Taratibu mambo yameanza kuwekwa hadharani, na sasa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kinasema Mkurugenzi wao wa Idara ya Ulinzi, Wilfred Lwakatare, alirekodiwa na msaidizi wake, Joseph Ludovick. Hata hivyo, wakati Chadema wakiibua hayo, wanasema wanao ushahidi mzito unaonesha kuwa Ludovick alirubuniwa na Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Mwigulu Nchemba, kufanya uharamia huo.

Chadema kwa upande wao, habari za ndani zinasema Mwenyekiti Freeman Mbowe anataka ikithibitika mahakamani kuwa Lwakatare alishiriki kurekodi mkanda huo iwe kwa kurubuniwa, ‘kushikishwa’ au kuingizwa mkenge, itamlazimu kuwajibika kwa kosa la kukosa umakini.

 

Wakati Mbowe akiwa na msimamo huo, Katibu Mkuu, Dk. Wilbrod Slaa, anaamini Ludovick na Lwakatare wanasingiziwa kwani mkanda huo ni ‘feki’ umechongwa na CCM kwa kushirikiana na baadhi ya watumishi wasio waaminifu katika vyombo vya dola.

 

JAMHURI ilipowasiliana na Mbowe, alisema: “Kwa sasa siwezi kuzungumzia suala hili, kwa sababu nina kikao, labda wiki ijayo.” Hii ilikuwa ni baada ya mwandishi kumfuata katika ofisi za Bunge na kukutana naye uso kwa uso. Dk. Slaa hakupatikana zaidi ya taarifa kupatikana kutoka kwa watu wake wa karibu kuwa alikuwa nje ya Dar es Salaam.

 

Ukiacha sakata hilo ndani ya Chadema, Mnidhamu wa chama hicho, Tundu Lissu, yeye hataki kuuma maneno na hivyo ameamua kupasua jipu. Amesema ushahidi uliopatikana unaeleza kuwa siku chache baada ya kurekodi mkanda huo, Mwigulu Nchemba alimtumia Ludovick Sh 50,000 kupitia mtandao wa Vodacom, hivyo anahoji zilikuwa za nini.

 

Lissu anasema anashangaa kusikia Ludovick ameamua kuisaliti familia ya Lwakatare kwa kuwa alikuwa ni mtu wa karibu wa familia hiyo, kwani Lwakatare na mkewe ndiyo  waliosimamia na kufanikisha ndoa ya Ludovick.

 

Amesema Ludovick pia ndiye aliyekuwa wakala wa Lwakatare katika kusimamia kuhesabu kura wakati akigombea ubunge mwaka 2010 jimboni Bukoba. Hata hivyo, Lissu anakiri kuwa Ludovick alikuwa mwanachama mtiifu wa Chadema na alikuwa katika kikosi cha Blue Guard, ila anahoji:


“Hivi leo Sh 50,000, si milioni Sh 5,000,000 au kumi ni Sh 50,000 tu zinasababisha amsaliti mtu wake wa karibu na kumsabishia alale Magereza?

 

“Ninavyoijua afya ya Lwakatare ilivyo, asipokula tu inakuwa mgogoro unafikiri kesho Ludovick ataonekana vipi kwa watoto wa Lwakatare,” amesema.


Lissu amesema kupitia mkakati aliouita wa ‘kishamba’, kamwe Chama Cha Mapinduzi (CCM) hakitaiangusha Chadema bali ni kuzidi kukipa umaarufu siku za usoni.

Ludovick alivyorekodi mkanda

Amesema Desemba 28 mwaka jana saa 5 asubuhi Ludovick alikwenda nyumbani kwa Lwakatale na saa 5:59 na akiwa hapo alimpiga simu Nchemba kwa namba iliyoorodheshwa kwenye kitabu cha Bunge kutaarifu kuwa amefika.


Ameongeza kuwa kwa kuwa Ludovick alikuwa kama mtoto wa nyumbani, aliingia nyumbani kwa Lwakatare muda wowote na kukaa sehemu yeyote, hivyo siku hiyo ndiyo aliyoamua kufanya kazi hiyo kwa kumuliza Lwakatare maswali ya mtengo.


Amesema katika mkanda huo inasikika sauti ya Ludovick ikiuliza maswali ambayo yanatengeneza jibu, ambayo hutumika kama mtego wa kumtega muulizwaji ili atoe jibu analotaka muulizaji.


Lissu amesema, hata hivyo, anashukuru majibu yaliyotolewa na Lwakatare hayakuwa kama muulizaji alivyotaka. Amesema kuwa iwapo angejibu kama Ludovick alivyotaka Chadema ingekuwa na hali mbaya na kesi hiyo ingekuwa ngumu kwao.

 

Lakini kwa kuwa Chadema ni chama kilichotumwa na Mungu kwa ajili ya kuwakomboa Watanzania, Lwakatare akajibu kama anavyojua yeye na si kama muulizaji alivyotaka, amesema Lissu.


