Uchaguzi Mkuu wa Tano nchini Tanzania chini ya mfumo wa vyama vingi, umemalizika na Tanzania imepata Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano, Dk. John Magufuli.

Ajenda kuu ya wapinzani katika uchaguzi wa mwaka huu ilikuwa mabadiliko. Wakubwa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) walipinga haya ya kuwapo mabadiliko Tanzania. Waliwaita wapinzani wadai mabadiliko wapumbavu na malofa. Lakini, Dk. Magufuli alikubaliana na wapinzani. Aliona haja ya kuwapo mabadiliko ya kweli Tanzania. Na alikwenda mbali zaidi. Alisema kwamba yeye asingeleta mabadiliko tu, bali angeleta mabadiliko ya kweli.

Lakini, je, ni mabadiliko yapi wanayohitaji Watanzania? Kabla hatujapata jibu la swali hilo turudi nyuma.

Miaka 10 iliyopita wakati wa kampeni za uchaguzi wa mwaka 2005 zilizomwingiza madarakani Jakaya Kikwete, kaulimbiu ya CCM ilikuwa, ‘Maisha Bora kwa kila Mtanzania.’ Katika utekelezaji wa kaulimbiu hiyo, Kikwete alipoingia madarakani alitoa mabilioni ya shilingi kwa kila mkoa yaliyojulikana kwa jina la ‘Mabilioni ya Kikwete’ kwa lengo la kuleta maisha bora kwa kila Mtanzania. Maisha bora kwa kila Mtanzania hayakupatikana.

Kwa upande mmoja, fedha ziligawiwa kwa misingi ya itikadi ya kisiasa. Waliogawiwa fedha hizo ni vijana na wanawake wanachama wa CCM. Na kwa upande mwingine, sehemu kubwa ya fedha hiyo haikuwafikia walengwa. Ilitiwa mifukoni mwa hawa waliopewa jukumu la kugawa fedha hizo na hakuna aliyefuatilia matumizi ya fedha hiyo mpaka leo.

Lakini jambo moja ni wazi. Hata kama Serikali ingekuwa na nia njema kiasi gani kwa Watanzania, maisha bora kwa kila Mtanzania yasingeweza kupatikana kwa kuwagawia fedha Watanzania wote. Fedha za kuwagawia Watanzania wote zingetoka wapi?

Basi, maisha bora kwa kila Mtanzania hayakupatikana kwa sababu fedha peke yake haiwezi kubadili maisha ya wananchi. Wakati ule CCM ilituhumiwa kwa kushindwa kuleta maisha bora kwa kila Mtanzania.

Lakini haikukosa cha kusema. Ilisema kwamba maisha bora kwa kila Mtanzania yasingewezekana bila kila mtu kufanya kazi kwa juhudi. Lakini CCM ilipokuja na kaulimbiu ya ‘Maisha bora kwa kila Mtanzania’ haikusema kwamba kila Mtanzania angejiletea mwenyewe maisha bora. Iliwaaminisha wananchi CCM ingewaletea maisha bora kama wangeichagua.

Kaulimbiu ya ‘Maisha bora kwa kila Mtanzania’ hapana shaka ilitokana na CCM kukubali kwamba Watanzania hawakuwa wanaishi maisha bora na kwamba kulikuwa na haja ya kuleta mabadiliko ambayo yangemwezesha kila Mtanzania kupata maisha bora.

Vilevile kaulimbiu ya kuleta mabadiliko katika maisha ya Mtanzania. Wakati wa kampeni, mwaka huu wanaukawa walikuwa wanajibizana: ‘Mabadiliko’ na wengine walijibu: ‘Lowassa’. Ni Edward Lowassa aliyetarajiwa kuleta mabadiliko hayo. Sasa ni Magufuli atakayeleta mabadiliko yanayoliliwa.

Lakini Dk. Magufuli hawezi kuleta mabadiliko peke yake. Anachoweza kufanya ni kuongoza mabadiliko. Mabadiliko yataweza kupatikana kwa mawaziri kujituma na wananchi pia. Na mabadiliko mengine wanayohitaji Watanzania hayahitaji fedha. Yanahitaji moyo na uzalendo.

