*Asema mchezo wa kutumia mahakama haumsaidii

*Amdonoa Rais JK, awatahadarisha wasaidizi wake

*Ataka Jaji Werema afikishwe mahakamani haraka

*CCM yawatosa rasmi Chenge, Prof. Tibaijuka, Ngeleja

 

 

Mwanasheria Mkuu wa chama kikuu cha upinza – Chama cha Maendeleo na Demokrasi (CHADEMA), Tundu Lissu amesema Mwanasheria Mkuu wa zamani wa Serikali, Andrew Chenge anachokifanya mbele ya macho ya Watanzania kwa sasa ni kukwepa kujieleza hadharani.

Anasema kitendo cha Chenge ambaye ni Mbunge wa Bariadi Magharibi kikumbilia Mahakama Kuu ni kucheza na akili za Watanzania ambao wengi wao kwa sasa wanafahamu kila hatua inayofanywa na mwanasiasa hao.

Lakini, Lissu ambaye ni Mnidhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, anasema Chenge hatafanikiwa kama anavyofiria kwani watu wanafahamu “madudu yote ya Escrow.”

“Amekimbilia Mahakama Kuu, huku akijua kwamba atapata nafuu kwa sababu Mahama hiyo nayo iko kwenye tuhuma kwa sababu majaji wake wametajwa kupokea mgawo wa Escrow,” anasema Lissu na kuongeza:

“Chenge amekimbilia Mahakama Kuu kwa sababu anajua wazi kuwa itamlinda kwa kuchelewesha kesi hiyo kila baada ya muda fulani. Usisahau kuwa mahakama hiyo ndiyo iliyotoa waraka wa kuzuia mjadala wa Escrow bungeni.

“Hii maana yake ni kwamba Chenge anataka kutumia Mahakama Kuu kumlinda dhidi ya tuhuma zake mbele ya Tume ya Maadili. Wakati yeye anazuia mahakamani, mtaani jambo hili halitapoa.”

Lissu alikiri kwamba itakuwa ngumu kwa Kamati ya Tume ya Maadili kumhoji Rais Jakaya Kikwete na hata wasaidizi wake walioandika barua ya kubariki fedha hizo kutoka, lakini itabaki kwenye kumbukumbu kwamba mgogoro wa Kampuni ya kufua umeme ya IPTL ulianza na Rais Jakaya akiwa waziri na kumalizika akiwa Rais wa Jamhuri.

Anasema kwamba kwa mujibu wa katiba ya nchi, Rais Kikwete analindwa lakini jambo hili lenye miaka 21 sasa lililoanzia kwake akiwa Waziri wa Maji, Nishati na Madini na linaishia kwake.

“Kwa kipindi chote tangu anatia saini, kelele zilipigwa. Kumbuka, wakati huo Andrew Chenge alikuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Kwa hiyo Chenge anajua anachokifanya kwa sasa na Mheshimiwa Rais Kikwete hili jambo linaishia kwake kama lilivyoanza kwake,” anasema.

Anasema wakati makubalino ya awali yanafanyika mwaka 1994 kati ya IPTL na Serikali, Waziri wa Nishati na Madini alikuwa Kikwete na mwaka 1995 wakati mkataba wa kununua umeme unasainiwa kati ya Serikali na wawekezaji hao, Waziri wa Fedha alikuwa Kikwete.

Suala la umiliki wa IPTL uliokuja mpaka Akaunti ya Escrow baada ya kulumbana na Tanesco kuna madai kwamba fedha hizo waligawawia baadhi ya viongozi wa Serikali akiwamo Mwanasheria Mkuu aliyejiuzulu Frederick Werema, aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka.

Ripoti ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) inayoongozwa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe wanamtaja pia Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja, kuwa alipokea rupia hiyo.

Lissu amesema kwa kila hali lazima Mwanasheria Mkuu wa Serikali aliyejiuzulu, Jaji Werema afikishwe kamahakamani kujibu tuhuma za matumizi mabaya ya Serikali.

“Huyu ni Mshauri Mkuu wa Serikali katika masuala yote ya kisheria. Katika hili la Escrow ni wazi alitumia vibaya madaraka yake na asipofikishwa mahakamani, ‘kitanuka’,” Lissu ameliambia JAMHURI.

Baraza la Maadili la Utumishi wa Umma wiki iliyopita lilikwama kumhoji Chenge baada ya mwanasiasa huyo kukata rufaa Mahakama Kuu ya Tanzania kupinga kujadili tuhuma zinazomkabili za kukiuka maadili ya uongozi wa umma kwa kujilimbikizia mali binafsi katika kipindi cha uuzwaji wa hisa za VIP Engireering kwenda Independent Power Tanzania Limited (IPTL).