“Maswali kama haya hayaruhusiwi kisheria. Hakimu au jaji makini hawezi kuruhusu kufanywa ushahidi hapa ndo urahisi wa kesi hii ulivyo. Tunashinda saa ya kwanza tu, ya tatu tunaanua virago na kuwaacha wakitoka vichwa chini,” amesema.


Amesema Desemba 29, mwaka jana, Mbunge wa Chadema, Kabwe Zitto, ambaye naye anadaiwa kuwindwa na chama chake, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, Mwigulu Nchemba na Naibu Katibu Mkuu Bara wa Chama cha Wananchi (CUF), Julius Mtatiro walionekana katika moja ya vituo vya televisheni huku Nchemba akijigamba kuwa ana mkanda wa Chadema wakipanga mauaji.


“Hata CD yenyewe hairuhusiwi kutumika katika ushahidi wa kesi kwani muda wote walikuwa wapi kuupeleka hadi wakatangaze kwenye televisheni? Hizi ni fitina za kishamba, lazima mahakama itilie shaka ushahidi huo labda kama wanao mwingine,” amesema.


Amesema Lwakatare ameshitakiwa kuwa alifanya mkutano kwa mujibu wa sheria ya ugaidi ya mwaka 2002 inaeleza kuwa ili uitwe mkutano wa ugaidi ni lazima kuwe watu watatu na kuendelea. “Lakini katika mkanda huo unaonesha kuwa waliofanya mkutano katika nyumba yake ni watu wawili na si watatu na kuendelea hivyo hilo hawatupati,” alijigamba.


Amesema Lwakatare ameshitakiwa kwa mashitaka manne – moja ni la kuruhusu nyumba yake kutumika kwa kikao cha ugaidi ambapo alibainisha kuwa kosa hilo halina kifungu cha hukumu. Amesema shitaka la pili ni kushawishi ugaidi ambalo iwapo atakutwa na kosa atahukumiwa kifungo cha kati ya miaka 15 na isiyozidi 20.


Kufanya mkutano kufanikisha ugaidi, ni kosa ambalo adhabu yake ni kifungo cha miaka ya kati ya 10 na isiyozidi 15.

Historia ya Ludovick utata

Wakati mahakama ikisubiriwa kusikiliza na kutoa uamuzi wa mashitaka yaliyofunguliwa dhidi ya watuhumiwa, habari zilizopatikana zinasema Ludovick amekuwa akiishi maisha ya “aina yake”.


Habari za uhakika zinasema kwamba mtuhumiwa huyo amepata kupewa hifadhi katika familia moja mjini Morogoro, baada ya kujitambulisha kuwa ni yatima. Kwa maelezo yake, aliomba msaada wa kusomeshwa, na akafanikiwa kupelekwa katika Chuo cha Ualimu Morogoro.

 

Imeelezwa kwamba katika kipindi hicho, alifahamiana na mtu mmoja mwenye asili ya Mkoa wa Mara (jina tunalo), ambaye alimwezesha kupata hifadhi nyumbani kwa mmoja wa viongozi katika mhimili mmoja hapa nchini (jina tunalihifadhi kwa sasa).


Hapo alieleza kwamba alikwama kusoma seminari kutokana na kufiwa na wazazi. Imeelezwa kwamba, akiwa nyumbani kwa msamaria mwema huyo, siku moja, usiku wa manane, aliruka ukuta na kutokomea, lakini aliweza kurejea saa 9:30 usiku.


“Baada ya kutoka tulimweleza bosi wetu, akaamua tukae nje tusubiri tuone kama atarudi. Kweli, alirudi 9:30 usiku, ajabu ni kwamba ukuta ulikuwa mrefu sana, lakini aliweza kuruka kwa namna ambayo sote tulishangaa.

“Bosi wetu kuona hivyo akaamua kumfukuza. Lakini kabla ya hapo alimhoji na yeye akasema hajui namna anavyoweza kuruka ukuta, akasema ana matatizo ya akili,” amesema mmoja wa walinzi.


Habari nyingine zimesema kwamba akiwa Morogoro aliweza kuongoza ibada kadhaa za mazishi za madhehebu Katoliki. “Hatukumsikia tena baada ya kutoka Morogoro hadi tulipopata taarifa kwamba anasoma DUCE jijini Dar es Salaam,” kimesema chanzo chetu.

 

Kanisa Katoliki lafanya uchunguzi

Katika hatua nyingine, JAMHURI imepata taarifa za kina kuwa Kanisa Katoliki nchini limeshitushwa na taarifa kwamba Ludovick amewahi kufanya kazi kwenye makazi ya Papa jijini Vatican.


“Mimi si msemaji, lakini tumefanya uchunguzi kwenye ubalozi na huko Vatican, hakuna kumbukumbu zozote za Ludovick kupata kutumikia au hata kuajiriwa, ila tusubiri taarifa rasmi,” alisema mtoa habari wetu.


JAMHURI imepeleka maswali rasmi kwa Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), ambapo wameahidi kulichunguza suala hili na kutoa majibu ya kina.

1287 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!