Kwa kitambo sasa, Mbunge wa Jimbo la Nyamagana, mkoani Mwanza, Ezekiel Wenje (Chadema), anatuhumiwa kuendesha kwa siri mkakati wa kuhujumu harakati za vijana wanaoonekana kuwa tishio la wadhifa wake huo.

Kwamba Mbunge huyo kwa sasa anajizatiti kutumia wadhifa wake huo kuzima nguvu ya vijana wanaoonekana kung’ara kisiasa ndani ya chama hicho jimboni humo. Inaelezwa kwamba uongozi wa Chadema ngazi ya Taifa umeshapata taarifa za tuhuma hiyo dhidi ya Wenje, lakini haujaonesha dhamira ya kuingilia kati kwa uzito unaostahili, yaani ni kama umeipuuza.


Kwa upande wake, Wenje amekuwa akikanusha tuhuma hiyo akidai kuwa ni mkakati unaosukwa na watu wachache kwa nia ya kuchafua heshima na jina lake mbele ya wakazi wa Nyamagana na umma kwa jumla. Hata hivyo, ni jambo lisilo na kificho kwamba viongozi wengi hawapendi kuondolewa na au kuondoka madarakani kwa hiari.

 

Viongozi wengi hutamani kuzeekea madarakani! Kwa hivyo, Mbunge huyo wa Nyamagana naye ni binadamu, anaweza kujenga kinyongo dhidi ya wanachama wenzake wanaoonekana kujinyooshea mapito ya kugombea ubunge wa Nyamagana.


Msuguano wa aina hiyo umeanza kujitokeza pia kuhusu kinyang’anyiro cha ubunge katika Jimbo la Tarime mkoani Mara. Mgombea ubunge wa jimbo hilo mwaka 2010 kupitia Chadema, Mwita Waitara, kwa sasa anavutana na Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Chadema (Bavicha) Taifa, John Heche.


Licha ya kuangushwa na Nyambari Nyangwine wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Waitara anajifafanua kuwa bado ndiye anayestahili kupeperusha bendera ya chama hicho kikuu cha upinzani nchini katika kinyang’anyiro cha ubunge jimboni hapo, mwaka 2015.

 

Kutokana na dhana hiyo aliyojijengea, Waitara kwa sasa anaonekana kutofurahishwa na hatua ya Heche kutangaza nia yake ya kugombea ubunge katika Jimbo la Tarime itakapofika mwaka 2015.


Lakini Heche kwa upande wake anasema ana haki ya kikatiba inayompa jeuri ya kugombea wadhifa huo, huku pia akijipambanua kuwa ndiye mwenye uwezo wa kuivusha Chadema katika kinyang’anyiro hicho dhidi ya vyama vingine, hususan CCM. Inawezekana mvutano wa aina hiyo haufukuti ndani ya Chadema katika majimbo ya Tarime na Nyamagana pekee, inawezekana unafukuta pia katika vyama vingine vya siasa kwenye majimbo mbalimbali nchini.


Turudi kwenye msuguano wa Wenje na baadhi ya vijana wa Chadema katika Jimbo la Nyamagana. Inadaiwa kuwa Mbunge huyo anatumia kofia ya ubunge na uwezo wa fedha kuandaa wanachama wanaomtetea katika uongozi wa juu wa Chadema. Pengine ndiyo sababu hadi sasa uongozi huo haujaonesha dhamira ya kweli katika kushughulikia tuhuma inayomkabili Wenje. Dalili zinaonesha kuwa suala hilo linazidi kupungua nguvu kwa kadiri siku zinavyozidi kusonga mbele.


Wakati msuguano huo ukiendelea, Kamati Kuu ya Chadema imetangaza kuwavua uanachama Diwani wa Kata ya Igoma, Adam Chagulani, na Henry Matata wa Kata ya Kitangiri jijini Mwanza. Madiwani hao wamevuliwa uanachama wiki iliyopita kutokana na kilichoelezwa na Kamati hiyo kuwa wamekuwa wakikihujumu chama hicho, ikiwa ni pamoja na kusimamia hoja iliyosababisha kuondolewa madarakani kwa Meya wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Josephat Manyerere.


Hata hivyo, kwa upande wake, Chagulani anasema hatua hiyo ya kuvuliwa uanachama imetokana na msukumo wa ‘watu’ wanaoanza kupanga safu ya uongozi, lakini pia akiitazama hatua hiyo kama kiburi cha Chadema baada ya kuona chama hicho kinaaminiwa na  wananchi.


