qGl24RvrKatika hali isiyotarajiwa kwenye kizazi cha sasa, kizazi cha sayansi na teknolojia, kizazi kinachosifika kwa kuwa na maono mapana, Mbunge wa Jimbo la Karagwe (CCM), Innocent Bashungwa, amelishangaza Taifa na ndugu zangu Wanyambo.

Bashungwa, kijana matanashati, mbunge kijana aliyepata fursa ya kuwawakilisha wananchi wake bungeni, tumemshuhudia akiwakilisha wapiga kura wake kwa kuomba Uwanja wa Kayanga, uliopo makao makuu ya Wilaya ya Karagwe ujengwe kama kumbukumbu ya kitendo cha mgombea urais kupitia CCM, John Pombe Magufuli, kupiga ‘push up’ jukwaani!

Kufuatia ombi hili, sikuyaamini masikio yangu bali ilinilazimu kuomba msaada kwa jirani yangu na baadhi ya jamaa zangu, ili kuhakikisha kile kilichosemwa na mbunge huyu kijana; Wallahi mheshimiwa Bashungwa ana utani mbaya sana kwa Wanyambo.

Kweli mbunge mwenye maono, uthubutu wa kupambana na umasikini wa wapiga kura wake na kuungana kumfukuza adui ujinga, anaweza kuomba jambo hilo? Ah! anawaza kwa sauti.

Wakati akichangia hotuba ya Wizara ya Maliasili na Utalii, Bashungwa alisikika akisema kuwa jimboni kwake watu hawaoi wanawake wazuri, kwani wanaogopa kufanya hivyo kwa sababu wanachukuliwa na wanajeshi! Pia aliiomba Serikali kuhakikisha inaimarisha ulinzi kwenye kata ya Bweranyange ambako wanajeshi wengi hulinda mpaka wa nchi.

Nashindwa kuelewa nia yake ya kugombea ubunge wa jimbo hili lenye changamoto lukuki, huku yeye kama mwakilishi wa wananchi akiishia kuongea mambo yanayochefusha ubongo wa wapiga kura wake na Watanzania kwa ujumla.

Nyaishozi, Nyakahanga, Kishaho, Bushangaro, Chabalisa, Nyabiyonza Kihanga na kwingineko kero zao ni hizo alizozisema mbunge huyu?

Karagwe ina hospitali  moja tu ya wilaya, hospitali ya Nyakahanga ambayo ina umri wa zaidi ya miaka 100 tangu kuanzishwa kwake, ilijengwa na wamisionari Wajerumani mwaka 1912 na ikiwa inamilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania. 

Hospitali hii ilitaifishwa mwaka 1972 na kuwa hospitali teule ya wilaya na hivi sasa iko mbioni kubadilishwa kutoka hospitali teule ya wilaya kuwa hospitali ya Halmashauri ya Wilaya. 

Hospitali hii inahudumia wagonjwa wengi tofauti na uwezo wake. Ina changamoto nyingi katika kutoa huduma ya afya wilayani humo. Mbunge hajaliona hili kama jambo la kupigia kelele na kuitaka Serikali kuokoa maisha ya ndugu zetu kwa kuboresha hospitali hii, ameona bora uwanja wa kumbukumbu.

Bei ya mazao yanayolimwa wilayani Karagwe inapangwa na wafanyabiashara kutoka nchi jirani ya Uganda. Wakulima wananyonywa jasho lao na wafanyabiashara kutoka nchi jirani, kutokana na kutokuwa na soko la uhakika la mazao yao. Karagwe inalima mazao mengi – kahawa, maharage, karanga, mahindi, ndizi na kadhalika, lakini hayana soko la uhakika. Mbunge ameona bora uwanja wa kumbukumbu!

Wilaya ya Karagwe ni miongoni mwa wilaya zenye shida kubwa ya maji safi na salama na hadi sasa hakuna mpango wowote wa kuhakikisha huduma ya maji inatafutiwa ufumbuzi wa kudumu. Wananchi wanatumia maji yanayohatarisha usalama wa afya zao. Bila huduma ya maji ya uhakika, maendeleo hayawezi kuja kwa kasi inayotarajiwa. Mbunge anataka uwanja wa kumbukumbu ya ‘push up’!

Pamoja na kuwa moja ya wilaya zinazoka wasomi wengi, umeme katika baadhi ya maeneo ni anasa, wapo waliozaliwa na kukulia maisha ya vibatari, hili mbunge wala halioni, kipaumbele chake ni kumbukumbu ya uwanja wa kumbukumbu ya ‘push up’!

Nitakuwa mchoyo wa fadhila iwapo sitamshukuru Rais wa Awamu ya Nne, Dk Jakaya Kikwete, kwa kuweza kujenga barabara ya lami kutoka Kyaka mpaka Bugene ambayo imesaidia kupunguza matukio ya ujambazi katika eneo la Uzuri wa Kondoo na Kitengule. Pia JK angalau amesaidia baadhi ya ndugu zetu wanafahamu lami ni nini.

Ukiondoa barabara ya Kyaka-Bugene, nyingine ziko katika hali mbaya. Bila kuwa na barabara nzuri ni vigumu kufikia maendeleo ya kweli. Bashungwa hajaliona hili, ameona jambo la maana kwa wapiga kura wake ni uwanja wa kumbukumbu ya ‘push up’!

Elimu ni msingi wa maendeleo. Karagwe wamejitahidi kujenga sekondari za kata. Hivi leo kila kata ina sekondari na kata nyingine zina sekondari zaidi ya mbili. Lakini hakuna jitihada zinayofanyika kuziboresha sekondari hizi zikawa na walimu wa kutosha na vifaa vya kufundishia. Bashungwa yeye kipaumbele ni uwanja wa kumbukumbu ya ‘push up’. Hapana, ni bora akafikiria kitu cha maana zaidi!

By Jamhuri