Loliondo yageuzwa Kenya

*Siri sasa yafichuka, asilimia 70 si Watanzania

*Uhamiaji Mkoa Arusha lawamani kwa rushwa

 

 

Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Arusha inatuhumiwa kuwa chanzo cha raia wengi wa Kenya kujipenyeza ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), na kutangaza kuwania nafasi mbalimbali katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Desemba, mwaka huu.

Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umebaini kuwa juhudi za kuwabaini na kuwachukulia hatua za kisheria wahamiaji haramu na walowezi kutoka taifa hilo jirani zinakwamishwa katika ngazi hiyo ya mkoa.

Katika Kijiji cha Ololosokwan Tarafa ya Loliondo, Ngorongoro, raia wa Kenya, Esophio Parmwat; licha ya kubainika kuwa si raia wa Tanzania, Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Arusha ‘imebariki’ awanie uenyekiti wa Serikali ya Kijiji hicho.

Idara ya Uhamiaji Wilaya ya Ngorongoro, katika barua yake ya Novemba 3, mwaka huu kwenda kwa Katibu wa CCM wa Wilaya hiyo, ilisema kuwa Parmwat si raia wa Tanzania, na kwa sababu hiyo hapaswi kuwania nafasi yoyote ya uongozi.

Hata hivyo, imebainika kuwa katikati ya mwezi huu Parmwat alisafiri hadi Arusha, na aliporejea Loliondo siku mbili baadaye, alisikika akitamba kwa kusema” “nimerejeshewa uraia wangu”.

Kuna habari kwamba Parmwat ana ndugu zake wengine wengi nje na ndani ya Serikali, ikiwamo Wizara ya Maliasili na Utalii ya Serikali ya Tanzania. Mtumishi huyo ambaye kwa sasa JAMHURI inahifadhi jina lake, amekuwa mtetezi mkuu wa ndugu zake Wakenya kupitia mitandao ya kijamii, hasa ule wa Jamiiforums.

Mwingine anayetajwa kuwa si raia wa Tanzania, asili yake imebainika kuwa ni Mombasa, Kenya; lakini sasa ni Mtendaji wa moja ya Kata. Jina na Kata anavyoongoza tunavyo. Tutamtaja baada ya kuzungumza naye.

Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umebaini kuwa karibu asilimia 70 ya watu wote waliopo Loliondo na Wasso na vijiji kama Ololosokwan, Soitsambu na Oloipir ni Wakenya.

Wengi wao wameshika nafasi za uongozi wa vijiji ili iwe rahisi kuwakaribisha wenzao wanaoingiza mifugo kwa ajili ya malisho; na wengine ni walimu na pia makanda wa CCM.

 

Uhamiaji Mkoa wajitetea

 

Mkuu wa Idara ya Uhamiaji (R.I.O) Mkoa wa Arusha, Daniel Namomba, amelithibitishia JAMHURI kuwa tatizo la wahamiaji haramu na walowezi katika Wilaya ya Ngorongoro, hususa Tarafa ya Loliondo, ni kubwa.

Hata hivyo, amekanusha madai ya kuwapo vitendo vya rushwa katika ofisi yake vinavyosababisha watu hao wasio raia kuendelea kuishi kwa raha mstarehe na kuendesha vitendo vya uvunjifu wa amani nchini.

“Hao mnaosema wahamiaji haramu, si wahamiaji haramu. Hapa kuna makundi mawili-kuna wahamiaji haramu na walowezi. Walowezi ni wale ambao wazazi wao walikuja nchini miaka mingi, babu zao walikuja miaka mingi na wakazaliwa hapa, lakini sheria zetu hazisemi ukishazaliwa hapa wewe ni raia wa Tanzania. Kuna taratibu za kufuata ili uwe raia halali wa Tanzania.

“Tumepokea maelekezo kutoka ngazi za juu tuwatambua na kuwaorodhesha walowezi wote na kisha tupeleke taarifa Makao Makuu ya Uhamiaji ili uamuzi utolewe.

“Kwa sasa hicho ndicho tunachokifanya. Lakini utaona mambo haya ya uraia yanaibuka sana wakati uchaguzi unapokaribia, mambo haya yanakuzwa kisiasa zaidi,” anasema Namomba.

Alipoulizwa kuhusu Parmwat kutamba kuwa amerejeshewa uraia wake, alisema si kweli.

“Si kweli kabisa, mimi najua habari ya huyo mtu, kama anasema amerudishiwa uraia si kweli. Taarifa tulizonazo ni kwamba si raia wa Tanzania kwa hiyo hapaswi kugombea uongozi,” amesema.

R.I.O huyo ametoa wito kwa walowezi wote kujitokeza kwa hiari yao ili waweze kuorodheshwa.

“Watoe ushirikiano. Wahamiaji haramu wafuate sheria, wakipuuza sheria itawabana. Wananchi watupatie ushirikiano – wawataje wahamiaji haramu na walowezi wote. Tunaahidi kuwalinda wananchi watakaotoa taarifa,” anasema.

 

Kamishna Abdullah azungumza

Kamishna wa Huduma za Uhamiaji na Udhibiti wa Mipaka, Abudallah Abdullah, amezungumza na JAMHURI na kukiri kuwa suala la walowezi na wahamiaji haramu katika eneo la Loliondo ni kubwa.

