Ukweli na uongo havikai pamoja kama ilivyo nuru na giza. Tumeyasema na kuyaandika mengi kuhusu Pori Tengefu Loliondo. Bahati nzuri wasomaji hawajachoka kuyasoma; na tunaendelea kuwaomba msichoke.

Mapambano ya kulinda uhai wa Loliondo yanachochewa na ukweli kuwa bila kuwapo kwa Pori hilo, Hifadhi ya Taifa Serengeti (SENAPA) itakufa. Bila kuilinda Loliondo, raha wanayopata walimwengu ya kufaidi wanyamapori, ndege na uwanda ‘usio na kikomo’ itatoweka!

Kwanini Loliondo? Pori Tengefu Loliondo lina ukubwa wa takribani kilomita za mraba 4,000. Linapakana na Senapa kwa upande wa magharibi na eneo la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) kwa upande wa kusini. 

Kaskazini mwa Pori Tengefu Loliondo kuna nchi ya Kenya. Katika Pori hili, shughuli za maisha ya binadamu kama vile makazi, kilimo na ufugaji hufanyika. Vilevile shughuli za uhifadhi wa wanyamapori na matumizi ya uwindaji na utalii wa picha hufanyika. Kampuni za uwindaji wa picha hazilipi ada za Serikali kwa sababu zipo kwenye kitalu ambacho kisheria kinaendeshwa na Kampuni ya Ortello Business Corporation (OBC). 

Kuna sababu kadha wa kadha zinazotajwa kuwa ndiyo chimbuko la mgogoro katika Pori hili. Mosi, ni kuongezeka kwa idadi ya watu na mifugo inayotokana na wenyeji na wahamiaji haramu kutoka Kenya. 

Mifugo hiyo isiyodhibitiwa imeathiri maeneo muhimu kwa utalii katika Hifadhi ya Taifa Serengeti na NCAA, hasa eneo la Ndutu. 

Pili, kuongezeka kwa shughuli za kilimo na shughuli nyingine za kibinadamu pamoja na kukosekana kwa mipango ya matumizi bora ya ardhi katika eneo lote la Pori Tengefu Loliondo, kumesababisha kuwapo kwa matumizi holela ya ardhi. 

Hii inajumuisha kuongezeka kwa vijiji vipya (vijiji kuanzishwa kadri waanzishaji wanavyojisikia), vijiji kuingia mikataba holela na wawekezaji; (mfano wa mkataba ulioingiwa na Kijiji cha Ololosokwan na kampuni za AndBeyond na Buffalo ambako mapato yanayotokana na uwekezaji huo hayaingii serikalini). 

Shughuli hizi, hasa za mifugo, si tu zimeathiri uhifadhi katika Pori Tengefu Loliondo, bali pia katika eneo la Mamlaka ya Ngorongoro na Hifadhi ya Serengeti ambazo ndizo kitovu cha utalii nchini. 

Tatu, chanzo kingine kikuu cha migogoro kinachotajwa ni mashirika yasiyo ya serikali (NGOs). Haya yamekuwa yakijipatia fedha nyingi kutoka kwa wafadhili wa ndani na nje ya nchi, na hivyo kuzisaidia kuendeleza migogoro. Watumishi wengi wa Serikali ndiyo hao hao wamiliki na waajiriwa katika NGOs hizo. Kwa maneno mengine ni kwamba NGOs haziko tayari kuona Loliondo ikitulia kwa sababu, kufanya hivyo maana yake ni kukata vyanzo vyao vya mapato.

 

Umuhimu wa kutenga eneo la uhifadhi

Lengo mojawapo kuu ni kulinda vyanzo muhimu vya maji kwa Hifadhi ya Serengeti kwa matumizi ya wanyamapori na binadamu. 

Pori Tengefu Loliondo lina vyanzo vya maji ya mto Grumeti ambao unatiririka kuelekea mbuga ya Serengeti hadi Ziwa Victoria. Vyanzo hivi vinachangia asilimia 48 ya maji yote yanayotumiwa na wanyama ndani ya Hifadhi ya Taifa Serengeti. 

Ni kwa sababu hiyo, shughuli za kibinadamu (kilimo na mifugo mingi) katika eneo hili la Loliondo zisipodhibitiwa zitasababisha vyanzo hivyo kukauka na Hifadhi ya Taifa Serengeti itaathiriwa au hata kutoweka. Hivyo basi, kuhifadhi eneo lenye vyanzo vya maji katika Pori Tengefu Loliondo kuna umuhimu mkubwa sana katika ustawi wa Hifadhi ya Taifa Serengeti. 