Mwenyekiti wa Tume ya Maadili ya Utumishi wa Umma, Jaji mstaafu, Hamis Msumi aliahirisha kumhoji Chenge baada ya kupitia kwa makini zuio lililowasilishwa na kujiridhisha kuwa baraza lake halina mamlaka ya kujadili na kuongeza kuwa sheria inamruhusu Chenge kukata rufaa.

Mrufani Chenge katika rufaa yake anasema Tume ya Maadili hairuhusiwi kujadili suala lililoko mahakamani kwa mujibu wa Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 Kifungu cha 114(1)(d) kinachozuia mtu au chombo chochote kujadili suala lililoko mahakamani.

Kifungu hiki kinapata nguvu kutoka Ibara ya 107A ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 inayosema mamlaka ya kutoa haki katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yapo mikononi mwa Mahakama pakee na si chombo kingine chochote.

Kwa upande wake, aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka yeye alisema fedha hizo ilikuwa halali kwake kusaidiwa na James Rugemalira na akasema fedha hizo ni kidogo mno kwani kwa wastani anatumia Sh milioni 10 kununua mboga katika siku mbili.

 

Ikulu yajichanganya

 

Awali, Ikulu iliyoidhibitisha ulipwaji wa fedha hizo wastani wa Sh bilioni 202 ambazo baadae ziligawiwa kama njugu kwa watu mbalimbali, ilikanusha kuwa haijafanya hivyo.

Hatua ya Ikulu kudai kwamba Katibu wa Rais, Prosper Mbena, hakuandika barua ya maelekezo ya kulipwa kwa fedha kutoka Akaunti ya Tegeta escrow, ilizidi kuibua maswali juu ya siri inayoendelea serikalini kuhusu kashfa hiyo kubwa kuwahi kutokea nchini.

Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, ilijaribu kumsafisha Mbena kutoka kwenye kashfa hiyo ambayo kwa mujibu wa taarifa ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), hatua zote za utoaji fedha hizo zilipelekwa kwa Waziri Mkuu na Rais.

Kwenye kipengele cha 7.0 cha utetezi huo wa BoT kinahusu ‘Ushauri wa kuujulisha uongozi wa nchi’. Kinasema hivi: “Mnamo tarehe 24 Oktoba, 2013, BoT ilimuandikia PST, ikimuomba kuchukua hatua kadhaa kuhusiana na malipo ya IPTL. Miongoni mwa mambo yaliyoshauriwa na BoT yalikuwa ni:

“(i) Kwamba ufungaji wa Escrow Account uzingatie kwamba mamlaka ya kufanya hivyo yako kwa Paymaster General;

“(ii) Kwamba, kwa kuzingatia unyeti wa suala hili na ukubwa wa malipo husika, Waziri wa Fedha apate fursa ya kuwajulisha Mheshimiwa Rais na Mheshimiwa Waziri Mkuu ili waeleze kama wanaridhia au la; na

“(iii) Kwamba GoT iombe kutolewa kwa kinga itakayoikinga GoT dhidi ya madai yanayoweza kujitokeza baada ya malipo hayo kufanyika.”

Maelezo hayo ya BoT yanafafanuliwa na wafuatiliaji wa sakata la escrow kwamba yanathibitisha ushirikishwaji wa viongozi wakuu kwenye utoaji fedha hizo.

Ofisa mmoja ndani ya BoT, aliyezungumza kwa masharti ya kutotajwa jina, amesema: “Ikulu haiwezi kuchomoa katika hili, pengine inataka kusema Mbena alishiriki yeye mwenyewe kama yeye bila kufuata utaratibu. Ikulu inataka kusema Mbena, ama alighushi barua, au hakuwashirikisha wakubwa kutoa maelezo hayo.”

Anasema BoT isingeweza kuchukua hatua kubwa ya kuruhusu utoaji fedha kama isingepata baraka kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu na Ikulu.

Kipengele cha 10.0 cha utetezi wa BoT kinahusu Kibali cha kuhamisha fedha kwenda IPTL.

Kinasema: “Mnamo tarehe 14 Novemba, 2013, PST aliwasilisha kwa utekelezaji, maagizo ya Mheshimiwa Rais ambaye aliagiza kwamba ‘Maamuzi ya Mahakama Kuu yatekelezwe kama alivyoshauri AG (Werema)’. Maagizo ya Mheshimiwa Rais yaliwasilishwa kwa PST kwa barua ya tarehe 13 Novemba, 2013, na ilisainiwa na Katibu wa Rais, Bwana Prosper Mbena.”

