Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania (11)

 

Katika sehemu ya kumi, Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere alisema kwa hiyo Waziri Mkuu alipomwambia Rais kwamba hoja ya Serikali Tatu ikijadiliwa Bungeni yeye mwenyewe atakuwa na utatizi wa uamuzi, alikuwa anajisemea kweli yake. Alikuwa katika hali hii ya “dilemma”. Baadaye, kama tunavyojua, alipoambiwa kuwa asipokubaliana na wenzake ataachwa katika mataa, aliamua kusarenda na wote wakaunga mkono hoja ya Utanganyika.

Ifuatayo ni sehemu ya kitabu cha Mwalimu Nyerere alichokiandika mwaka 1994 cha Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania. Endelea…

 

Hawa si watu wajinga, na wala  si wapumbavu; wanajua wafanyalo. Wamefanya uamuzi huu wakijua matokeo yake. Kwa hawa sasa, makosa ya “Wazanzibari” yawe ya kuvunja Katiba au ya aina nyingine, kwao sasa ni faraja; ni hoja ya kudai Utanganyika. Hawa hawawezi tena kutaka makosa hayo yazungumzwe na yasahihishwe; maana yakisahihishwa kama lilivyosahihishwa lile la OIC msingi wake wa hoja yao utabomoka.

Katika hili, “Wazanzibari” na “Watanganyika”, ni mbuya wakuu; ni washiriki na wabia kwenye mradi ule ule wa kutaka kuvunja Tanzania.

 

Lakini hata kama wangekuwapo mawaziri ambao si “Watanganyika”, bali ni Watanzania halisi wanaopenda kukaa na Watanzania wenzao wa Visiwani ili kuzungumza masuala ya Katiba hawawezi kufanya hivyo chini ya uongozi wa sasa wa Serikali ya Muungano. Katiba inayozungumzwa ni Katiba hii ya sasa ya muundo wa Serikali Mbili. Hoja ya Utanganyika ilipoletwa Bungeni Serikali ilikuwa tayari imeteua au inakusudia kuteua  kamati  ya kutazama migogoro ya Katiba iliyopo hivi sasa kati ya Serikali ya Muungano na Serikali ya Zanzibar, na kufanya mapendekezo ya kuiondoa.

 

Tulitazamia kuwa Serikali ya Muungano itapinga hoja ya Utanganyika, na kuwaarifu Wabunge kwamba Kamati hiyo itapokamilisha kazi yake Serikali itafikisha mapendekezo yake Bungeni. Badala ya kufanya hivyo, Serikali ya Muungano ikaamua kuwa mfumo wa Serikali Mbili haufai, kinachofaa ni mfumo wa Serikali Tatu. Hivi sasa sera ya Serikali ya Muungano ni muundo wa Serikali Tatu.

Itawezekanaje Serikali hiyo hiyo ikae chini na Serikali ya Zanzibar kuzungumzia umuhimu wa kutii, au jinsi ya kurekebisha muundo wa Serikali Mbili? Kwao Katiba hiyo inachongojea ni kufutwa tu.

Mapendekezo ya Kamati ya Ndugu Shellukindo na wenzake hayana maana tena kwa Serikali hii. Serikali ya sasa inachosubiri na inachokishughulikia ni Shirikisho la Serikali Tatu- kwa kweli kufa na kuzikwa kwa Tanzania.

 

Hawana uhalali, wala uwezo, wala nia ya kuzungumza Muungano wa Serikali Mbili. Kwa kweli jambo moja ambalo waheshimiwa hawa wamefaulu ni kufanya watu waache kabisa kuzungumza Katiba ya sasa na mambo mengine yale muhimu, na wabaki kumkimbiza sungura wa Serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano”.

Maadamu matatizo halisi ya Muungano hayazungumzwi wala hayashughulikiwi, watu wenye nia mbaya, wa Bara na Visiwani, wanaopenda kuitumia hali hiyo kuivunja nchi yetu wanaendelea kufanya hivyo.

 

Na wale, wa huku na huku, wanachocheana kama mifukuto ya shetani. Na hiyo inawafanya hata watu wasio na nia mbaya ila ni wajinga tu, waamini kuwa inafaa wote tushiriki na tujiandae kuivunja Tanzania tusije tukashtukia kuwa Tanzania imevunjika na tumeachwa katika mataa! Anayedhani kuwa viongozi wetu ni wajinga yafaa akachunguzwe akili zake! Wanajua wafanyalo.

Nimesema awali kwamba “Wazanzibari” na “Watanganyika” ni marafiki wakuu. Matendo ya “Wazanzibari” ni kisingizio kizuri cha matendo ya “Watanganyika”: na matendo ya “Utanganyika” ni kichocheo cha ukabila wa upande wa pili. Wenyewe wanauita “Utaifa”, na ni sawa maana ni wakupinga Utanzania. Serikali yenye msimamo wa Utanganyika haiwezi kukaa na Serikali ya Zanzibar kuzungumza katiba hii ya Serikali Mbili. Hilo linaweza kufanywa na Serikali mpya ya Jamhuri ya Muungano: Serikali inayokubali na kuheshimu Katiba tuliyo nayo.

