LowassaEdward Ngoyai Lowassa kaamua kufanya mabadiliko ya kweli ya siasa hapa nchini. Kakihama chama chake cha siku zote na kuingia kwenye chama kingine, chama kikuu cha upinzani hapa nchini – Chadema. Huo ni uamuzi ambao Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, kaamua kuupa jina la kubadilisha gia hangani.


Tukio hilo limetazamwa kwa hisia mbalimbali zilizo tofauti na wananchi. Wapo waliolipenda na kulifurahia sana jambo hilo, wapo waliolichukia na wapo walioduwaa tu wasielewe ni kipi kilichotokea! Vilevile wapo wanaoliona hilo kama uamuzi wa kishujaa wa kisiasa.
Kwa upande wangu, tukio hilo naliona kama uamuzi wa kishujaa. Tanzania tumezoea kuwaenzi mashujaa wa nchi hii bila kujiuliza watu hao walikuwa viumbe wa aina gani. Watu hao bilashaka walikuwa wanadamu kama tulivyo sisi, na moja kati ya mambo waliyoyafanya mpaka sasa tunawakumbuka na kuwaenzi ni kama hilo walilolifanya akina Mbowe na Lowassa. Ni mashujaa.


Nalazimika kumtaja Mbowe nikiwa na maana ya wote walioubariki ujio wa Lowassa katika Chadema. Bila kuubariki ujio huo sidhani kama sasa hivi tungekuwa tunaongelea kitu hicho. Wamefanya kitu cha aina yake katika siasa za nchi yetu, na ndiyo maana baadhi ya watu wanaduwaa kwa sababu ni kitu ambacho hakikuzoeleka.
Pamoja na kutozoeleka, uamuzi huo wa Lowassa kukihama chama chake na kujiunga na chama cha upinzani sioni kama una utata wowote, sababu kabadilisha tu makazi ndani ya nchi yake ileile. Mimi ningemuona ni mtu wa ajabu kama angekuwa amebadilisha uraia wake, pengine kuhama nchi na kwenda kuwa raia wa nchi nyingine.


Lakini kuhama chama nakuchukulia kama kuhama chumba ndani ya hoteli ileile ambayo mtu anakuwa ameipanga. Sioni kwa nini hilo liwape watu taabu ya kulielewa.
Kama watu hawawashangai wanaotelekeza taaluma zao na kuingia kwenye siasa, kama vile uhandisi, udaktari, uanasheria, ualimu na kadhalika, iweje wamshangae mtu aliyehama chama cha siasa na kuingia kwenye chama kingine cha siasa kuendeleza taaluma yake ileile ya siasa?
Baadhi ya watu wameuona huo kama ni usaliti kwa pande zote mbili, wapo wanaomuona Lowassa kama mtu aliyekisaliti chama chake, CCM, kwa kukiacha na kuingia kwenye chama cha upinzani. Wenye mtazamo huo hawauongelei usaliti ambao Lowassa amefanyiwa ndani ya chama hicho! Hiyo ni kushindwa kuyapima mambo kwa usawa na uwazi.


Sababu hata mitume wa Mwenyezi Mungu kule walikofanyiwa usaliti walipangusa miguu yao na kuondoka wakiwa wameachana nako. Ushahidi uko kwenye maandishi ya dini, Biblia Takatifu na Koran Tukufu. Iweje leo Lowassa aonekane wa ajabu?
Wakati wa harakati za chama cha TANU kupigania uhuru wa Tanganyika, chini ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, wapo waliomuona Nyerere kama mtu anayetaka kuwapeleka wasikokutaka kwa tabia yake ya kutopenda kuwabagua watu wa rangi nyingine, wakidai kwamba msimamo huo haukuonesha uzalendo. Nyerere alikuwa anataka kura tatu zilizowekwa na wakoloni kama mtego, lakini akautegua.


Huo ulikuwa mwanzo wa kuanzishwa kwa chama cha ANC chini ya Zuberi Mtemvu, ambacho hakikufika kokote kutokana na itikadi zake za ubaguzi. Bado Nyerere akaonekana shujaa na TANU yake.
Nchini Afrika Kusini, ndani ya chama cha wazalendo cha ANC kuna waliochukizwa na neno la “sisi watu wa Afrika Kusini” wakitaka litumike neno la “sisi weusi wa Afrika Kusini”. Wakisema kwamba weusi ndiyo wazalendo wa nchi hiyo, kwa vile neno “sisi watu wa…” lilizijumuisha na rangi nyingine walizotaka wazitenge.
Ndipo Machi 1959 kikaanzishwa chama cha PAC kikiongozwa na Robert Sobukwe. Watu waliopinga ubaguzi wa rangi ulioendeshwa na makaburu wakaanzisha chama kwenye misingi ileile ya ubaguzi wa rangi! Kwa hiyo, ikaonekana walichokitaka ni kuuondoa ubaguzi wa Wazungu na kuusimika ubaguzi wa weusi!
Chama hicho hakikufika kokote, mpaka sasa kimebaki tu kwenye historia. Kwa mantiki hiyo ndiyo maana nauona uamuzi wa Chadema kumkaribisha Lowassa kama uamuzi wa kishujaa. Ni uamuzi wa kuukana ubaguzi, kumbagua Lowassa na wengine watakaotaka kufuatana naye, kwa sababu ya ‘wao CCM’ na ‘sisi Chadema’.


