Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, amesema staha ya Bunge itazidi kuporomoka ikiwa utaratibu wa kumtumia Spika anayetokana na chama cha siasa hautabadilishwa.

Kauli hiyo ya Profesa Lipumba imeungwa mkono na Katibu wa Chama cha Mabadiliko ya Demokrasia (ADC), Kadawi Lucas Limbu, akisema, “Spika wa sasa anawapendelea wabunge wa chama tawala na kuminya wa vyama vya upinzani.”

 

Akizungumza na JAMHURI jijini Mwanza hivi karibuni, Mwenyekiti huyo wa CUF amesisitiza kuwa Spika asiyefungamana na chama chochote cha siasa ndiye atakayerejesha nidhamu na heshima ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

 

“Ili wabunge waweze kufuata taratibu, nidhamu na kudumisha heshima ya Bunge, Spika asitoke katika chama cha siasa, awe ni mtu atakayechaguliwa na Bunge kutoka nje ya chama cha siasa, huyo atakuwa na uwezo wa kutenda haki ndani ya Bunge,” amesisitiza Profesa Lipumba.

 

Profesa huyo wa uchumi amependekeza pia itungwe sheria itakayotumika kumshughulikia Spika haraka iwezekanavyo mara anapoonekana kukiuka kanuni za Bunge.

 

Naye Limbu, akizungumza na JAMHURI jijini Dar es Salaam hivi karibuni, amesema ndoto ya kumpata Spika asiye mwanasiasa inaweza kutimia endapo Chama Cha Mapinduzi (CCM) kitaondolewa madarakani.

 

“Tumwombe Mungu afanye muujiza CCM iondolewe madarakani 2015, halafu tupate Spika mzuri kama Sitta [Spika mstaafu, Samuel Sitta], tutakuwa na Bunge lenye kujali maslahi ya umma,” amesema Limbu na kuongeza:

 

“Wapinzani tunapaswa kuungana tuiondoe CCM madarakani mwaka 2015. Usimamizi wa Sitta ulisababisha Waziri Mkuu [mstaafu Edward Lowassa] akajiuzulu.”

By Jamhuri