 

Kudhibiti mifugo

Ikiwa mifugo na watu kutoka nje ya Tanzania watadhibitiwa na mpango bora wa matumizi ya ardhi utaandaliwa na kutekelezwa na vyanzo mbadala vya maji kupatikana, eneo lililopendekezwa kubakizwa kama Pori Tengefu halitaathiri mifugo kwa kuwa eneo litakalobaki litakidhi mahitaji ya malisho ya mifugo na shughuli nyingine za binadamu – kilimo na makazi. 

Kuna umuhimu mkubwa kabisa wa kuwa na ufugaji unaozingatia uwezo wa eneo la malisho, kudhibiti mifugo kutoka Kenya na kuboresha miundombinu ya  mifugo (malambo ya maji yenye mtawanyiko mzuri, majosho, minada, njia za mifugo na uendelezaji na uboreshaji wa malisho na pia uanzishwaji wa viwanda vya kusindika mazao ya mifugo) ili kudhibiti mifugo kuvamia eneo litakalokuwa limetengwa kama Pori Tengefu.

 

Ushoroba

Kutenga eneo la Loliondo maana yake ni kulinda mapito (ushoroba) na eneo la mtawanyiko wa wanyamapori. 

Eneo hilo lina wanyama wa aina nyingi muhimu wakiwamo twiga, tembo, nyati, nyumbu, simba, pundamilia, swala na ndege wa aina mbalimbali. 

Kiikolojia, eneo hilo ni muhimu kwa kuwa ni sehemu ya mapito ya nyumbu na pundamilia – kundi la wanyamapori wahamao kutoka katika mbuga za Serengeti, Maasai-Mara (Kenya) na Ngorongoro. Mzunguko wa kundi hili kubwa la wanyamapori una umaarufu wa pekee duniani. Mzunguko huo ni kivutio cha watalii wengi sana wanaoliingizia Taifa fedha za kigeni na kodi mbalimbali. Loliondo ndilo eneo la mazalia ya nyumbu.

 

Juhudi za Serikali

Kwa kutambua umuhimu huu wa Pori Tengefu Loliondo, kwa miongo kadhaa sasa kumekuwapo juhudi za makusudi zinazofanywa na Serikali katika kuhakikisha linalindwa kwa maslahi ya nchi na ulimwengu. 

Tangu kuibuka kwa mgogoro mwanzoni mwa miaka ya 1990, kamati zaidi ya tano zimeundwa kuchunguza na kutoa mapendekezo ya kumalizwa kwa mvutano huo. Mapendekezo mengi yametolewa, lakini kubwa zaidi ni la kutengwa kwa eneo la kilometa za mraba 1,500 ili litumike kama ‘buffer zone’ kwa ajili ya kuilinda Serengeti na pia Loliondo yenyewe. Mpango huo umekuwa ukikwamishwa na NGOs zinazoshirikiana na mawakala wao wa ndani na nje ya nchi. 

Mwishoni mwa mwaka jana, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alizuru Wilaya ya Ngorongoro. Alitoa maagizo kadha wa kadha, lakini kubwa likiwa kumalizwa kwa mgogoro huo. Alimuagiza Mkuu wa Mkoa wa Arusha kushirikiana na wizara husika pamoja na wadau ili hatimaye ifikapo Mei, mwaka huu, mgogoro huo utangazwe kuwa ‘umefikia tamati’.

Kwa maelekezo hayo, iliundwa Kamati shirikishi ya mapendekezo ya kumaliza mgogoro huo.

Kamati ilianza kazi kwa kupata maelezo machache kuhusu hali halisi ya pori na namna ya kuanza kazi ya kutembelea Pori Tengefu.

Baadaye kikosi cha wataalamu kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, taasisi za Uhifadhi, Wilaya na wawekezaji kiliungana na viongozi wa kata na vijiji kufanya matembezi katika eneo lililopendekezwa la kilometa za mraba 1,500 ili kujionea mipaka, hali ya uhifadhi, hali ya miundombinu, shughuli za kiuchumi/utalii na mambo mengineyo.

Wadau waliweza kuzuru kata saba za Tarafa ya Loliondo ambazo ni Loliondo, Soitsambu, Oloipiri, Olorien/Magaiduru, Losoito/Maalon, Arash na Piyaya.

Baadaye, wajumbe walipata mawasilisho na maoni ya wataalamu, wawekezaji na wanajamii na mwishowe wakawa na majadiliano ya mawasilisho na makubaliano ya mapendekezo.

 

Kijichoonekana katika vijiji

Wajumbe wote waliozuru maeneo hayo walijionea hali mbaya kabisa ya namna mazingira yalivyoharibiwa. Walishuhudia matrekta kutoka Kenya yanavyolima katika vijiji kama Karkamoru; wakashuhudia ukataji miti uliopindukia; wakajionea namna vyanzo vya maji vilivyovamiwa na kuharibiwa. Chanzo kimoja kimeshikwa na aliyekuwa Mbunge wa Ngorongoro, Mathew ole Timan.