“Tunazo taarifa na ukubwa wa tatizo. Tunaomba wananchi waendelee kutupatia taarifa. Ninachoweza kukuhakikishia ni kwamba ‘moto unakuja’…utaunguza hadi mchanga. Taarifa zote tunazo na tumejiandaa.

“Walowezi na wahamiaji haramu tunaendelea kuwashughulikia katika mikoa ya Kigoma, Geita na Kagera. Wakati ule waliondoka, lakini wapo waliorudi.

“Kigoma wamejitokeza wengi sana waliorudi, sasa na Loliondo wajue moto unakuja…lini tutakwenda, hilo hatulisemi kwa sasa lakini wananchi wajue tupo kwa ajili ya kuilinda nchi yetu dhidi ya wahamiaji haramu na walowezi. Tunachoomba kutoka kwao (wananchi) watupatie ushirikiano, wasikubali kuwaficha au kuwaonea haya watu waso raia. Watupatie taarifa,” amesema Kamishna Abdullah.

 

Waziri Chikawe

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe, amezungumza na JAMHURI na kukiri kuwa tatizo la wahamiaji haramu na walowezi katika eneo la Loliondo ni kubwa.

Chikawe alipoulizwa kama anajua rushwa kwa baadhi ya watendaji wasio waaminifu inachangia tatizo la wahamiaji haramu na walowezi, alisema: “Ile Idara ina matatizo. Nimezungumza nao. Wapo wachapakazi wazuri sana, lakini wapo wanaokwamisha mambo. Hao nimeagiza washughulikiwe bila woga ili kuifanya Idara hii iwe na heshima zaidi na iaminiwe na wananchi.

“Tatizo ni kubwa, nami nalikubali. Juzi tulipokuwa Kiteto kwenye mgogoro kati ya wakulima na wafugaji tulibaini mambo ya ajabu sana. Kuna watu wanapelekwa Kiteto kwenda kufanya vurugu. Wanatolewa Loliondo na wengine kwa hakika inawezekana kabisa si raia. Nawahakikishia wananchi kuwa wote hao watashughulikiwa kisheria.”

 

Wakenya ndani ya CCM

 

Katibu wa CCM Mkoa wa Arusha ambaye ndiye Mkurugenzi wa Uchaguzi ndani ya chama hicho mkoa, Alphonce Kinamhala, amezungumza na Gazeti la JAMHURI na kusema:

“Hilo suala limenifikia, nimemwagiza Katibu wa CCM Wilaya ya Ngorongoro alifuatilie, bado hajanipa taarifa rasmi, lakini kama unasema Uhamiaji wameshatoa majibu, basi hatuna uamuzi mwingine zaidi ya kuheshimu walichosema.

“Sisi CCM kwa upande wetu hatuwezi kuwa na pingamizi, hata akilalamika lakini Uhamiaji wakawa wamethibitisha, basi. Tena yupo mwingine naye imebainika siyo raia wa Tanzania.”

Barua ya Uhamiaji kwenda kwa Katibu wa CCM Wilaya ya Ngorongoro, imeandikwa na Kaimu Afisa Uhamiaji Wilaya ya Ngorongoro, Paul Gasper. Ina kichwa cha habari: “Pingamizi kwa Ndugu Esophio Parmwat kugombea nafasi ya Mwenyekiti katika Kijiji cha Ololosokwan kwa tiketi ya CCM”.

Inasema, “Nimepokea nakala ya barua ya Oktoba 27, 2014 uliyoandikiwa na Kirimbuot Dukuny kuhusu mada hapo juu na kutaka Ofisi ya Uhamiaji Wilaya kutoa ufafanuzi au uthibitisho wa jambo hilo.

“Ni kweli kwamba Ndugu Esophio Parmwat aliwahi kukamatwa kwa mahojiano kufuatia (kutokana na) kesi ya uraia ya mdogo wake Ndugu Kunday Parmwat iliyoanza tangu mwaka 2009 na bado inaendelea.

“Kwa uthibitisho wa kumbukumbu zetu zinaonyesha mtajwa hapo juu si raia wa Tanzania, na katika mahojiano dhidi yake naye alikiri kuwa uraia wake una utata na mpaka leo hakuweza kuithibitishia Ofisi kuwa baba yake ni nani na ni  raia wa nchi gani, japo alikubali kuwa mama yake ni raia wa Kenya.

“Kwa kuwa ndugu Esophie Parmwat anayo kesi ya kujibu na taratibu zingine za ofisi zinaendelea kuhusu kesi yake, asingefaa kushiriki kwa namna yoyote katika majukumu makubwa na muhimu kwa Taifa hili ikiwa ni pamoja na kuchagua au kuchaguliwa na kugombea nafasi yoyote katika jamii inayohusu au kumpa uwezo wa kuwa katika nafasi ya kutoa maamuzi (uamuzi) katika jamii.

“Lakini pia Ofisi ya Uhamiaji Wilaya inapenda kuishauri Ofisi yako kwamba ni vizuri wanachama wako kuheshimu na kuzingatia sheria za nchi katika kipindi hiki cha mchakato wa uchaguzi wa Serikali na vyama kwa jumla.”

Nakala ya barua hiyo imepelekwa kwa Afisa Uhamiaji Mkoa wa Arusha, Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, na Kirimbuot Dukuny ambaye ndiye aliyeweka pingamizi dhidi ya raia huyo wa Kenya.