Lini atapatikana Samata mwingine

Ahsante Mtanzania Mbwana Samata, nyota wa TP Mazembeya DRC kwa kuchaguliwa kuwa Mwanasoka Bora wa Afrika wa wachezaji wanaokipiga ligi za ndani.

Mwaka 2015 umekwisha, mwaka 2016 ndiyo kwanza umeanza na ‘zali’ la Samata, lakini tutapotazama mbele, tuonaona nini?

Nani anasema 2018 Tanzania itakuwepo Kombe la Dunia  pale Mwanza, Dar es Salaam, au Arusha ya Russia? Tutamwita chizi tena chizi asiyejitambua. Kuna Mwanafalsafa mmoja   anaitwa Winston Churchill aliwahi kusema: “Success is not final, failure is not fatal: It is courage to continue that count.”

‘Courage’ ya kusonga inapatikana wapi kama ‘failure’ ni za kutengeneza na sio changamoto za kikazi tu . Mtu akisema hakuna changamoto  huo ni ‘upuuzi’ wa mambo, ila makosa tengenezi kama una fikra pana huwezi kubali Taifa Stars itachukua Kombe la Mataifa ya Afrika miaka  mitatu mbele. 

Unakataa tu hakuna namna, ukubali vipi hata miujiza sio kirahisi hivyo.

Tutashangaa Yanga  kuchukua klabu Bingwa Afrika mwakani. Ni kuwa haiwezekani. Kwenye ‘imani’ bila ubidii ni kazi bure hata vitabu vya dini vimeandika. Wakristo wanaamini katika mstari usemao: “Asiyefanya Kazi na Asile…” Uwekezaji, uongozi mbovu, makocha kupangiwa kikosi, viwanja vibovu, na mashabiki kukwepa viingilio viwanjani, hapo hujafanya kazi, unataka ule (Mafanikio na Vikombe) nani kasema? Mganga wa Msata?

Ratiba za ovyo, Bodi ya Ligi ilichemsha, hasa msimu uliopita, ratiba imebadilika pasipo uchunguzi tosha kwa mwelekeo wa ligi za ndani na nje. Zaidi pale ilipobadilika mara mbili kwa wiki moja pekee, haikuleta mantiki kwa wadau na klabu husika kwa gharama na uungwana kutumika,  Prisons ya Jiji la Mbeya ilifika Dar es Salaam kwa ajili ya mechi na Azam, na Bodi  ya Ligi kuwataka warudi Jiji Mbeya  wacheze na Yanga baada ya hapo warudi Dar es Salaam kuvaana na  Azam. Azam na Yanga pia walihitajika na mechi za kimataifa, kucheza mechi ndani ya siku nne. Mechi za Ligi na kimataifa, nini kilitokea. Walifungwa. Ratiba ngumu, kupanga. Je mikakati itafanikiwaje kimataifa zaidi? 2015 hiyo!

Kuna lile  la vyanzo vya mapato ili kuchangia mfuko wa timu ya Taifa ya siku za nyuma kidogo klabu zilikatwa asilimia ya mapato. Ushauri wa wadau uliwataka  TFF watafute vyanzo vingine. Hivi TFF imekosa mbinu ya ‘kuuza maneno’ kwa wadau kibao, mashirika, taasisi na Serikali  kuwekeza kwa kiasi kikubwa? Mpira kwa sasa ni nembo ya biashara kubwa yoyote, hivyo unalipa. 

Hivi viwanja madimbwi, mitaro ‘upuuziaji’’ usio na tafakuri nani mmiliki? Jiji (Serikali), CCM, watu binafsi wanahusikaje wasiikwepe aibu endelevu. Pale uwanja wa Kambarage, Shinyanga vyumba vya kubadilishia nguo havina hadhi inayotakiwa si Simba, Ruvu Shooting na Mbeya City walilalamika. Kule Sheikh Amri Abeid, Arusha kubwa ni vyoo vibovu. Michezo pia ni siasa, siasa zisizo na maboresho zinaboa. Si kuwa ‘nawashupalia’ CCM ila nao ni  wanamiliki wa viwanja kadhaa, mfano tosha  wao wanavyo vingi kiuwiano. Kambarage-Shinyanga, Jamhuri-Morogoro, Sheikh Amri Abeid-Arusha, Mkwakwani-Tanga, vyote hakuna chenye afadhali. Arusha na Shinyanga walikarabati. Sasa je vimeleta hadhi hata ya kikanda  kwani  kitaifa na kimataifa ni mbali?  Mipango endelevu ikoje?  Naikumbuka 2015 ilivyoisha!