 

Serikali ya sasa haina uhalali wala uwezo wala nia ya kuizungumza, ukiacha mazungumzo ya kuitia maji ili kuwafurahisha “Wazanzibari”, au kuifuta ili tulete Shilikisho la Serikali Tatu na hivyo kuwafurahisha “Watanganyika”.

MWELEKEO WA CHAMA:

Huko nyuma nimetumia maneno “mwelekeo wa Chama” bila maelezo. Inafaa sasa nieleze maana yake. Ili kusisitiza umuhimu wake. Kujenga nchi si jambo rahisi. Kujenga Tanganyika tuliyorithi iwe Taifa moja imara lisingekuwa jambo rahisi. Tulikuwa tumeanza. Na kujenga Zanzibar tuliyorithi iwe taifa moja imara isingekuwa kazi rahisi.

 

Mimi naamini kuwa kutokana na historia yake ya nyuma na ya karibu kuifanya Zanzibar kuwa Taifa moja imara kungekuwa kazi ngumu zaidi kuliko kuijenga Tanganyika na kuyafanya makabila yake kuwa kitu kimoja. Lakini hatukuruhusiwa kujua. Historia haikuturuhusu kujenga Tanganyika kuwa Taifa wala kujenga Zanzibar kuwa Taifa. Wa Bara tulikuwa raia  wa

 

Tanganyika huru tangu tarehe 9 Desemba, 1961 mpaka tarehe 26 Aprili, 1964; muda wa miaka miwili, na miezi minne, na siku kumi na saba, ukiihesabu na siku ya tarehe 26 Aprili, 1964.

Mimi nilikuwa Rais wa Tanganyika kwa muda wa mwaka mmoja na miezi minne na siku 17 hizo hizo. Wala historia haikuturuhusu kujenga Zanzibar iwe Taifa. Uhuru wa kutoka kwa mkoloni ulipatikana tarehe 10 Desemba, 1963 na Mapinduzi ya kung’oa usultani wa Mwarabu yalifanywa tarehe 12, Januari 1964. Hatukujenga nchi mbili. Badala yake tukafanya kitendo cha pekee katika historia a nzima ya Afrika huru.

 

Tanganyika tuliyokomboa kutoka kwa Wakoloni lakini hatukuiunda mipaka yake ni ya kurithi; na Zanzibar’ tuliyonyakua kutoka kwa Wakoloni na Masultani wa Kiarabu, lakini hatukuiunda, mipaka yake ni matokeo ya unyang’anyi na unyang’au wa Waingereza na Wajerumani, tukaziunganisha zikawa nchi moja. Tanzania ni lulu ya pekee kabisa katika historia ya Afrika huru. Nchi nyingine zote ni za kurithi kutoka katika Ukoloni. Tanzania ni ya kuundwa na sisi wenyewe, kwa hiari yetu wenyewe baada ya kukomboa sehemu zake ilivyo kutoka katika ukoloni.

Wako Watanzania wa ajabu kabisa wanaosema kuwa uamuzi huo, au vyombo vilivyotumiwa, au njia iliyotumiwa, au vyote, havikuwa halali. Hao hawana shaka na uhalali wa Tanganyika,

ambayo iliunganishwa na Wajerumani, na ikamegwa-megwa na Waingereza na wenzao.

 

Kwa hao kama Rwanda na Burundi na Tanganyika zisingetengwa na mabeberu tukazirithi kama zilivyokuwa chini ya Wajerumani, wasingeushuku uhalali wa nchi moja hiyo. Lakini kama baada ya uhuru Rwanda na Burundi na Tanganyika zingeamua kuungana ziwe Nchi Moja. kwa utaratibu wo wote ambao zingekubaliana, “Wazalendo” hawa wangesema muungano huo si halali!

 

Pwani ya Tanganyika na Zanzibar ya sasa zilikuwa pamoja kwa muda mrefu sana kabla ya kutengwa na Wakoloni Waingereza na Wajerumani. Kama zingebaki zimetengana kwa “wazalendo” hao hiyo ingekuwa ni halali, maana zilitengwa kwa hila na mitutu ya bunduki za Mabwana.

 

Lakini uamuzi wa Tanganyika huru na Zanzibar huru kuungana, na hivyo kuwaunganisha tena ndugu waliokuwa wametengwa na Mabeberu, tendo hila kuna viongozi wetu wanaosema kuwa halikuwa halali.

