Mheshimiwa Rais, kwanza nakupongeza kwa mchango wako wa hali na mali katika kusaidia wahanga wa tetemeko lililoukumba Mkoa wa Kagera mwezi uliopita kwa nafasi yako kama Rais, na pia kwako binafsi. 

Kutokana na uhaba wa nafasi ya makala, sitataja kila kitu ulichokifanya, ama kilichofanywa kwa niaba yako, au kutokana na wewe, katika kusaidia wahanga. Na wala hilo si kusudio la makala hii. Kusudio langu kuu ni kuwapa wahanga wanyonge zaidi sauti ya kukufikia ili uwaokoe.

Kabla sijaanza kuwasilisha hoja na maombi ya makala hii, naona ni muhimu nikufahamishe misingi wa nitakayoyasema. Kwanza kabisa, ninayoyasema yanatokana na kufuatilia kwa karibu sana maafa yaliyowapata wakazi na watu wengine waliokuwa mkoani Kagera siku ya Jumamosi tarehe 10 Septemba 2016. 

Pia nimesoma na kusikiliza taarifa za maafa hayo tangu yatokee, naendelea kuzifuatilia kwa karibu kupitia vyombo vya habari; na pale ambapo naona kama taarifa zinakinzana nafanya mawasiliano na walio kwenye maeneo husika kujua lipi lina ukweli au uhalisia, na lipi halina.

Kama mtu yeyote mwenye akili dadisi au tambuzi ambavyo atakuwa ameishahisia, ninazo sababu za kufuatilia maafa haya kwa karibu. Binafsi nimezaliwa na kukulia Kagera, nina ndugu na jamaa wengi huko, na hivyo ni nyumbani kwetu na nina maslahi na mkoa huo. Ingawa si maskani yangu kwa sasa.

Pili, ni mwanataaluma wa mazingira na maendeleo endelevu mwenye kupenda kuchambua sababu za matukio na madhila yake, na nimesajiliwa kisheria kama mtaalamu wa tathmini ya athari za kijamii na kimazingira. Tatu, napenda kusaidia jamii kila ninapokuwa na uwezo wa kufanya hivyo na kwa namna ninayoweza.  

Mheshimiwa Rais, katika janga hili la Kagera ni dhahiri kuwa umefanya uamuzi mgumu, ikifuatia kauli nzito, na matendo maridhawa, hususan kutoa msaada moja kwa moja kwa mama mmoja mjane wa Karagwe aliyekuwa ameanza kujijengea na kushindwa kuendelea. Kwa kuchambua haya uliyoyafanya, napata faraja kiasi kuwa unajua kilichojiri na kinachoendelea kutokana na janga hilo. Nazungumzia sehemu hizi kwa maana ndizo zenye wahanga ambao ni wanyonge na ambao wanahitaji msaada zaidi na ambao ni vigumu kufikisha kilio chao kwako.

Wasiwasi wangu ni kwamba taaswira ya kilio cha mnyonge aliyeathiriwa na tetemeko, mpaka sasa inaonekana kuwa ni ya kuungaunga (checkered). Na kama unavyofahamu. Taarifa ndiyo mpango mzima (of paramount importance) katika kuhudumia wahanga wa janga lolote. Kutokuwa na taarifa sahihi na kamili kunaweza kukasababisha juhudi na misaada mikubwa ikawa haina tija inayotarajiwa.

Aidha, kukosekana kwa taarifa sahihi na kamili kunaweza kukasababisha misaada kutoakisi hali halisi ya uhitaji wa wahanga, kuchelewa, ama kutopelekwa kunakotakiwa. Kwa hiyo, ni jambo la faraja kusikia kuwa kutafanyika uhakiki upya, ikiwa ni kiashiria kuwa tatizo limegundulika na kuna nia ya kuliondosha.

Hata hivyo, bado kuna hofu kuwa uhakiki unaotarajiwa kufanywa usiweze kukidhi haja ya taarifa sahihi kama wahusika katika kufanya zoezi hilo watakuwa wale wale, na kutumia mbinu zile zile zilizotumiwa awali.  Na ikitokea hivyo, itakuwa Taifa limeingia gharama nyingine isiyokuwa na tija na kupunguza fedha ambazo zingetumika kusaidia wanyonge. Nasema haya kutokana na ukweli kuwa tija ya uhakiki inategemea sana usahihi wa takwimu za msingi; na kama hazipo, basi kuwepo na watoa taarifia wakweli na waadilifu. Hapa ndipo kwenye tatizo kubwa, na tatizo hili ni la kitaifa.

Wote tumeshuhudia ugumu unaopambana nao katika kurudisha nidhamu, uaminifu, na uadilifu katika utendaji wa kazi ngazi za juu serikalini. Mambo yako vile vile chini. Na kutokana na hilo, kuna wanyonge wasioweza kujirudishia makazi, na ambao itakuwa vigumu kufikiwa na misaada kutokana na udhaifu wa baadhi ya viongozi, watendaji, na watoa huduma.

Kwa bahati mbaya sana tunakaribia majira ya mvua za vuli, na mvua hizo zikinyesha kabla wahanga hao kupata makazi, tunaweza tukajikuta na janga jingine la magonjwa na vifo kutokana na maji machafu kusambaza maradhi yatokanayo vinyesi. Hili linaweza kuwa tatizo kubwa sana kwenye viunga vya manispaa na miji kama Hamugembe na Rwamishenye ambako tayari miundombinu ya maji machafu imeharibiwa na tetemeko pamoja na kuwepo kwa msongamano wa watu. Waziri wa Afya ameliona.