Michezo ya kimataifa utaionea wapi? Kila Siku Uwanja wa Taifa Dar es Salaam, na vipi ikitokea ukifungwa kwa ukarabati na sisi tungoje burudani, yule  Salum Aboubakar “Sure Boy Jr” nani atamwona na ‘michejo’ yake, sawa tutamwona pale Chamanzi. Shamba ni uwanja tutalimaje kama ni ‘magumashi’.

Nani anakumbuka “Taifa Cup” ilileta chachu fulani kuchangamsha ligi kuu, unamkumbuka Gaudence Mwaikimba akiwa na Mapinduzi Stars (Mbeya), aliibuka mfungaji bora katika michuano hiyo mwaka 2011. Hivi hiyo michuano iko wapi sasa hivi? ilileta  vipaji visivyojulikana kwenye ligi kuongeza mvuto  imebaki wachezaji wa kimataifa tunaowaita “mapro” kumbe wamekuja kumalizia soka nchini baada ya kuhangaika duniani. Viwango vyao ni kama Elius Maguli au Mudadhir Yahya tu! kwanini ‘pro’ asiye pro kuwepo nchini?

Mpira wa kileo ni biashara nani akubali kwenye suala la kujitoa na nguvu anakutana na ‘pesa udafu’ na posho za kusubiri miezi kadhaa, na heshima za msimu kama kwa Juma Kaseja kwa ‘vigelegele’ kutoka Misri 2003 leo wamekwishamwambia  “kauza timu” kwa magoli ya siku moja, ngoja amalizie pensheni yake Mbeya City, yule Peter Schiemiel miaka yote Manchester United hakuwahi kufungwa kizembe? Alifungwa si mara moja. Mbona alidumu. Wazungu wanajua “changamoto za kazi” mtu hana ukamilifu tunajitahidi. Inachukiza kutaja mfano kutoka kwa ‘Wazungu” ila tutafanyaje, ndio “uhalisi” wapo hatua kadhaa mbele yetu. Usipokubaliana na ukweli, ni ujinga.

Klabu kubwa Afrika kama vile  Etoile du Saleh, Al Ahly na Esperance wanalipa wachezaji kuanzia dola 10,000 kwa mwezi, Azam na Coastal Union watatoa kweli na udhamini huu wa mashirika kutoka Mkoa wa Kilimanjaro (ubahili), wachezaji nao wanajithaminisha kweli au ni Elimu ndogo juu ya maslahi na huduma  wanayoitoa klabuni? Bora liende tu au ni ‘kuuza sura’ pale Azam au Simba na “umaarufu kuonekana” wakipita Posta na Mbagala mashabiki tuombe kupiga “selfie”.

Athuman Machuppa, tazama JKT Ruvu walimchukua 1997 kwa uhamisho wa 15,000, enzi hizo ilikuwa na thamani, mchezo haukuwa na kipaumbele kama sasa, haukuwa na nguvu ya kushawishi ‘wazazi’ ni ajira, msitupeleke kule!

Mapenzi na klabu yapo, ila si kiasi kikubwa  kama  enzi za Mecky Mexime pale Mtibwa Sugar. Mchezaji ajue thamani yake apige fedha kama Emmanuel Okwi, Yanga na Simba wanamjua  huyu jamaa vyema msimu uliopita.

Mapenzi na ‘Taifa Stars’ ni “automatically”  nani ayatengeneze, tatizo mfumo wa kuweka sawa kuleta faraja kwa Watanzania haujafikiwa. Ari na nia ya kuunganisha Watanzania  kwa michezo ulifanikiwa enzi za Marcio Maximo, usipomshukuru huyu kwa historia ya hivi karibuni ya Taifa Stars tutakuita “asiyejielewa”.

Uzalendo ulipachikwa kama vile upo kambini Mafinga JKT  ukiwa  “kuruta”.

Unajua nini maana ya Taifa Stars. Watu walitoa machozi tulipofungwa, tatizo lake na boronga yake?

Juma Kaseja na uwezo wake, Ivo Mapunda akawa kikosini, ni kama ile sinema iliyoisha hivi karibuni ya  Mart Nooij ambaye ‘ufundi’ upo ila benchi lake lilimwelekeza vipi? mchezaji hakuwepo benchi alijuaje uwezo wake. Wadau walishangaa Ally Mustafa yupo kwenye ‘fomu’ na  klabuni yupo kikosi cha kwanza, na alikuwa  nje kwa mechi za karibuni (COSAFA), tulizotolewa kwa aibu bila hata goli moja mechi zote dakika 270, Deo Munishi na Mwadini Ally hawakuwa kiwango chake.