Tuanze na Polisi. Watanzania wanahitaji mabadiliko yapi kutoka kwao? Kwanza polisi watekeleze kwa vitendo dhana ya ‘Polisi ni usalama wa raia’ kwa sasa raia si salama mbele ya polisi. Kuna habari za polisi kuwabambikizia kesi, hasa vijana wasio na hatia. Inadaiwa kwamba vijana wengi wako mahabusu na magerezani kwa sababu hiyo.

Halafu polisi wamegeuza Tanzania kuwa nchi yenye utawala wa kipolisi. Hakuna tena utawala wa kiraia. Ilivyo polisi inatumiwa vibaya na chama tawala kukandamiza wapinzani. Pia wanatumiwa na wawekezaji na watu wenye fedha kukandamiza haki za watu maskini.

Halafu polisi wanakamata wapinzani wanaokusanya matokeo ya upinzani huku CCM wakifanya kazi hiyohiyo. Wanalinda demokrasia au nafasi zao za kazi? Kwa upande huohuo wa polisi kutumiwa vibaya na chama tawala hatujasahau bado polisi walivyotumia nguvu kubwa kupambana na raia waliokuwa wakidai matokeo ya uchaguzi yatangazwe.

Wananchi walijua kwamba kucheleweshwa kutangazwa matokeo ya uchaguzi kulitokana na kutafutwa mbinu za kutafuta matokeo hayo kwa lengo la kukandamiza wapinzani. Na wapinzani bila wao kufanya vurugu, ushindi wao unaporwa.

Kwa ujumla kinachotakiwa siyo polisi kupambana na raia wanaodai matokeo yatangazwe, bali kuhimiza wahusika watangaze matokeo kwa lengo la kudumisha amani. Hayo ndiyo mabadiliko ambayo Watanzania wanayohitaji. Polisi wasitibu matokeo. Watibu chanzo cha watu kufanya vurugu.

Watambue kwamba bila haki hakuna amani. Kwa hiyo wasimamie haki ili amani idumu. Kwa njia hiyo tutakubali kwamba kweli polisi ni usalama wa raia.

Tumeendelea kushuhudia pia polisi wanavyozuia wananchi kuandamana wakiwa na lengo la kulinda chama tawala na Serikali yake ili kuleta picha, eti Watanzania wanaridhika na kila kitu kinachofanyika nchini.

Maandamano ni njia halali katika nchi zote ya kidemokrasia ya kudai kitu fulani kifanyike au kisifanyike. Jukumu la polisi ni kulinda maandamano; siyo kuyazuia kwa kisingizio cha taarifa za kiintelejensia! Kumbe lengo ni kulinda chama tawala na Serikali yake.

Watanzania wanataka mabadiliko. Wanataka utawala wa kiraia nchini mwao. Hawataki utawala wa kipolisi. Polisi wasione fahari kupiga watu mabomu na rungu wananchi wasio na hatia, kuwamwagia maji ya upupu, kuwakokota wananchi ardhini mfano wa gogo.

Polisi wanaofanya hivyo wanajiweka mbali na raia. Halafu, askari waache kunyanyasa wajasiriamali na kupora vitu vyao. Watanzania wanataka pia mabadiliko katika uendeshaji wa uchaguzi nchini mwao. Tukitaka kusema kweli (na ni lazima tusema kweli) tangu ulipoingia mfumo wa vyama vingi Tanzania mwaka 1992, Watanzania wamekuwa na uchaguzi huru, lakini si uchaguzi wa haki.

Chama tawala kimeendelea kushinda uchaguzi kwa madai ya kutoa rushwa na kutuhumiwa kuiba kura tume ya uchaguzi. Mwaka huu uwe wa mwisho wa kupatikana ushindi kwa kutoa rushwa na kuiba kura.