“Issue (chanzo cha msuguano) hapa ni ubunge mwaka 2015, watu wameanza kupanga safu zao… unaweza ukajikuta unapigana vita ambayo huijui, lakini siasa na ukombozi wa Tanzania si lazima uvipiganie ukiwa Chadema,” Chagulani alinukuliwa na gazeti moja la kila wiki nchini. Baadhi ya wanachama wa Chadema jijini Mwanza wamepongeza uamuzi wa kuwavua uanachama madiwani hao, lakini wengine wamekosoa hatua hiyo wakisema ni ishara ya kuminya uhuru wa kutoa mawazo na maoni miongoni mwa wanachama wa chama hicho.


Tukio la kufukuzwa kwa madiwani hao limekuja takriban mwaka mmoja baada ya Kamati Kuu ya Chadema kuwavua uanachama madiwani kadhaa, waliokuwa wakikiwakilisha chama hicho katika Halmashauri ya Manispaa ya Arusha. Mbunge Wenje na wanachama kadhaa wa Chadema wanajigamba kwamba kufukuzwa kwa madiwani Adam Chagulani na Henry Matata hakutayumbisha chama hicho katika juhudi za kujijenga zaidi kwa wananchi jijini Mwanza.  Lakini ikumbukwe kwamba madiwani hao bado wanakubalika katika maeneo yao ya uongozi. Lakini pia wamekuwa wakikubalika ndani ya Chadema na ndiyo maana hoja yao ya kumwondoa madarakani Meya wa Jiji la Mwanza, Manyerere iliungwa mkono na kutimia.


Hivyo basi, kusema kwamba kufukuzwa kwa madiwani hao hakutapunguza nguvu ya Chadema kisiasa ni ndoto za mchana kweupe. Si ajabu tukasikia na kuona baadhi ya wanachama wanajiondoa Chadema na kuwafuata viongozi hao. Fikra ya Hekima inazidi kusisitiza kuwa linalosemwa kuhusu Mbunge Wenje lisipuuzwe na uongozi wa Chadema ngazi ya Taifa, vinginevyo chama hicho kitajikuta kikijipunguzia mvuto kwa wakazi wa Jiji la Mwanza.


Ingawa hadi sasa hakuna ushahidi wa moja kwa moja unaodhihirisha kuwa Wenje anatekeleza mkakati haramu wa kuzima nguvu ya vijana wanaoanza kung’ara kisiasa ndani ya chama hicho, lakini tusisahau maneno ya wahenga kwamba lisemwalo lipo na kama halipo liko njiani linakuja. Chadema kilianza kupata nguvu ya kisiasa jijini Mwanza wakati wa Uchaguzi Mkuu uliopita (mwaka 2010), wakati wagombea wake walipofanikiwa kuwabwaga kwa kishindo wagombea wa CCM katika majimbo ya Nyamagana na Ilemela.

 

Utafiti unaonesha kuwa chanzo cha ushindi huo wa Chadema ni wimbi la migogoro ya kugombea madaraka, makundi ya kuhasimiana na wingu la rushwa lililokuwa limetanda ndani ya CCM. Baada ya kuona hivyo, wanachama wengi wa CCM wakajitambua na kuona hawana sababu ya kuwachagua wanachama wenzao waliojitokeza kugombea ubunge kwa misingi ya makundi na rushwa. Hivyo wakaamua kuwachagua wagombea kutoka Chadema ili kukishikisha adabu chama hicho tawala.


Leo Chadema nao wakianza kukaribisha na kukumbatia makundi yanayohasimiana kutokana na msukumo wa ‘roho mtakavitu’ wa viongozi na wanachama wachache hakitakuwa na muda mrefu wa kuendelea kukubalika na kuaminiwa na Watanzania wengi. Wakati fulani katika moja ya makala zangu, niliwahi kuhimiza Watanzania kujenga dhana ya kutumia kigezo cha mtu badala ya chama kuchagua kiongozi bora, kwa vile chama ni njia tu ya kufikia lengo la kuwapata viongozi wenye dhamira ya kweli ya kuwatumikia wananchi.

 

Chadema ni sehemu ya njia hizo, lakini uongozi wake ngazi ya Taifa ukiendelea kupuuza tuhuma ya Mbunge Wenje, anayedaiwa kuhujumu nguvu ya wanachama wanaoanza kung’ara kisiasa katika Jimbo la Nyamagana, chama hicho kitaparaganyika siku si nyingi zijazo, ingawa binafsi siombi hilo litokee.

 

1689 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!