Waziri wa Nishati na Madini wa Tanzania, Profesa Sospeter Muhongo, na viongozi wa miji ya Hammerfest na Sandnessjoen nchini Norway, wamekubaliana kuanzisha ushirikiano baina ya miji hiyo na miji ya Lindi na Mtwara.

Uamuzi huo umefikiwa katika mkutano baina ya viongozi wa miji hiyo na ujumbe wa Wizara ya Nishati na Madini nchini Norway, ambapo viongozi kutoka pande zote wamekubaliana kuwa mji wa Harmmerfest utashirikiana na Lindi na ule wa Sandnessjoen utashirikiana na Mtwara.

 

Ushirikiano huo unalenga kuzitumia fursa zilizopo kujikwamua kiuchumi. Akizungumza mara baada ya kufikia makubaliano hayo, Waziri Profesa Muhongo amesema ili kuhakikisha mikoa ya Kusini mwa Tanzania inanufaika na rasilimali zake, Serikali imeamua kushirikiana na wadau wa maendeleo kutimiza azma hiyo.

 

Kabla ya ugunduzi wa gesi na mafuta, miji hiyo ya Harmmefest na Sandnessjoen ilikuwa ikijishughulisha na uvuvi kujipatia kipato na kuwawezesha kugharimia maisha kabla ya Serikali ya Norway kuanzisha shughuli za uchimbaji wa gesi na mafuta, baada ya kufikia makubaliano na wananchi wa maeneo hayo.

 

Kwa upande wake, mwakilishi wa wavuvi katika mji wa Sandnessjoen amesema uhusiano mzuri kati ya Serikali na kampuni za mafuta, umechangia kubadilisha historia ya watu wa maeneo hayo ikiwamo kuwawezesha kukua kiuchumi na kuwasaidia kupata huduma mbalimbali za kijamii.

 

Akizungumzia umuhimu wa kampuni za mafuta katika mji wa Sandnessjoen, Meya wa mji huo, Bard Anders Lango, amesema kwa kiasi kikubwa mapato ya mji huo yanatokana na mafuta.

 

Kadhalika, Lango ameongeza kuwa asilimia 22 ya mapato yanayotokana na mafuta yanatumika kutoa huduma muhimu za kijamii katika sekta za afya na elimu. Naye Mkurugenzi wa Uhusiano na Mawasiliano wa Shirika la Mafuta la BP, Olav Fjellsa, amesema moja ya mbinu ambazo zimeliwezesha shirika hilo kujenga uhusiano na jamii ni kuhakikisha wanatoa misaada katika maeneo husika, kuwekeana mikataba mizuri pamoja na kujihusisha na ununuzi wa bidhaa za wazawa.

 

Kuanzishwa kwa ushirikiano baina ya miji hiyo na mikoa ya Kusini mwa Tanzania, kutasaidia kufungua ukurasa mpya wa uhusiano na hivyo kuwawezesha wananchi kuwa sehemu ya mafanikio ya kuanzishwa kwa miradi ya umma katika maeneo yao.

By Jamhuri