Wiki moja baada ya gazeti hili kuchapisha makala kuhusu mgogoro wa ardhi kati ya Mamlaka ya Bandari ya Mtwara na wananchi wa Kitongoji cha Ng’wale, Mtwara Vijijini, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), Deusdedith Kakoko, na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, wamejitokeza na kutoa ufafanuzi juu ya mgogoro huo.

Kakoko ameiambia JAMHURI kuwa mgogoro wa ardhi ya Ng’wale siyo sababu kuu iliyokwamisha upanuzi wa bandari tangu mwaka 2000 hadi sasa, na kwamba kilichokwamisha ni kutokufikiwa kwa makubaliano ya kibiashara kati ya bandari na wawekezaji waliotarajiwa na bandari kufanya ujenzi wa upanuzi huo.

“Kilichopita ni bandari kutaka kuingia mikataba na wawekezaji binafsi ambapo mara mbili hawakufikia mwafaka. Lakini sasa tutapanua kwa awamu TPA wenyewe. Serikali haiwezi kushindwa kutwaa eneo kwa miaka 17. Sheria zipo wazi kuhusu taratibu zinazotakiwa na ni rahisi sana kwani ardhi ni mali ya umma na ushirikishwaji wa wananchi siyo shida,” amesema Kakoko.

“Ninachofahamu ni kuwa hakuna jambo lililotuzuia kupanua Bandari ya Mtwara na mwaka huu tunaendelea na hilo. Wala Mkuu wa bandari ya Mtwara hana agenda ya huo unaoitwa ‘mgogoro’ mezani kwake kwani angeshatoa taarifa,” amesema Kakoko.

Awali Meneja wa Bandari Mtwara, Juma Kijavara, aliiambia JAMHURI, yawezekana mgogoro huo ni moja ya sababu zilizokwamisha upanuzi wa bandari hiyo na yeye kwa nafasi yake haruhusiwi kulizungumzia suala hilo isipokuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari.

Wakati huohuo, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, ameitaka Kamati ya Maendeleo ya Kitongoji cha Ng’wale na Bandari kumwandikia barua ya kumweleza juu ya mgogoro huo ili ikibidi aunde timu ya kusuluhisha pande zote.

“Bandari na wananchi hawana haja ya kubishana. Ninachowaomba bandari waniandikie barua wanieleze walipokwama, mimi nitateua timu kwenda kusuluhisha. Jambo hili lipo ndani ya uwezo wangu. Mbona mgogoro ya Ruangwa tumeumaliza na watu wamelipwa fidia?” amehoji Waziri Lukuvi.

“Labda kama bandari walikuwa wanalihitaji eneo hilo kwa matumizi ya baadaye, lakini kama wanasema wanalihitaji kuanza kuliendeleza basi wanieleze kwani suala hili ni la maslahi ya Taifa na bandari ni taasisi ya Serikali. Hata wananchi wa kitongoji hicho nataka waniandikie barua wanieleze kwamba kuna tathmini ambayo ilifanyika na wao wameonewa nichukue hatua. Waandike barua kwangu na mimi nakuhakikishia mgogoro huu utaisha,” anasema Lukuvi.

“Kuhusu wataenda wapi, fidia stahiki ndiyo huamua wataenda wapi. Sheria haisemi kuwa baada ya kulipwa mtoa fidia ndiyo aamue utakakokwenda. Ni fidia uliyoipata ndiyo itakayokufanya wewe uamue. Kama ardhi yako ni kubwa si itafanyika tathmini utalipwa? Na kama tathmini ilifanywa chini ya sheria ya 1999 basi ardhi peke yake ina fidia hata kama hakuna mmea wala nyumba,” amesema Lukuvi.

Waziri Lukuvi amesema kwamba watu wa Ng’wale bado wanayo haki ya kisheria ya kulipwa stahiki zao na jambo muhimu ni pande zote kufikia maridhiano yenye maslahi kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.

Akizungumzia wito wa Waziri Lukuvi, Mwenyekiti wa Kamati ya ufuatiliaji wa mgogoro wa ardhi katika Kijiji cha Sinde, Marijani Dadi, amesema kuwa baada ya kesi yao kutupiliwa mbali na Mahakama, mgogoro huo ulibaki chini ya mamlaka ya mkoa ukisimamiwa na Kamishna wa Ardhi Mkoa Mtwara.

“Sisi hatuna tatizo na kauli ya Waziri lakini ikumbukwe kwamba tumeshawasiliana sana na wizara yake huko nyuma kupitia kwa Kamishna Mkuu lakini mgogoro huu haujapatiwa ufumbuzi. Hata baada ya kesi kufutwa tumekuwa tukizungushwa tu bila majibu ya msingi. Tutaangalia namna ya kutekeleza mwito huo wa waziri,” amesema Dadi.

Kamishna wa Ardhi Mkoa wa Mtwara, Gasper Luanda, amekataa kuzungumzia mgogoro huo.

1862 Total Views 1 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!