Amri Kiemba na John Bocco, walikuwepo uwanjani halafu ilikuwepo damu mbichi nani atawapeleka Kimataifa?

Benchi la ufundi lilileta majina yaleyale. Mandawa yule wa  Kagera Sugar, Ajibu wa Simba ama yule Deus Kaseke wa Yanga  wangetakiwa kuwepo. Ni lazima, wanastahili.  Ninavyoiaga 2015 kwa huzuni!

Uzoefu wapatie wapi? Hata moja ya klabu zao kipindi kile hazikuwepo michuano yoyote ya Kimataifa (Klabu Bingwa au Kombe la Shirikisho). Unamkumbuka kocha Kim Paulsen kutoka timu ya vijana “Serengeti Boys” mpaka Taifa Stars. Kipindi kile alitisha kwa kiasi chake akiwa Taifa Stars unajua kwanini? Alitoka na “makinda” yake kuja kikosi kikubwa. 

Hiyo ni kadhia, balaa lile la wiki (bao 7) kutoka kwa Waalgeria? Huo ndio mwaka 2015 ulivyokwisha kwa staili yake, nauanza kwa kumwangalia shujaa alipouawa “scene” ya kwanza sasa sijui “movie” itaendeleaje? Hakuna kilichoharibika sana. Unajua kwanini?

Nauaga mwaka 2015 nikifikiria Mohamed Dewji  atafanikiwa  wazo lake la kubadilisha mpira hasa klabu aliyo na mahaba nayo Simba, au nimpe wazo tu aanzishe Mo FC ili wazo lake lisije kufa kukuza soka.

Enzi naanza kuusikia  mpira kwa uzuri  nilivutiwa na Juma Kaseja na yule marehemu Cristopher Alex “Massawe” ilikuwa mwaka 2003, ilikuwa mechi ya kimataifa,  Klabu Bingwa Afrika Simba dhidi ya Zamalek. Kisa maajabu yao wamenivutia mpaka leo, uliyaona “mapenalti” ya wale Waarabu yalivyomwogopa Kaseja?  Je uliuona mkwaju wa mwisho wa  Alex (Christopher)? shujaa wangu huyu ,nakuomba Mungu akupe heri huko ulipo.

Leo teknolojia imekua kila kona, na mpira wa Ulaya umetawala dunia, yule Lionel Messi anajulikana kuliko Simon Msuva, huku mtaani wanasema mbio za Gareth Bale yule Mrisho Ngassa wa klabu ya Bidvest hafiki hata robo. Misingi gani inahusika kuanzia ngazi ya chini, ili  “dogo” fulani pale Mbagala, Usangi, Daraja mbili, Tukuyu   au Nyamagana  aujue uzalendo. Chakushangaza kwas asa anajua jezi namba 7 aliwahi kuivaa David Beckham, timu ya Taifa na Klabu zake alizopitia,lakini  Edibily Lunyamila hajui alicheza nafasi gani uwanjani? 

Siku hizi uzungu mwingi. Nani anajali? “Mdingi “ wake kakazania  mpira wa bongo hauna mvuto, mara ushabiki wa kinazi zaidi, shabiki wa Simba haipi sapoti timu  Yanga kwenye mechi za kimataifa, anashangilia timu pinzani. Uzalendo haupo.

Unahisi nini kitatokea kwa “dogo” yule? “Mtoto umleavyo ndivyo akuavyo”.

Pale Uwanja wa Taifa, Uwanja unajaa mahasimu wa Jiji wakichuana, yule wa Msimbazi na Jangwani wakati kule Uingereza haijalishi nani anacheza .Mashabiki watajaza Uwanja tu. “Dogo” atajua Tanzania kuna Simba na Yanga, kama “Mdingi” wake anavyowaza. Unajua kitakachotokea?

 

Ni rahisi kama ilivyo kawaida ‘dogo’  huyu aliyezaliwa enzi za Mheshimiwa Rais  Kikwete yupo madarakani kumjua Cristiano Ronaldo kuliko  yule beki mpambanaji wa Azam, Aggrey Morris. Kwa kwa kuwa shujaa wao (starring) alishauawa  “scene” ya kwanza. Karibu 2016 labda hawa wanaozaliwa au kukulia zama za   “Mzee wa hapa kazi” wanaweza tumbuliwa jipu la kutokuwa wazalendo na  shujaa mpya anaweza kuzaliwa kwa mikakati na mipango itakayoanzia kwako!

 

Simu Na: +255 656 859045