kuwa mwalimu mpya.

 

Hapo ndipo ilipouona mwezi kwa kuirarua JKT Ruvu kwa mabao 4-1 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na kupanda hadi nafasi ya saba ikitanguliwa mbele na Simba, Azam FC, Prisons, Coastal Union, JKT Olojoro na Mtibwa Sugar.

 

Baada ya kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya mahasimu wake wakubwa wa soka nchini, Simba kwenye Uwanja wa Taifa, huku Wekundu hao wa Msimbazi wakidaiwa kubebwa, Yanga ilifikisha pointi nane baada ya awali kuvuna pointi tatu kwa kuishinda African Lyon katika mechi ya nne.

 

Hapo ndipo vijana hao wa Jangwani kupitia kwa kocha wao msaidizi, Fred Felix Minziro, walipoanza tambo kuwa sasa wameingia rasmi katika mbio za kutaka kuikamata Simba, nyodo ambazo hata hivyo zilitibuliwa na Kagera Sugar walipofungwa bao 1-0 na timu hiyo kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.

 

Lakini katika mechi ya saba dhidi ya Toto African iliyochezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza, Yanga ilifufua vita yake kwa Simba ilipotoka kifua mbele kwa mabao 3-2 na kupanda hadi nafasi ya tatu ikiwa na pointi 11.

 

Katika kipindi hicho, Simba ilikuwa imeanza kutoka sare za mfululizo huku Yanga ikishinda au pia kutoka sare, hatua iliyosababisha ianze kujongelea kwa kasi kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo.

 

Wakati kocha Milovan Cirkovic akiwalaumu waamuzi kwa timu yake ya Simba kuzidi kutoa sare akidai wanaiminya, Brandts kwa upande mwingine alikuwa akichekelea kupanda kwa kuongeza pointi zaidi.

 

Mathalani, Yanga ilikusanya pointi tisa kutokana na mechi tatu mfululizo dhidi ya Ruvu Shooting, JKT Oljoro na Polisi Morogoro iliyoisimamisha Simba, siku hiyo hiyo ya Jumatano iliyopita na kusababisha wachezaji wa Yanga walingane pointi na mahasimu wao hao kwa kuwa na 23 kila mmoja.

 

Hapo ndipo mashabiki wengi wa soka nchini wanapoona kuwa tayari Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara ni kama imeanza upya.

 

Sasa wanasubiri kuona endapo Simba itaanza tena kushinda mfululizo mechi zake ikianza na mbili za kumalizia mzunguko wa kwanza au itabaki inasuasua. Wanangoja kushuhudia kama Yanga nayo itazidi kushinda ama ilikuwa ikipata ushindi huo kutoka timu dhaifu.


1216 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!