 

Hatukutafuta maoni ya watu kwa njia ya demokrasia wanayoijua wao. Wajerumani na Waingereza walitafuta maoni ya wazee wetu kwa mtutu wa bunduki! Hiyo iIikuwa halali. Nchi walizoziunda kwa njia hizo zilikuwa halali. Tunatakiwa tujivunie Utanganyika na Uzanzibari uliopatikana kwa njia hizo;

 

lakini tuuonee haya Utanzania, tunda la uhuru wetu wenyewe. Sikuamini kuwa wakoloni walifaulu kiasi hiki katika kuzinywesha kasumba na kuzitawala akili za baadhi yetu!

Nilitoka nje ya mstari. Narudia: Tulikuwa Nchi Mbili, lakini kwa hiari yetu wenyewe, tukaamua kuwa Nchi Moja. Kwa sabaabu ambazo nimezieleza mara nyingi, na kama hapana budi nitaendelea kuzieleza tukakubaliana kuwa ni Muungano wa Serikali Mbili. Aidha, tulikuwa na vyama viwili vya ukombozi, TANU na ASP. Na ni vizuri kuendelea kuwakumbusha wale ambao wangependa tusahau, kwamba TANU na ASP vilikuwa vyama vya ukombozi, havikuwa vyama vya uongozi.

 

Hatua ya pili katika historia ya kuijenga Nchi yetu, tuliichukua tarehe 5 Februari, 1977, miaka 13 baada ya Muungano. TANU na ASP, Vyama vyetu vya Ukombozi, ambavyo vilijua kuwa Umoja ni silaha kubwa ya Ukombozi, viliungana vikawa chama kimoja, Chama Cha Mapinduzi, CCM chama ambacho kina nasaba inayofanana na nasaba ya Tanzania. Tanzania ni Tanganyika na Zanzibar, na CCM ni ASP na TANU.

 

Sitaki kusema kuwa CCM nayo ni lulu ya Afrika, lakini naeleza tu mwelekeo wa historia ya nchi yetu na vyama vya ukombozi wetu. Tuliokwisha kuunganisha nchi mbili zikawa nchi moja, sasa tukaunganisha vyama viwili vikawa chama kimoja Hiyo haikuwa hatua ndogo hata kidogo katika kujenga nchi yetu.

Kuna nchi gani nyingine zilizofanya hivyo? Vyama tunavyoviona katika Bara letu siku hizi vinashindwa hata kuunganisha mbinu tu, ili viweze kushinda wapinzani wao katika uchaguzi.

TANU na ASP vilikuwa vyama viwili na vyote vikitawala. Vikajiua kwa hiari ili vizae chama kimoja kiongoze na kuendeleza historia ya nchi yetu. Tumejenga nchi ambayo ilikuwa inaheshimiwa duniani kote ndani na nje ya Afrika.

 

Mwaka huu tumetimiza umri wa miaka thelathini. Kama si maajabu haya yaliyozushwa bure na viongozi wetu watukufu ilitupasa kushangilia sana umoja wa nchi yetu, na kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutufikisha hapa salama.

 

Tungali na Serikali Mbili, lakini tuna Serikali moja tu ya Muungano. Na nani hawezi kuona kwamba hapo haja ya kubadili muundo wa sasa wa Muungano wa Serikali Mbili itakapodhihirika, historia ya Nchi yetu na mwelekeo wa chama chetu vitatuongoza kwenye muundo wa Serikali moja?

 

Kitu kimoja ambacho hatuwezi kutazamia ni kwamba siku moja Nchi Moja hii itakuwa nchi mbili, kwa uongozi wa CCM. Lakini hiyo ndiyo shabaha ya kuwa na Serikali ya Tanganyika. Na hata kama wajinga na wapumbavu hawatambui hayo bado hayo ndiyo yatakayokuwa matokeo ya ujinga wao: ukifufua Tanganyika, utaua Tanzania. Kwa uongozi wa CCM?

Ila narudia tena,

Niliyokwisha kunena,

Sera hii, nilisema,

Si ya umma ni ya chama.

Ni Sera ya Viongozi,

Wa Chama Cha Mapinduzi,

Na waungao mkono,

Uvunji wa Muungano.

Chama hiki Mapinduzi,

Kimeleta mageuzi,

Si Chama pekee tena,

Viko aina aina.

Na Chama Cha Mapinduzi,

Watambue Viongozi,

Ni Chama cha Muungano,

Si Chama cha Utengano.

Kama mwanachama wake,

Hazipendi sera zake,

Atoke, asichelewe,

Aanze chake mwenyewe.

Kama viongozi wetu,

Hawapendi sera zetu,

Watoke waende zao,

Waanzishe vyama vyao.

Viko vyama bozibozi,

vyatafuta viongozi,

Waende waviongoze,

Na hiki tukipongeze!

WASlTEKE CHAMA NYARA,

WAKILAZIMISHE SERA,

AMBAZO KATU SI ZAKE,

NI ZA WAPINZANI WAKE.

HASA KAMA SERA KAA ZINO

ZA KUVUNJA MUUNGANO

Inaendelea wiki ijayo

 

1489 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!