“Mtoto wa nyoka ni nyoka.” Usemi huu wa wahenga unajionesha wazi kwa baadhi ya familia zilizojaaliwa kuwa na vipaji vikubwa.

Vipaji hivyo vinaweza kuwa vya kucheza mpira, muziki, kucheza sarakasi, riadha, ndondi n.k.

Mifano halisi ni kwa wanadada wawili Wamarekani weusi —  Serena na Venus Williams — ambao ni mabingwa kimataifa katika kucheza mpira wa tenisi.

Hapa nchini, familia ya Uvuruge ina watoto walio na vipaji vya kutunga nyimbo na kupiga muziki. Ndugu hawa — Jumanne, Stamili, Huluka na Maneno — walijijengea sifa tele katika muziki hapa nchini.

Familia ya akina Kihwelu nayo ilikuwa na vipaji vya kucheza mpira wa miguu. Walikuwapo akina Mtwa, Jamhuri ‘Julio’ na ndugu zao wengine. Kwa upande wa ngumi, familia ya Matumla imerithisha kucheza mchezo wa ndondi takribani familia nzima.

Makala hii leo itaangazia familia ya Longomba kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). Vicky ndiye aliye kuwa baba wa familia ya watoto wengi waliojaaliwa vipaji hivyo vya muziki.

Kipaji kuanzia kwake Mzee Vicky Longomba, ambaye alikuwa mmoja wa wanamuziki waliokuwa waanzilishi wa Bendi ya TP OK Jazz, iliyokuwa ikiongozwa na Franco Luanzo Makiadi.

Pia ikumbukwe kwamba  Vicky ndiye  aliyekuwa  mwanzilishi wa bendi ya Lovy du Zaire, iliyotamba kwa muziki nchini Kongo mwaka 1971.

Kwa kuwa familia hiyo ina wanamuziki wengi, katika makala hii, nitamzungumzia mmoja wa watoto wake — Lovy Longomba.

Wasifu wa mwanamuziki huyo unaelezea kwamba alianza muziki katika bendi ya Orchestra Macchi mwaka 1976, akiwa na mwimbaji mwenzake Dindo Yogo.

Aidha, wakishirikiana na mpiga gitaa Nseka Huit, waliondoka katika Bendi ya Macchi na wakaunda bendi yao ya  Etumba na Ngwaka wakiwa na waimbaji wengine akina Lofanga, Gaby Yau-Yau na Mukolo, aliyekuwa akiimba sauti ya kwanza. Wanamuziki wengine waliokuwapo katika bendi hiyo ni pamoja na Huit Kilos, ambaye baadaye alikwenda kuwa nyota katika bendi ya Afrisa International ya Tabu Ley Rochereau. Mwanamziki Ricardo aliondoka na kwenda katika bendi ya Lemvo Makina Loca, iliyo na makao yake huko Los Angeles, Marekani.

Lovy alikuwa kaka wa wanamuziki Awilo Longomba. Awilo kabla ya kuanza kutunga na kuimba, alikuwa mcharazaji hodari wa ngoma (drums) katika bendi mbalimbali nchini humo.

Lovy pia alikuwa baba wa familia yenye watoto wanamuziki akiwamo binti yake aliyerithi uimbaji — Elly Longomba, na mapacha Christian na Lovy — ambao wote ni nyota katika muziki wa Hip-hop, wakimiliki Kampuni ya ‘Longambas’ huko Nairobi, nchini Kenya.

Baadaye  Agosti 1978, Lovy aliiacha Bendi ya Orchestra Macchi, na kuamua kuondoka  Kinshasa. Alitinga katika jiji la Nairobi, Kenya ambako alijiunga katika Bendi ya  Les Kinois.

Kwa kuwa ‘kiu’ yake haikuwa imekidhiwa, Lovy alidumu kwa miezi mitatu tu, akatimkia katika Bendi ya Boma Liwanza.

“Maisha ni kutafuta.” Mbio za kutafuta maisha zikaendelea. Baada ya miezi sita Lovy alitimka na kuiacha Boma Liwanza, akajiunga na bendi ya Super Mazembe iliyokuwa ikiongozwa na  Mutonkole Longwa Didos.

Katika bendi hiyo alionesha uhodari wa kutumia sauti yake ilivyokuwa nyembamba na nyororo, ambayo ndiyo iliyosababisha kwa yeye kupachikwa jina bandia la ‘Ya Mama’. Sababu kubwa ni kwamba alikuwa na uwezo wa kuimba sauti ya juu ambayo alipashwa aimbe mwanamke.

Katika bendi hiyo alikutana na  wanamuziki wenzake mahiri akina Joseph Okello Songa, Kasongo wa Kanema, Musa Olokwiso Mandala na Fataki Lokassa ‘Masumbuko ya Dunia’ aliyekuwa ametokea katika Bendi ya Les Noirs.

Baadhi ya nyimbo alizoachia katika Bendi ya Super Mazembe ni pamoja na ‘Lovy’, ‘Yo mabe’, ‘Ndeko’, ‘Nanga’, ‘Mokano’ na ‘Elena.

Sauti yake nyororo mara nyingi husikika katika baadhi ya nyimbo za bendi hiyo, akibwagiza akitamka “Vuta sigara SM, maana yake Super Mazembe…” Hata hivyo, umahiri wa kutunga na kuimba katika bendi hiyo, ilisababisha kuhitajika takribani na kila bendi.

Kwa mara nyingine Lovy aliondoka Super Mazembe mwaka 1981 na kwenda kuimba katika Bendi ya Shika Shika, iliyokuwa ikiongoza na Jimmy Monimambo, kwa miaka miwili. Ndoto za kumiliki bendi yake zilitimia baada ya yeye na wanamuziki wenzake kuunda bendi yake Super Lovy ikiwa na nembo ya AIT.

Lakini kwa kile alichokieleza ni kuepuka mkanganyiko na mvutano, aliamua kutumia jina Bana Likasi  wakati aliporekodi  katika  Kampuni ya Audio Productions Ltd. Mwaka 1988 Lovy aliingia Tanzania katika jiji la Dar es Salaam na akapigia katika Bendi Orchestra Afriso Ngoma.

Bendi ya Afriso ilikuwa ikimilikiwa na Mzee Mwendapole. Katika bendi hiyo alikutana na wanamuziki wengine, kati yao ni Belly Kankonde, Kinguti System na Anania Ngoliga, Toffy Mvambe, Salim Shaban na Malik Nduka Masengo (Maliky Star). Hao walikuwa waimbaji. Wapigaji gitaa walikuwapo akina John Maida, Peter Kazadi, Robert Tumaini Mabrish, Mjusi Shemboza, George na Kasongo. Upande wa drums, walizicharaza Karume na Abdul wakati ngoma zilidundwa na Magoma Sony. Kwa upande wa tarumbeta (trumpet) walikuwa akina Juma Urungu, Ramadhani na Mbaraka Othman.

Baada ya hapo aliwahi kujiunga katika bendi ambayo ilikuwa na wanamuziki kadhaa kutoka Sikinde, ikijulikana kwa jina la Sikinde Academia, ambayo haikudumu sana.

Maisha ya nguli huyo yalikatishwa ghafla katika ajali iliyosababisha kifo chake katika ardhi ya Tanzania mwaka 1996. Mungu aiweke roho yake Mahali Pema Peponi, amina.

 

Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa namba: 0784331200, 0767331200 na 0713331200.

By Jamhuri