Baada ya kupata maelekezo hayo, ndipo BoT ilipomwandikia PST, ikiomba mwongozo kuhusiana na suala la madai ya TRA kuhusiana na VAT. Barua hiyo iliandikwa Novemba 15, 2013, na nakala yake kupelekwa kwa AG.

Kilichozingatiwa na BoT ni kwamba madai ya kodi za Serikali yanachukuliwa kama madai yenye umuhimu wa juu katika malipo yoyote.

Kwenye taarifa yake, BoT inasema: “Hata hivyo, BoT ilikwenda mbali kuhakikisha kwamba utekelezaji wa uamuzi wa Mahakama, pamoja na makubaliano ya kukabidhi fedha unapata baraka za wakuu wa nchi kama vile Mheshimiwa Rais na Waziri Mkuu.”

Rekodi za Bunge (Hansard) zinaonesha kuwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, aliihusisha Ikulu moja kwa moja na uchotwaji wa fedha hizo, Sh bilioni 320, ambazo wakati mwingine zinatajwa kama Sh bilioni 202 kutoka Tegeta escrow. Alimtaja Mnikulu, Shabani Gurumo, kwamba ni miongoni mwa waliopata mgawo wa Sh milioni zaidi ya 800. Kuna taarifa sasa kuwa Gurumo atahojiwa.

 

Kafulila aibana Ikulu

Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila, anasema jeuri ya vigogo wa Serikali kukataa kujiuzulu ni mtego kwa Rais Jakaya Kikwete.

Anasema ushahidi unaonesha baadhi ya maofisa wa Ikulu wamehusika kwenye kashfa ya escrow kwa kuchotewa mamilioni ya shilingi.

Anasema ni kwa sababu hiyo ya kuhusika kwao, ndiyo maana wahusika wanapata jeuri kuona kuwa hawapo peke yao kwenye sakata hilo.

“Rais anapaswa kusafisha kuanzia Ikulu ili kuipa ofisi yake uhalali kwani watendaji wake wasio waadilifu kama hawa wanaotakiwa kujiuzulu na kugoma,” anasema.

Anasema Baraza la Mawaziri halikujulishwa zaidi ya kujadili suala hilo baada ya sakata hilo kutokea. Alisema huo ni ushahidi tosha kuwa Ikulu inahusika. Kwa mtazamo wake, kama Spika angekuwa makini, Serikali yote ingeanguka.

Anasema ripoti ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) juu ya IPTL iliyojaa jinai za wahusika kama ilivyofichwa ya mwaka 2000, haitatolewa hadharani.

“Ndiyo maana nasema hii siyo mara kwanza Ikulu kuficha ripoti za Takukuru kuhusu ufisadi wa IPTL. Mwaka 2000 ilichunguza kuhusu vigogo waliohusika katika mkataba huu na namna rushwa ilivyotumika lakini haikutoka,” anasema.

 

CCM yawachinjia baharini Chenge, Ngeleja, Tibaijuka

 

Kwa upande wake, Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kikao chake kilichokaa mwishoni mwa wiki, imeamua kuwaondoa kwenye vikao vya kwa kukiuka maadili viongozi waliopokea mgao kutoka kwa Rugemalira.

Andrew Chenge, ambaye ni Mbunge Bariadi Magharibi, Anna Tibaijuka ambaye ni Mbunge wa Muleba Kaskazini na William Ngeleja ambaye ni Mbunge wa Sengerema, hawa walikuwa wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, huku Tibaijuka akiwa Mjumbe wa Kamati Kuu. CCM imewavua nyadhifa hizo.

Mbali na ujumbe wa NEC, ikumbukwe kuwa Chenge na Ngeleja walikwishavuliwa nyadhifa zao za uenyekiti wa Kamati za Bunge. Chenge alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti na Ngeleja alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba na Sheria. Nyadhifa hizi pia wamezipoteza.

Fedha zinazowatesa ni kiasi cha Sh bilioni 1.6 kwa Prof. Tibaijuka, Sh bilioni 1.6 kwa Chenge aliyejinadi kuwa yeye ni nyoka mwenye makengeza anayetafuta fedha kwa akili, huku Ngeleja akiponzwa na Sh milioni 40. Mgao huu waliupata kupitia akaunti zao zilizopo Benki ya Mkombozi, jijini Dar es Salaam.

CCM kinasema viongozi hawa wamekiuka sheria ya maadili kwa kupokea fedha hizi na wastangaze au kuziingiza katika fomu za matamko yao wanayotoa kila mwaka kwenye Tume ya Maadili kuonyesha mali na madeni waliyonayo.

1923 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!