Mbowe kajitahidi kuikwepa dhambi hiyo ya ubaguzi, dhambi ambayo Baba wa Taifa aliifananisha na dhambi ya binadamu kula nyama ya binadamu mwenzake.
Wapo wanaodai kwamba Lowassa ni mzigo, wakiwa wamemchukulia Mbowe kama aliyekisaliti chama chake!  Sielewi hilo wanalisema wakiwa wamejibanza wapi. Kama wananchi wako tayari kumbeba Lowassa kwa namna wanavyojionesha, inawezekanaje mtu mmoja mmoja amuone kuwa ni mzigo?
Mimi nadhani atakayemuona ni mzigo ni bora akajiweka pembeni na kuwaachia walio tayari kuubeba mzigo huo. Haiwezekani walio wengi waseme tunataka tumbebe mtu huyu pembeni atokee mtu mmoja na kudai kuwa anayebebwa ni mzigo na walio wengi washawishike bila kuuona uzito wake.
Mzee mmoja wa Tabata, ambaye hakutaka jina lake liwekwe gazetini, amesema kwamba linaweza kuwa jambo la ajabu kuwaacha samaki walioletwa na mafuriko na kubaki nchi kavu watu wakaogopa kuwakamata wakidai kwamba wanataka wawavue majini, ziwani au baharini. Akaongeza kwamba vilevile litakuwa jambo la kushangaza mtu kukuta dhahabu juu akaiogopa eti mpaka aichimbe ardhini ndipo aamini kwamba kapata dhahabu ya kweli!


Kwa hiyo, yeye anaamini kwamba kilichotokea kwa Lowassa kujiunga na Chadema ni sawasawa na dhahabu iliyokutwa juujuu bila kuhangaika kuchimba sana ardhini kuitafuta. Hivyo eti wanaolitilia shaka hilo ndiyo watu wa kuwatazama kwa umakini.
Lowassa alikuwa amejipanga kuyaleta mabadiliko kupitia kwenye chama chake kwa kutumia kaulimbiu aliyoiibuni ya “Safari ya matumaini”, lakini kutokana na chama chake hicho cha zamani kuwa na kila dalili za uhafidhina, ikaonekana safari hiyo ambayo chama hicho hakikuwa na uhakika nayo inaweza ikakiletea mambo mapya. Chama kikaamua kumtema ili kuondokana na safari hiyo.


Chadema ambacho kipo kwa ajili ya mabadiliko yaliyolenga kwenye maendeleo kama jina lake linavyojionesha, Demokrasia na Maendeleo, kikaona mtu huyo hakutendewa demokrasia alikokuwa, na pia hakupewa nafasi ya kuanzisha safari yake ya Matumaini, ambayo bilashaka yalikuwa ni matumaini ya maendeleo, kikamkaribisha. Tatizo liko wapi?
Masuala yanayosemwa ya kwamba Chadema ilishamtaja Lowassa kama fisadi ni mambo madogo tu ambayo yanatokana na msukumo wa kiitikadi. Mtu anaweza kuonekana ni fisadi kutokana na mahali aliko lakini akiachana nako na kuamua kupakana mwonekano wake unabadilika mara moja. Ndiyo maana watu wanaamua kuokoka na kuanza kutoa ushuhuda wa waliyokuwa wakiyafanya kabla ya kuokoka bila ya watu kuwahofia.


Katika ushuhuda unaotolewa na walokole utasikia wakisema, mimi nilikuwa jambazi, nilikuwa mchawi na wengine kufikia kusema walikuwa wakila nyama za watu, lakini sijawahi kusikia hata mara moja mtu anayekamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria kutokana na ushuhuda wa aina hiyo.
Nihitimishe kwa kuwashauri wapenda mabadiliko wote nchini kulichukulia tukio hili na Lowassa kuhamia Chadema kama moja ya mabadiliko tuliyoyasubiri kwa kipindi kirefu, na huo uwe mwanzo wa mabadiliko kamili. Heko Mbowe, heko Lowassa, uamuzi wenu ni wa kishujaa.
 
prudencekarugendo@yahoo.com

 
4660 Total Views 2 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!