Wakaona maboma yasiyo na idadi yaliyojengwa mpakani kabisa mwa Pori Tengefu Loliondo na Hifadhi ya Taifa Serengeti.

Japo maeneo mengine walifika mchana, waliweza kuwaona ng’ombe walio katika mazizi. Walipowauliza wenyeji wakajibiwa kuwa mchana ng’ombe hushinda katika mazizi, lakini usiku hufunguliwa na kuingizwa ndani ya Serengeti. Wakafanikiwa kuwaona baadhi ya raia wa Kenya wenye mamia ya mifugo.

Kitendo hiki cha kuwapa fursa wajumbe kuzuru maeneo hayo, kikawafanya wengi wajionee hali halisi kinyume kabisa na propaganda za awali kwamba Loliondo iko shwari, na kwamba waandishi wanaoandika kuwa imeharibiwa wanafanya hivyo kwa kuhongwa!

Lakini wale wenye NGOs, viongozi kadhaa wa Serikali wenye maslahi na mgogoro wa Loliondo, pamoja na viongozi kama Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, Maiko Laizer, wakawa wanaendelea na mikakati ya kuwahamasisha wananchi vijijini wasikubaliane na mpango wa utengaji kilometa za mraba 1,500 kwa ajili ya Pori Tengefu.

Miongoni mwa waliotumiwa kufanya kazi hiyo ni Ngotee Joseph Parsambei wa NGO ya TPCF na  Emmanuel Saringe Naronyo (Parkimalo) ambaye yuko PINGOS Forums; pamoja na Sinandei Mako wa UCRT.

Lengo la NGOs likawa kuchochea wananchi vijijini ili wakatae mpango wa Serikali na wadau wa uhifadhi wanaoamini katika kuligawa eneo hilo ili kuilinda Loliondo na Serengeti.

Awali, mpango huo ulionekana kuwa na baraka zote za Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro na Mkuu wa Mkoa wa Arusha. Viongozi hao walionekana dhahiri kukinzana na msimamo wa Serikali wa kulilinda eneo hilo, lakini baadaye wameonekana kubadilika.

Nini kimewabadilisha? Hili ni swali ambalo halijapata jawabu la moja kwa moja. Wapo wanaoamini kuwa kubadilika kwao huenda kukawa kumetokana na kukemewa na wakuu wao.

Lakini wapo wanaoamini kuwa baada ya kujionea hali halisi ya uharibifu wa mazingira uliopindukia, na kutambua hatari inayoikabili Loliondo na Serengeti kiuhifadhi, wakawa hawana namna isipokuwa kuungana na wahifadhi.

Hata hivyo, wapo wanaomini kuwa kubadilika kwao ni kiinimacho kama njia ya kuwapumbaza baadhi ya wafuatiliaji wa sakata la Loliondo, kwani uhusiano wao na NGOs umekuwa hautiliwi shaka kwa muonekano na kwa vitendo.

 

Gambo, Nasha watoleana maneno makali

Gambo na Nasha, kwa nyakati fulani, walionekana kuwa na ajenda moja. Katika mkutano wa hadhara uliofanyika Ololosokwan, na kuhudhuriwa na Waziri Mkuu Majaliwa, Gambo alionesha ukaribu wake wa moja kwa moja kwa Nasha ambaye ni Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, na pia Mbunge wa Ngorongoro.

Kwa muda wote inajulikana wazi kuwa Nasha na viongozi wengine wa NGOs kama vile Samwel Naingiria wa NGONET; wamekuwa watumishi waaminifu wa mashirika hayo. Hawa wote ni marafiki wakuu wa jasusi raia wa Sweden, Suzan Nordlund, aliyefukuzwa nchini kwa PI, lakini wakawa wanamsaidia kuingia nchini na kufanya ujasusi Loliondo. JAMHURI ina vielelezo vinavyothibitisha ukaribu wa watu hao.

Nasha amekuwa mmoja wa wanufaika wakuu wa shirika la Oxfarm ambalo mara kwa mara limekuwa halisiti kuonesha ushiriki wake kwenye mgogoro wa Loliondo na mapenzi yake kwa Nasha. Oxfarm imekuwa ikifadhili NGOs mbalimbali, ikiwamo Pingos Forum.

Wakati ikitarajiwa kuwa Gambo angekuwa pamoja na Nasha, hali ilikuwa tofauti Jumamosi iliyopita ambako baada ya kuwasilishwa kwa mapendekezo, Gambo alisikika akimtolea maneno makali Nasha; hali iliyoibua maswali kadhaa miongoni mwa wajumbe.