Pia kwa kuwa Dk. Magufuli anataka mabadiliko ya kweli, basi ahakikishe kwamba sheria inayokataza kuhoji mahakamani matokeo ya uchaguzi wa rais inafutwa mwakani. Sheria hii inahalalisha Tume ya Uchaguzi kuiba kura kwa niaba ya CCM. Watanzania hawahitaji uchaguzi huru tu bali na wa haki.

Kwa upande wa huduma za jamii hapa ndiyo mahali hasa Watanzania wanapohitaji mabadiliko ya kweli. Wanataka wasiendelee kutoa Sh 10,000 kwa kumuona daktari bila kupewa dawa yoyote. Hata wakati wa ukoloni haikuwa hivyo. Ni kweli Watanzania wana wajibu wa kuchangia huduma za jamii, lakini wasiishie kuchangia kumuona daktari tu, wapewe dawa. Walale vitandani. Wajawazito wakute vifaa vya uzazi hospitalini. Na madaktari na wauguzi wawe na lugha safi.

Mashuleni wananchi wanataka kuona mabadiliko. Watoto wa maskini wapewe elimu bora na wasiendelee kukaa sakafuni. Pia michango idhibitiwe na Serikali. Haitoshi kudai kuwa michango inapitishwa na Kamati za Shule, wakati wazazi wenye kamati hizo hawaelezwi gharama halisi ya vitu wanavyotakiwa kuchangia.

Walimu, kwa mfano, waeleze wananunua mitihani inayotoka nje kwa bei gani na wanauzia wanafunzi kwa bei gani? Serikali irejeshe posho kwa walimu iliyokuwa ikitolewa wakati wa utawala wa Rais Ali Hassan Mwinyi, ili walimu wasiendelee kutafuta maisha kwa kudai michango isiyo na idadi na kusumbua wanafunzi ambao wazazi wao hawana uwezo wa kulipa michango hiyo.

Watanzania wanahitaji pia huduma nzuri ya maji na umeme. Hawataki kutafuta maji ya matope mabondeni hata Dar es Salaam, makao makuu ya utawala. Pia hawataki kukatiwa umeme kila siku. Hiyo ndiyo hali halisi ya Tanzania ya leo.

Serikali mpya inatakiwa pia kupambana vikali na rushwa. Watanzania wanajua ukweli wa mambo. Rushwa haiishi nchini kwa sababu inadaiwa kuwa wanaotazamiwa kupambana na rushwa ndiyo wapokeaji wakubwa wa rushwa. Vilevile inadaiwa kwamba Tanzania imeendelea kuwa soko kuu la dawa za kulevya barani Afrika kwa sababu wanaotazamiwa kupambana na dawa za kulevya hupokea rushwa kutoka kwa wafanyabiashara wakubwa wa dawa hizo.

Watanzania pia wanataka mabadiliko polisi na mahakamani kwa upande wa upatikanaji wa haki. Inadaiwa kuwa mtu hapati haki sehemu hizo bila kutoa rushwa. Kwa hiyo wanaopewa haki wakati wote ni wale watoa rushwa lakini maskini hapati haki.

Wakulima pia wanahitaji mabadiliko. Wasikopwe mazao yao na watafutiwe masoko ya mazao yao. Tusiishie kwenye kilimo kwanza tu bila kujali wakulima. Serikali ya Rais Magufuli iwajali pia wastaafu. Siyo kwa kuwapata fedha bali kwa kuwatumia.

Serikali iliyomaliza muda wake haikujali wastaafu. Ilijali vijana wa Bongofleva. Sasa tunataka mabadiliko. Hatuwezi kuorodhesha mabadiliko yote wanayoyahitaji Watanzania. Kwa kuwa Rais Magufuli amedhamiria kuwaletea Watanzania mabadiliko ya kweli hapana shaka anajua fika mabadiliko wanayoyahitaji Watanzania.

Kikubwa, Serikali yake idumishe amani ya Tanzania kwa kutenda haki. Bila haki hakuna amani. Amani tuliyonayo mpaka leo haikutokana na Serikali kuwatendea haki Watanzania bali iImetokana na Watanzania kuwa wavumilivu.

993 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!