Vifo vingine vinaweza kutokana na watu kuangukiwa na kuta zilizodhohofishwa na tetemeko zikijalainishwa na mvua. Nyumba nyingi zimejengwa kwa tope badala ya saruji kwenye viungio vya matofali. Kwa hiyo, hata nyumba ambazo zinaonekana zimesimama zina udhaifu huo; na zisipokarabatiwa kabla ya mvua, zinazweza kuanguka mvua zikianza. Hali hii inaweza kukuza maafa maradufu, hasa kwa wasiojiweza kutokana na umaskini, uzee, maradhi sugu, ulemavu, ujane, na uyatima. Ukweli ni kwamba wahanga hawa ni wengi!

Ni kutokana na hofu ya mkoa na nchi kujikuta na janga juu ya janga, nimeona haja ya kuandika makala hii kama kupaza sauti ya wanyonge niliowataja hapo juu na kukuomba uwangalie kwa jicho la ziada na kuwaonea huruma ile ile ambayo umekuwa unaonesha kwa wanyonge; uwalegezee msimamo wa kutojenga nyumba za watu binafsi, na kuruhusu wasaidiwe kujenga makazi ya kujikinga na madhara ya hali ya hewa. 

Natambua kuwa uamuzi na msimamo wako kuhusu utoaji msaada wa kujenga kwa wahanga ulikuwa wa kimkakati, ikiwa umezingatia mahitaji mapana ya jamii kuliko mtu mmoja mmoja kutokana na uwezo kuwa mdogo na mahitaji kuwa makubwa sana. Huu ni uamuzi maridhawa, hasa ukizingatia uwezo wa serikali kifedha, michango iliyokwisha kupatikana, na mahitaji ya wahanga.

Hata hivyo mimi bado naona la kuwajengea wasiojiweza linawezekana kabisa kama kutakuwa na mbinu mahususi za kukusanya na kugawa misaada, ikiwa ni pamoja na kuunda vikosi vya vijana vya kujengea wasiojiweza nyumba; kwa mfano, nyumba ndogo za vyumba vitatu vya futi 9 kwa 9 kwa familia kubwa, na vyumba viwili kwa familia ndogo. Na wale walioanza kujijengea wakashindwa, wasaidiwe kumalizia ujenzi kulingana na kilichobakia.

Mheshimiwa Rais, kama unavyofahamu, kawaida watu wakijua kuwa wanaolengwa ni wanyonge, wasiojiweza, au wahanga wa maafa, huwa wanaguswa kwa kuona kuwa huo ni msaada wa kibinadamu na kujisikia kuwiwa kusaidia. 

Jambo la muhimu ni wachangiaji kuwa na imani kuwa wanachotoa kinafikia walengwa. Katika hili, kwa bahati mbaya, kwa zama tulizoko, haitoshi kusema wahusika wanaaminika au mfumo unaaminika; ni muhimu kuwa na viashiria bayana kuwa kilichotolewa kimefika kunakotakiwa na kufanya lililolengwa. 

Hivyo, naamini kukiwa na mchango mahsusi, mathalani wa kutumia mtandao wa simu kama wafanyavyo taasisi mbalimbali, yakatolewa maelekezo bayana namna ya kutuma fedha, mrejesho wa mara kwa mara kutaarifu umma kiasi cha fedha na misaada mingine inayopatikana, ikiwa ni pamoja na matumizi yake. Uwezekano wa kupata misaada mingi zaidi katika muda mfupi bado upo. 

Ukweli huo umedhihirishwa na kamati ya maafa ya tetemeko Kagera katika tangazo lake kupitia vyombo vya habari ya kuwa Watanzania wakituma kwa simu shilingi 100 kila mmoja itapatikana bilioni tano! 

Watanzania, na hata wahisani wengineo, wakijua michango yao inakwenda kwa waathirika wasiojiweza na wakaelekezwa namna ya kutuma fedha kwa simu, walio wengi wala hawatatoa shilingi 100 tu; watatoa zaidi. Tuseme wakipatikana wachangiaji asilimia kumi tu ya Watanzania, na wakatoa wastani wa shilingi 2,000/- kila mmoja, fedha za kuwajengea wahanga wa tetemeko wasiojiweza zitatimia, maana zinaweza kufikia zaidi ya shilingi bilioni 10.

Kuhusu ufundi, napendekeza kuhamasisha na kuchagua vijana waliomaliza JKT na wengineo ambao watapangwa katika vikundi/vikosi na kupewa jina mahsusi kama Youth Corps for  Settlement Construction and Rehabilitation watakaofanya kazi na wahandisi na mafundi ujenzi kutoka vyuo vya Veta, Suma-JKT, Folk Colleges, na taasisi zozote ambazo zinaweza kujumuika katika kupiga makambi na kujenga nyumba za wasiojiweza.

Ili kujengea jamii husika uwezo wa kujengea wengine, vyema vikundi hivyo vikaunganishwa na vijana na mafundi kwenye vijiji husika. 

La kuzingatia ni kwamba kuweko na uratibu na usimamizi; na watenda kazi wote walipwe angalau posho ya kutwa na kupewa chakula na malazi kama mahema (kwa wasioishi kwenye jamii husika). 

 

Mshauri Mwelekezi wa Maliasili, Mazingira na Maendeleo  Endelevu

tkaiza@gmail.com

1721 Total Views 4 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!