LUIZA MBUTU… ‘Kizizi’ cha Twanga Pepeta

TABORA

Na Moshy Kiyungi

Miongoni mwa wasanii wa kike waliowahi kufanya makubwa enzi za muziki wa dansi nchini na kuwavutia wengi, ni Luiza Mbutu. 

Lakini kabla yake wamewahi kuvuma wanamuziki kadhaa wa kike maarufu kama akina Tabia Mwanjelwa, Asia Darwesh ‘Super Mama’, Salome Kiwaya, Pauline Zongo, Kida Waziri, Rahma Shari, Anna Mwaole, Taji Mbaraka Mwinshehe na Nyota Abdallah Kinguti.

Wakaja akina Luiza, Khadija Mnoga ‘Kimobitel’, Jessica Charles na Halima Ngaluma ‘Japanese’.

Leo tumzungumzie Luiza; mwimbaji na mnenguaji maarufu wa Bendi ya Twanga Pepeta ambaye hajawahi kuondoka katika bendi hiyo tangu alipojiunga.

Licha ya kuwa na umri mkubwa, akiwa jukwaani huonekana kama binti mdogo kutokana na umbo ambalo hulitumia kupamba jukwaa sambamba na wanenguaji wengine wakiongozwa na Super Nyamwela.

Luiza alianza kuonekana kwenye TV miaka ya 1990 akicheza na kuimba na mwanamuziki Chemundugwao katika wimbo ‘Tulitoka wote Mahenge’, wakati huo akifahamika kama Luiza Nyoni.

Dada yake mkubwa, Modesta, alikuwa mwimbaji wa Bendi ya Kalunde chini ya Deo Mwanambilimbi.

Wawili hawa ni miongoni mwa watoto saba wa familia yao; ni wao pekee ndio wasanii.

Wototo wa Modesta; Rose na Joseph, wamerithi mikoba ya mama yao wakiimba katika hoteli kubwa tofauti.

Luiza ni mzaliwa wa Lugalo, Dar es Salaam aliyesoma Shule ya Msingi Mkamba, Kilombero mkoani Morogoro pamoja na shule za Mzinga, Morogoro na Mushono, Arusha.

Baadaye akasoma Shule ya Sekondari Mabibo jijini Dar es Salaam, kisha akasomea utunzaji wa bohari Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) na kupata stashahada.

Wakati wote huo alikuwa akijilipia karo. Akasomea pia kompyuta pale Msimbazi Centre upande wa kuandaa kurasa za magazeti.

Muziki haukuja kama miujiza kwani Luiza alijiunga na masomo ya muziki yaliyokuwa yakitolewa na Kanisa la Mtakatifu Joseph jijini humo, hivyo kutimiza fikra na ndoto zake za kufanya kazi ya muziki.

Mwenyewe anasema kipaji cha kuimba kilianza tangu akiwa darasa la nne akiimba katika kwaya ya kanisa.

Luiza alianza kuimba muziki wa dansi mwaka 1997 kwenye bendi ya Magoma Moto ya mmiliki wa Hoteli ya Travertine, iliyopo Magomeni Mapipa.

Jina la Luiza Mbutu ambalo kwa sasa ndilo maarufu zaidi alilipata baada ya kufunga ndoa na Faiara Mbutu, muungurumishaji mashuhuri wa gitaa la besi.

Wanandoa hawa wamejaaliwa kupata mtoto mmoja anayeitwa Brian.

Tangu Luiza alipojiunga Twanga Pepeta mwaka 1998 akitokea Magoma Moto Sound, hata mara moja hajawahi kuihama bendi hiyo!

Mkongwe huyo anasema hajataka kuhama bendi hiyo kwa kuwa anapenda kuishi kwa kujifunza kutokana na wenzake wengi ambao wakihama, baada ya kipindi kifupi hurejea tena Twanga.

“Kuhama kwa mwanamuziki kunasababisha upoteze mashabiki wako. Kuna wanamuziki wamepotea katika tasnia kwa sababu ya kuhamahama.

“Mimi hilo sikulitaka. Nikaamua kudumu kwenye bendi moja, ukizingatia makubaliano yangu ya kimasilahi ni mazuri; kwa kweli nimeridhika nayo.

“Changamoto zipo kwenye bendi, hupaswi kuzikimbia kwa kuwa hazikosekani hata kwenye nyumba tunakoishi. Hiyo ndiyo siri ya kukaa Twanga zaidi ya miaka 20 sasa,” anasema.

Katika maadhimisho ya miaka 20 ya Twanga Pepeta Oktoba 20, 2018, Luiza alikumbuka mengi aliyowahi kuyashuhudia ndani ya bendi hiyo.

“Ninamshukuru Mungu kwa kuniweka hai mpaka leo, kwani wenzetu wengi tuokuwa nao wametangulia mbele ya haki.

“Tulipenda tunaposherehekea, wangekuwapo ila Mungu amewapenda zaidi. Kwa hiyo ninamuomba awape pumziko la milele,” anasema.

Anaamini tatizo kubwa kwa bendi hiyo ni la kuhama kwa wanamuziki wake na kuiyumbisha.

Mama Brian pamoja na mafanikio aliyoyapata, anausifu uongozi wa African Stars Entertainment Tanzania (ASET).

“Uongozi chini ya Asha Baraka umeisimamia vema Twanga Pepeta na kuifanya moja kati ya bendi kongwe nchini,” anasema Luiza.

Mambo mengine aliyoyakumbuka wakati wakielekea katika sherehe za miaka 20 ya Twanga Pepeta, ni kupata fursa ya kutembelea sehemu mbalimbali binafsi au na bendi yake.

“Safari hizo zimenifanya nijifunze na kuona vitu vingi, hivyo kupitia hilo kwangu ni kitu kizuri sana,” anasema.

Pamoja na mengine, kwa upande wa vitu vibaya ilikuwa ni kushuhudia wanamuziki wanahama, akidai kuwa kilikuwa kikimpa mshtuko sana.

“Nakumbuka Ramadhan Masanja ‘Banza Stone’ alipoondoka Twanga kwenda TOT, wakati huo tulikuwa tunaandaa albamu ya pili ya ‘Jirani’, akahama. Haikuwa vema japo alitupa funzo,” anakumbuka kwa masikitiko.

Uso wa Luiza ulibadilika na kuwa wenye huzuni alipokumbuka jambo jingine kubwa kwake; kumpoteza kiongozi wao, Abuu Semhando.

“Semhando alikuwa kiongozi, babu, meneja na katibu wa bendi aliyekuwa akituunganisha vizuri wanamuziki na uongozi,” anasema.

Semhando alifariki dunia kwa ajali ya pikipiki wakati akitokea kazini usiku wa Desemba 18, 2010 jijini Dar es Salaam.

Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa simu namba: 0784331200, 0713331200 na 0713331200.