Hata hivyo, watu walio karibu na wanasiasa hao vijana, wanasema chanzo cha mzozo huo ni uamuzi wa Kamati wa kuwa na mapendekezo mawili kuhusu Loliondo. Mapendekezo hayo mawili ni la ama kuanzishwa kwa Jumuiya ya Hifadhi (WMA), au kutengwa kwa kilometa za mraba 1,500 kwa ajili ya Pori Tengefu Loliondo.

Nasha ni miongoni mwa wanaotaka Loliondo iwe WMA kama ilivyowahi kuripotiwa na JAMHURI katika matoleo kadhaa ya mwishoni mwa mwaka jana. Mpango huo unaungwa mkono na Mwenyekiti wa CCM, Laizer. Pamoja nao, wengine wanaotaka Loliondo iwe WMA ni wawakilishi wote wa NGOs, Frankfurt Zoological na baadhi ya viongozi wa kimila walioshiba ushawishi wa NGOs.

Katika kuhakikisha hoja ya WMA inapata nguvu, NGOs hizo zilimwalika Damian Bell ambaye ni kiongozi wa asasi ya Honeyguide. Huyu ni mmoja wa ‘manabii’ wa uanzishwaji wa WMA.

 

Vita ya Wazungu na Waarabu?

Kinachoonekana kuwapo Loliondo kwa muda mrefu ni vita isiyotangazwa rasmi, kati ya raia wa kigeni (Wazungu) dhidi ya anayeendesha kitalu cha Pori Tengefu Loliondo (Mwarabu). Licha ya kuwapo kampuni nyingi katika eneo hilo, vita kuu ipo dhidi ya Waarabu. Ushahidi wa mpambano huo ni namna wafadhili kutoka Ulaya na Marekani wanavyomwaga fedha kupitia NGOs ambazo miongoni mwazo zimeanzishwa na kuendeshwa na raia wa Kenya. Waziri Mkuu Majaliwa, akiwa Loliondo Desemba, mwaka jana, alisema ana rekodi zote za NGOs na namna zinavyopokea fedha na nyingine kuzitunzia Kenya.

Baadhi ya Wakenya wanaohusishwa kwenye vurugu za Loliondo ni Maanda Ngoitiko na Tina Timan ambao wote ni madiwani kupitia Chadema.

 

Mkakati mpya wabuniwa

Kuwapo kwa mapendekezo mawili ili lipitishwe moja, la ama kuanzishwa kwa WMA au kutenga Pori Tengefu; kumeonekana kuwavuruga wale wanaopenda kudumu kwa mgogoro wa Loliondo.

Baada ya kikao cha Jumamosi iliyopita, wajumbe wa Kamati watakutana baada ya wiki tatu kama Gambo alivyotangaza. Kwa muda huo, kamati ndogo ya wataalamu imeundwa ili iandae ripoti ambayo itapelekwa katika ngazi za juu za uongozi wa Serikali kwa uamuzi.

Hofu ya NGOs, Nasha, Laizer, Bell, Diwani wa Ololosokwan na wengine kwenye kundi hilo, ni kuwa endapo suala hilo litafikishwa huko juu, ni wazi kwamba mapendekezo ya kitaalamu ya kuilinda Loliondo na Serengeti, yatazingatiwa. 

Kikao cha Jumamosi kilipoahirishwa, baadhi ya wajumbe, hasa kutoka kwenye NGOs na baadhi ya wazee wa kimila, walisusa chakula na kwenda kufanya kikao cha dharura kujadili mapendekezo hayo mawili.

Taarifa kutoka kwenye kikao hicho zinaonesha kuwa waliazimia kuendelea na ‘mapambano’ ya kuanzishwa kwa WMA.

Kwanini WMA? Kuanzishwa kwa WMA kuna maana kuwa NGOs, viongozi wa vijiji na wale wanaowaunga mkono watakuwa na nafasi ya kufaidi zaidi fedha zitakazotokana na mikataba watakayoingia na wawekezaji. Katika matoleo yajayo, tutaainisha faida na hasara za kuanzishwa kwa WMA na vilevile faida na hasara za kutengwa kwa kilometa za mraba 1,500. Lakini lililo muhimu ni kwamba Loliondo ni eneo lenye sifa na umuhimu wa kipekee katika uhai wa Serengeti, Ngorongoro na Maasai-Mara.

Walau sasa ukweli unaanza kubainika kuwa Loliondo inahitaji ufumbuzi wa haraka. Kutembea ni kuona. Wajumbe waliozuru wamejionea hali halisi ya uharibifu wa mazingira iliyovuka kiwango. Kama Waziri Mkuu Majaliwa amepitishwa japo nusu tu ya eneo ‘alilofichwa’ wakati wa ziara yake Ngorongoro, naamini tayari msimamo wa Serikali ungekuwa umeshatangazwa. Ukweli na uongo havikai pamoja kama ilivyo nuru na giza.

By Jamhuri